Home Afrika Mashariki Nec, Tcra, zichukue tahadhari

Nec, Tcra, zichukue tahadhari

2915
0
SHARE

OKTOBA 25 mwaka huu ni siku ambayo Uchaguzi Mkuu wa urais, ubunge na udiwani utafanyika nchini kote. Hii ni siku maridhawa ambayo kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura atafanya uchaguzi kwa wagombea wanaomfaa.

Rai tunatarajia kuwaona watanzania wakishiriki zoezi la upigaji kura kwa namna ya pekee, kwamba kudumisha amani, utulivu, ulinzi na usalama katika vituo vyao kabla na baada ya uchaguzi. Tunaamini zoezi hili linatawaliwa na shamra shamra nyingi huku kila upande ukijitangazia ushindi.

Tumeona wagombea wa vyama mbalimbali wakishiriki zoezi hili na wafuasi wao wamekuwa kwenye pilika nyingi. Tunatarajia kuona sifa za ulinzi na usalama zikiendelea kutawala na kudumishwa. Pamoja na kusema hayo ni vema tukatoa tahadhari kwa vyombo vinavyohusika zaidi kwenye uchaguzi huu.

Kwanza kabisa tunatarajia kuona msimamizi mkuu yaani Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikitimiza majukumu yake kwa haki na bila upendeleo. Tunaamini kuwa NEC itasimamia mambo yote kwa kushirikiana na vyombo vya usalama ili kufanikisha zoezi hili liende kwa amani.

NEC inalazimika kuhitaji ushirikiano wa hali ya juu kwenye suala la uchaguzi na Mamlaka ya Mwasiliano nchini (TCRA). Mamlaka hii inategemewa kwa kiasi kikubwa kulinda na kusimamia taarifa za upotoshwaji zinazoenezwa kwenye mitandao hususani ya mitandao ya kijamii. Tunaamini kuwa TCRA italazimika kufanya juhudi kubwa kuhakikisha inasimama imara na kuzuia kila aina ya upotoshwaji, tukizingatia kuwa nchi yetu haina uezoefu wa kutosha na matumizi ya mitandao hii.

Aghalabu tumeona makosa mengi yakifanyika huku taarifa za uzushi na upotoshwaji zikiota mizizi kila kukicha. Tumeshuhudia taarifa za vifo, majanga na mambo mengine ya upotoshwa ambayo hayakustahili kufanywa. Tumeshuhudia baadhi ya wanasiasa wakifungua mashauri TCRA kulalamikia kuchafuliwa kupitia mitandao ya kijamii. Tunadhani huu ni wakati ambao TCRA na NEC kwa kushirikina na Jeshi la Polisi wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa ili kukabiliana na hali hiyo.

RAI tunaamini kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kudhibiti usambaaji wa tarifa za upotoshaji. Mathalani uwezekano mkubwa wa kupotosha masuala mbalimbali siku ya uchaguzi, yakiwemo kura zilizopigwa kwenye vituo mbalimbali nchini. Madhara ya upotoshwaji wowote kwenye suala la upigaji kura linaweza kusababisha maafa ndani ya Taifa letu ama kushuhudia wimbi la watumiaji wake wakifikishwa mahakamani kwa makosa hayo. Tunaamini kuwa ili kuondokana na hayo lazima TCRA na NEC wasimame kidete kulinda amani yetu kwa watanzania kwa ujumla.

Tahadhari hii ni sehemu ya kukumbushana namna watu wanavyoweza kuathiriwa na njia hasi ya mitandao ya kijamii ambayo lengo lake lilikuwa kuhabarishana. Tunaamini mamlaka ya taasisi hizi yatafanyiwa kazi ili tuwe na uchaguzi wa amani.