Home Makala Kimataifa OPRAH WINFREY KUMVAA TRUMP UCHAGUZI 2020?

OPRAH WINFREY KUMVAA TRUMP UCHAGUZI 2020?

1824
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Wakati bado wakijitafakari jinsi walivyoisalimisha Ikulu ya White House kwa mtu maarufu wa runinga (TV celebrity), Donald Trump, viongozi wa chama cha Democratic nchini Marekani sasa wana mikakati wa kumshawishi mwingine maarufu wa runinga Oprah Winfrey kuirejesha Ikulu hiyo upande wao.

Hivyo maneno kama ya “Rais Oprah” yameanza kusikika, tena kwa dhati inavyoonekana, na si muda mrefu ujao mikakati itaanza kushika kasi. Vyanzo vinasema ishara ya mikakati hiyo ilionekana usiku wa kuwatunuku “nyota wa filamu” pale wazo la Oprah 2020, lilipotajwa katika hafla ya Golden Globe wiki iliyopita iliyofanyika Beverly Hills, Los Angeles.

Katika hafla hiyo Oprah alikubali kupokea kikombe kilichopewa jina la mwongozaji filam maarufu na mfuasi wa chama cha Republican, tukio lililotafsiriwa na wafuasi wa chama cha Democratic waliopo Hollywood na kwingineko, kwamba ni kuanza kuota ndoto ya kile kinachhonekana kutowezekana.

Lakini hotuba ya Oprah katika hafla hiyo ilikuwa ni tiba ya ya machungu yanayotolewa kila siku na Rais ambaye wiki iliyopita tu alithibitisha tabia yake hiyo pale alipoitikisa dunia kwa kusema Marekani ilikuwa inaingiza wahamiaji wengi weusi kutoka nchi alizoziita “matundu ya choo” kutoka Afrika na Haiti, na si wengi kutoka nchi ya watu weupe ya Norway.

Lakini hata hivyo wazo la mwanamke maarufu wa runinga, Mmarekani wa asili ya Afrika kupambana katika kugombea urais na Mmarekani mweupe msema hovyo, linazidi kuchukuliwa kwa umakini na viongozi na wafuasi wa chama cha Democratic ambao wana kiu kubwa ya kumuondoa Donald Trump mwaka 2020.

Hivyo mpambano wa wawili hawa maarufu kupitia runinga pia utavutiwa na watazamaji wengi wa runinga kwani majina yao yalipata umaarufu mkubwa kutokana na ushawishi wao mkubwa kupitia runinga.

Trump alizipokea habari za awali za Oprah kupendekezwa kuwania urais kwa kawaida yake ya kejeli huku akikumbushia kwamba mwanamama huyo alikuwa katika “ukoo wa Trump” si muda mrefu uliopita na kwamba atamshinda vibaya sana.

Akijibu mapigo, Oprah, kupitia wapambe wake katika runinga na kwingineko, alionyesha hamu yake iliyokuwa inajengeka ya kuwa rais wa Marekani ingawa huko nyuma alisikika kuwa na hamu ya kubwa ya kuwa mkuu wa kampuni kubwa ya runinga, na siyo kuwa mkuu wa nchi.

Kuhusu hela Oprah anazo, pia ana kipaji cha kujieleza kwa ufasaha, na historia ya kuibuka kwake kutoka umasikini wa kupindukia hadi utajiri mkubwa inafahamika na Wamarekani wengi. Waliomtangulia – Bill Clinton na Barack Obama walisaidiwa na hali kama hiyo hiyo hadi kutinga Ikulu.

Hata hivyo pamoja na umaarufu wake mkubwa wa runinga kitu kimoja ambacho Oprah hana ni ufahamu na uzoefu katika masuala ya utawala, kitu ambacho ni muhimu kuwa rais wa nchi. Aidha wadadisi wa mambo wanasema umuhimu wa kuwa na sifa hizo kunatiwa nguvu katika enzi hizi hatari za urais wa Trump.

Katika kampeni zake bila shaka Oprah atajiweka katika nafasi ya kumshambulia Trump huku akijitangaza yeye mwenyewe kuwa ni mtu mpole, mpenda watu, mkarimu, sifa ambazo amekuwa akizivuna kutokana na maonyesho yake kupitia runinga hadi kufikia medani ya siasa.

Na kama mcheza sinema nyota maarufu na aliyebobea, Oprah atatumia sifa hiyo ya kujionyesha kama “Rais” kila pale hali itakapohitajika.

Hivyo kwa tafsiri yoyote ile Oprah atakuwa mgombea wa nguvu na kuzoa ushawishi mkubwa nchini kote na pia kutoka kwa mashabiki wake wakubwa, Barack Obama na mkewe Michelle.