Home Makala RAIS MAGUFULI KUZUIA MAKINIKIA SIYO TIBA, NCHI INAUMWA

RAIS MAGUFULI KUZUIA MAKINIKIA SIYO TIBA, NCHI INAUMWA

1936
0
SHARE

NA LUQMAN MALOTO


Tupo kwenye kipindi cha joto la makinikia, ule mchanga wenye madini ambao husafirishwa na wawekezaji wa sekta ya madini kwenda kuuchenjua nje ya nchi.

Rais John Magufuli alichungulia na kuona nchi inaibiwa, kwa hiyo alizuia makontena ya makinikia yasisafirishwe kisha akaunda Kamati Maalumu ya Wataalamu, iliyochunguza.

Majibu ya Kamati hiyo ndiyo yameongeza mshtuko. Nchi imekuwa ikipoteza matrilioni ya fedha kwa udanganyifu wa wawekezaji, kwamba hutaja kiasi kidogo cha madini ambayo huyapata kuliko hali halisi.

Ripoti ya Kamati Maalumu ya Rais imeshitua Watanzania kwa wingi wao. Hakuna Mtanzania wa kweli ambaye anaweza kufurahia kuona nchi yake inaibiwa. Wanaumizwa.

Hapa sasa ni lazima kuukiri ukweli, hakuna adui wa Watanzania isipokuwa Watanzania wenyewe. Wanaoaminiwa na kupewa dhamana ndiyo ambao wamekuwa msaada kwa wawekezaji kuiibia nchi.

Katika kuwasaidia wawekezaji, Watanzania husaini mikataba kama vipofu na kupitisha masharti ambayo huiumiza sana nchi. Hili ndilo janga la Tanzania. Huu ndiyo hasa ugonjwa ambao nchi inaumwa.

Tatizo kubwa zaidi ni kuwa mikataba hiyo Serikali inapoamua kushughulika nayo kwa jazba, huambulia pigo kubwa. Mkataba wa Richmond wa kuzalisha umeme wa dharua megawati 105 kati ya Tanesco na Kampuni ya Kimarekani ya Richmond Development LLC, ulikuwa wa hovyo kupita kiasi.

Pamoja na uhovyo wake, Richmond iliposhindwa kutekeleza masharti ya mkataba, iliamua kuuhamishia majukumu yake kwa Kampuni ya Dowans Holdings S.A katika mazingira ya hovyo lakini yaliyowezeshwa na Watanzania, kipindi ambacho nchi ilikuwa haihitaji tena umeme wa dharura kwa sababu ilikuwa inaweza kuzalisha kupitia vyanzo vyake.

Bunge lilipoamua kufanya uchunguzi na kubaini madudu yote, lilitoka shinikizo kubwa lililosababisha uamuzi wa jazba uchukuliwe kwa kuuvunja Mkataba wa Richmond, wakati Dowans wakiwa kazini. Matokeo ya jazba hizo yakawa Serikali ya Tanzania kuilipa Dowans takribani Sh100 bilioni baada ya kushindwa kesi mahakamani.

Somo la Richmond na Dowans, linatosha kuwasha taa nyekundu wakati huu wa sakata la makanikia. Nchi inaumwa ugonjwa hatari sana, ugonjwa wa usaliti kutokana na baadhi ya Watanzania kukosa uzalendo. Bila kuushughulikia huo ugonjwa, makanikia yatawaumiza Watanzania, maana wao ndiyo walipa gharama na fidia.

 

UGONJWA WENYEWE

Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaumwa. Linasumbuliwa na ugonjwa mbaya. Gonjwa la utovu wa uzalendo kwa nchi.

Nchi inakosa wazalendo. Wasom wanapewa nafasi nyeti ambazo badala ya kuzitumia ipasavyo kuiendeleza nchi, wao wanazigeuza fursa za kutajirika.

Mtumishi wa umma kumiliki nyumba 74! Hii inatisha mno. Kipato chake hakifanani kabisa na mali anazomiliki. Shida ni moja tu. Kukosekana kwa uzalendo.

Kuna watumishi wa umma siyo Watanzania. Ni Watanzania kwa kujitambulisha tu. Mtanzania wa moyoni hawezi kuihujumu nchi yake. Kujinufaisha mwenyewe na ndugu zake wanaangamia.

Yote yanasababishwa na mfumo wa elimu. Wanafunzi hawafundishwi uzalendo kwa nchi yao. Wanafundishwa kujitajirisha bila nyenzo za kimsingi.

Waliopo shuleni wanajionea jinsi vigogo wanaishi nje ya vipato vyao. Wanasoma kwa tabu, huku wengine wakichezea fedha. Tanzania haina ulinganifu kati ya mwananchi wa kawaida na wale wenye meno serikalini.

Mfumo wa elimu ya Tanzania unazalisha watu wabinafsi. Kila anayepata fursa anawaza jinsi ya kuvuna kwa namna yake. Watu wanaonekana wapo kwenye nafasi za heshima kumbe wenyewe hawajiheshimu.

Ni kwamba siku haziendi tu, kiu yangu nione kile ambacho kitawapata viongozi wapigaji, waliodiriki kuhujumu nchi mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 80 bandarini. Watanzania wa hali ya nchini wanateseka, kumbe wasomi wa nchi wanahujumu.

Tunahitaji kuona hukumu ya wahuni wanaovaa suti, wenye ratiba nzuri ya kula, kulala na kuamka, wamekwenda shule vizuri, ni akina baba wazuri wa familia, ila ni majambazi kuliko watumiao bunduki.

Wasio na huruma na nchi! Wengi wamesomeshwa kwa kodi za walalahoi, wakapewa ‘michongo’ ya kwenda kusoma mpaka vyuo vikuu vya nje, wamerudi na kupata kazi, badala ya kutumia elimu yao kizalendo kuwasaidia Watanzania wenzao kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, wanaamua kuiba.

Ni wasaliti wapanga mipango isiyotekelezeka. Miradi mingi haitekelezwi mpaka fedha za wahisani. Shule zetu hali mbaya, vijijini madarasa ni majanga, kote mpaka mijini hakuna vifaa vya kufundishia, maabara ni tatizo la miaka yote 54 ya uhuru. Hospitali hazina dawa, wagonjwa wanalazwa chini, halafu watu wanachota mabilioni.

Wanahusika uporaji wa mabilioni ya shilingi halafu hawataki wasemwe. Wengine mwaka 2014 walipoambiwa ukweli, wakachukia, wakaamua kutukana wabunge waibua hoja, mara “tumbili”, wakawaita “wabunge washenzi”, nao walipojibiwa ni wezi, ‘wakapaniki’, wakaropoka “I shall cut your neck.”

Desemba 2015 tulitikiswa na utoroshwaji wa makontena bandarini, mwaka 2014 tulikuwa na wizi Tegeta Escrow. Hoja ya kwanza tuliambiwa zaidi ya shilingi bilioni 200 zilitafunwa. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), ikasema zaidi ya shilingi bilioni 300 zililiwa.

Baadaye tukaona kila dalili kwamba fedha zote, zaidi ya shilingi bilioni 400 katika akaunti ya Tegeta Escrow zilibebwa kihuni. Huu ni ufisadi mkubwa kuwahi kutokea nchini.

Zipo taarifa kuwa PAP, ile kampuni ya ‘Singasinga’ (kama anavyoitwa na David Kafulila), ikiwa na mtaji wake wa shilingi milioni 500, ilijitwalia zaidi ya shilingi bilioni 270. Kwa namna ilivyo, ni mpango wa wavaa suti waliokwenda shule na kubeba dhamana katika nchi, kupora fedha kihuni.

Kabla hata CAG hajakamilisha uchunguzi wake, binafsi nilikuwa naamini kwa asilimia zote kuwa wahuni wameshafanya yao. Shaka ilikuwa kubwa sana kutokana na mazingira halisi ya utoaji wa fedha hizo. PAP shaka! VIP majanga! Haraka ya kulipa fedha za IPTL ilitokea wapi? Mpango wa wasomi waliokosa uzalendo.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyejiuzulu, Fredrick Werema, wao walikuwa wanawatumikia akina nani mpaka waone sawa fedha za Escrow zilipwe haraka wakati Tanesco ya Watanzania ndiyo walalamikaji wa kukamuliwa tozo kubwa kuliko kiwango halisi?

Hata hivyo, sakata zima la Escrow na jinsi ambavyo lilifanyiwa majaribio ya kuzimwa, linanikumbusha mchezo mchafu wa Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na wabunge kadhaa wahuni, walivyozima hoja ya ukiukwaji wa sheria ya manunuzi wakati wa kununua mafuta mazito kwa ajili ya mitambo ya umeme. Nitaeleza!

 

KWANZA ESCROW NI NINI?

Escrow ni neno lililotoholewa kutoka kwenye kamusi ya kizamani ya Kifaransa. Neno halisi ni “escroue” likiwa na tafsiri yenye kuelekeza upande wa tatu unaoshikilia amana ya watu wanaolumbana mpaka pale ufumbuzi wa kisheria unapopatikana na kukubalika nani apate stahili ipi.

Tafsiri ni ileile; Escrow ni fedha katika akaunti ya tatu kwa niaba ya pande mbili zinazosuguana katika malipo. A anatakiwa kulipwa fedha zake na B, lakini A na B wanaingia kwenye mgogoro, kwa hiyo C anafungua akaunti ya Escrow na fedha zote zinawekwa humo kusubiri mwafaka wa A na B.

Vivyo hivyo, Tanesco ilifungua kesi kulalamika chaji kubwa iliyokuwa inatozwa na IPTL. Kwa kifupi ni kwamba Tanesco ilifungua madai kwamba IPTL ilikuwa inaipiga, kwa kuitoza gharama kubwa kinyume na kiwago halisi kinachotakiwa.

Tanesco mlipaji, IPTL mlipwaji, kukawa kuna utata, mwamala hauwezi kufanyika moja kwa moja, kwa hiyo Benki Kuu iliagizwa kufungua akaunti ya Escrow, ili fedha zote zinazolipwa na Tanesco zihifadhiwe humo mpaka pale kesi ya msingi itakapokamilika na hukumu kutolewa.

Waliokuwa wanalipa fedha ni Tanesco ambazo zinatokana na viwango wanavyotozwa Watanzania. Halafu mtu anathubutu kusema zile fedha hazikuwa za umma, ni za IPTL. Hao IPTL walikuwa wanapata fedha wapi? Na kwa nini zikae Benki Kuu ya Tanzania?

Tanesco waliendelea kulipa mpaka zikafikia zaidi ya shilingi bilioni 400 (dola milioni 270 kwa sarafu ya mwaka 2014). Fedha zipo Benki Kuu. Watu wakaona zimekaa tu, ikabidi waanze mchakato wa kuzipiga kama vile ilivyotokea katika Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Ikaibuka PAP eti ikauziwa hisa za Kampuni ya Menchmar iliyokuwa inamiliki asilimia 70 za IPTL, na kwa mtaji wake wa shilingi milioni 500, PAP ikatengenezewa mazingira kisha ikapiga bilioni 270 (Singasinga hakula peke yake, anaweza kutaja aliokula nao). VIP nayo ikajitwalia mabilioni yaliyosalia. Tanzania yenye neema tele!

Niulize tena, Maswi na Werema, waliharakisha malipo ya nini na kwa faida ya nani ikiwa hakukuwa na hukumu inayosema Tanesco imeshindwa kesi? Maana kama ingeshinda, ingebidi fedha zirudi na fidia. Tanesco ilifungua kesi kwa ajili ya kurudisha unafuu wa maisha kwa Watanzania, sasa hao Maswi na Werema ni wana wa taifa gani?

KUSEMA NA KUUMBUANA BUNGENI HAISAIDII

Kusema sana na kuumbuana bungeni haisaidii. Tatizo kubwa la nchi yetu ni mfumo uliokosa maadili ya utumishi. Taifa limejaza viongozi na watendaji wabinafsi ambao kwao maisha yao binafsi yana maana kubwa kuliko maendeleo ya nchi.

Janga kubwa linaanzia Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (PCCB). Hii ni taasisi nyeti sana lakini sheria za nchi na mtindo wake wa kufanya kazi, haupambani na watoa rushwa, bali unasaidia maofisa wa Takukuru nao kula kwa urefu wa kamba zao.

Takukuru inavyofanya kazi hivi sasa, inawalinda watoa rushwa na kuwakamata wasiowapa rushwa. Kwa sura hiyo, unadhani kigogo gani atakamatwa? Kigogo gani mla rushwa atakosa uwezo wa kuhonga maofisa wa Takukuru wanapomzonga kumkamata?

Takukuru ipo mitaani ikishughulikia rushwa ndogondogo, haijikiti kwenye mitandao ya taasisi binafsi zinazofanya kazi na serikali ili kushughulikia rushwa kubwakubwa. Maana huko ndiko kwenye upigwaji wa mabilioni mamia kwa mamia.

Kati ya taasisi binafsi na serikali, ndipo kwenye biashara ya kuuziana tenda, malipo kuongezwa cha juu ili kiwe kinanufaisha watendaji wa serikali walioidhinisha biashara kufanyika kati ya serikali na kampuni fulani binafsi. Tuachane na rushwa za trafiki, shilingi 10,000, Takukuru ijikite kwenye rushwa kubwa ili kuokoa nchi.

Nilitamani kuona Escrow inakuwa kashfa ya mwisho ya wizi wa fedha za Watanzania. Nikitumai ya kwamba baada ya skendo hiyo, tungeona muundo mpya wa njia za kudhibiti rushwa nchini na wala rushwa pamoja na wapokeaji, wanapewa kibano cha maana ili wakome pia iwe fundisho kwa wapigaji wengine.

Escrow iliisha kama Richmond. Serikali ilipata hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa kitendo chake cha kuipa tenda kimagumashi Kampuni ya Richmond. Mpaka leo, tangu mwaka 2008, ukiachana na adhabu ya kuumbuana bungeni na kukoseshana tonge (kulazimishana kujiuzulu), hakuna hatua kali zilizochukuliwa.

 

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu (AG), Johnson Mwanyika yupo zake anaendelea na maisha, licha ya kuhusika na hasara hiyo. Kwa nafasi yake, aliwajibika kuishauri serikali isiingie mkataba na Richmond lakini hakufanya hivyo. Angepelekwa kortini, tungejua kama alihongwa au vipi.

Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, mawaziri wa Nishati na Madini waliopokezana ofisi, Nazir Karamagi na Ibrahim Msahaba (alikuwa Wizara ya Afrika Mashariki wakati anaumbuliwa), baada ya kudhalilishwa bungeni, hakuna hatua yoyote iliyofuata.

Huu ni mwaka wa tisa na miezi mitatu (tangu Februari 2008), Richmond iliponyamazishwa kwa staili ya kufunika kombe mwanaharamu apite. EPA tunakumbuka ilivyokuwa moto, wezi waliambiwa warudishe fedha zaidi ya shilingi bilioni 130 walizoiba kisha wakasamehewa, walioshindwa kulipa (wale dagaa), walitolewa kafara.

Ni zaidi ya aibu kama yaleyale ya Richmond na EPA, yalijirudia kwenye Escrow. Tunahitaji kuona mabadiliko ya hatua za kinidhamu kwa watendaji waovu. Familia zao zitaumia ila si vibaya zikionja matokeo ya kuwa na akina baba wasio na maadili, wenye hulka ya kuifilisi nchi.

 

KUNA WABUNGE WASOMI WAHUNI

Wakati wa Bunge la Bajeti mwaka 2014 ndipo hoja ya Escrow ilipoibuliwa. Wabunge walioanzisha hoja, Kafulila, Christopher Ole Sendeka na Zitto Kabwe (aliyechangia kwa maandishi), walisemwa kuwa wanatumika na kwamba wamehongwa ili kudhoofisha jitihada njema zinazofanywa na Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo pamoja na Maswi.

Wapo wabunge walisimama na kuwasuta wenzao waziwazi. Hawakutaka kabisa Muhongo na Maswi wasemwe. Eti wabunge hao wanatumiwa na wakili tajiri, Nimrod Mkono pamoja na mfanyabiashara, Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi.

Nilimshuhudia Muhongo akimtusi Ole Sendeka (eti hakuwa na akili darasani), kisha akamwambia John Mnyika ni sifuri. Kundi kubwa la wabunge, wakiwemo wa upinzani, walishangilia matusi ambayo Muhongo aliyatoa.

Kwenye korido, baadhi ya wabunge walikuwa imara kupakaza; “wale jamaa wamelipwa kukwamisha bajeti ya Nishati na Madini lazima tuwashughulikie.” Huu ndiyo uhuni wa baadhi ya wabunge wetu. Ni rahisi kurubuniwa kwa uongo kisha kuwasaliti wenzao wanaoanzisha hoja zenye maslahi kwa taifa.

Kuna katabia haka bungeni; wabunge wakiambiwa wenzao wamekula mlungula, wanakuwa na hasira kali kuwashughulikia bila hata hoja wala ushahidi. Si kwamba kwa vile hawapendi rushwa, bali kwa kijicho “kwa nini wale peke yao?”

Mwaka 2012, mtikisiko mkubwa ulitokea pale Zitto Kabwe alipoomba idhini ya Spika wa Bunge, Anne Makinda ili kamati yake ya Hesabu za Mashirika ya Umaa (siku hizi haipo) ichunguze mgogoro wa Tanesco, kati ya bodi na mkurugenzi aliyefukuzwa, William Mhando, kwa vile ilitajwa skendo ya ukiukwaji wa sheria ya manunuzi wakati wa kununua mafuta mazito (ghafi).

 

Zitto akaunganishwa na wabunge wengine, Sara Msafiri, Christopher Ole Sendeka, Munde Tambwe na wengine wote waliokuwa wanaunda Kamati ya Bunge Nishati na Madini, kwamba walihongwa kila mmoja shilingi milioni 10 kukwamisha bajeti.

Bungeni palinuka, Zitto (kutokana na umaarufu wake), akaona yeye ndiye mlengwa hasa. Dodoma hapakukalika na Dar hapakumfaa. Siku bajeti inapitishwa, wabunge tajwa wote hao hawakuwepo bungeni kwa aibu. Walivaa sura mbaya, wenzao waliwasakama.

Makinda kwa hatua ya haraka, aliivunja Kamati ya Nishati na Madini, vilevile akaunda kamati teule iliyoongozwa na Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi ambayo ilibaini kuwa ile kashfa kwa akina Zitto na wenzake, ilikuwa janja ya nyani ya Maswi na Muhongo kuficha madudu yao.

Kamati ilibaini kuwa bodi ya Tanesco ilikiuka sheria ya manunuzi kwa kumpa tenda mzabuni aliyeshindwa. Upo ufisadi na mambo ya kimapenzi yaliyobainishwa lakini acha tu. Spika akasema, sasa natoa adhabu kali, watu tukatega sikio, kumbe adhabu yenyewe aliyosema ni kali, iliishia kuwapa onyo Maswi na Muhongo kwa kulidanganya bunge.

Onyo halikuwa na mashiko kama hoja stahili ingepewa nafasi yake. Hata hivyo, ilifunikwa kwa staili ya kuwashambulia wabunge waanzisha hoja. Na Escrow ilianza hivyohivyo, akina Maswi walidhani ya 2012 yangejirudia tena, ikashindikana.

Alipokuwa anazindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Amiri Jeshi Mkuu, Mkuu wa Nchi, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Magufuli alisema katika awamu yake atatumbua sana majipu.

Alisema ufisadi nchini ni jipu ambalo halina dawa zaidi ya kulitumbua. Akasema yeye amejipa kazi ya kutumbua majipu. Watanzania wamembariki kwa nafasi hiyo. Nami namwita Mtumbua Majipu Mkuu.

Na kwa hakika ufisadi ni jipu kubwa. Ila ndani ya serikali kuna vijipu uchungu vingi mno. Ni vile vinavyohusu matumizi ya hovyo. Watendaji wanalazimisha fedha nyingi zitumike kwa mipango ya kifisadi.

Jipu uchungu la kwanza ikawa fedha za sherehe ya wabunge. Wapo walionuna lakini mbele ya Dk Magufuli walipiga makofi. Wangefanyaje sasa na Baraza la Mawaziri halijatangazwa? Nani anataka kukosa ulaji? Usoni tabasamu, moyoni mkunjo.

Sherehe ya wabunge shilingi milioni 250, kama zingetumika zote hizo ingekuwa ufisadi mkubwa mno. Kwa vile wabunge wa Ukawa walisusia, maana yake kwa wastani, kila mbunge angetumia shilingi milioni moja. Sherehe ya muda usiozidi saa tatu!

Dk. Magufuli akalitumbua jipu hilo kwa kuagiza fedha za sherehe ziende kununulia vitanda vya wagonjwa Hospitali ya Taifa Muhimbili. Vitanda vilinunuliwa na sherehe ilifanyika. Ufahari wa nini wakati wagonjwa wanalala chini hospitalini?

Jipu uchungu lingine likawa msafara wa kwenda kwenye mkutano wa Jumuiya ya Madola. Alifyeka watu 50 na kuokoa shilingi milioni 700 ambazo zingetumika kwenye posho na tiketi ya ndege.

Lilipotumbuliwa liliwatesa wengi. Watendaji wengi serikalini wamekuwa wakinufaika kwa mgongo huu. Safari nyingi, posho mlima. Tena tiketi za ndege za daraja la vibopa (business class).

Jipu uchungu lingine limekuwa sherehe za Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) Desemba 2015, alibadili uelekeo. Watu wakaitumia siku hiyo kufanya kazi za usafi ili kulikabili janga la ugonjwa wa kipundupindu.

Sh4 bilioni ambazo zingetumika kwenye sherehe ziliokolewa. Kwa mara nyingine amewavunja moyo na kuwaumiza mno wale wote waliokuwa wamejipanga kuvuna mamilioni kwa mgongo wa Siku ya Uhuru.

Tusimame kwenye ukweli kuwa serikali imekuwa ikihujumiwa na watendaji wenye hulka za kihuni. Matumizi ni mengi kuliko utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Wapo watumishi serikalini mishahara midogo lakini wanaishi kitajiri. Kumbe ni kubebwa na mianya ya shughuli za kiserikali. Kijishughuli kidogo fedha mabilioni yanateketea.

Na hili ndiyo eneo ambalo sasa naamini Dk Magufuli atakamua majipu uchungu mengi. Maana watendaji wengi wa serikali wameshajitengenezea mazingira ya kuishi kifisadi kutokana na kuvuna fedha za sherehe.

Kumbe haiwi sherehe kwa maana ya maadhimisho, bali mavuno kwa watendaji wa serikalini. Na hii imekuwa sababu ya wengi kupenda maadhimisho ya kitaifa. Vilevile kujidaia safari.

Ikumbukwe kuwa alianza kwa kupiga marufuku safari zote za nje ya nchi. Akaagiza watendaji wawe wanakwenda vijijini ili kujionea matatizo ya wananchi.

Kimsingi ndani ya serikali kuna majipu uchungu mengi mno. Sina shaka na uwezo wa mtumbuaji. Dk Magufuli kazi anaiweza hiyo kazi. Lazima watu wawe na nidhamu na rasilimali za nchi.

Hata hivyo, msisitizo wangu ni kuwa wakati Dk Magufuli akitumbua majipu, ushauri wangu ni kuhusu muundo wa elimu yetu. Lazima vijana wa Tanzania waandaliwe kuisaidia nchi. Wailinde nchi yao. Wawe wazalendo. Uzalendo ukikolea ndani ya wanafunzi, hatutakuja kuuona ufisadi nyakati zao za utumishi.