Home Latest News Samatta awabeba wachezaji Ulaya

Samatta awabeba wachezaji Ulaya

2214
0
SHARE


samattaNA ASHA MUHAJI

KAMA fursa ndiyo hii sasa washindwe wenyewe. Watanzania wanapaswa kuwa nayo makini kama Waswahili wanenavyo; ‘bahati haiji mara mbili’, hivyo bila shaka nafasi hii ni nyeti na muhimu kuikumbatia isiponyoke.

Baada ya kilio cha muda mrefu kwa wanasoka wa Tanzania kutafuta njia ya kutokea, inavyoonekana ni kama vile sasa mwanga umeanza kupatikana.

Ni Mbwana Samatta mwanasoka wa Tanzania anayecheza soka katika klabu ya TP Mazembe baada ya kupambana mwenyewe kwa nguvu zake takribani miaka minne akiwa juani sasa kuna kila dalili ya ‘kulia kivulini’ akiwa na wanasoka wenzake kutoka nchi hii.

Kitendo cha mwanasoka huyo wa kimataifa wa Tanzania aliyetwaa hivi karibuni Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani kushinikiza mkataba wake mpya na klabu ya K.R.C Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji uwekwe kipengele kitakachokua na masilahi kwa taifa lake, kinapaswa kupongezwa na kila Mtanzania.

Katika mkataba huo wa Samatta na Genk kipengele hicho cha masilahi kwa taifa kinaeleza wazi kuwa klabu hiyo itachukua wanasoka wawili vijana kila mwaka kwa muda wote wa mkataba wake na kuwaingiza katika mpango wa mafunzo katika ‘academy’ ya klabu hiyo.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, wanasoka hao watakaokuwa na umri chini ya miaka 20, watakuwa wakitafutwa na wakala wa mchezaji husika na watapata nafasi ya kujifunza katika shule hiyo ya michezo na iwapo wataonesha kiwango basi wanaweza kupewa nafasi ndani ya klabu hiyo au kuuzwa kwavile Genk ina kitengo cha uuzaji wa wachezaji.

Uamuzi huo siyo faraja tu kwa wanasoka wa nchi hii bali iwapo nafasi hiyo itatumiwa vizuri itawakomboa wachezaji wengi na hata kuitangaza vizuri kimataifa Tanzania hii.

Je, ni Watanzania wangapi wanaothubutu kutumia nguvu zao kuwanyanyua na kuwabeba ili nao wakaribie mafanikio yao? Ni Samatta!

Kimsingi kama siyo uzalendo na utaifa hakukuwa na haja ya kupigania nafasi ya wengine bali kujipigania mwenyewe hasa ikizingatiwa kuwa hata yeye hakushikwa mkono na mtu wakati akitafuta fursa hiyo bali jitihada zake mwenyewe ndizo zilizomfikisha hapo.

Hiyo inaonesha wazi siyo tu mwanasoka huyo anaangalia masilahi yake binafsi bali pia ameweka uzalendo mkubwa kwa kutaka kuwapatia wenzake nafasi kupitia mgongo wake.

Ni Watanzania wangapi waliopata mafanikio lakini hawakukumbuka kuwakomboa wenzao? Kupitia mwanasoka huyu ana ujumbe mzito kwa Watanzania wenzake hasa katika suala la kuweka kando ubinafsi na kujali masilahi ya wengi.

Wadau wa Tanzania wakiwemo wanasoka wenyewe wanapaswa kuiangalia nafasi hiyo kama mboni ya jicho yao kwani wakiitumia vibaya ni wazi watamchafua na kumuharibia Samatta pamoja na kuipaka tope Tanzania kupitia mchezo huo wa soka.

Kama ambavyo ilitokea kwa Samatta mpaka akapata nafasi ya kuichezea TP Mazembe, basi wahusika wa utafutaji na uteuzi wa wanasoka uwe ni wa kuzingatia sifa na viwango ili watakaopatikana wawe ni wanaokidhi vigezo na uwezo wa kufaulu.

Ni jukumu la kila mdau kumpa sapoti Samatta ili afanikiwe zaidi kwani dalili zinaonesha wazi mafanikio yake yana faida kwa Watanzania wengine hivyo kufanikiwa kwake ndiyo kufanikiwa kwa soka la Tanzania.

Hakuna asiyefahamu soka la Tanzania liko katika hali mbaya na kila siku kumekuwa na mikakati mbalimbali ya kutaka kuwatoa wachezaji ili wapate nafasi ya kwenda kucheza nje hasa barani Ulaya, lakini historia ya soka ya nchi hii imekuwa tatizo kubwa kwao.

Taasisi zinazosimamia mchezo wa soka kuanzia ngazi za mikoa mpaka Taifa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zinapaswa kuweka mikakati ya kukuza na kusimamia soka la vijana hasa ikizingatiwa kuwa kweli fursa zipo tatizo hatuna maandalizi ya kuwapata wanasoka vijana.

Mbali na Samatta ‘pacha’ wake Thomas Ulimwengu waliyekuwa wakicheza wote TP Mazembe naye yuko mbioni kujiunga na Klabu ya Besiktas ya Ligi Kuu ya nchini Uturuki, kwa pamoja wanaweza kuibeba Tanzania na soka lake kwa ujumla hivyo wapewe sapoti ya nguvu.

Iwapo mipango itawekwa na kwa kushirikiana na Samatta kuna uwezekano mkubwa sasa Tanzania ikaanza kusikika na kujulikana kimataifa. Siku si nyingi Tanzania itasikika.