Home Makala PHILIP EMEAGWALI: BINGWA WA KOMPYUTA ALIYEIPA KASI INTANETI

PHILIP EMEAGWALI: BINGWA WA KOMPYUTA ALIYEIPA KASI INTANETI

1585
0
SHARE

NA KIZITO MPANGALA

SOTE tunafurahia kutumia mtandao wa kimataifa “International Network” ambapo kwa utaalamu zaidi wa lugha maneno hayo mawili yamefupishwa kwa kuchukua herufi tano za mwanzo za neno’ INTERnet’ na herufi mbili za mwanzo za neno ‘NETwork’ na kupata neno ‘INTERNET’ yaani mtandao. Kwa Kiswahili tuseme Intaneti.

Leo tunaye Mnigeria Philip Emeagwali ambaye amechangia katika maendeleo ya nguvu na kasi ya intaneti. Yeye si mvumbuzi wa intaneti lakini kwa kifaa alichokibuni kimesaidia kuboresha na kuipa nguvu na kasi zaidi intaneti tunayofurahia sasa hivi ambapo tunaweza kuwasiliana.

Philip Emeagwali alizaliwa mwaka 1954 katika mji wa Akure nchini Nigeria katika jamii ya kabila la Igbo. Mwaka 1967 aliacha shule kutokana na vita vya Biafra  na alishiriki vita hivyo kama askari kwa lazima alipokuwa na umri wa miaka 14. Vita vilipomalizika alihitimu masomo ya sekondari kwa kufundishwa nyumbani na baba yake. Shule nyingi zilifungwa. Baba yake huyo alikosa fedha za kumlipia ada hivyo akaingia vitani Biafra.

Wakati alipokuwa akifundishwa nyumbani na baba yake, alifundishishwa hisabati na kupewa maswali 100 kila siku na aliambiwa awe anayafanya kwa muda wa saa moja tu awe amemaliza! Hakika aliweza jambo hilo! Katika zoezi hilo maana yake ni kwamba alikuwa anafanya kila swali kwa wastani wa sekunde 36 tu!

Philip anatushirikisha kumbukumbu ya maisha ya familia yake baada ya mapigano ya vita vya Biafra, ansema “tulikuwa tukiishi kama watumwa. Chakula tulikuwa mara moja tu kwa siku na wakati mwingine siku ilipita bila kupata chakula. Nilijitahidi kuwa na fikra ya kufanikiwa kimaisha ndio maana nilijijengea bidii”

Alikuwa akiishi kwenye nyumba ambayo ni banda tu lililozungushiwa mabaki ya roketi zilizolipuliwa vitani. Alikuwa akijisomea kuanzia saa 6 mchana hadi usiku saa 4. Ndipo alipofaulu mtihani wa kujinga na chuo kikuu cha Oregon nchini Uingereza kwa udhamini. Alidhaminiwa kutokana na nia yake thabiti ya kupenda kujisomea vitabu na kujifunza zaidi.

Alijiunga na chuo kikuu cha Oregon nchini Uingereza ambako alitunukiwa shahada ya kwanza ya Hisabati. Baada ya kumaliza masomo na kutunukiwa shahada ya kwanza ya hisabati nchini Uingereza. Baadaye alitunukiwa shahada ya uzamili katika chuo kikuu cha George Washington katika uhandisi wa ubaharia na mazingira (Ocean & Marine Engineering and Ecology). Pia alitunukiwa shahada ya pili tena ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Maryland katika Hisabati Tumizi (Applied Mathematics). Aliajiriwa na mamlaka ya ardhi mjini Wyoming kama mhandisi.

Emeagwali alitunukiwa shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani katika masomo ya Sayansi ya kompyuta. Baadaye chuo hicho kilificha taarifa zake kutokana na rangi yake nyeusi, maana yake ni kwamba lilikuwa ni jambo la kibaguzi. Alifungua kesi mahakamani kuhusiana na hujuma hiyo ya kufichwa taafifa zake kwamba isijulikane kama alisoma hapo lakini kesi yake ilifutiliwa mbali kwa vigezo vileveile vya kibaguzi.

Kwa elimu yake ya mazingira alifanya uchunguzi wa kina jinsi nyuki wanavyotengeneza asali kwa haraka na ufanisi. Baada ya kumaliza uchunguzi wake huo kwa siku nyingi alichapisha matokeo yake ambayo aliyaongezea nguvu kwa elimu ya sayansi ya kompyuta. Lengo lake lilikuwa ni kuunda kompyuta yenye kasi zaidi. Alifanikisha jambo hilo ambapo alitumia vifaa vidogo vidogo 65,000 vya kielektroniki kuunda kompyuta hiyo ambayo ndiyo yenye uweza wa kasi kubwa duniani. Yeye ndiye mbunifu wa kwanza Kompyuta kubwa (Supercomputer) yenye uwezo wa kukokotoa toni bilioni 3.1 kwa sekunde moja.

Philip ndiye aliyebuni kanuni inayoruhusu kompyuta nyingi kufanya kazi kwa wakati mmoja zinapotumia intaneti. Alifanikisha pia kuunganisha kompyuta 8 kubwa na kupata kile tunachoita Kompyuta mahsusi (Super computer). Hii alifanikisha katika maabara ya sayansi ya kompyuta jijini Los Alamos ambapo wanasayansi waliomtangulia walikata yamaa kutokana na ukweli kwamba kompyuta walizokuwa wakitumia hazikuwa na kasi sana kwa kuwa walitaka kuunda kompyuta itakayoweza kulisisimua bomu la nyuklia lilipuke haraka endapo mitambo itasetiwa mbali na bomu lilipo.

Uvumbuzi huo ulimfanya apate tuzo ya nishani ya taasisi ya elimu ya elektroniki ya Gordon Bell mwaka 1989. Anakiri kwamba familia yake ilikuwa masikini wa kutupwa duniani kati ya familia masikini zilizokuwepo duniani. Philip ndiye mwanzilishi na mboreshaji wa sekta ya mafuta nchini Marekani, ushauri wake wa kitaalamu kwa sayansi ya kompyuta ulifanyiwa majaribio na kuona ya kwamba unafaa na mpaka sasa ndio unatumika na unaiingizia serikali ya Marekani mabilioni ya dola.

Milinganyo ambayo aliiasisi kutokana na kipawa chake cha hisabati na ambayo inatumika katika mashine za kuchimba mafuta inapofanyiwa kazi huweza kukupa mwelekeo wa kiasi cha mafuta unachoweza kuchimba na kama unaweza kuongeza uzalishaji au kama uzalishaji unaweza kupungua basi milinganyo hii inakupatia majibu.

Philip anasifika kuwa gwiji wa hisabati na mwenye bidii ya kujifunza bila kukata tamaa. Mara nyingi yeye hakupenda kuitwa hivyo kwani aliamini gwiji ni baba yake aliyeuhamishia kwake. Philip anasema “wakati fulani silipendi jina hilo, yaani sipendi kuitwa gwiji kwa sababu watu wengi hudhani ugwiji upo kwenye hisbati tu, si kweli. Sidhani kama kila mmoja kati yetu wenye nguvu ya kujipa ugwiji yeye mweyewe, mimi sikuzaliwa nikiwa gwiji na sikufahamu kama itakuwa hivyo. Ugwiji ulipandwa na baba yangu ndani yangu, hivyo, baba yangu ndiye gwiji. Watu huniita mimi gwiji wa hisabati, lakini nawaambia kuwa yeyote anaweza kuwa gwiji kama akikokotoa maswali 100 kwa muda wa saa moja”. alisema akiwa katika mkutanao wa wazazi nchini Nigeria mwaka 1999.

Philip aliwasisitiza wazazi katika mkutano huo kuwa mtoto akipewa kazi kutoka shuleni akaifanya nyumbani waichukulie kwa uzito kwa kuwa kazi za nyumbani zina umuhimu kwa mwanafunzi yeyote duniani. Philip kwa sasa ana uraia wa Marekani na ana taasisi yake inayoshughulikia masuala ya mawasilianao. Mpaka sasa ametunukiwa tunzo zaidi ya 80.

0692 555 874, 0743 369 108