Home Uchambuzi RC Makonda usituangushe- 1

RC Makonda usituangushe- 1

3540
0
SHARE

MAKONDASAFIHATIMAYE ule uteuzi uliokuwa ukisubiriwa sana baada ya kuundwa kwa Baraza la Mawaziri umefanyika. Wakuu wa mikoa iliyopo Tanzania Bara wametangazwa.

Pamoja na kuwapo kwa majina yaliyozoeleka kisiasa hata hivyo kuna uteuzi wa mtu mmoja ambao umewafurahisha wengi wanaoamini kwamba ujana unaweza kuwa ni mzuri katika utendaji.

Uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni al maarufu kama DC Makonda kushika wadhifa wa ukuu wa Mkoa wa Dar es Salaam umepokelewa vizuri na wale wanaoamini kwenye ujana na uwezo wao wa kuthubutu. Ni kwa msingi huo ndio sababu nimeona ni jambo jema katika safu hii wiki hii nilonge na kiongozi huyu kijana na kujaribu kumpatia mawazo yangu, mapungufu makubwa ya jiji alilokabidhiwa na kile ninachoamini kwamba kinaweza kumsaidia kuleta mabadiliko ya kukumbukwa kwa miaka mingi kama si milele.

Sitaki akubaliane nami katika lolote lile isipokuwa nataka ayachukue haya nitayomwambia kama hoja ya kubungua bongo na kutafuta walau sentesi moja itayomfaa katika ndoto yake ya kutaka kuwa kiongozi wa kukumbukwa kwa kuibadilisha Dar es Salaam.

Ukweli ni kwamba Jiji la Dar es Salaam lipo hovyo sana pamoja na jitihada za ujenzi wa majengo makubwa na marefu unaofanyika katikati. Ni mji ambao hauwezi kushindanishwa na miji ya wenzetu kwa sababu ni jiji lenye kiza na ni jiji linalonuka kwa uchafu.

Ninaamini kama alivyojitahidi kufanya akiwa Kinondoni ambako ni wazi alitaka kuondoka na kuacha alama za zama zake vivyo hivyo atapenda kuondoka Dar es Salaam na kukumbukwa kama kiongozi kijana aliyeweza kuthubutu na kubadilisha mandhari ya jiji hilo.

Aondoke aliache jiji likiwa na mwanga kila kona na likinukia waridi na yasmini badala ya uoza wa takataka kila kona. Inawezekana ili mradi aendelee na utaratibu wake wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo kama alivyokuwa akifanya alipokuwa DC.

Ni imani yangu kwamba Makonda ambaye sasa ni RC anaweza kulibadilisha Jiji la Dar es Salaam kutoka jiji la kiza na kuwa jiji la mwanga ambalo litaonekana kutoka katika satalaiti za wakubwa zinazopiga picha usiku katika bara letu la Afrika. Ukichukua picha za satalaiti ambazo zimepigwa usiku na wanaanga wa Marekani na wa Urusi picha za Bara la Afrika zinaonyesha Afrika ni bara la giza totoro tofauti na miji ya wenzetu ambako tofauti ya picha ya usiku na mchana si kubwa kwani huko mitaa ina taa.

Miaka takriban hamsini na ushei baada ya uhuru bado hatuwezi kuwa na taa za barabarani na tunataka tujiaminishe kwamba miji yetu ni mizuri na salama. Hiyo ndiyo Afrika yetu na Dar es Salaam- kiza kila kona na tunakasirika tukiambiwa hili ni bara la giza.

Ukweli ni kwamba tunaishi kwenye kiza na hiyo inapunguza si tu ubora wa maisha ya raia wa kawaida bali ni hatari kwani kwenye kiza hakuwezi kuwa salama. Ni matumaini yangu kwamba hili RC Makonda ataliona na kulichukulia kwa uzito.

RC Makonda anachotakiwa kufahamu ni kwamba ili kuwa na mitaa yenye taa si lazima kukimbilia Tanesco. Tanzania ina jua kwa takriban saa 12 siku 365 yaani mwaka mzima. Teknolojia katika uhandisi wa umemejua imepiga hatua kubwa katika miaka ya karibuni.

Kama ilivyo teknolojia ya simu za kiganjani au mobaili vivyo hivyo na umemejua. Miaka ya tisini wakati simu za kiganjani zilipoingia nchini nakumbuka aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Adolar Mapunda alitushawishi kumnunulia Mwenyekiti wa Dimba simu ya kiganjani ambayo wakati ule ilikuwa inauzwa takriban Dola za Marekani 5,000. Leo hii tunazo simu nzuri za kisasa zinazouzwa hadi Dola 10 za Marekani. Ndiyo maendeleo ya sayansi na teknolojia na ni lazima RC Makonda utumie fursa hiyo kulibadilisha Jiji la Dar es Salaam kuwa la kisasa.

Miaka kumi iliyopita ilikuwa ukimsikia mtu anazungumzia umemejua ilikuwa si rahisi kumuelewa kutokana na gharama ilivyokuwa kubwa. Umemejua ulikuwa ni wa mabishoo kama wasemavyo vijana wa leo. Ulikuwa ni aghali na si rahisi kupata vifaa vya kukupatia umeme huo.

Hivi leo umemejua umekuwa ni teknolojia ya kila mtu. Tatizo letu kama kawaida ni kwamba hatuhangaiki kutafuta ukweli kuhusu mwenendo wa sayansi na teknolojia duniani na unavyoweza kutumiwa kuyabadili maisha yetu.

RC Makonda inawezekana kabisa kwa muda mfupi sana na kwa gharama ndogo kulifanya jiji letu la Dar es Salaam kuwa na hadhi ya kimataifa kwa kuweka taa za barabarani katika kila kona na kwa kuanzia na kule wanakoishi walalahoi ambako ndiko usalama ulipo mashakani zaidi.

Taa za umemejua zimesambaa duniani kote. Ukizingatia ukweli kwamba tunavyo vyuo vyetu vya ufundi vya serikali na binafsi mradi wa uwekaji wa taa za barabarani za umemejua unaweza kuwashirikisha na hauna sababu yoyote ya kushindwa.

Katika soko la dunia unaweza kupata taa ya mita nane kwa kati ya dola 150 hadi 1,000 kulingana na ubora na idadi. Taa hizo zitapowekwa zitageuka kuwa ni milingoti ya kutundikia matangazo ya biashara hivyo basi manispaa zako zitatengeneza fedha si haba ambazo zitarejesha gharama ya uwekaji wa taa hizo na ziada. Taa hizo hazilipiwi bili ya kila mwezi kama ambavyo zingeunganishwa na Tanesco.

Ni imani yangu kwamba RC Makonda wazo hili utalichukua kama changamoto na kulifanyia kazi kwani ukilikubali na kulitekeleza bila shaka sote tutakuwa tumefaidika.

Nasema hivi inawezekana kuwa na Jiji la Dar es Salaam bila ya kiza na hiyo itabadili maisha ya wakazi wa jiji. RC Makonda naamini unao uthubutu wa kulitafakari hili na wananchi wanasubiri kusikia majeshi yako katika manispaa zako tatu yatapata amri gani.

RC Makonda usituangushe kwa hili la kwanza.