Home Afrika Mashariki Nani mwenye namba ikitokea kura ya kutokuwa na imani dhidi ya Ruto?

Nani mwenye namba ikitokea kura ya kutokuwa na imani dhidi ya Ruto?

3372
0
SHARE

ISIJI DOMINIC

SIASA ambayo wanasiasa kutoka Kenya wamekumbushwa kuhubiri ni ile ya kuendeleza msisitizo wa njia sahihi za kujikinga na kuenea maambukizi ya virusi vya corona, ambavyo vimetikisa uchumi wa dunia ukisababisha biashara nyingi kufungwa.

Mashirika ya ndege ni miongoni mwa yale yalioathirika na janga la virusi vya corona yakilazimika kusitisha safari zao kwa baadhi ya nchi huku nayo serikali za nchi mbalimbali zikiwataka wananchi wao kuahirisha safari zao ambazo si za muhimu.

Virusi vya corona vimezuia kufanyika mkutano wa kuhamasisha ripoti ya jopo kazi ya Building Bridges Initiative (BBI), iliyokuwa ifanyike mwishoni mwa wiki iliyopita katika kaunti ya Nakuru.

Wanasiasa wengi wanaounga mkono BBI iliyotokana na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, kuzika tofauti zao za kisiasa, wamekuwa wakimshutumu Naibu Rais William Ruto na washirika wake wakidai wamekuwa wakipinga kile kinachofanywa na Serikali wanayoitumikia.

Kutokana na kumwona Ruto kama mpinzani ndani ya Serikali anayoitumikia, viongozi wa Chama cha ODM ambacho kina idadi kubwa ya wabunge wa upinzani, walidokeza mpango wa kuwasilisha muswada bungeni wa kutokuwa na imani na Naibu Rais.

Hoja hiyo imechangizwa na Ofisi ya Naibu Rais kumulikwa katika sakata la mamilioni ya ununuzi wa silaha feki na baadaye kufuatiwa na taarifa mbaya za kuuawa kwa Sajenti Kipyegon Kenei aliyekuwa anafanya kazi katika ofisi hizo.

Seneta wa Siaya, James Orengo alisema matukio hayo ambayo yameifanya Kitengo cha Upelelezi ya Makosa ya Jinai (DCI) kuwahoji watu akiwemo waziri wa zamani wa michezo, Rashid Echesa imekichefua ofisi ya Naibu Rais na ndiyo maana ODM inafikiria taratibu za kikatiba kumshughulikia Ruto.

Hata kupiga kura ya kutokuwa na imani kumwondoa naibu rais, aliyechaguliwa katika uchaguzi mkuu pamoja na rais ni mchezo wa namba ambapo itahitajika upatikanaji wa theluthi mbili ya wabunge katika mabunge yote mawili; Bunge la Taifa na Bunge la Seneti, kuupitisha.