Home Makala SADC iomboleze kifo cha Rais Samora Machel wa Msumbiji

SADC iomboleze kifo cha Rais Samora Machel wa Msumbiji

1805
0
SHARE

Na JOSEPH MIHANGWA

WAKATI wakuu wa nchi zinazounda Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wakikutana jijini Dar es Salaam mapema wiki hii, yafaa tuwakumbuke waasisi wa jumuiya hiyo miaka 40 iliyopita, waliokutana mjini Arusha mwaka 1979 kukamilisha kazi hiyo.

Wakati huo SADC ikiitwa Taasisi ya Kuratibu Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, kabla ya kuwa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi hizo mwaka 1992 iliasisiwa na marais Julius Nyerere (Tanzania), Kenneth Kaunda (Zambia), Agostinho Neto (Angola), Samora Machel (Msumbiji) na Seretse Khama (Botswana).

Kati ya waasisi hao watano, ni Rais mstaafu Kenneth Kaunda aliye hai mpaka sasa; wengine wote wanne walikwishatangulia mbele ya haki, isipokuwa Rais Machel ambaye kifo chake kinahusishwa na hujuma ya kutunguliwa kwa ndege aliyokuwa akisafiria.

Pamoja na kwamba Afrika inapaswa kuomboleza vifo vya wanaharakati wa ukombozi hawa, kifo cha Samora Machel kinagusa kwa uchungu mioyo yetu kwa namna alivyouawa kikatili na maadui wa Afrika kwenye kilele cha harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika. Ndege yake ilitunguliwa angani wakati akirejea nyumbani akitokea Ndola, Zambia.

Ni wangapi tunaelewa sababu, mazingira na ilivyotokea akauawa?

Angekuwa na mtabiri wa kumuonya maadam tu asibeze onyo, kama ambavyo tu alivyoonywa mtawala wa Rumi ya kale, Julius Kaisari (Caesar) na mtabiri wake kujihadhari na siku ya 15 ya Machi (Ades of March) asitoke nje siku hiyo, kwamba angeuawa; Rais Samora Machel wa Msumbiji asingesafiri kwa ndege siku ya 19 ya Oktoba 1986, kwenda kuhudhuria Mkutano wa Viongozi wa Nchi za Mstari wa mbele (Frontline States) katika Ukombozi Kusini mwa Afrika, uliopangwa kufanyika mjini Mbala, Zambia siku hiyo na kukumbwa na kifo.

Tofauti na Kaisari aliyekataa onyo la mtabiri wake kuwa huo ulikuwa uoga usio na msingi unaosumbua wanadamu, akisema: “Watu waoga hufa mara nyingi kabla ya vifo vyao”, na kwamba yeye alikuwa “hatari kuliko hatari ambayo huniogopa”.

Lakini Samora Machel hakuonywa wala hakujua kilichokuwa kikimngojea siku hiyo, hadi ndege yake aina ya Tupolov 134A, iliyotengenezwa nchini Urusi, ikiendeshwa na Rubani wa Kirusi ikibeba ujumbe wa watu 33 wa Serikali ya Msumbiji, ilipotunguliwa angani na kuangukia mita 200 kutoka mpaka wa Msumbiji ndani ya ardhi ya Afrika Kusini. Rais Machel na Maofisa wengine, walifariki dunia.

Nchi hizo za Mstari wa mbele, zilikuwa ni Zambia, Tanzania, Botswana, Zimbabwe, Angola na Msumbiji zilizopania kutokomeza ukoloni, ubaguzi wa rangi wa Makaburu Afrika Kusini na mashambulizi ya waasi, mahaini na mamluki dhidi ya nchi huru za Kusini mwa Afrika.

Siku tatu kabla ya ajali, Oktoba 16, 1986, Machel alikuwa ameendesha kikao cha pamoja Ikulu ya Maputo, kati ya ujumbe mzito wa kijeshi wa nchi yake na vyombo vya Usalama kutoka Zimbabwe, kuzungumzia jinsi ya kuvidhibiti vikundi vya waasi wa NMR, kwa jina lingine, RENAMO, vilivyokuwa vikiendesha mapambano dhidi ya Serikali yake kutokea Malawi na Afrika Kusini.

Swali linaloendelea kuulizwa na wengi mara nyingi bila kupata jibu kuhusu kitendawili hiki ni nani alimuua Rais Machel na wenzake?.

Swali kama hili liliulizwa pia kufuatia kifo cha kutatanisha cha Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo sasa DRC, marehemu Patrice Emery Lumumba mwaka 1960; lakini ni siku za karibuni tu jibu limeanza kupatikana, baada ya kubainika kuwa, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ndilo lililomuua kwa madai ya kuwa wakala hatari wa Ukomunisti nchini Congo na  barani Afrika.

Wapo wanaoamini kwamba, ndege ya Machel ilipigwa bomu ikiwa angani na kuanguka katika kijiji cha Mbuzini nchini Afrika Kusini; wapo pia wanaoamini kuwa Ndege hiyo iligonga miti juu ya kilima wakati ikijiandaa kutua uwanja wa Maputo; kadhalika, wapo wanaodhani kwamba ilivutwa kwa nguvu ya sumaku ya vyombo vya kivita na kuangukia Afrika Kusini. 

Bado kuna wengine wanasema, ndege hiyo ilipigwa radi, ikapoteza mwelekeo na mawasiliano na kuanguka. Wote hawa hakuna aliye na jibu kamili.

Juu ya utata wa ndege na jinsi ilivyoanguka lipo swali kwamba ni nani aliyehusika na hujuma hiyo? Wenye kuhoji hivyo ni wale wanaoamini kwamba ndege ya kiongozi huyo ilihujumiwa.

Hapa tena hakuna mwenye jibu kamili.  Wapo wanaodai kwamba Afrika Kusini ilihusika kama njia ya kuikomoa Msumbiji kwa sababu ilikuwa ikiwahifadhi wapigania uhuru wa Chama cha African Nationalist Congress (ANC) cha Nelson Mandela dhidi ya utawala dhalimu wa Makaburu. 

Wapo wanaodai pia kuwa Rais Hastings Kamuzu Banda wa Malawi, alihusika kwa sababu Msumbiji na Zambia hazikuwa na uhusiano mzuri kisiasa na nchi yake. Ukweli ni upi na unapatikana wapi? 

Wakati ndege ya Machel ikiondoka Maputo kuelekea Mbala, Zambia siku hiyo asubuhi, ikiwa na marubani wawili wa Kirusi; hapakuwa na taarifa ya ubovu wowote kwa ndege hiyo. 

Kikao kilimalizika jioni siku hiyo hiyo na Rais Machel na ujumbe wake wakaanza safari ya kurejea nyumbani kupitia anga la Zimbabwe na hatimaye kuingia Msumbiji kabla ya kuangukia Afrika Kusini ‘kimiujiza’.

Inaelezwa kwamba, rada ya Jeshi la Anga la Afrika Kusini (SAAF) ilifuatilia na kuiona ndege hiyo ikiingia anga la Msumbiji kuelekea Maputo saa 2.45 usiku, na kwamba saa 3.12 ilikata anga kugeuza mwelekeo kwa nyuzi 30 kulia kuiacha Maputo na kuendelea kuelekea Kusini – Kusini Magharibi, kisha kupotea kabisa jichoni mwa rada saa 3.16.

Haikujulikana kwa uhakika saa ndege hiyo ilipoanguka na vipi iliangukia katika ardhi ya Afrika Kusini, Kijiji cha Mbuzini, mita 200 toka mpaka wa Msumbiji na nchi hiyo.

Upo ushahidi wa kutiliwa shaka kuhusu saa ya ajali.  Mmoja wa Makaburu wa kwanza kufika katika eneo la tukio, Luteni Jenerali Neethling anasema, inawezekana ajali hiyo ilitokea kati ya saa 3.15 na 3.30 (21.15/21.30 hrs) usiku, kwa mujibu wa saa za mkononi za wahanga wa ajali zilizokuwa zimesimama. 

Mmoja wa wahanga na majeruhi wa ajali hiyo, Fernando Joa, anaeleza kuwa, kabla ya ajali, rubani alikuwa amekwishatoa agizo kwa abiria kufunga mikanda tayari kwa kutua Maputo. 

Nao wataalamu wa Jeshi la Anga la Afrika Kusini (SAAF), wanadai kuwa, wakati wakikagua mabaki ya ndege hiyo waligundua kwamba, chombo cha kupima umbali (DME) kilionyesha ndege ilielekea Maputo na kwamba tayari taa za mji huo zilikuwa zikionekana kwa rubani.

Inasemekana, pamoja na rubani kuweka mafuta ya kutosha pale Lusaka, ukaguzi wa ndege kwenye eneo la tukio ulionyesha hapakuwa na salio la mafuta kwenye Matanki, wala hapakuwa na dalili za kumwagika mafuta au ndege kuwaka moto ilipoanguka. 

Hicho nacho ni kitendawili kingine.  Swali  Je, ni kweli rubani aliweka mafuta Lusaka au ilikuwa geresha tu? Na kama aliweka, yaliishia wapi? Na kama hakuweka, lengo lake lilikuwa lipi; kuua na kujiua pia?.

Jambo moja ni dhahiri, kwamba hapakuwa na sababu nzuri kwa rubani kupita karibu au ndani ya anga la Afrika Kusini kwa kuwa hiyo haikuwa njia ya mkato kutoka Zambia kwenda Msumbiji.  Lakini, kwanini alipita huko?.

Tuangalie sasa dhana mbalimbali zinazotolewa kuhusu kifo cha Machel. Je, ni kweli ndege yake ilipigwa bomu kutoka ardhini au kutoka ndani ya ndege?.

Dhana hii haina uzito kwa sababu inasemekana, ukaguzi uliofanywa haukuonesha ndege kufumuka wala kuwepo matundu ya risasi. Hata silaha alizokuwa nazo mlinzi wa Rais, hazikuonyesha kutumika, kama ishara ya purukushani za kumwokoa Rais, ndege na abiria.

Na hata kama dhana ya bomu ingekuwa sahihi, basi itakuwa bomu hilo liliwekwa kwenye ndege, ama huko Mbala au wakati wa kujaza mafuta pale Lusaka.

Au je, ndege hiyo ilivutwa kwa nguvu za sumaku na Makaburu ndani ya ardhi yao?. Hapa tena, hatudhani kwamba dhana hii ni sahihi, kwani Makaburu si wajinga hivyo kiasi cha kukubali kiongozi wa nchi nyingine afie au auliwe waziwazi katika ardhi yao.

Je, ndege hiyo ilipigwa radi?  Hapana.  Kama hali ya hewa iliripotiwa kuwa shwari dakika 15 tu kabla ya ajali na taa za mji wa Maputo zilikuwa zikionekana, suala la radi linatoka wapi?.

Tuchukulie mfano wa dhana moja inayoonekana kuwa karibu na ukweli, kwamba rubani wa TU – 134A aliamua kuruka pembezoni mwa mpaka wa Afrika Kusini na Msumbiji kwa hofu ya kutunguliwa na magaidi wa MNR waliotandawaa eneo kubwa la Msumbiji.  Tuchukulie pia kwamba ndege hiyo ilianguka kwa mlipuko wa bomu toka ndani ya ndege na kwamba haikuwaka moto kwa sababu haikuwa na mafuta ndani ya matanki yake. 

Kuna ushahidi kuonyesha kwamba, uhusiano kati ya Serikali ya Rais Machel na Serikali ya Dakta Banda, haukuwa mzuri kwa sababu ya Rais Banda kuwapa vituo vya kuanzishia mashambulizi vikundi vya NMR kwa kushirikiana na Afrika Kusini dhidi ya Msumbiji.

Ingawa katika Mkutano wake na makamanda kutoka Zimbabwe, Oktoba 16, 1986; Machel alidai kuwa adui wa Msumbiji hakuwa Malawi yenyewe, bali Afrika Kusini ambayo ilikuwa ikiitumia Malawi kuchafua amani nchini Msumbiji na Zimbabwe kwa kuwapa msaada NMR, ukweli ni kwamba Serikali ya Banda na ile ya Machel vilikuwa vitu viwili mbalimbali.

Mwezi mmoja kabla ya kifo chake, Machel na Marais wenzake, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na Kenneth Kaunda wa Zambia, walilazimika kwenda Malawi kumwomba Banda aache kuvisaidia vikundi vya MNR, lakini badala yake, hatua hiyo iliongeza chuki ya Banda dhidi ya Machel na Mugabe kutokana na Banda kuamini kwamba, Machel na Mugabe walidhamiria kuuangusha utawala wake.

Kwa upande mwingine, wakati huo, uhusiano kati ya Msumbiji na Afrika Kusini ulikuwa umeanza kuonyesha kurekebika, kufuatia kutiwa sahihi kwa makubaliano ya Nkomati (Nkomati Accord), ambapo Msumbiji iliahidi kutowaunga mkono wapiganaji wa ANC dhidi ya Afrika Kusini na vivyo hivyo kwa Afrika Kusini kuacha kuviunga mkono vikundi vya NMR dhidi ya Msumbiji.

Kwa mtizamo huu, tuhuma inamwelekea zaidi Banda na NMR kupitia “kazi ya ndani” na kwa kuponzwa na mdomo wake. Tunajua kulikuwa na Setelaiti za ki-elektroniki za ujasusi angani, zenye uwezo wa kufuatilia mwenendo wa ndege ya Machel na kupiga picha.

Lakini kwa sababu ambazo hazijaelezwa, hakuna picha iliyotolewa mpaka leo. Kwa yote haya, swali litaendelea kuulizwa:

“Nani alimuua mwana mpendwa huyu wa Afrika, Rais Samora Machel? Tunaamini, historia itatoa jibu kwa wapenda haki kesho, kama leo haitoshi.