Home Latest News Rais ! eti Makonda naye RC

Rais ! eti Makonda naye RC

52648
0
SHARE

RAI-MCHOCHEZIKAMA kuna jambo limenishangaza na kujiuliza maswali mepesi yenye majibu magumu ni uamuzi wa Rais John Magufuli, kumteua kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Kwangu napenda kuweka wazi kwamba sina tatizo kabisa wala ugomvi na mkuu huyo mpya wa Mkoa wa Dar es Salaam wala chama chake CCM.

Nampongeza Makonda kwa kupata bahati hiyo ya mtende ambayo hakutarajia kuipata kirahisi kiasi hicho kilichokamilisha msemo maarufu wa kiswahili unaosema “unalala masikini unaamka tajiri”.

Tatizo kwangu lipo kwa taasisi iliyomteua ya urais, ambayo imetafakari kwa kina na kujiridhisha pasi na shaka kwamba, Makonda ndiye alama ya uchapakazi wa kupigiwa mfano kwa makada wa chama hicho.

Kuna maswali mepesi ninayojiuliza ni je? Dk. Magufuli alitumia vigezo gani, kumteua Makonda mtu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam?

Swali jingine ameteuliwa kwa sababu ile iliyowahi kuandikwa na vyombo vya habari kwamba alijitoa kuvuruga mkutano wa kukataa Katiba Pendekezwa uliokuwa umeandaliwa na Taasisi ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere?

Je, ni kwa sababu ile iliyowahi kuripotiwa kwamba alihusika kuratibu na kumfanyia vurugu aliyekuwa mtoa mada mkuu wa siku hiyo, Jaji mstaafu Joseph Warioba?

Sababu hiyo ya vurugu kwa Warioba ambayo iliwahi kuelezewa kuwa sababu ya kupewa ukuu wa wilaya na serikali iliyopita inaweza ikawa ndiyo imembeba?

Ni kwa sababu ya kujitokeza akipita sehemu mbalimbali na miswada mbalimbali ya kuomba fedha za kuwezesha kusimamia mashindano ya vijana wenye vipaji katika wilaya ya Kinondoni?

Ama ni kwa sababu ya kuibuka mara kadhaa kuzungumzia mipango inayopangwa kufanywa na Manispaa ya Kinondoni kabla ya kupitishwa katika vikao kwa kutaka kujionyesha kwamba jitihada hizo ni za CCM.

Je, ni kwa sababu ya kujaribu kuwakatisha tamaa viongozi wa vyama vya upinzani kwa mara kadhaa kuingilia majukumu yao ya kila siku?

Je, alidhani kuibuka kwa Meya wa Kinondoni, Boniface Jackob kumlalamikia kuingilia majukumu ya Kinondoni kinyume cha taratibu inawezekana alimtafsiri kuwa mwiba wa wapinzani?

Je, alichanganywa na ujanjaujanja wa Makonda wa kutumia vyombo vya habari kwa kutoa matamko ya kuwasimamisha kazi wafanyakazi ambao kisheria hana mamlaka juu yao?

Je? alifanya hivyo kutokana na kutoa ahadi nyingi ambazo hakuwa na uwezo wa kutimiza kwa mfano ujenzi wa machinjio ya kisasa Kinondoni ambayo hadi sasa imeota mbawa?

Je, ni kwa sababu ya kutumia polisi kama Mwenyekiti wa Ulinzi na usalama wa Wilaya ya Kinondoni kumzuia Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea kuhutubia wafanyakazi wa Kiwanda cha Took Tanzania kilichopo EPZ waliokuwa wamemuita kuwatafutia ufumbuzi wa madai ya nyongeza ya mshahara?.

Je, ni kwa sababu ya kuwaahidi walimu wa Dar es salaam kupanda mabasi bure ahadi ambayo ilishindwa kutekelezeka na kupita kama upepo?

Swali jingine ni kuwa je, Dk. Magufuli alishawishika na ahadi za Makonda zisizotekelezeka za kuahidi kuhakikisha anamalizia jengo la hospitali ya Palestina ambalo hadi leo halijajengwa?

Inawezekana Dk. Magufuli atakuwa alifurahishwa na ahadi ya Makonda aliyotoa katika Hospitali ya Mwananyamala ya kuwepo kwa askari polisi watakaokuwa na kazi ya kutoa Huduma ya Karatasi namba Tatu (PF3) ya jeshi la polisi?

Inawezekana rais Magufuli alifurahishwa na ujasiri wa Makonda wa kutoa ahadi anazojua hawezi kuzitekeleza bila kujali kama hiyo ya askari kuwekwa katika hospitali kutoa PF3 ili wagonjwa wenye uhitaji waweze kuipatia hospitali?

Tangu ameteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete sijawahi kuona jambo la kimaendeleo aliloahidi Makonda limefanyiwa kazi na wananchi wakafaidika nalo.

Jambo ninalokumbuka alilosema na kulisimamia hadi mwisho ni shindano la kusaka vijana wenye vipaji wa Kinondoni ambao walikuwa wakishindanishwa.

Kama Rais Magufuli atakuwa ameingia mkenge kwamba atawabana wapinzani kuchukua mkoa atakuwa ameteleza katika hilo.

Hapa nikiweka rekodi sawa akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ukawa imefanikiwa kutwaa Manispaa hiyo.

Akiwa Mkuu wa Wilaya wa Kinondoni, Ukawa wamefanikiwa kutwaa majimbo manne na hakuna alichoisaidia CCM.

Hali hiyo inaonyesha dhahiri ni kwa namna gani wapinzani wanavyomshinda nguvu na ujanja kada huyu mwaminifu wa CCM.

Kwa uteuzi wake wa ukuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni furaha kwa Ukawa kupata meya kirahisi kutokana na kuwekewa mtu ambaye wanajua mbinu za kumshinda asubuhi kabla hata jogoo hajawika.