Home Latest News Tambo za kampeni hufutwa na kiapo

Tambo za kampeni hufutwa na kiapo

2093
0
SHARE

NA MWANDISHI  WETU

BAADA ya matokeo ya uchaguzi kutolewa na wagombea wa nafasi mbalimbali kutangazwa moja ya taswira ambayo wapiga kura au watu walioshuhudia jinsi kampeni zilivyokuwa zikiendeshwa lazima ataibuka na maneno kuwa zilijaa tambo nyingi.

Neno tambo linamaanisha ufumbaji wa jambo au kitu kusudi upatikane ufumbuzi wake. Katika ufumbaji huo ndani ya kampeni lengo kubwa lilikuwa ni kutafuta ufumbuzi wa kuchaguliwa katika nafasi ya kuongoza katika kiti kimojawapo cha Udiwani, Ubunge na Urais.

Kwa maana nyingine ni kwamba tambo nyingi zilizokuwa zinatumika kushawishi wapiga kura kuunga mkono upande mmoja  na waupe  kisogo upande wa pili.

Kimsingi tambo zilitumika kuzinadi sera na kuonesha ubora wa sera moja dhidi ya sera nyingine na wapiga kura waliweza kuingia kwenye zoezi la kupiga kura wakiwa na mwangwi wa tambo zenyewe na hususani sauti ya waliozitoa tayari kuwapigia kura.

Wakati tambo hizo zikitolewa wahusika walikuwa kama watoto wanaoomba mahitaji yao kwa wazazi kwa unyenyekevu licha ya kwamba wakati mwingine walikuwa wakiingiwa na mhemuko katika kusisitia kile walichokuwa wanakiomba.

Haiyumkini wapiga kura nao waliingiwa na mhemuko hususani pale walipokuwa wanazikubali na kuzishangilia tambo zenyewe na hali hiyo pia huenda ilikuwepo kwa wafuasi na wanachama wa vyama vya watoa tambo.

Kama tambo zingekuwa zinarejewa kwa wengine inaweza kuwa vigumu kuzirejea kwa sababu ule mshawasha wa kuomba na kunyenyekea ulishatoweshwa na matokeo ya zoezi zima.

Baada ya hali kama hiyo utapita nusu muongo ndipo tambo zitasikika tena na unyenyekevu kurudi licha ya kwamba unyenyekevu unakuwa ni jambo endelevu kuna sehemu ambapo wanyenyekevu hukengeuka  lakini kwa wanaojielewa  hurudi katika mstari kwa kuwa hurejea kanuni za dhamana walizopewa na wapiga kura.

Kilichofanya tambo kufika ukomo ni  matokeo na kubwa zaidi ni kuapishwa kwa viongozi waliobahatika na ambao tambo zao zilikubalika na kupokelewa kwa mikono miwili na wapiga kura.

Taswira ya hali hiyo ni yale yaliyoelezwa baada ya  kuapishwa na Mkuu wa Kaya  kwamba ‘Uchaguzi Umekwisha, Uchaguzi Umekwisha, Uchaguzi Umekwisha’ na maneno hayo ndiyo yaliyofikisha ukomo tambo za uchaguzi.

Kimsingi kauli hiyo ilikuwa inamaanisha kuwa ni nafasi kwa waliochaguliwa kwenda kuziishi tambo walizokuwa wanazitema kwa kufumbua mambo yatakayowezesha kupatikana kwa maendeleo ya jamii.

Miongoni mwa tambo ambazo zilikuwa zinafikirisha ni ile ya ‘msiponiletea hao watatu mtakuwa mnakwama katika harakati za maendeleo’  ambayo kimsingi ni ushawishi uliolenga kuwapata  wagombea watatu.

Inakuwa sahihi kusema kuwa ni ushawishi kwani kiapo kilifuta tambo hiyo kwa kuwa  Mkuu wa Kaya alisikika akiapa  kuwatumikia watu wote bila ubaguzi na kuhitimisha kwa kuomba Mungu awe mbele katika utendaji wake wa kazi.

Hali hiyo katika ulimwengu wa siasa ilikuwa ni kuzingatia dhana nzima ya demokrasia kwani hakuna demokrasia ya wazi isiyoangalia na kuzingatia mazingira ya kiutamaduni, kihistoria na kijamii.

Upo mfano kwenye  sera za maendeleo za nchi wahisani ambazo zinataka kuhakikisha kuwa watu na makundi ya watu yanaishi kwa uhuru na heshima, wanaweza kuzifikia haki zao na maslahi yao na kusimamia maisha waliyojipangia wao wenyewe.

Katika mazingira ya aina hiyo ndipo kila mmoja anaweza kuonesha ujuzi na ujuvi wake katika kuchangia maendeleo binafsi na maendeleo ya jamii.

Misingi ya kidemokrasia ambayo imekita mizizi yake katika ngazi zote za jamii hutumika na kuzingatiwa kama msingi imara wa maendeleo.

Uhalisia wa mambo upo katika Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya mwaka 2002, ambayo ilisisitiza kwamba  demokrasia ni njia nzuri ya  kufikia maendeleo endelevu ya binadamu na kuongeza kuwa ushirikishwaji ni lengo la maendeleo na si tu namna ya kufikia maendeleo hayo.

Demokrasia  inaweza kuchukua maumbo tofauti lakini kigezo fulani muhimu zaidi kinaweza kutumiwa kwa mifumo yote ya demokrasia kama vile mgawanyo wa madaraka na ulinzi kwa makundi madogo ya jamii.

Vigezo vingine ni pamoja na haki za binadamu, uwezo wa kutoa ushawishi kwa maamuzi ya serikali nje ya hatua za uchaguzi, uhuru wa vyombo vya habari na utawala wa sheria.

Katika mazingira ya aina hiyo utawala wa sheria na usalama kisheria hutoa mchango mkubwa kwenye  maendeleo endelevu ya kiuchumi kwa nchi.

Kwa mfano kampuni huwekeza tu kwenye soko la nchi za nje kama zinaweza kuegemea kwenye uimara wa sheria na kuelewa kuwa fedha zake zimewekezwa katika sehemu iliyo na usalama.

Hali kadhalika misingi hiyo huchukuliwa kulinda wananchi, usalama kisheria na utawala wa sheria na uhuru kwa maendeleo ya mtu binafsi kwa pamoja huchangia maendeleo ya amani ya jamii na kupunguza rushwa.

Demokrasia na maendeleo yanaweza kuwa endelevu kwa jamii ambayo haina woga wa kujieleza na ambayo imewezeshwa vya kutosha katika kuhakikisha kuwa maslahi yake yenyewe ni sehemu ya michakato ya kisiasa.

Mijadala ya kitaifa ambayo ni muhimu kwa mageuzi ya kidemokrasia inaweza kutumika kwenye miundo isiyo rasmi na ikawa ndio njia ya kukuza demokrasia.

Katika dhana nzima ya kuleta maendeleo kwa jamii  wawakilishi wa jamii wanatakiwa kuondokana na tofauti za kisiasa na kufahamu kuwa uwakilishi wao ni dhamana ya utumishi waliyopewa na wanatakiwa waiishi.

Kinachosikitisha ni kujengeka kwa dhana za kiitikadi ambapo baadhi ya wawakilishi kusahau kuwa suala la maendeleo si la kiitikadi bali ni la umma bila kujali itikadi zao za kisiasa.  Kukiuka hili ni sawa na kujirudisha kwenye tambo wakati uchaguzi umeshakwisha.

Matarajio ya umma ni kuona kuwa kanuni au misingi ya kupata maendeleo inasimamiwa kwa  kuzingatia utii na utaratibu kwani ufanisi katika maendeleo  suala kongwe katika siasa za nchi na ufafanuzi wake umo katika baadhi ya marejeo ya viongozi waliotangulia.

Mfano hai upo na hususani kutoka kwa  Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye Kitabu cha Maongozi.

 Anafafanua, “Lazima pawepo na utii na utaratibu katika mambo yote ya maisha yetu. Na hauna budi uwe ni utii unaokinai; yaani  unakubalika kwa hiari; maana ni sehemu  muhimu ya uhuru na maendeleo…yote hayawezekani bila  ya kufuata  utii na utaratibu wa kutimiza uamuzi uliokubaliwa.

“Lakini utii ni njia ya kutimiza  uamuzi. Tunapodai utii katika mazungumzo ni kwa sababu ya kusaidia  mazungumzo yaendeshwe vizuri na kwa utaratibu. Utii tunaousema  hapa na kushurutisha ni mambo mawili mbalimbali.

“Wakati wa majadiliano ni lazima kufuata utaratibu ili kupata  uamuzi. Kama tunataka kila mtu apate nafasi ya kusikilizwa, lazima uwepo utii na utaratibu. Lakini mkutano ambao kila mtu anakubali tu kila wazo linalotolewa si mkutano wenye utaratibu.

“Mkutano wenye utaratibu ni ule ambao sheria za mkutano zilizokubaliwa kuwa ni za haki zinafuatwa na kila mmoja kwa hiyari.

“Kwa mfano kila mtu anasema kwa ruhusa ya mwenyekiti; na kila mtu anaruhusiwa kutoa mawazo yake bila ya kuzomewa au kutukanwa. Maana utaratibu ndiyo unaofanya mambo yakaenda vizuri; ndiyo njia ya kutimiza uamuzi siyo njia ya kuufanya uamuzi wenyewe.”

Katika mazingira hayo ni dhahiri kile kinachofanywa kwa utii na utaratibu lazima kitafikia mwafaka mwema  utawaridhisha watu wote licha ya kwamba watakuwa wanatofautiana kiitikadi lakini ni kwa manufaa ya jamii yote.

Katika hilo Mwalimu Nyerere katika kitabu hicho alisema, “Maendeleo ni yetu  na ni juu yetu wenyewe; na maendeleo tunayoyataka ni maendeleo ya watu; yaletwe na watu; yaendeleze watu; yawafae watu.”

Katika hali yoyote ile  wapiga kura waliokuwa wakilishwa tambo na wakaingia katika mkondo mnyoofu wa mpiga tambo na kujenga imani ambayo ikileta ufanisi wanakuwa wamejitenga na  kujiondoa katika mkondo ambao Profesa PLO Lumumba   alisema ni kujigeuza, “Waandishi wa majanga yetu wenyewe…Tunachagua fisi  kuwachunga mbuzi …pindi  wanapoliwa tunashangaa ni  kwanini.”

Kwa vyo vyote vile jambo la kufuatilia  linabakia kwamba je, viapo vilivyofuta tambo walioviapa wanaviishi.