Home Uchambuzi TATIZO LA AJIRA LINAKUZWA NA MFUMO WA MITAALA MIBOVU

TATIZO LA AJIRA LINAKUZWA NA MFUMO WA MITAALA MIBOVU

3174
0
SHARE

WIKI iliyopita kuna sms imejirudia mara nyingi kwenye simu yangu ilikuwa ni tangazo la kuhusu vijana wa CCM waliomaliza vyuo vikuu kupeleka CV zao pale Lumumba.

Binafsi nikiri kabisa kuwa sijui wanaohitaji vijana hao wanataka kwenda kuwaajiri au kuwafanyia jambo gani ila nimechukua tangazo lile kama agenda yangu ya leo kuhusu tatizo la ajira linavyowatesa vijana wengi Tanzania.

Najua mateso wanayoyapata vijana kwa kukosa ajira uwe umesoma au hukusoma kukaa mtaani tu bila kazi ni adhabu tosha. Na ndio maana kila siku nimekuwa nikilisemea hili.

Tanzania kila penye vijana 10 saba wanakuwa hawana ajira kabisa kwa hiyo tukakaribia kufikia asilimia 70 ya ukosefu wa ajira nchini hasa kwa kundi la vijana ambao ndio waathirika wakuu.

Kwa Taarifa ya shirika la kazi duniani ya mwelekeo wa ajira kwa vijana ulimwenguni [GrobaL employment trend for youth] inaonesha kuwa tatizo la ajira kwa vijana Tanzania wenye elimu kuanzia sekondari na kuendelea ni kubwa kuliko wale wenye elimu ya kiwango cha chini. Aidha watanzania wenye elimu za chini wamepata ajira lakini ajira zao ni duni ama kipato cha chini na za mazingira hatarishi kama sehemu mojawapo ya kuwatumikisha kwa kuwa uelewa wao juu ya masuala sheria na taratibu za kazi ni mdogo.

Zaidi ya wahitimu 80,000 huhitimu elimu ya juu kila mwaka. Katika kundi kubwa kama hili kwa hali ya ajira ilivyo sasa hivi nchini ni asilimia 12 tu ya vijana hawa wenye uhakika wa kupata ajira. Zaidi ya asilimia 88 ya wahitimu wa vyuo vikuu huzagaa mitaani bila kazi yoyote inayoweza kichangia pato la Taifa.

Waziri Jenister Mhagama mwaka jana mwanzoni alisema asilimia 71 ya watanzania hufanya kazi zisizochangia pato la taifa kabisa. Yaani hawa wanafanya kazi ya kujikimu tu apate mlo wake ili kesho ifike maisha yaendelee.

Pamoja na Tanzania kujitapa kuwa kinara wa sera za maendeleo ila bado hawajaweza kuandaa soko la ajira kwa vijana wanaohitimi katika ngazi mbalimbali za elimu. Ni aibu kwa mhitimu wa chuo kikuu kwenda kupigania abiria kwenye vijiwe vya bodaboda. Nasema hivi kwa kuwa hii nayo si ajira rasmi na ni ajira ya Muda tu na hatarishi kwao. Kuna umri utafika ataona aibu kuendesha bodaboda hizi na ni hatari sana kama taifa kukubali nguvu kazi hii ya vijana kukimbilia wote kwenye bodaboda.

Lazma tukubali kuwa kilichotufikisha hapa ni aina ya elimu tunayoipata kutoka mashuleni. Hatua ya kwanza ya kulitatua tatizo hili ni kugusa mitaala yetu kwanza. Bado ipo kikoloni ndio maana kila kijana anawaza kuajiriwa zaidi kuliko kujiajiri na hili sio kosa lao. Yaani hakuna kitu tunachokiogopa kama mitaala yetu ya elimu….

Tunajifunza mambo mengi shuleni ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja na mazingira yetu. Niliwahi kusema kuwa kwa nini mfano tusikubali kuingiza masomo ya ufundi kwenye shule zetu zote za sekondari kutegemeana na mazingira shule ilipo? Cha ajabu hata zile zinazotoa fani za ufundi kwa sasa zipo taabani nendeni kwenye shule hizo mkaulize wangapi wanasomea masomo hayo ya ufundi.

Kwa nini tusikubali kubadili lugha yetu ya kujifunzia shuleni? Ni jambo la kushangaza mwanafunzi katika miaka saba anapokuwa shule ya msingi kusoma kwa kiswahili halafu akitoka hapo anaenda kusoma kwa lugha nyingine ya kiingereza. Wanafunzi wengi sekondari wanakariri tu badala ya kujifunza. Kwa nini tusiamue kutumia Kiingereza kuanzia msingi hadi sekondari?

Tunasema vijana wajiajiri ila tulishawahi kujiuliza wanajiajirije? Hiyo mikopo wanaipataje? Si mnajua masharti magumu ya benki zetu hapa nchini? Benki hawakupi fedha bila kuwa na asset ya kuweka kama bondi hawa vijana wana asset gani? Ni kijana yupi mwenye hati ya nyumba au kiwanja?

Ni kijana yupi anayejua mfuko wa vijana uliopo kwenye jimbo lake una shilingi ngapi? Au nani aliwahi kunufaika nao?… Any way tusubiri 2020 tuendelee kudeki barabara wanasiasa wapite.