Home kitaifa NI KWELI UKITAKA MAMBO YAKUNYOOKEE UIKUMBATIE CCM?

NI KWELI UKITAKA MAMBO YAKUNYOOKEE UIKUMBATIE CCM?

1381
0
SHARE

fredrick-sumaye

NA HILAL K SUED

 

UKITAKA mambo yako yaende vyema ingia CCM. Kauli hii iliwahi kutolewa na si mwingine, bali Waziri Mkuu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, kwenye mkutano mmoja wa hadhara katika Mkoa wa Kilimanjaro.

 

Ni kauli ambayo hawezi kuirejea, lakini sasa ilikuwa na ujumbe mahsusi, mzito na wenye dhamira makini, hasa kwa wafanyabiashara na wengine wanaotafuta manufaa au ahueni fulani inayotokana na matatizo yao mbali mbali. Nimetamka wafanyabiashara kwa sababu wakishafanikiwa katika biashara zao, hawa wamekuwa wachangiaji wakubwa wa mapesa kwa chama hicho kikongwe – hasa wakati wa uchaguzi.

 

Na baadhi yao walikuwa wanajua namna ya kuzirejesha fedha zao na hata kulimbikiza zaidi kutokana na dili/zabuni wanazopewa serikalini, ama kukwepa kodi bila kuulizwa sana.

 

Ilikuwa ukienda popote hapa nchini, katika miji mikubwa ya mikoa au hata ile ya wilaya, ilikuwa nadra sana kumkuta mfanyabiashara mkubwa katika wilaya fulani ambaye haikumbatii CCM. Nakiri kwamba walikuwapo wafanyabiashara wakubwa ambao si wafuasi wa CCM, lakini hawa ni wachache mno na mara nyingi walikuwa hawajionyeshi.

 

Kwa wafanyabiashara kuwa wafuasi wa chama tawala si dhambi au jinai, kwani ni hali ya kupita tu. Nasema hivi kwa sababu endapo chama hicho kitapoteza dola kwa kupokonywa na chama kingine, yumkini wafanyabiashara hao hao baada ya muda, wangehamia chama hicho kingine bila taabu yoyote.

 

Huko Zambia kwa mfano, wafanyabiashara wengi wakubwa waliokuwa wakikikumbatia Chama cha UNIP wakati wa utawala wa Mzee Kenneth Kaunda, baadaye walikikumbatia kilichokuwa Chama tawala cha MMD cha Rais Frederick Chiluba na baadaye Levy Mwanawasa.

 

Lakini hapa kwetu katika awamu hii ya utawala wa John Magufuli, mambo hayo sasa yanabadilika, kwani wafanyabiashara wengi wamejikuta wakigonga mwamba katika harakati zao hizo. Kwa mfano, tangu Magufuli aingie madarakani wafanyabiashara wengi katika maeneo mbali mbali walijikuta wanakadiriwa upya kodi ya mapato na kutakiwa kulipa.

Aidha, zabuni za Serikali sasa hazipatikani kiurahisi kama ilivyokuwa zamani na zile zilizotolewa katika awamu zilizopita zinapitiwa upya – chukulia mfano mikataba ya madini.

 

Kama nilivyosema hapo juu ingawa si jinai au dhambi kwa wafanyabiashara kukikumbatia chama tawala, maovu hutokea iwapo mahusiano yao yatakwenda kinyume cha taratibu za halali zinazokubalika. Na matokeo yake ni kuzuka kwa ufisadi katika ngazi za juu, hali inayosababishwa na uhusiano wa karibu mno baina ya wakuu wa Serikali na wafanyabiashara hao. Na athari zake ni ukwepaji wa kodi, zabuni zilizozidishwa bei, mikataba mibovu isiyo na masilahi kwa taifa na mengineyo mengi.

Lakini haya yote ingawa yalikuwapo tangu awamu za tawala za chama kimoja, yalizidi kuanzia mfumo wa utawala wa vyama vingi ulioanza mwanzoni mwa miaka ya 90. Wakati wa enzi ya utawala wa chama kimoja, wafanyabiashara wakubwa hawakuwa wanakitetemekea sana chama tawala, ingawa walitakiwa kuwa wanachama kwanza ili kupata liseni za biashara zao. Baadhi yao walikuwa wanakataa kutoa michango kwa chama wanapochangishwa na chama au serikali hazikuwa zinawafanya kitu chochote.

Lakini baadaye, katika hali ya ushindani – ushindani mkubwa wa kisiasa na wa kibiashara pia, hali ni tofauti sana kwani wafanyabiashara wakubwa wenyewe walikuwa wanaiendea CCM kuipa michango kwa matarajio ya kupata upendeleo fulani wa kibiashara kutoka serikalini ili waweze kuwapiku wafanyabiashara wenzao.

Na kwa upande wake, Serikali ili ivipiku vyama vingine vya siasa katika kuwania uongozi wa dola, ilikuwa inaonyesha “makucha” yake kwa wafanyabiashara wakubwa ili wachangie na kukiweka chama hicho madarakani kwa manufaa ya pande zote mbili.   

Katika enzi za mfumo wa chama kimoja, ulazima wa kuwa mwanachama ulikuwapo hasa kwa baadhi ya watu wa kawaida tu – hususan wanafunzi wanaofukuzia masomo nchi za nje na pengine kupandishwa vyeo kwa baadhi ya wafanyakazi wa serikalini na mashirika yake.

Lakini, kama nilivyosema hapo mbele, baadhi ya watu mbali na wafanyabiashara waliokuwa wakikikumbatia chama tawala hufanya hivyo kwa lengo maalumu, kama vile kusaka manufaa au ahueni fulani inayotokana na matatizo yao mbali mbali.

Nitatoa mifano kwa matukio ya kweli yaliyotokea: Miaka kadhaa iliyopita, kuna kiongozi mmoja kutoka mojawapo ya vyama vya michezo hapa nchini alifikishwa mahakamani akituhumiwa kutafuna fedha za chama hicho.

Baada ya kesi kusikilizwa, ikaja siku ya hukumu, siku ambayo mshitakiwa alikuja mahakamani akivalia T-Shirt iliyoandikwa “CCM No 1.” Hakimu alimkuta na hatia na akamhukumu kwenda jela. Tukio hilo liliwekwa vyema kwa njia ya katuni katika gazeti moja siku iliyofuata. Bila shaka alikuwa na sababu maalumu ya kuvaa T-Shirt yenye maandishi yale kujaribu kumyumbisha hakimu.

Mfano mwingine: Miaka kadhaa iliyopita kulikuwapo mpango wa kubomoa nyumba zilizokuwa za Shirika la Reli na zilizouzwa kwa baadhi ya wafanyakazi wake katika maeneo ya Kamata, jijini Dar es Salaam, ili kupisha ujenzi wa kituo cha mabasi ya Mradi wa Mwendokasi.

Baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo walipinga hatua hiyo ya kubomolewa nyumba hizo, ambazo walikuwa wameuziwa karibuni tu, ingawa mamlaka husika ilitaangaza kulipa fidia. Wananchi hao walijihamasisha katika umoja na kuandaa mkutano pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

 

Katika mkutano huo baadhi ya wenye nyumba hizo waliosimama kuzungumza walikuwa wamevalia sare na kofia za kapelo zilizoandikwa “Chagua CCM.” Lengo lao ni kujaribu kuuyumbisha uamuzi wa Serikali ambao tayari ulikuwa umeshatolewa. Mifano hii miwili inaonyesha kwamba hakuna garantii katika ule ujumbe wa “Ukitaka mambo yako yaende vyema kumbatia CCM.”

 

Na tukizungumzia sare katika vyama vya siasa, hakika chama tawala kinaongoza katika kuzihamasisha. Kwa mfano, hata katika shughuli ambazo moja kwa moja ni za kiserikali, kama ziara za kiserikali za Rais Magufuli, utaona watu na makada wa CCM wakizivalia sare hizo.

 

Ilikuwa tofauti kidogo wakati wa utawala wa Jakaya Kikwete. Siku moja alikwenda maeneo ya Jangwani, jijini Dar es Salaam kukagua mafuriko baada ya mvua kubwa na picha za runinga zilimwonyesha akiwakaripia makumi ya makada wa CCM waliojazana karibu yake wakiwa katika sare za chama. Aliwaambia: “Huu si mkutano wa chama.”