Home Makala Tunaibiwa uhuru wetu katika Katiba

Tunaibiwa uhuru wetu katika Katiba

1773
0
SHARE

MobutuNa Yericko Nyerere

MWAKA 1889 Taifa letu lilianza kupigania uhuru na utu wa mtu, wazee wetu akiwamo Chifu Mkwawa na wengine walipinga kwa nguvu zote uvamizi na utawala wa kidikteta wa wakoloni. Mwaka 1961 Taifa lilipata uhuru, chama kilicholeta uhuru kilikuwa TANU, si kwamba hakukuwa na vyama vingine vya siasa la hasha! vilikuwepo vingi  mfano, ANC, AMNUT, NTU, BANTU, na vingine vingi.

Ikumbukwe kuwa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1957 akiwa Rais wa chama cha upinzani cha TANU aliteuliwa na Gavana Twining kuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria (Bunge).

Akahudumu nusu mwaka, kisha akajiuzulu na kuendelea kuhubiri siasa na makongamano ya kisiasa yenye nguvu za hoja. Uteuzi wake kuingia ndani ya baraza hilo haukuwa na tofauti na uteuzi alioufanya Rais mstaafu Jakaya Kikwete  kwa James Mbatia.

Utawala wa TANU chini ya mfumo wa vyama vingi ulidumu kwa mwaka mmoja tu, baada ya Tanganyika kuwa Jamhuri 1962, vyama vingi vilifutwa kwa sababu ambayo mpaka leo haijawahi kuelezwa ikajitosheleza zaidi ya kusema ilikuwa kuunda umoja na mshikamano.

Utawala wa kiimla uliendelea huku vuguvugu la kutaka mageuzi ya kidemokrasia likipamba moto hadi Azimio la Zanzibar la 1992 lilipopitishwa na kuruhusu uhuru wa kisiasa na uhuru wa mawazo huru.

Leo mwaka 2016 katika dunia ya utandawazi uliopanuka ambapo dunia imekuwa kijiji, tunarejeshwa kwenye utawala ule wa kijima, utawala wa katazo la kuhoji, katazo la kusikia mapya, katazo la kuona mapya, katazo la kuamua mapya, yaani ni utawala ule 1962 hadi 1992 wa sauti ya Mwitongo tu ndio twaurejea kwa kusikiliza sauti ya Chato tu.

Ushauri wangu kwa upinzani ni kuwa, kwa Afrika nchi zote zinaongozwa kidikteta kwa karibu asilimia 51, zingatieni kuwa madikteta wasomi ni hatari kuliko madikteta wajinga. Dikteta msomi hutawala huku umma ukilia moyoni wakati  machoni ukichekelea, madikteta wajinga hutawala huku umma ukicheka moyoni wakati machoni ukilia.

Utawala wowote wa kidikteta ni adui wa mawazo kinzani, yaani vyama vya siasa havina nafasi kwenye tawala za kidikteta, hii ni duniani kote.

Nieleweke vizuri, wapo wale wenye akili za visoda wasije kunilisha maneno, sijasema Mtukufu Rais wetu mpendwa Dk. John Pombe Magufuli ni dikiteta, narudia rais wetu mpendwa SI dikteta. Lakini aina ya utawala wake unaviashiria vinavyoweza kutafsiriwa kuwa ni udikteta japo si dikteta kabisa, msema kweli ni mpenzi wa Mungu.

Angalizo langu upinzani Afrika ujitathimini na kubuni njia mpya za kupambana na tawala za aina hii, kitendo cha kuruhusu baadhi ya mambo yanayotafsiriwa kuwa ni udikteta yakapita mbele ya umma bila kupingwa kisawasawa ni kuipa nguvu serikali inayoongozwa na  utawala wa kiimla.

 

Upinzani Afrika una njia tatu

KWANZA: Kulazimisha upingaji wa uimla huu kwa njia ya maandamano. Hapa matokeo yanaweza kuwa mawili;

  1. Kuuawa kwa waandamanaji lakini mwisho serikali ikakubali kulegeza msimamo au ikatia mkazo, hili tumeliona Burundi na Uganda na kwingineko. Njia hii imeshapitwa na wakati.
  2. Kuogopa kwa serikali na kulegeza msimamo bila kumwaga damu, hili tumeliona Tunisia, Bukinafaso, Misri, na kwingineko.

MBILI:   Kubadili njia ya siasa kwa kutumia muundo wa chambuzi za hali ya nchi. Chambuzi hizi ziwekwe kwenye muundo wa hotuba za kitaifa za kila mwezi na zinatakiwa kufanywa na viongozi wa juu  kwa kutumia vyombo vya habari.Hapa lazima vyama vya siasa viwekeze nguvu kubwa kwenye ujasusi ili kupata habari sahihi na stahiki, mfano afya, elimu, nishati na maeneo mingine.

Na kisha kila mwezi kutakuwa na hotuba ya saa moja ya kiongozi mkuu wa chama ama katibu mkuu ilimradi awakilishe chama taifa. Hii inaweza kukumbana na kikwazo katika vyombo vya habari ambavyo vingi vinaweza kutishiwa ama kufungiwa kabisa.

Lakini hili lazima chama kigharimie mafunzo muhimu kwa watu wake, elimu ndio silaha muhimu kwa hapa, watu wapelekwe Ujerumani, Israel, Urusi, Uchina, Bulgaria, nk. Utaratibu huu huendeshwa na nchi nyingi duniani hasa zile zilizopevuka kifikra na kisiasa.

TATU:  Kutumia udhaifu wa chama tawala, mfano mpasuko wa chama tawala ama makosa ya serikali yake. Njia hii ndio hutumiwa na vyama vingi Afrika kutokana na kuwa vyama vingi vina itikadi zisizofahamika kwa wanachama wao, hii ikiwemo Tanzania kwa miaka yote na ndio iliyovipa mafanikio na umaarufu vyama vya upinzani, ambapo kwa muono wangu awamu hii ya tano kwa kiwango fulani CCM imeonyesha kuizuia njia yetu, kwa kuwa wakifanya kosa wanatumia vyombo vya habari kuziba makosa hayo mapema kwa kutumia kitu kiitwacho “kutumbua  majipu”. Zingatieni jamii zetu za Afrika zinapenda siasa za urembo ama za rangirangi (Decorates politicals) na CCM wanafaulu hilo.

Zipo ajenda ambazo kwa kisayansi ni za umma, mfano ufisadi hii ni ajenda ya umma kwa Afrika, hivyo akitokea mtawala akawarubuni wananchi kuwa anapambana nao hata kwa geresha tu watamuunga mkono, na kwa kuwa tawala za kidikteta kote duniani hudhibiti vyombo vya habari hivyo geresha ya vita dhidi ya ufisadi hutangazwa kwa nguvu zote.

Kisiasa akitokea mtu yeyote mwenye uelewa mzuri akapinga aina ya vita hivyo inavyopambanwa atapingwa na umma kwa kuwa hana uungwaji  mkono kwa wingi.

Binafsi kwa Tanzania kitendo cha upinzani nikiwemo mimi kukosoa utawala huu hasa aina ya jaribio la kufuta upinzani na viinimacho vya utumbuaji majipu wa serikali ya Rais John Magufuli ni tendo la ushujaa na utii wa itikadi, lakini hausaidii siasa za Upinzani kwakuwa nguvu ya kutetea ni ndogo tofauti na nguvu ya kutangaza utumbuaji huo inayofanywa na serikali.

Serikali imedhibiti vyombo vya habari vyote vikabaki kuhubiri majipu tu kila kona, na kwa mantiki ya sayansi ya siasa, suala la majipu limefanikiwa kutengenezwa kuwa “ajenda ya umma”, hivyo kulipinga ni kujimaliza kisiasa.

Werevu wachache tunatambua kuwa chama tawala kinarubuni umma, lakini wananchi wengi wenye uelewa mdogo wanatushangaa wakati huo propaganda ya utumbuaji inashika kasi.

Licha ya hali mbaya ya maisha inayoendelea kuwakumba lakini ni ukweli kuwa jamii kubwa ya Waafrika huwa haishtuki mpaka ianze kufa kwa njaa ndipo huamka, Sukari bei juu, nk. Lakini muhimu zaidi kwa vyama vya mageuzi Afrika lazima viwe na sauti ya pamoja, madikteta hawa wapya wanalingana kwa kila jambo na kila mazingira, mpaka rangi zao ni nyeusi tiii!

Vyama vya upinzani Afrika viunganishe nguvu zao kwanza ili kuondoa vyama vilivyokuwa vya ukombozi vilivyogeuka kuwa mkoloni. Vifanye hivyo kabla yakusaka misaada toka Ulaya. Makoloni na mabeberu haya ya ndani ambayo zamani vilikuwa vyama vya ukombozi viliungana vikashinda enzi hizo.

Mfano kulikuwa na mashirikiano makubwa kati ya TANU na KANU ambapo makamanda na makomred walikuwa wakiazima ujuzi na mapambano katika uwanja wa vita.

TANU chini ya Rais wake Hayati Julius Nyerere iliwahi kuwatuma Bibi Titi Mohamed na Mzee Tambaza kwenda Kenya kuwasaidia KANU iliyokuwa chini ya Kenyatta na Tom Mboya. Mpaka leo wanashirikiana. Yanayotokea Rwanda, Burundi, Kenya na Afrika kwa ujumla yote yana baraka za Tanzania. Yaani haiumizwi.

Leo Live Tv Bunge ni marufuku, wapinzani wamefukuzwa bungeni, wapinzani majukwaa ya siasa marufuku, gharama ya maisha imekuwa kubwa maradufu, uhuru wa maoni marufuku,

Hii ni siasa hivyo mchezo upo upande mmoja.Tujisahihishe.  Siasa si lazima tuziendeshe kwa mikutano ya hadhara katika nyakati hizi za mkono wa chuma. Tuwaige wale waliokomaa Republican, Democratic, Labor, Conservative wao katika kuendesha siasa, mikutano ya hadhara katika kujenga vyama si muhimu, kwao muhimu ni Tv, mitandao ya internet, midahalo ya ndani na magazeti.