Home Afrika Mashariki Suluhu mgogoro wa Burundi ipatikane haraka kuepusha mauaji ya kimbari 

Suluhu mgogoro wa Burundi ipatikane haraka kuepusha mauaji ya kimbari 

5697
0
SHARE


HILAL K SUED

Mgogoro wa kisiasa unaoendelea Burundi usipodhibitiwa kwa haraka unaweza ukazua machafuko makubwa nchini humo – na hata mauaji ya kimbari kama vile ya nchi jirani yake ya Rwanda ya mwaka 1994 ambapo zaidi ya watu 800,000 wa kabila la Watutsi waliuawa na wanamgambo wa Kihutu.

Ikumbukwe kwamba katika nchi zote hizo mbili watu wa kabila la Kihutu ni wengi – asilimia 85 na Watusi ni chini ya asilimia 15.

Viungo vikuu vya janga hilo kutokea nchini Burundi siyo vipo tu, bali pia vinazidi kurutubishwa, kama vile ilivyokuwa kwa Rwanda miaka 25 nyuma. Isitoshe kuna mauaji ya kimbari yaliyowahi kutokea nchini Burundi – hasa yale ya 1972 ambapo maelfu ya Wahutu waliuawa na wanamgambo wa Kitusi.

Wakati huo ilikuwa ni miaka 12 baada ya nchi hiyo kujipatia uhuru. Mauaji haya hayakupata kuzungumzwa sana au hata kulaniwa sana kama yale ya Rwanda ya 1994 kwa sababu nchi za nje na jumuiya za kimataifa zilikuwa bado hazina mwamko wa masuala ya mauaji ya kimbari hususan katika Bara la Afrika.

Sababu nyingine ni kwamba utawala ulioingia madarakani kule Rwanda baada ya mauaji yale ulikuwa wa Kitutsi ambao ndiyo walikuwa wahanga hivyo serikali hiyo iliyatangaza kwa nguvu zote hayo mauaji kuonyesha ubaya wake na pia kupata huruma na kukubalika kwa utawala mpya. Ni tofauti na ilivyokuwa kwa Burundi ambapo “wauaji” (Watutsi) waliendelea kushika serikali kwa zaidi ya miongo miwili baadaye.

Lakini safari hii kuna uwezekano mkubwa kabila litakaloathirika huko Burundi iwapo mauaji yatatokea ni Watutsi – kama ilivyokuwa kwa Rwanda mwaka 1994.

Wakoloni wa Kibelgiji waliziacha nchi mbili hizi na tawala za makabila mawili tofauti – Rwanda iliongozwa na serikali ya Wahutu (walio wengi) chini ya Rais Gregoire Kayibanda, na Burundi iliongozwa na utawala wa kifalme wa Kitusi chini ya Mwami (mfalme) Mwambutsa V. Lakini baada ya matukio kadha ya mapinduzi na mauaji ya viongozi wake utawala wa jamhuri chini ya chama kimoja (UPRONA) ulianzishwa chini ya mwanajeshi kapteni Michel Micombero, Mtusi.

Mauaji ya viongozi wa Kitusi yaliyokuwa yanapangwa na Wahutu yalisababisha malipizo kisasi uliofanywa na Watusi wakisaidiwa na jeshi la nchi hiyo lilikuwa likiongozwa na hao hao Watusi – na hali ilikuwa mbaya mwaka 1972 ambapo yalitokea hayo mauaji ya maelfu ya Wahutu, na wengi kukimbilia nchi jirani ikiwemo Tanzania.

Kuanzia hapo Burundi haikuwa imetulia kabisa hadi amani halisi ilipokuja kupatikana mwaka 2005, na hapo ni baada ya miaka 12 ya vita ya wenyewe kwa wenyewe baina ya waasi wa Kihutu dhidi ya msururu wa serikali za kijeshi zilizokuwa zikiongozwa na Watusi. Mwaka huo ndiyo aliapishwa Pierre Nkurunziza (Mhutu) baada ya iliyokuwa serikali ya mpito – na hivyo ikawa ndiyo mwisho kabisa ya utawala wa Kitusi uliodumu takriban tangu uhuru.

Sasa haidhaniwi kabisa iwapo Watusi, pamoja na uchache wao, watakuwa wameridhika, na suala hili la ukabila ndiyo kiini kikubwa cha migogoro ya nchi zote hizo mbili, Burundi na Rwanda.

Rwanda, baada ya mauaji ya kimbari ya Watusi na kuingia utawala wa Paul Kagame (Mtusi) imejaribu sana kuondoa ukabila kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine demokrasia halisi imekuwa ikibanwa. Nyenzo yake kubwa ni kukumbushia ubaya wa mauaji ya kimbari. Kagame anajua fika kwamba akiachia demokrasia ichukuwe mkondo wake na kufanya uchaguzi ulio huru kabisa – uwezekano mkubwa ni kwa serikali ya Kihutu kuingia madarakani. Kama ilivyo kwa Burundi hivi sasa.

Hilo ni suala ambalo Kagame mwenyewe linamtia hofu, na serikali ya Nkurunziza katu haisiti kutamka kwamba Kagame anaweka mkono wake katika kuchochea mgogoro – bila shaka akiwa na nia ya kuwasaidia Watutsi. Mgogoro huu wa sasa wa Burundi umeanzia mwaka 2015 baada ya Nkurunziza kuamua kuendelea kujipa muhula wa tatu kinyume cha makubaliano ya Arusha ya mwaka 1998.

Wiki mbili zilizopita msuluhishi wa mgogoro wa Burundi, rais wa zamani Benjamin Mkapa alijitoa kutoka jukumu hilo alilokuwa amekabidhiwa na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) miaka minne iliyopita.

Mkapa alitangaza uamuzi huu wa kusikitisha, ingawa si wa kushangaza mbele ya kikao cha wakuu wa Jumuiya hiyo mjini Arusha kwa kusema utawala wa Burundi umeshindwa kuonyesha udhati wake katika mchakato huo na kwamba mara kadha umekuwa ukisusia vikao vya mazungumzo kati yake na wapinzani alivyokuwa akiviitisha.

Kwa mfano, utawala wa Pierre Nkurunziza uliendelea na mchakato wake wa kura ya maoni ambayo ilikuja kuondoa ukomo wa vipindi vya urais na pia kuongeza urefu wa vipindi kutoka miaka mitano hadi saba bila ya kushauriana na msuluhishi huyo.

Aidha alisema pale ambapo vikao vilikuwa vimepanga mazungumzo muhimu, serikali ya Burundi ilikuwa inatuma wawakilishi wa hadhi ya chini waliokosa mamlaka kamili ya kukubaliana na maamuzi mazito ya mazungumzo.

Hivyo katika kikao hicho cha wakuu wa EAC Mkapa alilisalimisha jukumu la usuluhishi wa mgogoro wa Burundi kwa ‘Msuluhishi Mkuu’ wa suala hilo zima – Rais Yoweri Miuseveni wa Uganda, ambaye naye alijaribu kumpasia Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye alillikataa jukumu hilo. Matokeo ni kwamba sasa hivi mgogoro huo umekuwa mgumu zaidi kwani tayari umebebeshwa ushawishi mkubwa kutoka nje.

Rais Pierre Nkurunziza anasema kwamba suala la kura ya maoni ya 2018 ya kubadilisha katiba na kuondoa ukomo wa rais lilitokana na uamuzi wa wananchi wa Burundi na lilikuwa halikinzani na ule Mkataba Mkuu wa amani wa 1998, msimamo ambao Mkapa alikuwa hakubaliani nao.

Lakini kikubwa zaidi ni kwamba kuondoka kwa Mkapa katika usuluhishi kumeondoa kabisa matumaini ya kupoatikana kwa suluhu, na inaweza kutoa mwanya kwa vikundi vya misimamo mikali kujiingiza na kuzua ghasia – kwani Burundi inayo sana histora ya aina hiyo – ukiachilia mbali eneo la jirani ambalo kwa miaka kadha limekuwa na migogoro – kama vile congo DRC.

Aidha suala la ombi la serikali ya Burundi la kuwepo kwa mazungumzo na Rwanda inayoituhumu kuingia na kuchochea mambo yake ya ndani ni vyema likaangaliwa pia, haidhuru katika lengo la kulimaliza suala ili Burundi isiwe na visingizio vingine vya kuyapa mgongo mazungumzo makuu ya kuleta uweleano nchini humo.