Home Afrika Mashariki Siasa ilivyokwenda kutibua urafiki wa Chameleone, Rais Museven

Siasa ilivyokwenda kutibua urafiki wa Chameleone, Rais Museven

5347
0
SHARE

KAMPALA, Uganda

WIKI iliyopita, siasa za Afrika Mashariki zilipokea jina jipya kutoka katika tasnia ya burudani. Safari hii ni Joseph Mayanja, maarufu Jose Chameleone, mwanamuziki wa Uganda aliyetanga nia ya kukitaka kiti cha Meya wa Jiji la Kampala katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021.

Haijasahaulika kuwa msanii huyo aliyewahi kutamba Afrika Mashariki na wimbo ‘Shida za dunia’, alikuwa akihusishwa na mpango wa kugeukia siasa kwa muda mrefu, hasa mwanzoni mwa mwaka huu, lakini mara zote zilionekana kuwa ni habari za uzushi.

“Nilianza kuwa na mpango wa kuwa meya tangu mwaka 2005. Ndoto yangu ilikuwa ni kuwa meya mwenye umri mdogo zaidi katika Jiji la Kampala,” anasema Chameleone.

“Nimekuwa kiongozi kwa maisha yangu yote, hivyo haitakuwa changamoto kangu kuwaongoza watu wa Kampala ikiwa watataka nifanye hivyo, niwe Meya wao.”

Ifahamike kuwa Chameleone mwenye umri wa miaka 40 ni mwendelezo wa wimbi la wasanii waliouvamia ulingo wa siasa katika miaka ya hivi karibuni.

Miezi miwili iliyopita, Ukraine ilishuhudia mwigizaji Volodymyr Zelensky (41) akiukwaa urais, tena kwa kishindo, akizoa asilimia zaidi ya 70 dhidi ya kiongozi aliyemaliza muda wake, Petro Poroshenko, aliyeambulia asilimia 24 pekee.

Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati nao umewahi kuwashuhudia wasanii wengi wakifanya hivyo, ikitosha kuwataja Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’, Joseph Haule ‘Prof. Jay’ na Joseph Mbilinyi ‘Mr. Sugu’.

Tafiti zimebaini kuwa ushiriki wa vijana katika kuziwania nafasi mbalimbali umeongezekea, sababu kubwa ikiwa ni wengi wao kutoridhishwa na mambo yanavyokwenda chini ya serikali zao.

Mfano mzuri katika hilo ni kile kilichotokea katika Uchaguzi Mkuu wa Nigeria uliofanyika mapema mwaka huu, ambapo tarkibani vijana 18 walijitokeza kuitaka fomu ya urais, wakiwamo Chike Ukaegbu (35), Eunice Atuejide (39) na Adamu Garba (35).

Aidha, bado changamoto ya rasilimali fedha na kutoaminiwa kwa upande mwingine zimekuwa zikitajwa kuwa sababu za vijana wengi kubaki nyuma linapokuja suala la kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi.

Juu ya kilichomvuta Chameleone kujitosa ulingoni safari hii, Chameleone alisema ni kuzorota kwa huduma za serikali kwa jamii. Baada ya kuanika kuwa atajiunga na upinzani, Democratic Party (DP), ukweli ni kwamba ameongeza presha kubwa kwa Rais Museven wa chama tawala, National Resistance Movement (NRM).

Ikumbukwe kuwa Rais Museven anajiandaa kugombea tena katika Uchaguzi Mkuu ujao baada ya kufanikisha mabadiliko ya Katiba yaliyoondosha kipengele cha ukomo wa umri.

Awali, Katiba ya Uganda ilitamka wazi kuwa ukomo wa kiti cha urais ni miaka 75, hivyo ilimweka kando Rais Museven (73) katika uchaguzi ujao, kabla ya Mahakama ya Katiba kumpa ushindi.

Tukirejea kwa Chameleone, kwa muda mrefu amekuwa na uhusiano mzuri na Rais Museven. Hata kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2016, alikutana na Rais Museven katika kuandaa mpango wa kampeni.

Chanzo kilichokuwa katika kikao hicho kilisema mwanamuziki huyo aliahidi kumuunga mkono Rais Museven na NRM katika uchaguzi huo.

Kampeni zilipoanza, ikikumbuka kuwa Bob Wine aligomea, Chameleone aliwaongoza wasanii wengine kutumbuiza katika kila jukwaa kwa lengo la kumnadi Rais Museven.

Ni kipindi ambacho baadhi ya mashabiki wa mwimbaji huyo waligomea matamasha yake kuonesha kukerwa kwao na ushiriki wake katika kampeni hizo.

Lakini sasa, uadui kati ya Rais Museven na Chameleone ulianza ghafla wiki iliyopita, siku chache baada ya msanii huyo kutangaza nia ya kuingia katika siasa.

Katika kile ambacho hakikutarajiwa na wengi, Rais Museveni aliacha ‘kum-follow’ msanii huyo kwenye mtandao wa kijamii wa twitter, ikionesha kuwa ni mwanzo wa kupotea kwa ukaribu wao kutokana na mgongano wa masilahi ya kisiasa.

Kabla ya hapo, Chameleone alikuwa mmoja kati ya watu 24 tu ambao Rais Museven alikuwa ‘amewa-follow’, mwingine akiwa ni msanii mwingine, Bebe Cool waliyekuwa naye katika kampeni za uchaguzi uliopita.

Aidha, hilo la Chameleone linakuja huku bado kiongozi huyo aliyekaa madarakani kwa miaka 33 akiumizwa kichwa na mwanasiasa mwingine kijana, Bob Wine.

Bobi Wine amekuwa kaa la moto kwa Rais Museven, akiwataka wananchi wa Uganda kutumia mfano ya kilichotokea Sudan na Algeria kuwaondoka marais waliokuwa wamekaa madarakani kwa muda mrefu.

Ikiwa ni miaka miwili tu tangu alipotia mguu katika siasa za upinzani chini Uganda, Bobi Wine amejikuta akiandamwa na mkono wa Serikali ya Rais Museven.

Kutokana na msukumo mkubwa alionao kwa vijana, imeshuhudiwa mara kadhaa Rais Museven akitumia vyombo vya dola kumpa kashikashi mbunge huyo, sambamba na mwenzake wa upinzani, Dk. Kizza Besigye.

Moja kati ya matukio ya kushitua ni dereva wake, Yasiin Kawuma, kuuawa kwa risasi, ukiacha lile la mwanasiasa huyo kupigwa na kisha kwenda Marekani kwa matibabu.

Kauli ya hivi karibuni ya Rais Museven, kwamba mwanamuziki anatakiwa kwenda klabu za usiku kuimba na kunengua, inatajwa kuwa ni dalili kiongozi huyo kusumbuliwa na nguvu aliyonayo Bob Wine katika siasa za Uganda.

Ni wazi rais huyo amesahau kuwa si wanamuziki pekee waliovamia jukwaa la siasa bali hata viongozi waliopo madarakani wana taaluma zao zingine, mfano mzuri akiwa ni Meya wa Kampala, Erias Lukwago, ambaye ni mwanasheria.

Bahati mbaya kwake ni kwamba wakati akiwa hajafanikiwa kumzima Bob Wine, anaibuka Chameleone, ambaye wengi hawaoni kama anatofautiana sana na Bob Wine linapokuja suala la ushawishi.

Kulithibitisha hilo, katika moja ya mahojiano yake ya hivi karibuni, Chameleone alifichua kuwa vijana wa bodaboda wamekuwa wakimtaka kugombea kila anapokutana nao. “Nataka kuwa na mchango kama ambavyo Bobi Wine amefanya,” alisisitiza.

Kutokana na kazi yao ya muziki, Chameleone akiifanya kwa miaka 20 sasa, ameingia katika siasa akiwa amejikusanyia mtaji mkubwa wa nguvu ya ushawishi mbele ya vijana, ambao kimsingi ndiyo waliombeba Bob Wine kuingia bungeni mwaka 2016.

Ieleweke kuwa vijana ni asilimia zaidi ya 70 ya wananchi wote wa Uganda, likitajwa kuwa ndilo taifa lenye idadi kubwa ya wananchi wenye umri mdogo.

Wakiwa ndiyo wengi zaidi, bado vijana hao hawaoni umuhimu wa Serikali ya Rais Museven kwa kuwa kama ilivyo katika mataifa mengi ya Afrika, wengi wao wanashinda vijiweni wakiwa hawana kazi, fursa za kiuchumi zikishikiliwa na wachache.

Hivyo, haikushangaza kwa Bobi Wine kushinda kiti cha ubunge wa Kyadondo Mashariki katika Uchaguzi Mkuu uliopita akiwa mgombea binafsi mbele ya washindani kutoka NRM na Chama cha Forum for Democratic Change (FDC).

Wakimtazama Bobi Wine, kama itakavyokuwa kwa Chameleone, wanawaona kuwa ni wenzao na watakazipa kipaumbele changamoto zilizoshindwa na uongozi wa Rais Museven kwa miaka mingi aliyokaa madarakani.

Hata hivyo, kwa uamuzi wake wa kwenda upinzani, Chameleone anatazamiwa kukumbana na makali ya Rais Museven katika ulingo wa siasa. Ni kama alivyosema Mwenyekiti wa NRM Mashariki mwa Uganda, Mike Mukula, ambaye amemuonya Chameleone akimtaka kuwa makini na siasa.

“Ushahuri wangu kwa rafiki yangu kipenzi, Chameleon, aende taratibu na siasa. Itakutia umasikini na itapoteza kabisa kipaji chako cha muziki. Usije kusema sikukushahuri,” alisema.

Dhidi ya Rais Museven, Chameleone anakutana na mwanasiasa ambaye miaka 23 iliyopita alisema Afrika haiendelei kwa kuwa viongozi wake wanang’ang’ania madaraka. Ukija kwa upande wake, ameshaongoza kwa zaidi ya miongo mitatu.

Ni kiongozi ambaye mwaka 2014, wanasiasa wa upinzani nchini Uganda walimuonya, wakimwambia akiendelea kutumia nguvu kubwa ya vyombo vya dola, basi nao wataingia msituni.

Bobi Wine amewahi kukiri kuwa anapitia wakati mgumu chini ya upinzani dhidi yake, ikiwamo kiongozi huyo na watu wake kupanga kummaliza kiuchumi.

“Wanataka niwe na hali ngumu ya kiuchumi,” alisema Bob Wine akiongeza kuwa baadhi ya aliokuwa akifanya nao kazi ya muziki wamepigwa marufu kushirikiana naye.

“Viongozi wa serikali ya Uganda wamekuwa wakijaribu kuitangaza picha ya nchi hii kuwa ni yenye demokrasia,” alisema Bobi Wine na kuongeza: “Kwa miaka mingi, haki za watu zimekuwa zikipuuzwa, watu wamekuwa wakiteswa na wengi kuuliwa.”

Tangu alipoanza rasmi kazi ya uwakilishi wa wananchi wake bungeni mwaka juzi, matamasha yake zaidi ya 120 yamefutwa, pigo ambalo huenda likamkuta Chameleone, ambaye ameweka wazi mpango wake wa kuendelea na muziki hata baada ya kuwa Meya.

Licha ya Chameleone kusema hajaingia katika siasa kwa ajili ya kuwa kiongozi wa uhasimu dhidi ya serikali au kumtukana rais, kauli yake ya awali, kuwa amejitosa baada ya kuona huduma za serikali zimedorora, inaweza kuonekana ni ukosoaji wa uongozi wa Rais Museven.

Je, ni wakati wa Chameleone naye kupitia tanuri la moto kama inavyomtokea rafiki yake katika soko la muziki, Bobi Wine? Ni kwamba ameingia katika orodha ya wanasiasa wengi wa upinzani barani Afrika wanaopishana vituo vya polisi kila uchwao?tusubiri tuone.