Home kitaifa NEC, ZEC ni tume huru kwa mujibu wa sheria, nongwa inatoka wapi?

NEC, ZEC ni tume huru kwa mujibu wa sheria, nongwa inatoka wapi?

1271
0
SHARE
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage

NA DEOGRATIAS MUTUNGI

UCHAGUZI wa kisiasa lazima uwe huru na ni mtamu unapokuwa huru, kwa sababu unapokuwa huru hunogesha demokrasia na mifumo yake.

Raha ya uchaguzi kisiasa ni kuwa huru, demokrasia ustawi na kunoga kisiasa endapo tu haki itatamalaki wakati wa kupiga kura, haki ya kura hujenga imani, usawa na amani kwa viongozi wateule ndani ya jamii na nje ya mipaka yake.

Dhambi ya kupora haki haipimiki wala kulinganishwa na chochote kile hapa ulimwenguni, bakora ya mpora haki kutoka kwa Mungu ni chungu sana na kamwe huwezi kuifananisha na uchungu wowote ule katika uso huu wa dunia.

Siasa na falsafa ya uaminifu kwa kiongozi ndani ya jamii inayomzunguka hupimwa kwa mizania ya upatikanaji wake, aidha heshima ya kiongozi ni tunu inayojitambulisha kutokana na uhalali wake kwenye sanduku la kura.

Kura na haki ni moyo wa kisiasa wenye mapigo na mishipa inayosambaza amani ndani ya jamii ya Watanzania, mapigo ya moyo wa siasa yakikosa haki bin kura ni chanzo cha maelewano mabovu ndani ya nchi yanayoweza kupelekea uhasama wa kisiasa ikiwa ni pamoja na machafuko ya ndani kwa ndani “  Political Chaos”.

Kwa sasa tupo kwenye kipindi cha uchaguzi wa kuwapata viongozi watakaotuongoza miaka mitano kwa maana ya Rais, Wabunge na Madiwani, nyakati hizi zipo fununu zinajengewa hoja hasi juu ya tume hizi mbili yaani NEC “National Electoral Commission” Kwa maana ya Tanzania bara na ZEC “Zanzibar Electoral Commission” Kwa maana ya Zanzibar, bila shaka fununu hizi ni sehemu ya nongwa za kisiasa ambazo pengine uwa ni kawaida kwa mataifa yenye kufuata mkondo wa mifumo ya vyama vingi.

Hata hivyo ni dhambi kukaa kimya dhidi ya fununu hizi, ingawa historia ya siasa inasomeka na kuonyesha kuwa nongwa hizi zimetamalaki zaidi Afrika na viunga vyake na kwa uchache bara la Asia, sababu kuu ya nongwa ikiwa ni vyama vya siasa kutoamini mifumo rasmi ya vyombo vya utoaji haki mathalani tume zao za uchaguzi licha ya vyombo hivi kuwepo kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za nchi lakini bado kuaminiana imeonekana kuwa tatizo kubwa kwa wanasiasa wenye mrengo wa upinzani.

Makala haya yanatambua uwepo wa hoja zenye mrengo tofauti zinazojengwa na baadhi ya wadau na wanasiasa juu ya tume katika dhana ya utoaji haki kwa nukta ya upendeleo, hatuwezi kubeza hoja zao isipokuwa tu kuzijibu hoja hizo kwa hoja, ingawa dhana ya upendeleo kwao inazungumziwa katika muktadha wa jazba na hamaki tele pasipo na mantiki halisi inayotambulisha takwa lao.

Je hoja hii ni sahihi? Na kama si sahihi kusudio lake ni nini hasa? Je ni upotoshaji kisiasa au ni nongwa tu za kisiasa ili kupata huruma ya wananchi,  je ni kweli tume inakengeuka au wanaohoji ndio wanaokengeuka kwa sababu hawajui mamlaka na sheria, zinazoiongoza tume au wanajua tu ila wanapotosha mantiki ya  uwepo wa tume ya uchaguzi kwa sababu za kisiasa tu, maswali ni mengi na yanafikirisha.

Kwa muhtasari tume za uchaguzi kwa maana ya NEC na ZEC ni vyombo vilivyopo  kwa mujibu wa Katiba ya nchi na sheria zake, ukirejea ibara ya 74,-(1) inataja bayana uwepo wa tume ya uchaguzi, aidha 74,-(6) inataja majukumu ya tume ya uchaguzi, rejea vifungu vidogo vya (a), (b),(c),(d) na (e) vyote hivi vinaainisha wajibu wa tume katika kusimamia uchaguzi na kutenda haki kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za kisiasa.

Aidha ZEC kwa maana ya tume ya uchaguzi ya Zanzibar ipo kwa mujibu wa kifungu cha 119(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1994, ikiwa sambamba na kifungu cha 4 cha sheria ya uchaguzi namba 11 ya 1984, je hapa nongwa ni nini hasa kama tume zote hizi mbili zipo kwa mujibu wa katiba za nchi? Wasomaji wa makala haya tunahitaji kufikri chanzo cha nongwa hii dhidi ya tume ya uchaguzi kinatokana na nini.

Pengine inawezekana nongwa si neno “tume ya uchaguzi” bali tu watumishi wa tume, kama hoja ndio hii basi ni nyepesi na inayojibika bila kuumiza kichwa, kama kilivyo kitendawili cha kuku na yai nani alianza kuwepo kabla ya mwenzake pengine kuna ugumu wa kutegua kitendawili hiki cha kuku na yai, lakini si kwa dhana ya watumishi wa tume.

Ni dhahiri kuwa watumishi wa tume wapo ndani ya tume ya uchaguzi ili kutenda haki na kanuni za uchaguzi zinawaelekeza hivyo,  ni ngumu kwa mtumishi wa tume kuikwepesha haki iliyo wazi na kuutangaza uovu wake kinyume na matakwa ya tume kisheria na kikatiba.

Mfano ushindi wa wazi wa asilimia 87, asilimia 90, asilimia 95, au asilimia 100 kamwe hauwezi kuminywa na tume ya uchaguzi na kutangaza ushindi wa asilimia 13, asilimia 10, asilimia 5 au asilimia 1, tatizo la wanasiasa na wadau wa siasa wanaongozwa na kuishi katika “siasa za kutoaminiana na hofu iliyopitiliza”

Iko wazi kuwa nadharia ya “hofu ya haki” katika mazingira yoyote yale ni chanzo cha imani ndogo kwa yule unayemjengea dhana hiyo, wanasiasa wa Tanzania na wadau wa siasa hofu yao dhidi ya tume inaanzia kwenye ibara hii na vifungu vyake.

Ibara ya 74,-(1) “Kutakuwa na Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano ambayo itakuwa na wajumbe wafuatao watakaoteuliwa na Rais”-(a). (b), (c) na 74,-(2) ikumbukwe kuwa hawa ni binadamu wana mapenzi yao ndani ya mifumo ya kisiasa, wanaweza kuwa wamechaguliwa na rais lakini bado wakapendelea upande mwingine usio kuwa wa chama tawala.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid.

Aidha tunahitaji kuongozwa na dhana ya “watumishi wa tume” katika kufikiri yaani “Sapere aude” ikiwa na maana ya kutoogopa kutafakari mwenyewe na kuumiza ubongo juu ya jambo fulani.

Wanasiasa wa Kiafrika hutanguliza hofu ya kuporwa haki kabla ya kujenga hoja za ushawishi wa kushika dola, mantiki ya tume ni kutoa haki na si kupora haki za wanasiasa na vyama vyao, vyama vya siasa na wadau wa siasa waache lawama na nongwa kwa tume za uchaguzi badala yake tutambue kuwa hivi ni vyombo vilivyopo kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi.

Andiko hili linatafakari juu ya hoja inayojengwa juu ya tume kupora haki na kuminya baadhi ya wanasiasa kifitina,  tafakuri hii inakuja na jibu lenye historia na  mfumo wa vyama vingi na kujiuliza mbona vyama vinavyoinyooshea kidole tume dhidi ya utendaji wake wamekuwa sehemu ya watu waliotangazwa na tume hiyo kama washindi wa nafasi zao aidha ubunge, uwakilishi au udiwani sasa nongwa ni nini hasa, bila shaka kuna jambo lililojificha juu ya agenda hii inayojengewa hoja na baadhi ya vyama vya kisiasa.

Makala haya yanatambua bayana kuwa ulimwenguni kote kisiasa tume ya uchaguzi ni chombo muhimu sana katika utoaji wa haki dhidi ya vyama vya kisiasa, aidha ni chombo muhimu chenye kubeba dhamana na mustakabali wa amani ya nchi kwa sababu tume hubeba matumaini ya watu walio wengi dhidi ya haki bin haki, kuminya haki kwa tume dhidi ya haki ya mpiga kura ni sawa na mtoto Koku kuchezea rupia karibu na tundu la choo maana kifuatacho huwa ni kilio cha kusaga meno.

Tume ni kichocheo cha ustawi wa demokrasia ndani ya siasa za mfumo wa vyama vingi, tume imara na yenye weledi katika maamuzi ya kiutendaji hujenga imani ya kitaasisi katika utoaji wa matokeo ya kweli ndani ya vyama vya kisiasa.

Fununu za kisiasa zinazojengwa na wadau wa kisiasa na wanasiasa wenyewe ni hasi na zinafikirisha sana dhidi ya tume zetu za uchaguzi ambazo zimetambuliwa na sheria, kanuni za nchi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanaojenga hoja dhidi ya tume ni Watanzania wenzetu sharti wajibiwe na mamlaka husika au na mwanahabari yeyote anayeweza kutoa “elimu hoja” dhidi ya watu hawa ili wapate kuelimika na kuondoa upotoshaji unaoendelea kwa sasa na ndilo kusudio halisi la makala haya kutoa elimu pande zote mbili yaani wanasiasa, wadau wa siasa na wale wanaojiandaa kuingia katika ulingo wa siasa sambamba na wananchi ambao ndio wapiga kura.

Makala haya yanahitimisha uchambuzi huu uliojikita kuweka sawa uhalali wa uwepo wa tume za uchaguzi kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya nchi kwa kusema ni vema kujenga hoja na kuziwasilisha katika muktadha wa fikra pevu zinazojenga na kulinda amani ya nchi yetu ili kuepuka nongwa isiyo na mantiki.

Aidha tunalo jukumu la kutafakari neno kwa neno pale hoja za kisiasa zinapowasilishwa kwetu na wanasiasa, zipo hoja zinazojenga zenye kusudio la kubomoa, waswahili wanasema bora kujenga kuliko kubomoa, aidha ni bora kubomoa nyumba kuliko amani ya nchi kwa sababu ni ngumu kujengeka kama ilivyokuwa awali.

HYPERLINK “mailto:dmutungid@yahoo.com” dmutungid@yahoo.com

0717-718619