Home Uchambuzi TUNAKWENDA KULE WENZETU WALIKOTOKA

TUNAKWENDA KULE WENZETU WALIKOTOKA

3006
0
SHARE
Waandishi wa habari, wakiwa wameanguka chini, katika makao Wizara ya Mambo ya Ndani, Dar es Salaam juzi, wakati Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), wakupotumia nguvu dhidi ya wanahabari waliokwenda kufuatilia yaliyojiri baada ya mahojiano ya mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, na Jeshi hilo kwenye Polisi. Picha na Said Khamis

NA JOSEPH MIHANGWA


Wiki iliyopita tulichambua dhana ya jamii iliyojifunga na kubainisha kuwa ni ile isiyoruhusu mawazo huru kumea, ushindani wa fikra kushamiri, uhuru wa kujieleza na haki ya kupata habari na kuhabarishwa kutamba. Ni jamii isiyonufaika na dhana kongwe ya kidemokrasia yenye kuruhusu “maua mia moja kumea/kuchipuka; fikra kinzani mia moja kuibuka na kukinzana” ili kusafisha, kung’arisha na kupevusha jamii.  Kinyume cha hayo, ni kuihukumu jamii kuchakarika na kuteketea kwa kutu. Endelea..

Oktoba 24, 1997 Charles Onyango – Obo akiwa Mhariri wa gazeti la “The Monitor”, na mwenzake, Mwandishi Mwandamizi Andrew Mujuni Mwenda, walishitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa kosa la kuchapisha habari za uchochezi kwa kichwa cha habari:  “KABILA ALIILIPA UGANDA KWA DHAHABU”; ambapo ilidaiwa kwamba malipo hayo yalifanywa kuishukuru Uganda kwa kumsaidia [Kabila] katika vita nchini Zaire vya kumng’oa madarakani dikteta Mobutu Sese Seko wa nchi hiyo.  Mahakama iliwaachia huru kwa kuwaona hawakuwa na hatia ya “uchochezi”. Baada ya hapo, Waandishi hao Waandamizi walifungua kesi kwenye Mahakama ya Katiba, kuiomba itoe ufafanuzi kama Serikali ilikuwa na uwezo na haki ya kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu [Penal Code] kwa madai ya kulinda “maslahi ya umma”. Mahakama ya Katiba ilisema, “Serikali ilikuwa na haki na uwezo huo”.  Kwa hiyo maombi yao yalitupiliwa mbali. Wanahabari hao hawakuridhika; walikata rufaa Mahakama ya Rufaa [Supreme Court] dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Katiba.

Tunapotoa mfano huu, ikumbukwe kwamba Ibara ya 29 (1) ya Katiba ya Uganda ya mwaka 1995, inafanana na Ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania ya 1977 inayotumika hadi sasa.  Vivyo hivyo, kosa la “uchochezi” lililopo chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu [Penal Code Act] ya Uganda, ndilo hilo hilo lililopo chini ya vifungu namba 50 na 55 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu [Penal Code].

Suala katika kesi hii lilikuwa kuhusu kama kifungu cha 50 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu hakipingani na Ibara ya 29 ya Katiba ya nchi hiyo, inayotoa uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari bila ya kuingiliwa na mtu au chombo chochote. Katika hukumu yake, Mahakama hiyo ilibaini kuwa, kifungu cha 50 [kwa Tanzania, ni kifungu cha 50 na 55] cha Sheria ya Kanuni za Adhabu kimedumu tangu kabla na baada ya Uganda kuridhia Sheria ya Haki za binadamu [Bill of Rights], kama ilivyo pia kwa Tanzania, iliyoridhia haki hizo kwa Sheria Namba 15 ya 1984 na kuanza kutumika mwaka 1987.  Kifungu hicho cha Sheria ya Kanuni za Adhabu [PC] ni moja ya Sheria za Kikoloni zenye chimbuko la miaka ya 1200 nchini Uingereza. Mahakama ilisema, “kwa maslahi ya umma” yanakubalika iwapo tu yatakuwa na misingi ya uhuru na demokrasia, kwa maana ya kutoruhusu unyanyasaji wa kisiasa, kuweka watu kizuizini na udhalilishaji wa kibinadamu.

Mahakama ilibaini kuwa Uganda, kama moja ya jamii za kidemokrasia, inapaswa kuzingatia misingi ya demokrasia kwa viwango vya kimataifa; na kwamba chini ya viwango hivyo, si halali kuugeuza uchapishaji wa habari za uongo kuwa kosa la jinai, wakati Katiba ya nchi na zile za kimataifa kuhusu haki za binadamu [Bill of Rights] zinapingana na dhana hiyo. Wakifafanua matakwa ya Ibara ya 29 [Tanzania ni ibara ya 18] ya Katiba, Majaji wa Mahakama hiyo walisema, Katiba inatoa na kulinda uhuru wa hotuba, uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari: “Tunapenda kuweka wazi kwamba, uvumilivu kwa mwenendo na kwa hotuba hasidi katika jamii ni moja ya gharama inayopashwa kubebwa na jamii huru na iliyo wazi”, Mahakama ilisema, kumaanisha kwamba jamii na watawala wauone uhuru huo kuwa ni sehemu ya demokrasia na si “uchochezi”.

Ni aina gani ya mawazo yanayoweza kuvumilika?.  Majaji wa Mahakama hiyo walichukua ibara ya 9 ya Mkataba wa Afrika juu ya Haki za binadamu [The African Charter on Human and Peoples’ Rights], kama kielelezo na ambayo inafanana na ibara ya 29 ya Katiba ya Uganda kwamba:  “Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbali mbali duniani kote”, na kwamba, “kila mtu ana haki ya kutoa na kusambaza au kueneza mawazo yake”.

Wakasema: “ni kutokana na ukweli huu kwamba, haki ya uhuru wa kujieleza haijumuishi pekee haki ya kuhifadhi, kupokea na kutoa aina zote za mawazo kama vile maoni sahihi, mawazo mazuri au taarifa za kweli; bali inajumuisha pia haki ya kuhifadhi, kupokea na kutoa mawazo, maoni na taarifa ambazo si lazima zionekane kuwa za kweli”.  Kwa maana nyingine kwamba, ni kwa njia ya ushindani katika soko la habari kuwa, ubora na ukweli wa mawazo utajichuja wenyewe badala ya kuchujwa na Serikali, kwani katika jamii yenye demokrasia kamili si kazi ya Serikali kufanya hivyo, wala kuelekeza kipi kiandikwe au kusemwa na kipi kisiandikwe au kusemwa.

Ni kutokana na uamuzi wa jopo la Majaji hao saba kwamba kifungu cha 50 [Tanzania, kifungu cha 50 na 55] cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya Uganda [PC] kilikuwa ni kinyume cha Katiba, na hivyo ni batili. Uamuzi huu unatufunza nini, na una maana gani kwa Tanzania kuhusu uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari?.

Mahakama ya Rufaa ya Uganda [Supreme Court] na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania zina hadhi sawa ambapo hukumu zake [precedents] zina ushawishi [persuasiveness] mkubwa katika kufikia maamuzi ya kesi zinazofanana katika Mahakama ya kila nchi. Na kwa kuzingatia pia kwamba Uganda na Tanzania [pamoja na Kenya] zina mfumo mmoja wa Mahakama, aina moja ya mfumo wa Sheria [Common law system], uamuzi wa Mahakama hiyo ni kete tosha kwa mhimili wa Habari ndani ya nchi zetu kuwezesha kuisaka haki na uhuru huo uliopotea; kinyume chake ni kuruhusu kujengeka kwa jamii iliyojifunga, iliyochina na yenye kumomonyoka kwa kutu.