Home Makala RAIS, JAJI MKUU WATOFAUTIANA

RAIS, JAJI MKUU WATOFAUTIANA

1179
0
SHARE

NAIROBI, KENYA


ZIKIWA zimesalia wiki chache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu nchini Kenya, kumekuwa na tofauti za wazi kati ya  Rais Uhuru Kenyatta na Jaji Mkuu wa nchi hiyo David Maraga.

Tayari Maraga amemuonya Rais Uhuru Kenyatta kutowalazimisha wananchi kukosa imani na Mahakama.

Kauli hiyo ya Jaji Mkuu inatajwa kuwa ya kwanza kutolewa dhidi ya Rais, wadadisi wa mambo wanasema kauli kama hiyo haijapata kutolewa hadharani.

Maraga alitoa kauli hiyo akimjibu Rais Kenyatta baada ya kuituhumu mahakama baada ya upinzani kushinda katika Mahakama Kuu ya nchi hiyo dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo.

Rais Kenyatta alitoa kauli ya kutahadharisha kutumika kwa Mahakama katika kuchelewesha uchaguzi unatorajiwa kufanyika Agosti 8 mwaka huu.

Akihutubia mkutano wa kampeni katika kaunti ya Baringo Magharibi mwa Kenya Jumapili iliyopita, Kenyatta alisema mahakama ilikuwa inawachukulia wao kama wapumbavu.

“Nataka kuwaambia walio mahakamani tumewaheshimu sana, lakini msifikiri heshima hii inatokana na uoga. Hatuwezi kuruhusu wapinzani wetu kutumia mahakama kuiyumbisha IEBC, wakidhani watashinda kwa kutumia mlango wa nyuma.”

Saa chache baada ya kauli hiyo Jaji Mkuu alitoa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotoa tahadhari kwa viongozi wa kisiasa.

“Viongozi wa siasa wanapotoa kauli za kushambulia utawala wa sheria kwa kutoa tafsiri potofu kuhusu uamuzi wa mahakama, kunaweza kuathiri imani ya wananchi kwa mahakama zetu na hili linanihusu mimi binafsi kwa kiwango kikubwa.”

Upinzani, chini ya umoja wa NASA ulifungua kesi dhidi ya IEBC, pamoja na hii iliyoibua majibizano, ambapo Ijumaa iliyopita Mahakama Kuu iliamua kusitisha zabuni ya kuchapisha karatasi za kupigia kura za urais kwa hoja kuwa  haikuwa na uwazi.

Mahakama ilitoa uamuzi wa kusitisha uchapishaji wa karatasi hizo uliokuwa ukifanywa na kampuni ya Dubai ya Al-Ghurair ambayo inadaiwa kuwa na mahusiano ya karibu na Rais Uhuru Kenyatta.

Awali Mahakama Kuu ilisema matokeo ya uchaguzi yatakayotangazwa majimboni ndiyo ya mwisho na hayawezi kamwe kubadilishwa na chombo chochote isipokuwa tu baada ya kusikilizwa mahakamani.

Hata hivyo, Kenyatta na viongozi wengine wa chama chake cha Jubilee waliendeleza mashambulizi yao dhidi ya Mahakama.

Hatua hiyo ya kuikosoa Mahakama imekuwa ikipingwa na makundi mbalimbali nchini humo.

Miongoni mwa wanaowapinga ni kiongozi wa chama Kikuu cha Wafanyakazi (Central Organisation of Trade Unions -Cotu) Francis Atwoli na Mwenyekiti wa chama cha Wanasheria ( Law Society of Kenya -LSK) Isaac Okero ambaye alisema kauli ya Kenyatta ilikuwa ni ‘tusi’ na ina lengo la kuyumbisha uhuru wa Mahakama.”

Jubilee waliendelea kushikilia madai yao kwamba NASA walikuwa wanawatumia baadhi ya Majaji kuharibu mchakato wa uchaguzi ili usifanyike.

Mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, Kiongozi wake Bungeni Aden Duale, kiongozi mwenza katika Senate Prof Kithure Kindiki na Seneta Kipchumba Murkomen waliunga mkono kauli ya Uhuru Kenyatta.

Wote walidai kuwa Majaji walikuwa wanaipendelea NASA.

Aden Duale alisema Jubilee watakata rufaa ya kutaka kesi hiyo isikilizwe na jopo la majaji watano, katika suala la uchapishaji wa karatasi za kura – hasa katika tafsiri ya ushirikishwaji umma katika upatikanaji wa mzabuni wa kuchapisha makaratsi ya kura za urais.

Prof Kindiki alidai baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu waliosikiliza kesi dhidi ya IEBC walikuwa na mgongano wa kimasilahi. Hata hivyo hakufafanua.