Home Latest News NATO imesababisha mamilioni ya wakimbizi kutoka Syria

NATO imesababisha mamilioni ya wakimbizi kutoka Syria

3020
0
SHARE

MAPEMA mwezi huu maiti ya Aylan Kurdi, mtoto M wa Kisyria wa miaka mitatu, iliokotwa katika ufukwe wa bahari ya Mediterania. Alizama pamoja na ndugu yake Galip wa miaka mitano na mama yao wakati wakijaribu kuvuka kutoka Uturuki kuelekea Ugiriki Picha na habari za mtoto huyo zilienea kwa haraka katika vyombo vya habari na mtandao kote duniani. Waliokuwa wamesahau au wanajaribu kusahau wakalazimika kukumbuka kuwa kuna tatizo kubwa la wakimbizi kutoka Syria na kwengineko wanaojaribu kuokoa maisha yao kwa kuingia Ulaya Baada ya mashambulizi ya Syria yaliyodumu zaidi ya miaka minne, mamilioni ya wananchi wake wamegeuka wakimbizi ndani na nje ya nchi yao.

Idadi hii haijawahi kuonekana duniani tangu vita kuu ya pili Picha za mtoto Aylan zilienezwa katika mtandao na mtoto huyo akazungumzwa sana katika vyombo vya habari. Lakini ni wachache walielezwa kuwa kabla ya kufa kwa mtoto huyo wakimbizi 71 walikufa kwa kukosa hewa wakiwa wamefungiwa katika lori lililokuwa linawasafirisha hadi Austria. Habari hii haikupewa uzito Pia tangu mwanzo wa mwaka 2014 tayari wakimbizi zaidi ya 5,000 wamepoteza maisha yao wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kutoka Libya kuelekea Italia. Zaidi ya Wasyria milioni nne wamekimbilia nchi za jirani, wakiishi katika kambi nchini Uturuki, Lebanon, Jordan, Iraq na Misri. Wengine milioni nne wameyaacha makazi yao na wamebaki ndani ya nchi.

Hii ni Syria ilivyo leo, nchi ndogo yenye wakaazi milioni 17, nchi ambayo kwa karne nyingi imekuwa ikiwapokea wakimbizi kutoka nje. Bila shaka nchi za Kiarabu zimefurika na zinashindwa kuwahudumia idadi kubwa ya wakimbizi. Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi (UNHCR) nalo limeelemewa. Halina chakula cha kutosha kuwalisha. Kila mkimbizi anapewa chakula cha nusu dola kwa siku, lakini wengi wanakosa hata hicho kiduchu.

Kwa mujibu waUNHCR, inakisiwa kuwa takriban wakimbizi 366,400 wamevuka bahari ya Mediteranea na kuingia Ulaya. Kati yao 2,800 wamepoteza maisha yao. Waliobaki wameingia nchini Ugiriki, wamekuwa wakitembea kwa miguu zaidi ya kilometa 110 kupitia Macedonia, Serbia, Hungary hadi Austria. Wengi wao ni wanawake na watoto Licha ya Wasyria, idadi kubwa ya wakimbizi wamekuwa wakiingia Ulaya kutoka nchi za Kiarabu, Afrika na Asia.

Wanavuka bahari kutoka Libya au Uturuki hadi Ugiriki na Italy. Kutoka huko wanaelekea nchi za Ulaya magharibi kwa kupitia nchi za Ulaya mashariki Kuna wanaotoa hoja kuwa hawa si wakimbizi bali ni wahamiaji wa kiuchumi, ni watu wanaotaka kuzihama nchi zao ili kutafuta maisha bora. Kisheria mkimbizi ni yule ambaye anaondoka nchini mwake ili kuepukana na kukamatwa, kuteswa au kuuawa kwa sababu za kisiasa, kidini au kikabila. Tofauti na yule anayekimbia ili kuepukana na maisha magumu au umasikini Sasa katika hali ya kivita kama ile ya Syria au Iraq au Libya au Afghanistan ni vigumu kuanza kumchunguza kila mmoja katika halaiki ya watu wanaokimbia.

Inatoshakusema kuwa yule anayekimbia kwa sababu ya vita si tofauti ya yule anayesakwa kwa sababu ya dini au kabila lake. Mmoja atauawa kesho akipatikana na mwengine atakufa baada ya muda kutokana na njaa. Yote mawili ni mauaji ya kimbari. Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron ambaye ametumia neno la kejeli kama ‘kundi la nzige’ (swarms) ili kuwaelezea maelfu ya wakimbizi wanaojaribu kuingia Ulaya. Naye waziri mkuu wa Canada, Stephen Harper anasema wengi kati yao ni magaidi wa Al Qaeda au ISIS (Daesh) Ujerumani iko tayari kuwapokea wakimbizi 800,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Pia itawapokea milioni moja mwaka 2016 na 2017 Hii ni nchi yapeke katika Umoja wa Ulaya (EU) ambayo imetenga dola za Marekani bilioni 6.68 kuwagharamia wakimbizi hao Nchi mbili katika bara la Ulaya zinapaswa zipongezwe kwa ukarimu wao, nazo ni Ujerumani na Sweden. Katika mtandao tunaona wananchi wakijitokeza kuwakaribisha wakimbizi. Kamati za maandalizi zimeundwa ili kuwapokea wanapowasili Nchi zingine ambazo zimeahidi kuwapokea wakimbizi ni Austria, Norway, Finland na Iceland. Denmark imekataa katukatu.

Uingereza na Ufaransa zilikataa lakini zikakubali kupokea wachache. Uingereza imetangaza kuwachukua wakimbizi 10,000 wakati Ufaransa itawapokea 24,000 “katika kipindi cha miaka miwili ijayo”. Canada imesema itawachukua 10,000 katika muda huohuo, lakini baada ya kuwachunguza. Rais wa Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker amesema nchi nyingi za Ulaya zimekataa kushiriki katika mpango wa kuwapokea wakimbizi.

Amesema umoja huu wa nchi 28 umekosa umoja. Alizikumbusha nchi hizo kuwa wakati mmoja katika historia ni Ulaya ndiyo iliyotoa wakimbizi wengi zaidi ya Syria leo “Ni vizuri tukakumbuka kuwa bara zima la Ulaya ni bara la wakimbizi. Mamilioni kutoka Ulaya walikimbia vita, udikteta na udini na wakaomba hifadhi nchi za kigeni,” alikumbusha Juncker Juncker amesema haya baada ya polisi kuwashambulia wakimbizi 25,000 katika kisiwa cha Ugiriki cha Lesbos. Wakimbizi hao walifikia kutoka Uturuki wakiwa njiani kuelekea Ulaya magharibi.

Hasira zilipanda baada ya wakimbizi hao kusubiri zaidi ya wiki mbili bila ya kupata usafiri kama walivyoahidiwa Pia nchini Hungary serikali ya mrengo wa kulia ilitoa amri kwa majeshi kujenga uzio wa chuma mpakani ili kuzuia wakimbizi wasiingie. Serikali ikayakamata magari yaliyokuwa yakiwasafirisha wakimbizi kutoka Hungary na kuwaingiza Austria. Hata hivyo serikali haikufanikiwa, kwani wanaharakati wakatangaza katika mtandao na wakafanikiwa kukusanya magari zaidi ya 200 nawakawavusha wakimbizi kutoka mpaka wa Hungary Kati ya wanaharakati hao ni Erzsebet Szabo kutoka Austria.

Yeye alisema amesaidia kuwavusha wakimbizi kama 380. Alipoulizwa kama haogopi kukamatwa na polisi alijibu “hata kama watanikamata mateso nitakayopata hayafanani nayale wanayoyapata hawa wakimbizi. Marekani na wenzake wa NATO wamekuwa wakiishambulia Syria kwa lengo la kumuondoa madarakani Rais Bashar al-Assad, sawa na walivyofanya huko Libya ambako walimuua Kanali Gaddafi. Baada ya kuuawa kwa Gaddafi hali imezidi kuwa mbaya, pamoja nanchi kutekwa na majeshi ya mujahidina ambao sasa wamekuwa maadui wakubwa wa magharibi.

Lakini watawala wa NATO hawataki kujiuliza suali la msingi: je baada ya kumuondoa Assad ndio iweje? Hao vibaraka wa magharibi waliopewa fedha na silaha hawaonekani. Hivi sasa sehemu kubwa ya nchi inadhibitiwa na ISIS, nao wamekuwa wakiwachinja raia wa magharibi.

Je hawa watayeyuka hewani baada ya kuondoshwa kwa Assad? Tangu kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti (USSR) mwaka 1991 mataifa haya yaliamua kutumia nguvu za kijeshi ili kueneza himaya zao katika Ulaya mashariki, nchi za Kiarabu, bara la Afrika na kwengineko. Wameshambulia Afghanistan wakidai wanapigana na ugaidi kisha wakaishambulia Iraq kwa udanganyifu kuwa Saddam alikuwa na silaha za maangamizi. Matokeo yake ni kuangamiza jamii na kuwaua maelfu na maelfu ya wananchi, wakiwemo watoto na wanawake. Leo wanajifanya eti wanaomboleza kifo cha mtoto Ailan Kurdi Wakaishambulia Libya na kumuua kikatili Muammar Gaddafi.Nchi za magharibi zilishangilia wakati hata maiti ya Gaddafi ilipodhalilishwa. Leo Libya imesambaratika na matokeo yake ni maelfu ya wakimbizi.

Imekuwa ni njia ya wakimbizi kutoka Afrika na kwengineko kusafiri hadi Ulaya, wengi wao wakizama na kufa baharini Halafu wakaishambulia Syria ili kumpindua Assad.

Mamilioni ya dola na silaha zikaingia nchini ili kuchochea vita. Matokeo yake ni kuzuka kwa majeshi ya ISIS na mamilioni ya wananchi wakikimbilia nchi za jirani