Home Makala Sera ya elimu iwe na upendeleo kwa mtoto wa kike

Sera ya elimu iwe na upendeleo kwa mtoto wa kike

3040
0
SHARE

PENDO FUNDISHA

SERA ya Elimu bila malipo ya mwaka 2014 inazingatia uendeshaji wa shule zote za msingi na sekondari bila malipo ya ada na michango mingine kutoka kwa wazazi au walezi.

Mpango huu ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, waraka wake ulisambazwa kwenye shule mbalimbali nchini ukiwataka wakuu wa shule kutochangisha michango ya aina yoyote.

Kimsingi elimu bila malipo inawezekana na katika kipindi kifupi  imeweza kuzaa matunda kwa kufanikisha lengo la serikali la kuongeza wingi wa wanafunzi kutoka wanafunzi 289,699 mwaka 2001 hadi wanafunzi milioni 1.6 kwa mwaka 2010 kupitia takwimu zilizotolewa na serikali kupitia Wizara ya Elimu, Mafunzo na Ufundi.

Awali idadi kubwa ya watoto kutoka kaya masikini walishindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa uwezo wa kulipa ada na michango mingine. Sera hii inatajwa kufanikisha kuondoa changamoto hiyo kwa asilimia 80 kwa mujibu wa taarifa ya serikali iliyotolewa na Wizara ya Tamisemi, mwaka 2016 na Waziri George Simbachawene.

Hata hivyo, ipo haja kwa sera hii kuongezewa wigo zaidi hasa katika kuyatambua mahitaji muhimu ya mtoto wa kike kama tulivyooona kwenye makala ya wiki iliyopita, ambapo wadau mbalimbali wametoa maoni yao, akiwemo Mwenyekiti wa mtaa wa Imezu, Gorge Waziri.

Waziri  anasema miongoni mwa watoto waliopata mimba ni mtoto wake anayemlea Hanifa Waziri (15), ambaye alishindwa kuendelea na masomo ya kidato cha pili mwaka jana baada ya kupata ujauzito na sasa analea mtoto wa kiume wa miezi miwili.

Waziri anasema changamoto kubwa inayochangia tatizo la mimba kwa watoto wa kike ni mazingira yanayowazunguka, hali duni ya kipato katika familia na lingine ni tamaa za kimwili, hata hivyo anakiri kwamba kwa tukio la mtoto Hanifa hali ngumu ya maisha ya familia yake ilichangia.

Anasemashule ya Imezu imebahatika kuwa na hosteli, lakini wazazi na walezi wanakataa kuwapeleka watoto, wanasema kuishi mle ni gharama akiwamo Hanifa, ambaye ni mtoto wa kaka yake.

“Ukiondoa gharama ya godoro, ndoo, jembe, fyekeo ambavyo mtoto analazimika kwenda navyo shule, mzazi anatakiwa kuchangia kiasi cha Sh. 54,000 kwa mwezi kwa ajili ya chakula, hivyo anaona bora mtoto atoke nyumbani,”anasema.

SIMULIZI YA HANIFA NA MIMBA YAKE

Hanifa Waziri ni miongoni mwa wanafunzi walioathiriwa na mazingira na hali duni ya kipato kutoka kwa wazazi hivyo kujikuta akishawishika na kuingia kwenye mikono ya baadhi ya wanaume waharibifu na kupata mimba na kupoteza ndoto zake.

Anasema wazazi wake wanajishughulisha na biashara ya pombe kilabuni hivyo wakati mwingi hubaki nyumbani pekee yake akiendelea na shughuli za nyumbani na shambani, lakini kila alipokuwa akijiitahidi kutekeleza majukumu hayo ya kifamilia anakutana na changamoto ya kifedha katika kukidhi mahitaji yake muhimu ya shule kama vile, daftari, mafuta, dawa ya meno, nguo za ndani, pedi na chakula.

“Nikitoka shule mama ananitaka niende shamba nikirejea nyumbani chakula hakuna, bado mafuta ya kupaka, sabuni, daftari na pedi kwa ajili ya kujisitiri sina, hivyo nafikiria nitavipata wapi hapo ndipo nilipojikuta nikiingia kwenye mahusiano na wanaume wawili ambao walikuwa wakijitahidi kunitimizia yale niliyokuwa nikiyahitaji,”anasema.

Anasema mwanaume mmoja ni mkulima na mwingine ni dereva bodaboda ambao wote walikuwa wakimsaidia. Hata hivyo ana wakati mgumu kutaja baba wa mwanayekwani ana hofu atakamatwa na kufungwa wakati yeye atabaki na mzigo wa kulea mtoto.

“Kutaja baba wa mtoto ni ngumu na siwezi kwani ninafikiria nani atamtunza kama atafungwa? Wazazi hawahangaiki na mimi? Natamani kurejea shule na ninajuta, sioni msaada wowote, binafsi ninaiomba serikali ituangalie watoto wa kike na kutoa nafasi ya upendeleo hasa katika shule za bweni za kata kwa kutulipia gharama za chakula,”anasema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya na Diwani wa kata ya Imezu , Mwalingo Kisemba, anasema jamii ya eneo hilo inakabiliwa na changamoto kubwa ya uelewa, kwani sera ya elimu bila malipo bado inawapa shida sana, wengi wanaamini kwamba serikali inapaswa kugharimia mahitaji ya hostel na wao kazi yao ni kujenga majengo jambo ambalo linakwamisha maendeleo ya mtoto wa kike.

“Siamini kama kweli mzazi anashindwa kuchangia kiasi cha Sh.1,500 kwa siku ili mtoto wake aweze kupata huduma kwenye hostel aliyoijenga kwa nguvu kubwa, hapa tatizo lililopo ni uelewa tu, haiwezekani hostel ikajengwa na kukamilika, lakini watoto hawapelekwi na ukifuatilia eti mzazi au mlezi ameshindwa kumudu gharama. Hapana.Yatupasa kubadilika,”anasema.

Diwani huyo anasema jitihada za lazima zinahitajika kwa jamii ya eneo hilo kwani hata wazazi au walezi wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano kwenye vyombo vya dola wakati wa operesheni ya kuwakamata wahusika waliowapa mimba wanafunzi na wakati mwingine wanashirikiana kuwatorosha na kuwatisha watoto wasiwataje wahusika.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika, anasema kuwa kutokana na takwimu hizo za mimba kuwa juu, serikali imeweka mikakati madhubuti ya kumkomboa mtoto wa kike kwa kutekeleza kwa vitendo sheria ndogo zitakazo wabana wazazi watakaobainika kuwa watoto wao wamepata ujauzito wakiwa shule.

Anasema ukiangalia sheria ya mtoto ya mwaka 2009 sura ya 95 imetoa mamalaka kwa jamii ya kuripoti vitendo viovu wanavyofanyiwa watoto, sheria ya jinai sura ya 130 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, inasema mtoto aliyechini ya miaka 18 hana ridhaa ya kufanya mapenzi na endapo kitendo hicho kitafanyika kitakuwa ni ubakaji.

Akizungumzia changamoto ya wazazi kushindwa kuwapeleka watoto wa kike kuzitumia hostel kutokana na changamoto ya kiuchumi, Ntinika anasema kazi kubwa itakayofanywa na serikali ni kutoa elimu kwa jamii ili kutambua umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, na anaamini litafanikiwa kwani kama jamii iliweza kuzijenga hostel hizo hivyo haiwezi kushindwa kuwapeleka watoto.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja, anasema mpango wa elimu bila malipo umesaidia sana kupunguza idadi ya watoto wasiojua kusoma wala kuandika, lakini changamoto inabaki kwenye suala la mimba za wanafunzi hasa kwenye shule za kata ambazo hazimo kwa asilimia 100 kwenye sera ya elimu bila malipo.

“Shule za kata zipo chini ya serikali za mitaa, ambapo serikali kuu inawajibika kwa kulipa ada kwa wanafunzi, lakini suala la mabweni lipo kwenye nguvu ya wazazi kupitia kamati za maendeleo za kata ambapo jamii ikiona kuna haja ya eneo hilo kuwa na bweni basi watalazimika kujenga na kugharimia gharama za chakula na michango mingine muhimu,”anasema.

Akizungumzia hilo, mdau wa maendeleo ya elimu Mkoa wa Mbeya, Amani Mwansansu, anasema wakati umefika kwa serikali kutoa nafasi ya upendeleo kwa mtoto wa kike anayeishi maeneo ya pembezoni kwani mbali na changamoto kubwa inayotajwa ya kiuchumi kwenye familia wanazoishi, lakini elimu ina umuhimu mkubwa na jamii nayo inahitaji kuelemishwa.

“Siamini kwamba kama kunamzazi anashindwa kuchangia kiasi cha shilingi 1,500 kwa siku ili mtoto wake aweze kupata elimu na kutimiza ndoto zake, hapo kuna shida ya uelewa kwa baadhi ya wazazi, wengine wanawezaje kuwapeleka watoto wa kike bweni na wengine wanashindwaje? Lazima ifike mahala watu wabadilike na huu ni mtazamo hasi tu kwa baadhi ya watu ambao wamekuwa wakimchukulia mtoto wa kike kama ni mama wa familia,”anasema.

Pia, anasema serikali inapaswa kuangalia upya sera ya elimu bila malipo kwa kuzisaidia shule za kata ambazo zimekuwa na hostel kwa msaada wa chakula tu na majukumu mengine kuwaachia wazazi na walezi ambao nao wakibanwa na sheria za nchi na za maeneo husika lazima watatimiza wajibu wao.

Anasema jamii nayo inashida kwani haijaona umuhimu wa watoto wa kike kupewa haki sawa kama mtoto wa kiume, kipato cha hali ya chini kimekuwa ni shida kwa baadhi ya jamii hivyo uona bora kuwaozesha watoto wa kike, kuwapa majukumu ya kulisha familia hivyo hujikuta wakitafuta fedha kwa njia yoyote ile hata kujiingiza kwenye vitendo vya uhuni, baadhi yao kushindana kupata idadi kubwa ya mifugo hususani ng’ombe wanaotozwa wakati wa utoaji wa mahari.

Aliieleza kuwa hata serikali haijatoa kipaumbele cha kumlinda mtoto wa kike, kisera na kisheria, hivyo huonekana hana haki sawa na mtoto wa kiume na ndio sababu sheria ya elimu ya mwaka 1978 sura ya 30 ilichofanyiwa marekebisho mwaka 1995 na 2002  inamtaka mtoto wa kike akipata  mimba aende nyumbani.

Mdau huyo anasema hakuna mifumo mbadala ya kumsaidi mtoto wa kike anayepata mimba akiwa shule ambapo kwa asilimia kubwa kumekuwa na changamoto nyingi hasa zile za kitamaduni, kisera na umasikini.

Mimba za utotoni ni miongoni mwa vikwazo vinavyowapata watoto wa kike wa Tanzania na tatizo hilo bado ni kubwa kwenye baadhi ya maeneo sababu kubwa ni; umasikini, tamaduni na sera ambazo zimekuwa zikiifanya jamii kutokuona umuhimu wa watoto wakike kupata elimu, kuanza shule mapema na kumuweka pembezoni kwamba ni mtu wa kuolewa tu, hivyo misingi ya namna hiyo hata watoto wenyewe wanaona ni bora kuolewa tu.

Taarifa ya mwaka 2018, iliyotolewa na Idara ya Maendeleo ya vijana-Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu, inasema tatizo la mimba za utotoni nchini limeongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 27 mwaka 2016/17, kutokana na ukosefu wa huduma pamoja na elimu ya afya ya uzazi kwa vijana umri wa miaka 15 hadi 19.

Ripoti ya UNICEF, inasema karibia msichana mmoja kati ya wasichana 20 nchini Tanzania, huanza kuzaa akiwa na umri wa miaka 15, na uwiano huo huongezeka kwa kasi hadi msichana mmoja katika wasichana wanne miongoni mwa wasichana wa umri wa miaka 17 na zaidi ya msichana mmoja katika wasichana watatu miongoni mwa wasichana wa umri wa miaka 18.

Wasichana wa vijijini wana uwezekano wa karibu mara mbili ya wale wa mijini wa kupata watoto kabla hawajafikia umri wa miaka 19. Zaidi ya nusu ya wasichana ambao hawakupata elimu hupata watoto au mimba kabla ya kufikisha umri wa miaka 19, ikilinganishwa na asilimia 25 kwa wasichana waliomaliza elimu ya msingi na chini ya asilimia tano kwa wasichana waliohitimu elimu ya sekondari.

Katika ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia na Idadi ya watu (UNFPA) ya mwaka 2013 iliyoangalia hali ya idadi ya watu imebaini kuwa kati ya mimba milioni moja zinazotungwa nchini Tanzania, asilimia 23 ya mimba hizo zinawahusu wasichana waliochini ya umri wa miaka 19.