Home Makala Kimataifa Nyota ya warundi iliyozimika ghafla

Nyota ya warundi iliyozimika ghafla

1090
0
SHARE

MWANDISHI WETU NA MASHIRIKA

MAUTI imetamalaki na kuchukua Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza akiwa bado katika umri wa miaka 55, ambao kwa jamii na tamaduni za Kiafrika, bado ni kiongozi kijana.

Nkurunziza alitangazwa kufariki dunia kwa maradhi ya shinikizo la damu Jumanne wiki hii, Juni 9, 2020 akiwa kweny matibabu nchini kwake.

Taarifa za kifo chake imekuwa kama tetemeko la ardhi nchini Burundi, kutokana na namna wananchi walivyoipokea, kutokana na wasifu wa kiongozi huyo aliyeitawala nchi hiyo kwa miaka 15.

Ingawa Serikali inakanusha kwamba hajafariki kwa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, wachambuzi wanasema sasa Burundi haiwezi tena kuficha ukweli juu ya janga la corona baada ya kifo cha kiongozi huyo na baada ya mke wake kupelekwa Nairobi kwa ajili ya matibabu ya maradhi hayo!

Awali wachambuzi walitarajia kumwona Nkurunziza akivuta hatamu za uongozi nyuma ya kiongozi mpya Evariste Ndayishimiye na kiongozi huyo mpya huenda asingeweza kuonekana kwa uwepo wa Nkurunziza, ambaye alishawekewa mazingira ya kuwa na cheo cha juu zaidi ya mkuu wa nchi.

Mtaalamu wa masuala ya Burundi, Thierry Vircoulon anasema huenda kifo cha Nkurunziza kimetokana na mkakati wa kisiasa.

Kifo cha Nkurunziza kinakuja wiki kadhaa kabla ya rais mteule kutoka chama tawala cha CNDD-FDD, Evariste Ndayishimiye kuapishwa Agosti mwaka huu, baada ya kushinda uchaguzi mwezi Mei.

“Rais mpya anayetokea kwenye utawala wa zamani sasa atakuwa na uwanja huru,” anasema Vircoulon.

WIKI YA RAMBIRAMBI

Wakati wananchi wa Burundi wakiendelea kufuatilia kwa karibu taarifa za kifo cha kiongozi huyo, Serikali imetangaza wiki moja ya maombolezo.

Ni hatua ya kwanza ya Serikali ya Burundi katika kuanza utaratibu wa kuhifadhi na kutoa heshima kwa kiongozi huyo ambaye bado haijafahamika mara moja ni hatua gani itachukua baada ya kifo chake.

Kwa mujibu wa katiba ya Burundi, rais anapofariki akiwa madarakani kabla hajakabidhi madaraka kwa rais mwingine, spika wa bunge anachukua madaraka na kutayarisha uchaguzi mwingine.

HARAKATI ZAKE

Nkurunziza, ambaye alizua hali ya sintofahamu baada ya kuwania uchaguzi wa rais kwa awamu ya tatu, alikuwa kiongozi wa Burundi kwa miaka 10 tayari.

Mwaka 2015, rais huyo aliyeingia madarakani baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha mauaji ya watu 300,000 alisema kuwa hatawania tena nafasi hiyo ya urais kwa sababu ni kinyume na katiba.

Wafuasi wake walitetea kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2005 alichaguliwa na bunge na si wapiga kura na kutetea hoja hiyo katika mahakama ya katiba ya nchini humo.

Alisema baada ya kuwa kiongozi wa zamani wa waasi na kisha kufanikiwa kuongoza Serikali ya Burundi, alijisifu kuwa ameleta amani katika utawala wake nchini Burundi.

Iliripotiwa kuwa maofisa wa diplomasia walifika kuzungumza na Nkurunziza ambaye alikuwa nje kidogo ya mji mkuu, Bujumbura, walimkuta rais huyo akiwa analima na wanakijiji.

Alikuwa anapanda miti ya parachichi ambayo warundi wengi huwa wanaiita miti hiyo jina lake “ama Peter”.

Iliwahi kuandikwa katika mtandao wa Serikali wa Burundi kuwa kutokana na mfumo wake wa maisha ya kawaida, aliwavutia watu wengi wa vijijini kwa sababu ya muda mwingi ambao amekuwa akitumia kukaa nao kijijini.

MLOKOLE

Kabla ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, Nkurunziza ambaye alihitimu masomo ya michezo alikuwa mkufunzi msaidizi katika Chuo Kikuu cha Burundi.

Nkurunziza alikuwa muumini wa dhati wa dini ya kikristo (Mlokole) . Alikuwa pia kocha wa timu ya daraja la kwanza mwanzoni mwa miaka ya 1990 .

Na baadaye kumiliki timu ya hallelujah ambayo pia alikuwa akishiriki kucheza mpira katika nafasi ya ushambuliaji na alikuwa akifunga mara kwa mara.

Chapisho la wasifu wake linasema kuwa jina la timu hiyo linaonesha wazi imani yake ya dini ya kikristo.

Baba yake ambaye alikuwa mhutu aliwahi kuwa gavana, aliuawa katika mauaji ya halaiki ya wahutu mwaka 1972. Baba yake alikua Mkatoliki na mama yake ambaye alikuwa Mtutsi alikuwa muumini wa madhehebu ya Anglikana.

Alikuwa hawezi kusafiri bila timu yake ya mpira pamoja na kikundi cha kwaya. Yeye na mke wake waliwahi kuripotiwa kuwaosha miguu watu waliokuwepo kwenye mkusanyiko.

MTAWALA WA KIIMLA

Nkurunziza na mke wake, Denise waliwahi kuripotiwa kuwaosha miguu watu waliokuwepo kwenye mkusanyiko.

Sio tu watu ambao Nkurunziza alikuwa na imani kuwa wanamuamini. Bali uongozi wake pia aliamini ni kutoka kwa Mungu.

“Anaamini kuwa ni kiongozi kwa matakwa ya Mungu na hivyo anashughulika na serikali yake katika matakwa hayo,”msemaji wake, Willy Nyamitwe anaeleza.

Wakosoaji wake ikiwemo wapinzani kutoka vyama karibu 40 na watetezi wa haki za binadamu, wao wana mtazamo tofauti kumhusu.

Wanamtuhumu kuwa dikteta na ambaye hataki kuachia madaraka kutokana na kuongoza kwake kwa mihula mitatu.

Idadi kubwa ya watu waliuawa katika maandamano ya kumpinga kugombea muhula wa tatu. Wengine zaidi ya 100,000 walikimbia makazi yao kwenda nchi jirani kuhofia usalama wao na kwa hofu kuwa nchi hiyo ingetumbukia kwenye mzozo kwa mara nyingine.

JARIBIO LA MAPINDUZI

Mkuu wa zamani wa majeshi, Godefroid Niyombare aliongoza mpango wa mapinduzi kwa Serikali ya Nkurunzinza wakitaka kumwondoa madarakani mwaka 2015.

Mpango huo ulifanyika na kutangazwa wakati Nkurunziza akihudhuria kikao cha usuluhishi wa migororo cha viongozi wa nchi za maziwa makuu kilichukiwa kikifanyika jijini Dar es Salaam.

Baada ya kushindwa kwa mpango huo wapinzani wakadai kuwa uchaguzi wa mwaka huo haukua wa uhuru wala haki.

HUKUMU YA KIFO

Nkurunziza alihukumiwa kifo na mahakama ya Burundi bila yeye kuwapo mahakamani mwaka 1998 kwa kosa la kutega mabomu ya ardhini, lakini alipata msamaha chini ya makubaliano ya amani yaliyokuwa na nia ya kumaliza mapigano.

Mkuu wa Kitengo cha Haki za Binadamu cha Umoja wa Mataifa (UN), Zeid Raad al-Hussein alitoa wasiwasi wake kuhusu kundi moja la vijana la imbonerakure washirika wa Nkurunziza.

Kilishukiwa kufanya mauaji, kuwatesa watu na kuwapiga na kilisababisha hali kuwa mbaya nchini humo kwa muda.

Katika kikundi cha waasi cha wahutu cha CNDD-FDD kilichoongozwa na Nkurunziza wakati wa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha kifo cha rais wa kabila la wahutu, Melchoir Ndadaye mwaka 1993, alitajwa kuwa muhusika katika njama ya muaji hayo.

Iliwahi kuelezwa kuwa miongoni mwa matukio aliyotasimamia ni kutekeleza vitendo kadhaa vya uvamizi katika barabara kuu za nchini humo, kuwaua wasafiri wengi, wakiwemo watu wa kabila la Watutsi.

Alinyanyua silaha ili kupambana kukomesha utawala ulioongozwa na jamii ya kabila la waliokuwa wacheche Tutsi.

Mwaka 2014 alijaribu na kushindwa kubadili katiba, ambayo inatoa ukomo wa madaraka kwa chama chake cha CNDD-FDD kwa kutoa hakikisho kwa makundi ya jamii ya Watutsi kuwapatia nafasi mbalimbali katika taasisi za kiserikali.

Alikosolewa na umma kuwa anataka kusababisha vita nyingine ya kikabila.

UCHAGUZI WA 2020

Ni majuzi tu, Mei 22 mwaka huu Burundi imekamilisha uchaguzi wake mkuu huku Nkurunziza akitekeleza ahadi yake ya kutogombea urais kwa mara nyingine ambapo mgombea wa chama chake, ambaye ni chaguo lake, Evariste Ndayishimiye aliibuka mshindi.

Kampeni za uchaguzi huo zilishuhudia machafuko na vurugu, huku serikali ikishutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu katika jitihada zake za kuendelea kushikilia madaraka.

Jumatano hii, Mei 20, huku janga la Covid-19 likiwa kileleni, Burundi ilimchagua rais mpya wakati mataifa mengine yakizingatia kanuni za kukaa mbali, nchini humo, mikutano mikubwa ilikuwa ikiendelea bila kuzingatia hilo.

Nkurunziza alisemahewa na haja ya kuchukua tahadhari hizo akisema kuwa raia wa Burundi watalindwa na Mungu dhidi ya janga la corona.

Katika hali hiyo ya kutokuwa na wasiwasi, serikali hiyo hiyo ilitoa taarifa ya kuwa wasimamizi wa uchaguzi kutoka nje lazima wakae karantini kwa wiki mbili pindi wakiingia nchini.

Kwa kufanya hivyo waliwazuia kufuatilia uchaguzi huu. Uamuzi huo haukuwashangaza wachambuzi wa masuala ya Burundi.

Kwa mujibu wa shirika la Human Rights Watch, mauaji yasiyopungua 67 yaliyorekodiwa, yakiwemo mauaji 14 yaliyohusishwa na maofisa wa serikali katika miezi 6 iliyopita.

Pia kumekuwa na ripoti za watu waliotoweka, matukio ya uteswaji na zaidi ya watu 200 wa upinzani kukamatwa na kuzuiliwa.

Maofisa wa usalama pia wameshutumiwa kwa kutumia nguvu kupindukia kuzima maandamano au hata mikutano ya upinzani.

KITITA CHA MAFAO

Rais Nkurunziza anafariki dunia wakti akiwa tayariameshaandaliwa mazingira oevu ya kustaafia, ambayo yangempa fursa ya kuishi maisha ya kifahari akiwa uraiani, huku akiwa bado kijana.

Katika msururu wa marupurupu ambayo angeyapata iwpo angefikia hatua ya kumkabidhi mrithi wake madaraka Agosti mwkaa huu, Nkurunziza angepata mafao ya dola 530,000, makao ya kifahari na angeendelea kulipwa mshahara wake wa urais hadi kufa.

 Pia alitarajiwa kutawazwa kwa taji ya kiongozi mkuu baada ya kujiondoa, ambaye angekuwana mamlka ya juu ya kuweza hata kumrekebisha rais, akiwa na wadhifa wa utukufu, akiitwa “mwonyesha njia”.

Wabunge nchini Burundi tayari walishapitisha muswada wa sheria ambao utampa kitita hicho kikubwa cha fedha Nkurunziza.

Mswada huo wa sheria ulieleza kuwa katika kila kipindi cha miaka saba, baada ya rais aliyechaguliwa kidemokrasia kumaliza muhula wake, mbali na marupurupu hayo, kiongozi anayemaliza muhula wake atakuwa na mshahara na faida zingine sawa na makamu wa rais ambaye yuko madarakani.

Waziri wa sheria Aime Laurentine Kanyana, aliwahi kukairirwa akisema sheria ni vema rais anayemaliza muda wake kuheshimiwa na kukipa heshima kiti cha urais nchini humo.

“Inapendeza kuona rais anayeondoka madarakani akipewa heshima, hili tunafanya kwa raia huyu, wale wanaokuja, na wale waliopita,” alisema bungeni.

Hata hivyo, Agathon Rwasa mwanasiasa wa  upinzani amekuwa akikosoa hatua hiyo ya kutoa kiwango kikubwa cha fedha kwa rais anayeondoka madarakani  na kusema lengo ni kumliwaza  Nkurunziza ili asipate hamu ya kutaka kuwania tena.

“Pengine chama chake  kimeona kuwa  watumie njia hii ili  asitamani kurejea madarakani  ili asigombee tena, ila kwa hali ya uchumi wa nchi inashtua kidogo kuhusu kiasi hicho, ” anasema.

Mswada huo pia unaeleza kuwa rais anayeondoka madarakani atakuwa na kinga ya kutoshtakiwa.