Home Habari Ndoto ya Sumaye ya urais bado ipo?

Ndoto ya Sumaye ya urais bado ipo?

1592
0
SHARE

Leonard Mang’oha

AHADI ya kutojiunga na chama chochote cha siasa iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Mstaafu na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Frederick Sumaye, imeshindwa kutimia baada ya kurejea katika chama chake cha zamani CCM.

Sumaye alijiunga na Chadema Agosti mwaka 2015 kwa madai kuwa anakwenda kuimarisha upinzani ili uweze kuchukua dola na kuimarisha demokrasia nchini.

Alifikia uamuzi huo miezi michache baada ya kushindwa katika mchakato wa kumpata mgombea wa CCM, ambapo Rais wa sasa Dk. John Magufuli alipewa dhamana hiyo.

Desemba 4, mwaka jana Sumaye akaondoaka Chadema baada ya kutoridhishwa na mchakato wa uchaguzi wa viongozi ndani ya chama hicho, ambapo alidai kufedheheshwa na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho pamoja na uminywaji wa demokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa.

Uamuzi wake ulifanyika wakati kukiwa na minong’ono mingi kuhusu kutozingatiwa kwa demokrasia katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa chama hicho uliofanyika Desemba 8 mwaka jana.

Moja ya sababu za kuondoka kwake Chadema ni pamoja na kushindwa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chadema Kanda wa Pwani, akiwa mgombea pekee wa kiti hicho licha ya wanachama wa kumtaka agombee na kumchukulia fomu ya kugombea, lakini akaambulia kura 28 za ndiyo dhidi ya 49 za hapana.

Kulingana na maelezo yake kushindwa kwake kulichagizwa zaidi na hatua yake ya kutaka kugombea uenyekiti wa chama ngazi ya taifa ambapo hadi anachukua hatua hiyo, alikuwa miongoni mwa wagombea watatu waliorejesha fomu za kuwania nafasi hiyo wengine wakiwa ni Mwenyekiti Freeman Mbowe na Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe.

Kauli yake wakati anajiondoa Chadema alidai kufedheheshwa kutokana na hatua baadhi ya viongozi wa chama hicho kufanya jitihada na hata kutumia rushwa, ili kumnyima nafasi ya kuwania uenyekiti wa kanda hiyo ya Pwani.

Ni kweli angeweza kukaza shingo kama alivyodai yeye wakati huo lakini haikuwa rahisi kama kweli yale yanayoelezwa kuhusu ukuu wa Mwenyekiti wa Chadema na jinsi anavyoilinda nafasi yake.

Uamuzi wa Sumaye kujiondoa Chadema haukuwa na ajabu kwa kuzingatia kuwa kwa hadhi yake kitendo cha kushindwa uchaguzi katika ngazi ya kanda hata kama ni kwa magumashi lilikuwa ni doa kwake kama mwanasiasa na huenda ingempunguzia ushawishi wake katika siasa.

Pia kwa nafasi yake asingeweza kubaki katika chama kama mwanachama wa kawaida asiye na nafasi ya uongozi.

Tunapaswa kukubaliana hata kama kwa kutofautiana kuwa pamoja na nia yake ya kutaka kukuza demokrasia nchini, pia Sumaye alikuwa na nia nyingine zaidi ya kisiasa ikiwamo ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hili linaweza kudhihirishwa na hoja kadhaa ambazo zinaweza kutumika kama kielelezo cha kiu ya Sumaye kuitamani Ikulu ya Tanzania.