Home Habari Ngorongoro kugawanywa

Ngorongoro kugawanywa

3161
0
SHARE

Ni uamuzi wenye nia ya kuokoa Bonde la Ngorongoro   

ABRAHAM GWANDU, ARUSHA

SERIKALI inakusudia kuligawa eneo la Hifadhi ya Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro (NCAA) katika kanda nne maalumu.

Lengo kuu la hatua hiyo ni kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotishia na kuharibu uasilia wa eneo hilo muhimu kwa uhifadhi na shughuli za utalii.

Uamuzi huo unatokana na mapendekezo yaliyowasilishwa serikalini kuhusu matumizi bora ya ardhi kati ya wanyamapori na jamii za asili (binadamu) zinazoishi ndani ya eneo hilo, ambalo ni urithi wa dunia.

Akizungumza na RAI mwanzoni mwa wiki jijini Arusha, Kamishna Mkuu wa Uhifadhi wa NCAA, Dk. Freddy Manongi, alisema ili kulinusuru eneo hilo kwa kuligawa katika kanda nne, pia kuna haja ya kuwaondoa kabisa watu wanaoishi humo na kuwatafutia eneo jingine.

 “Kuna haja ya kugawa ardhi kama sehemu ya mkakati wa kulinusuru kutokana na changamoto hizi, na hata ikibidi hizi jamii zinazoishi humo zitolewe kwenda nje ya hifadhi, wapewe fidia kidogo, nchi yetu bado ni kubwa, kuna ardhi ya kutosha nje ya hifadhi,” alisema.

Dk. Manongi alizitaja kanda zinazopendekezwa kuwa ni eneo ambalo shughuli za binadamu hazitaruhusiwa kabisa isipokuwa kwa ajili ya uhifadhi na utalii wa picha pekee (Core Conservation Zone).

Kanda ya pili ni eneo la uwindaji wa kitalii ambalo litatokana na kumegwa kwa kilometa za mraba 1,500 za Pori Tengefu la Loliondo (Core Conservatin Sub-Zone).

Alisema kanda ya tatu ni eneo litakaloruhusu shughuli mseto, lakini halitaruhusiwa ujenzi wa nyumba (Transition Zone).

Kanda ya mwisho ni eneo ambalo shughuli za binadamu zitaruhusiwa kwa kufuata sheria namba 4 ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999 (Human Development zone).

“Mapendekezo haya yataenda kwa awamu. Awamu ya kwanza ni ya muda mfupi kati ya miaka miwili hadi mitano, muda wa kati miaka mitano hadi kumi na ya muda mrefu kuanzia miaka kumi na kuendelea,” alisema Dk. Manongi.

Pamoja na nia njema hiyo, lakini Dk. Manongi alikiri ugumu wa jukumu kubwa linaloikabili NCAA, hususani kutoka kwa wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu na mazingira, ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakipinga mipango na mikakati mbalimbali inayoweza kuondoa uasili wa eneo hilo.

“Nafahamu haitakuwa kazi rahisi, kelele zitakuwa nyingi, lakini tutawaelimisha wananchi hususani jamii za asili za eneo hili la Bonde la Ngorongoro wajue faida na matunda yatokanayo na uhifadhi kuwa ni kwa ajili ya Watanzania wote. Naamini wataelewa,” alisema.

Wakati mapendekezo hayo yakipelekwa serikalini, maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani yanafanyika wiki hii kwa kaulimbiu “Utalii na Ajira Malengo Bora kwa Wote”.

 Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imetimiza miaka 60 tangu ilipoanzishwa rasmi mwaka 1959.

Kwa mujibu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco), Bonde la Ngorongoro ni miongoni mwa maajabu na urithi wa dunia.

Lilianzishwa baada ya kumegwa kutoka iliyokuwa hifadhi kubwa ya Taifa Serengeti (The Great Serengeti), lengo likiwa kuruhusu matumizi mseto ya ardhi kati ya binadamu na wanyama.

Pamoja na matumizi mseto ya ardhi yanayoruhusu jamii za asili zinazoishi eneo hilo adhimu na la kipekee duniani kuishi pamoja na wanyama pori, NCAA haikuacha malengo yake makuu matatu ambayo ndiyo hasa msingi wa kuanzishwa kwake.

Malengo hayo ni pamoja na kuhifadhi mazingira asilia, kulinda na kuwatunza wanyama pori, kutangaza vivutio vyote vya utalii vinavyopatikana eneo hilo na kuhifadhi jamii za asili pamoja na mila na desturi zao.

Jamii zinazoishi ndani ya NCAA ni Maasai, Datoga na Hadzabe, japo kila moja inafuata mila, desturi na tamaduni zake.

Mathalani jamii za Maasai na Datoga ni wafugaji wa ng’ombe, lakini Hadzabe huendesha maisha yao kwa kuokota matunda, kurina asali na kuwinda wanyama pori.

Kutokana na sheria iliyounda NCAA kutoruhusu shughuli za kilimo, kujenga makazi ya kudumu na kuwinda wanyama ndani ya eneo lote la Hifadhi ya Ngorongoro, Serikali ililazimika kuunda chombo maalumu ambacho kinaitwa Baraza la Wafugaji.

Kupitia Baraza la Wafugaji, mafanikio kadhaa yamepatikana ikiwamo usimamizi mzuri katika sekta za elimu, afya na maji.

Hata hivyo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu kutoka 8,000 waliokuwapo wakati inaanzishwa hadi 93,136 waliopo sasa, kazi ya kuendelea kuzisaidia jamii hizo imekuwa mzigo mzito kwa NCAA.

Akizungumzia maadhimishio hayo, Dk. Manongi alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote cha miaka 60, lakini pia kuna changamoto nyingi zinazoendelea kutatuliwa kwa ubunifu na umahiri mkubwa.

“Idadi ya watalii imeongezeka, huduma zimeboreshwa sana ikilinganishwa na miaka iliyopita na mapato yatokanayo na shughuli za utalii mwaka jana yalikuwa takribani Sh bilioni 143. Hizi ni fedha za wananchi zinazosimamiwa na Serikali yao,” alisema.

Kuhusu changamoto, alisema ongezeko la idadi ya watu, idadi ya wanyama, uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa changamoto za muda mrefu ambazo kila wakati jitihada mbalimbali zinafanyika kuzitatua.

“Ongezeko hilo lina athari nyingi pande zote kwa binadamu na kwa wanyama. Kumekuwa na maambukizi ya magonjwa kutoka kwa wanyama pori kwenda kwa binadamu, kuvamiwa kwa binadamu na wanyama.

“Kutokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu na hasa mifugo kuongezeka, ardhi imeharibiwa, rutuba ambayo ilikuwa inatunza uoto wa asili imevurugwa, hali inayosababisha kuota kwa magugu vamizi ambayo ni hatari kwa mustakabali wa eneo lote.

“Mabadiliko ya tabia nchi nayo yamechangia mito na vijito kukauka, hali iliyosababisha uoto wa asili kuathirika na baadhi ya wanyama kutoweka na aina nyingine za wanyama kuongezeka wakiwamo fisi,” alisema.

Meneja wa Huduma za Utalii wa NCAA, Paul Fissoo, alisema katika kipindi cha miaka 60 yapo manufaa mengi ambayo yamepatikana, na kunufaisha wananchi na nchi kwa ujumla.

Miongoni mwake ni ajira kwa Watanzania, kuongezeka kwa mapato na makusanyo ya maduhuli ya Serikali, pato la taifa kuongezeka hususani katika eneo la fedha za kigeni ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Pia alisema ongezeko la idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi wanaotembelea NCAA, kuboresha mbinu za uhifadhi kiasi cha kuvutia watalii na wawekezaji ambao wengi wamewekeza katika huduma za hoteli na kambi za kisasa za kulaza watalii.

“Tunatumia gharama kubwa katika kuhifadhi na kutangaza vivutio vilivyopo Ngorongoro, lengo ni kuonyesha namna ambavyo maliasili inaweza kubadilisha maisha watu.

“Tumeboresha huduma zetu, tumeona utalii wa kutumia magari pekee haukidhi mahitaji ya wakati huu, ndiyo maana tukaongeza utalii wa kutumia balloon, utalii wa kutumia farasi, baiskeli pamoja na ndege,” alisema.

Alisema kuwa kutokana na kazi nzuri iliyofanyika katika kipindi cha miaka 60 ya uwepo wa NCAA, Serikali imeona iongeze majukumu mengine ya kusimamia maeneo mapya ya vivutio vya utalii ikiwamo Kimondo cha Songwe, mapango ya Amboni, eneo la Olduvai Gorge na michoro iliyoko kwenye miamba ya Mumba.

Olduvai Gorge ni eneo ambalo ziligundulika nyayo za binadamu wa kale aliyeishi miaka milioni 3.6 iliyopita, rekodi ambayo hadi sasa watafiti wa mabaki ya viumbe hai hawajawahi kuivunja.  

Alisema tayari kazi ya kuboresha miundombinu katika maeneo hayo mapya inaendelea, ili watalii watakaopenda kutembelea vivutio hivyo waweze kufika kwa urahisi.

“NCAA inatumia nguvu kubwa kutangaza maeneo haya mapya, tutafanya matamasha mbalimbali ya kitalii ndani na nje ya nchi, tutaweka mabango makubwa yatakayosaidia kutangaza vivutio hivyo.

“Matunda yaliyotokana na mafanikio ndiyo yametusukuma kuwekeza nje ya jukumu letu la uhifadhi kwa kujenga Kituo cha Utalii cha Ngorongoro Tourist Centre (NTC) jijini Arusha.

“Jengo la NTC limegharimu fedha zilizotokana na mapato yetu kiasi cha takribani Sh bilioni 45,” alisema Fissoo.

Uhifadhi wa wanyama na uoto wa asili, ubora wa miundombinu ya barabara, hoteli na makambi ya watalii ni miongoni mwa jitihada zilizochangia kuongeza idadi ya watalii kutoka ndani na nje ya nchi wanaotembelea Ngorongoro.

Katika ujumbe wake mwaka huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guteress, alisema duniani kote sekta ya utalii ni moja ya vyanzo vya ajira vinavyoongoza ikilinganishwa na sekta zingine.

“Utalii unasaidia kuimarisha kesho njema kwa kila moja, unasaidia kukuza uchumi, mamilioni ya ajira yanategemea sekta hii kitaifa na kimataifa,” alinukuliwa Guteress.