Home Makala TUANZIE KWENYE MAPINDUZI YA KILIMO

TUANZIE KWENYE MAPINDUZI YA KILIMO

1703
0
SHARE

NA DK. PHILEMON NDESAMBURO


Serikali ya Rais John Magufuli inataka kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Ina maana kwa sasa Tanzania si nchi ya viwanda. Pengine  kwa sababu kuna viwanda vichache vilivyohoi au havipo kabisa.

Viwanda vilikuwepo enzi za utawala wa Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Watawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliomrithi Nyerere, ndio walioua viwanda vyetu.

Vile viwanda alivyotuachia mwalimu, vingalikuwepo,kama nchi tungekuwa mbali sana kwenye sekta hii. Leo, tunalamika kuanza upya kutokana na watawala wa ccm kutoendeleza sera  ya viwanda. Viwanda vyetu vimefia mikononi mwa watawala wanaotokana na CCM.

Nilikuwa najaribu kukumbusha wasomi kuwa tulikuwa na viwanda vilivyofia kwa walewale wanaotaka kuvifufua leo. Hili nitalijadili kwenye makala nyingine nikipata nafasi wiki lijalo.

Leo, ninachotaka kujadili  kwa faida ya wasomaji wangu,ni  mambo mawili. Moja, ni njia  tunayopaswa kupitia ili kuelekea kwenye Tanzania ya viwanda na Pili, ni aina ya viwanda tunavyofikiria kuvianzisha na faida yake kwa wazalendo wa nchi hii.

Nikianza na jambo la kwanza,ninaona ni lazima tupitie njia ya kuboresha kilimo ili tufike kwenye Tanzania ya viwanda.Ni muhimu  viwanda hivi,vikawa na uhusiano wa moja kwa moja na sekta ya kilimo inayoajiri watanzania wengi.

Nimetembelea nchi nyingi duniani, ikiwemo Uingereza. Nimejifunza juu ya historia ya Mapinduzi ya viwanda ya uingereza karne ya 18. Uingereza ndio nchi ya kwanza duniani kuwa na mapinduzi ya viwanda.

Msingi wa mapinduzi ya viwanda nchini Uingereza ulikuwa ni mapinduzi ya kilimo (Agrarian Revolution.) Mapinduzi ya kilimo nchini uingereza yalichochewa na technolojia, mitaji na miundombinu bora.

Kabla ya kutokea kwa mapinduzi ya kilimo, waingereza walipitia kwenye kipindi cha kujikusanyia mitaji na kuboresha huduma za kibenki kwa ajili ya kuwajengea uwezo wakulima.

Ukusanyaji wa mitaji, ulisabisha Uingereza kuwekeza kwenye ugunduzi wa teknolojia.Ugunduzi wa teknolojia ulikuwa muhimu kwa ajili ya viwanda na kilimo.Waingereza,walikuwa wamejikusanyia mitaji ya kutosha kuwekeza kwenye kilimo.

Nchi ya Uingereza, haikuwa na  ardhi kubwa, kwa hiyo wakulima mabepari wakubwa waliendesha uporaji dhidi ya wakulima wadogo ambayo baadaye waligeuka nguvu kazi ya mabepari. Hakuna sababu ya uporaji kutokea Tanzania kwa sababu tuna ardhi ya kutosha.

Kilimo cha kutumia teknolojia ya kisasa nchini Uingereza kilileta tija kubwa katika uzalishaji wa malighafi wenye tija kwa ajili ya viwanda.Wakulima walitumia mbegu bora. Walitumia mbinu za kisasa kuzalisha,kuandaa na kutunza mazao.

Kwa sababu ya uwezo mkubwa wa kiteknolojia wakulima walikuwa hawategemei mvua pekee, bali walitumia raslimali maji kuhakikisha mazao yao yanastawi.

Serikali ya Uingereza iliboresha vizuri miundo mbinu ya  usafiri kwa ajili ya kusafirisha mazao ya Wakulima kwenda kwenye masoko, viwandani.

Tanzania inafaa tupitie njia hii kama kweli tunataka kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda.Utashi wa serikali pekee yake hautoshi.

Ni lazima tutumie njia sahihi na mikakati sahihi.Tusiishi kwa kauli tu,bali tuangalie namna ya kuiendea njia na mikakati sahihi ili kutengeneza Tanzania ya viwanda.Matangazo na kauli ya Tanzania visiwe na nguvu kuliko mikakati na matendo.

Serikali ya Tanzania chini ya  Rais John  Magufuli iweke mazingira ya mapinduzi ya kilimo.Kama nchi,tunapaswa kuwa na mitaji ya kuwekeza kwenye kilimo cha teknolojia ya kisasa.

Wenzetu Waingereza,walijikusanyia mitaji na kuboresha mifumo ya kibenki kwa ajili ya wakulima. Tanzania ya Viwanda inahitaji mitaji kwa wakulima. Tuhakikishe mitaji hii inakuwa kwa wazawa kwa asilimia kubwa. Kuruhusu kiasi kikubwa kutoka nje itakuwa sawa na ukoloni maomboleo.

Sisi watanzania tumshukuru Mungu daima, ametubariki kwa kutupa ardhi kubwa yenye rutuba na tunazungukwa na vyanzao vingi vya maji.

Lakini  raslimali hizi hatujazitumia ipasavyo kutokana na ukosefu wa mitaji na teknolojia.

Napenda kusisitiza tena; ili  kufanikisha mapinduzi ya kilimo, tunahitaj mtaji  na kuwekeza kwenye kilimo cha kiteknolojia  sambamba na kuboresha miundombinu. Kuwaza Tanzania ya viwanda huku wakulima wengi wanaendelea kutumia zana duni,ni mzaha mkubwa sana.

Wakulima wetu walio wengi wanatumia kilimo duni,wanaishi vijijini mahali ambako hakuna miundo bora.Wanategemea kilimo cha mvua za msimu. Mazingira haya hayawezi kuchochea mapinduzi ya kilimo.

Kama tupapitia njia ya kuboresha kilimo ili kuleta mapinduzi ya viwanda,basi mazao ya kilimo yatazalishwa kwa ajili ya viwanda vya hapahapa nchini,kutakuwepo na uhakika wa soko.Hakutakuwa na haja ya nchi kuudha malighafi nchi za nje kwa hasara kama tulivyozoea kufanya hivyo toka enzi la ukoloni.

Viwanda vitakavyoanzishwa vikitegemea mapinduzi ya kilimo basi kutakuwepo uhusiano mkubwa wa viwanda vyetu na wananchi ambao wengi ni wakulima. Wananchi watamiliki uchumi wa taifa lao.

Jambo laPili,ninataka kushauri juu  ya aina vya viwanda tunavyotaka kuvianzisha. Serikali ijiepushe kuaanzisha viwanda vinatakavyohodhi uzalishaji wa kila kitu; kuanzia malighafi na bidhaa yenyewe.

Nina maanisha kuwa kuanzishwe viwanda vinavyozalisha bidha tu lakini viwanda hivyo vizungukwe na viwanda vidogo vinatengeneza vitu kwa ajili kuviuzia viwanda vikubwa. Kwa kimombo viwanda vinavyozunguza viwanda vikubwa vinaitwa backyard industries.

Kwa mfano, kama kutaanzishwa kiwanda cha kutengeneza nguo nchini.Kiwanda hicho kisihodhi uzalishaji wa kila kitu kinachotakiwa ili kutengea nguo.

Kiwanda kikubwa dhima yake iwe ni kutengeneza nguo iliyokamilika. Vitu vya lazima kwa ajili ya utengenezaji wa nguo vizalishwe na backyard industries.

Serikali  inaweza kuruhusu kuanzishwa kwa backyard industries ambazo zitazalisha vifungo vya nguo, nyuzi, au vitamba kwa ajili ya kukiuzia  kiwanda vikubwa.Serikali isitoze ushuru kwa hizi backyard industries.

Kazi ya viwanda vikubwa ni kununua malighafi kwa viwanda vidogo na kutengeneza bidhaa.Serikali ikianzisha viwanda vya aina hii, watu wengi watapata ajira nchini,viwanda vitakuwa nchini ya miliki ya watanzania wenyewe.Wananchi watamiliki Uchumi wa viwanda wa taifa lao.

Kwa mfano, ilivyo hivi sasa kwenye kiwanda cha kuzalisha sukari cha TPC Hapa Kilimanjaro,wakulima wamenyimwa ajira.Kiwanda cha TPC kimehodhi mashamba na kinazalisha miwa chenyewe kwa ajili ya kuzalisha sukari. Watu wanaozunguka kiwanda hiki wanatazama tu mashamba ya miwa kwa ajili ya kuzalisha sukari.

Sasa kiwanda kama hiki ni mfano mbaya sana kwa viwanda kwa sababu kinapoka nafasi ya wananchi kuajiri katika uzalishaji wa miwa na kukiuzia kiwanda.

 

Mwandishi wa makala haya ni; Mbunge mstaafu wa jimbo la Moshi mjini Mwenyekiti wa chadema mkoa wa Kilimanjaro.