Home Latest News TRAWU: SERIKALI ISIPUUZE MADAI YA WAFANYAKAZI WA RELI

TRAWU: SERIKALI ISIPUUZE MADAI YA WAFANYAKAZI WA RELI

1439
0
SHARE
Baadhi ya wafanyakazi wa reli wakiwa kwenye mkutano

NA FARAJA MASINDE,

KUMEKUWA na mtazamo hasi ambao umekuwa ukijengeka kuwa sekta ya usafiri kwa njia ya reli si salama jambo ambalo halina tija yeyote.

Hali hiyo imekuwa ikichangia serikali kushindwa kuweka jitihada za makusudi kwenye sekta hii ya reli katika kuhakikisha kuwa inaimarika.

Anguka hilo ndilo limekuwa likiifanya Serikali kuanzisha jitihada za kufufua usafiri huo ili kurejesha imani ya watanzania wakiwamo wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiukacha usafiri huo na kutumia wa barabara na hata anga kulingana na kutokuwapo kwa uhakika wa usafiri huo.

Hata hivyo kusuasua kwa usafiri huo kumekuwa na mfululizo wa mambo mengi ikiwamo pia wafanyakazi wa sekta ya reli kutokupata stahiki zao kwa wakati jambo ambalo lilikuwa likizorotesha uimarikaji wa sekta hiyo kama anavyobainisha, Shehe Shuhuli ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha wafanyakazi wa Reli Kanda ya Dar es Salaam(TRAWU).

Anasema sekta hiyo imepitia kipindi cha mpito ambacho mapato yalikuwa hayaendani na matumizi wamekubaliana kuhakikisha kuwa watumishi wanaostaafu wanapatiwa mafao yao mapema.

Anabainisha sekta ya reli ambayo ni nyeti ni muhimili wa uchumi wa nchi na itaweza kuwafikia wananchi wote kwa bei rahisi na kwa haraka zaidi.

“Hii ndiyo sekta pekee itakayoweza kusafirisha mizigo kwa bei rahisi ili kuwafikia walaji katika kuhakikisha kuwa uchumi nchini unaimarika, hivyo ni wazi kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kiwango cha reli ya kisasa ‘Standard Gauge’ kwani kama treni hiyo itaweza kukimbia kwa kilometa 160 kwa saa tuna uhakika kuwa kwa muda wa saa 10 itakuwa imefika Mwanza jambo ambalo litakuwa limerahisisha mizigo kufika kwa haraka.

“Hivyo wananchi walio wengi watakimbilia kwenye sekta ya reli huku wafanyakazi nao wakifaidika kutokana na kipato kitakachokuwa kinapatikana kulingana na uzalishaji wa wakati huo. Pia watafaidifika kwa kiasi kikubwa kwani ni sekta ambayo katika kupindi cha miaka mitano ijayo itakuwa imebadilika sana,”anasema Shuhuli.

Anaendelea kubainisha kuwa jitihada zao za kuhakikisha kuwa kiongozi anatoka nje ya mamlaka hiyo zimekuwa na tija  na manufaa kwa kiasi cha kurejesha mwamko wa sekta hiyo.

“Unajua awali serikali ilikuwa ikiona kama wafanyakazi wa reli kama watu wakorofi licha ya kwamba walikuwa wakifanya kazi ya kuikumbusha mara kwa kwa mara mambo ambayo inapaswa kufanya jambo ambalo ilitii na kutuletea kiongozi mpya ambaye ni kutoka kwenye sekta ya benki na tumempa ushirikiano wa asilimia 100 ni wazi kuwa mwanga kwa sasa tunauona kwani jitihada za kulipa madeni yote yaliyokuwapo awali  zimeanza kuonekana ikiwamo ya mifuko ya hifadhi za jamii.

“Pia mbali na madeni hayo tumekuwa tukimshauri kulipa madai ya wafanyakazi ambayo hayajalipwa kwa muda mrefu kwani mara nyingi madai yetu yamekuwa yakilipwa kwa mgogoro jambo ambalo analifanyia kazi. Lakini pia kazi yetu ni kuhakikisha kuwa tunawasimamia wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii ili kuinua na kuimarisha sekta hii ya reli japo kuna haja ya serikali kuhakikisha kuwa sisi tunakuwa washiriki wakuu wa kuuza rasilimali kama kokoto na rasilimali nyingine zote  ili hiyo fedha isiende nje ya nchi ikiwamo pia kujenga kiwanda kidogo cha mataluma ya reli,” anasema Shuhuli.

Anabainisha kuwa uwepo wa kiwanda hicho kutafanya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kuuzwa tena kwa wageni watakaoshinda zabuni ya ujenzi wa reli ya kisasa ambayo itasaidia kurejesha mapato hayo ndani  ambapo anasema kuwa itakuwa na faida kubwa kwa Taifa na wafanyakazi kwa ujumla kutokana na kupanda kwa mishahara yao kama wafanyakazi wa reli ambao ndiyo uti wa mgongo wa nchi hii.

“Mpaka sasa chama chetu kinajumla ya wafanyakazi zaidi ya 4,000  ambapo kwa upande wa Tazara  bado kuna changamoto kwenye upande wa idara ya masoko ambayo imekuwa haifanyi kazi sawasawa lakini pia kukosekana kwa vitendea kazi na uhaba wa mabehewa ni baadhi ya mambo yanayoikwamisha, kwa sababu   tunauhakika wa kupata mizigo mikubwa kwa sasa kutokana na kuimarika kwa bandari.

“Pia kuna marekebisho kwenye upande wa sheria na vitendea kazi kwani mzigo unaosafirishwa sasahivi hata asilimia moja haifiki kwa mwaka jambo ambalo ni hatari hivyo ni bora vitu kama ‘scanner’ na vitu vyote muhimu vinavyohitajika katika kuhakikisha kuwa eneo la usafirishaji kwa njia ya reli linaimarika kwa asilimia 100

“Kwa lengo la kuweza kukabiliana na ushindani mkubwa uliopo hasa kwenye eneo la masoko  kwa sasa ambao umekuwa ukifanya sekta ya reli kurudi nyuma linapokuja suala la biashara  kwani kwasasa ni kiwango chake cha usafirishaji kimeshuka kuliko kawaida,” anasema Shuhuli.

Anasema ni jambo jema iwapo yatajengwa mazingira mazuri ya kusafirishia mizigo kwa njia ya reli pamoja na kusisitiza serikali iache kuziba masikio dhidi ya vilio vinavyotolewa na wafanyakazi mara kwa mara kwani wamekuwa na ufumbuzi wa matatizo yao kwa kiwango kikubwa.

“Serikali hainabudi kuendelea kusikiliza vilio vya wafanyakazi pindi vinapojitokeza kwani kwa nyakati tofauti serikali imekuwa ikishindwa kuitikia wito unaotolewa na wafanyakazi hao jambo ambalo limekuwa likishusha morali ya kuwajibika kwa wafanyakazi na hivyo kupelekea kuathirika kwa sekta nzima ya usafiri wa reli.

“Ni wazi kuwa wafanyakazi wamekwa wavumilivu hivyo ni wakati wa kuhakikisha kuwa serikali iliyoko madarakani inafufua kwa kiwango cha juu eneo hioli la usafiri wa reli kwani ndilo uti wa mgongo wa uchumi.

“Kwani sekta hii ya reli ni kati ya zile zinazotarajiwa kuwa kubwa na nyeti zitakazoshikilia uchumi wa nchini kwani pia bei zitashuka na zitakwua zikifika kwenye maeneo husika kwa wakati ikilinganishwa na ilivyo sasa ambapo magari makubwa ndiyo yamekuwa yakitumika kubeba bidhaa jambo ambalo limekuwa likikwama kutokana na changamoto za foleni za njiani na mambo mengine,” anasema Shuhuli.

Shuhuli anabainisha kuwa iwapo eneo hilo litatiliwa mkazo ma serikali ni wazi kuwa uchumi wa nchi utaimarika kwa kiwango cha juu ikiwamo maeneo ambayo reli hiyo ya kisasa itapita kwani biashara nyingi zitafanyika pamoja na wananchi wengi kupata ajira kwenye shirika la reli kama wafanyakazi.

Anaongeza kuwa kwasasa chama hicho na wanachama wake wako kwenye mwelekeo mzuri wa kufanya kazi kutokana na kuwa na imani na serikali kupitia kwa kiongozi ambaye amekuwa akiwasilikiza kero zao ikilinganishwa na hapo awali.

“Ili sekta hii iendelee kuimarika ni vyema serikali pindi inapokuwa inataka kufanya mabadiliko basi ilete watu ambao wanatoka nje ya TRL kama ilivyofanya kwa Masanja Kadogosa ambaye ni Mkurugenzi wa TRL anayesaidia kufufua hali ya shirika,” anasema Shuhuli.