Home Latest News SAUDI ARABIA YAENDESHA OPERESHENI KALI DHIDI YA UFISADI

SAUDI ARABIA YAENDESHA OPERESHENI KALI DHIDI YA UFISADI

1425
0
SHARE
RIYADH, SAUDI ARABIA

Haijawahi kutokea katika utawala wa nchi yenye utajiri mkubwa wa mafuta na yenye kujulikana wa ufujaji mkubwa wa pesa unaofanywa na wana wa ukoo wa mfalme ambao wengi wao hupewa nyadhifa mbali mbali katika serikali na taasisi zake.

Lakini ndivyo ilivyotokea Jumamosi iliyopita (Novemba 4) siku ambayo utawala ulitangaza kwamba makumi ya watu, wakiwemo watu wa ukoo wa mfalme wametiwa mbaroni katika operesheni kabambe dhidi ya ufisadi na ufujaji wa fedha za umma.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliotiwa nguvuni ni Mwanamfalme (Prince) Alwaleed bin Talal, ambaye ni bilionea na mwekezaji latika makampuni makubwa ya Marekani kama vule Citigroup na News Corporation.

Waliokamatwa ni pamoja na wanawafalme wengine wapatao kumi, makumi ya mawaziri walio madarakani na wa zamani, na mwenyekiti wa Saudi Binladin Group, kampuni kubwa ya ujenzi na mmiliki wa kampuni ya MBC – ambayo ni kampuni kubwa ya mtandao wa satellite katika Mashariki ya Kati.

Baadhi ya waliokamatwa wanashikiliwa katika hoteli moja ya anasa ya Ritz-Carlton iliyoko mji mkuu wa nchi hiyo Riyadh ambayo imesitisha kupokea wageni wengine na kuwaondoa waliokuwa tayari wamepanga.

Ndege binafsi (private jets) zote zimeamriwa kutoruka ili kuzuia wengine wanaotafutwa wasiondoke nchini.

Aidha hatua nyingine iliyochukuliwa na utawala wa nchi hiyo ni kuwafukuza kazi mawaziri kadha, akiwemo Prince Mutaib bin Abdullah ambaye ni kamanda wa vikosi vya ulinzi.

Kuondolewa kwa Abdullah kunatoa nafasi ya madaraka zaidi kwa Muhammad bin Salman, mtoto wa mfalme wa sasa na ambaye ndiye mrithi wa baba yake Mfalme Salman bin Abdul Aziz.

Kutokana na mabadiliko hayo sasa hivi wizara tatu muhimu – ile ya ndani, ya ulinzi na ya vikosi vya ulinzi vya Mfalne viko chini ya Muhammad bin Salman.

Muhammad alipewa uwaziri wa ulinzi masaa machache tu baada ya baba yake kurithi kiti cha ufalme mwaka 2015 baada ya kifo cha aliyekuwa mfalme wan chi hiyo Abdullah bin Abdul Aziz.

Mapema Juni mwaka huu aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, Muhammad bin Nayef, na ambaye ndiye alikuwa mrithi wa kiti cha ufalme alifukuzwa kazi na kuwekwa kizuizini nyumbani kwake.

Mwezi Septemba polisi iliwatia nguvuni makumi ya wapinzani wa utawala wa kifalme kuanzia viongozi wa dini hadi wanaharakati wa haki za binadamu.

Baadaye Mfalme Salman alitoa agizo kwamba wanawake wataruhusiwa kuendesha magari kuanzia mwaka ujao hivyo kufungua mlango uliokuwa umefungwa kwa miongo mingi.

Wiki chache baadaye Muhammad bin Salman aliitisha mkutano na wawekezaji mjini Riyadh ambako alitangaza nia ya kuwepo kwa kile alichokiita “Uisilamu wa wastani” na kutangaza mpango wa Dola za KImarekani 500 milioni za kujenga ukanda wa liuchumi (economic zone) utakaoitwa Neom, na ambao utahudumiwa na maroboti.