Home Uchambuzi Tunashindwa wapi kudhibiti ‘upigaji’

Tunashindwa wapi kudhibiti ‘upigaji’

2196
0
SHARE

LEONARD MANG’OHA

Ni kama ukungu umetanda miongoni mwa wananchi kutokana na madudu yanayofanywa na mashirika ya umma kama yaliyoibuliwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2017/2018.

Ukungu huu unatokana na juhudi za Serikali ya Rais Dk. John Magufuli, katika kupambana na rushwa na ufisadi ulioonekana kuota mizizi katika taasisi na idara za umma.

Rais ameonesha kuwa mkali na mwepesi wa kuchukua hatua dhidi ya viongozi wanaobainika kutenda, kushiriki ama kuisababishia Serikali hasara.  Tumeshuhudia viongozi mbalimbali wakifikishwa mahakamani pasi kujali nyadhifa zao.

Sote tumekuwa mashuhuda jinsi alivyoedesha mchakato wa kuwaondosha kazini watumishi wenye vyeti feki na mapambano dhidi ya wafanyakazi hewa, ili kukomesha kabisa mianya ua upigaji katika maeneo hayo na katika mchakato huo tulisikia kuwapo watumishi wa umma waliokuwa wakipata mishahara zaidi ya mmoja.

Pamoja na hatua hizo kali, bado ripoti ya CAG imeonesha kasoro mbalimbali katika idara na mashirika ya umma, ikiwamo Benki ya Posta (TPB), ambapo inadaiwa kutumia Sh. milioni 495.75 kubuni na kubadilisha muonekano wa benki hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya CAG inaonesha kuwa timu ya tathmini ya zabuni ilipendekeza kampuni ya M/s. CI Group Marketing Solution ipewe kazi hiyo kwa gharama ya Sh milioni 224, lakini Bodi ya Zabuni iliazimia kampuni hiyo isipewe kazi hiyo kwa kigezo kuwa ilichelewa kukamilisha kazi ya tawi la Kijitonyama lililotumika kama tawi la mfano.

TPB ni moja tu ya mashirika yaliyobainika kuwa na upigaji katika taarifa ya CAG, pia yamo mashirika na idara kama vile NSSF, NHC, Polisi, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na mradi wa mabasi ya mwendokasi.

Lakini haya yanaibuliwa na CAG zikiwa zimepita wiki mbili tu tangu Rais alipotilia shaka matumizi ya zaidi ya Sh. milioni 200 kubadilisha maneno na kuchora picha ya twiga, ili ndege hiyo ya Serikali, iweze kutumika kibiashara, kazi ambayo imefanyika nchini kwa gharama ya Sh. milioni tano tu.

Kuendelea kwa ubadhirifu huu kunaonesha wazi kuwa kwa watendaji wa umma si jambo la ajabu, bali ndiyo maisha ya kawaida pasi kujali fedha hizo ni za umma. Kwa sababu kama Rais amejipambanua kuwa yeye ni mpinga rushwa na picha imejengeka hivyo miongoni mwa wananchi wengi, lakini haya yanaendelea, hatuwezi kukataa kwamba wanaofanya hivi walishaliona hili kuwa ni jambo la kawaida.

Kwa ukali ambao Rais amekuwa akiuonesha, tulitegemea kuona vitendo vya aina hii vikipungua, lakini vinaendelea kuona mizizi. Kama hii imeshindikana, basi tutafute njia nyingine mbadala ya kukomesha tatizo hili, kwa sababu kinachoendela ni sawa na baba mkali kwenye familia anayechukua hatua kali, huwabana watoto wake wa kike, lakini wanapata ujauzito.

Ikiwa baba mwenye sifa ya ukali na mwenye kuwadhibiti watoto wake, lakini matokeo huwa hasi, basi anapaswa kubadilika na kuwa mpole badala ya kuwa mtu wa vitisho. Inabidi abadili mbinu na kuzungumza na wanawe, ili kukomesha fedheha dhidi ya familia.

Inapotokea hali kama hii, ni wakati sahihi wa kuangalia wapi tunakosea, ili kuepuka fedheha hii, maana inaibua maswali mengi yasiyo na majibu. Je, watendaji wanafaya haya kwa makusudi ili kuichafua Serikali na Rais aliyepo madarakani, ili ionekane ni dhaifu kwa kuwa na matumizi mabaya ya fedha.

Nadhani iko haja ya kuwa na mfumo maalumu utakaodhibiti hali hii kwa kuweka sheria kali zaidi, au kuanzishwa kwa idara maalumu itakayokuwa na jukumu la ununuzi na utoaji zabuni na kuondoa utaratibu wa kila idara kujiamlia mambo yake, ili kuhakikisha kila idara inapohitaji kufanya manunuzi, inapeleka maombi ambayo yatashughulikiwa na wataalamu, kisha kurudisha majibu kwa taasisi husika.

Serikali ni lazima ichukue hatua kali, ili kujisafisha na kukwepa fedheha kama zile zilizowahi kuzikumba Serikli za Brazil baada ya Bunge nchini humo kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais Dilma Rouseff, Malawi iliyokuwa ikiongozwa na Joyce Banda ambaye hata hivyo alitupwa nje katika uchaguzi wa mwaka  2014 na Afrika Kusini chini ya Jaco Zuma aliyeondolewa madarakani na chama chake.

Kuendelea kwa vitendo vya matumizi mabaya ya fedha za umma, ufisadi na rushwa miongoni mwa watumishi wa umma, kunaondoa dhana ya utawala bora unaozingatia utu, na kuwakandamiza walipa kodi wanyonge, ambao huachwa bula  huduma bora za kijamii kama elimu, afya na maji, huku fedha zao zikiteketea katika midomo ya wajanja wachache waliopewa dhamana ya kuzisimamia taasisi na mashirika haya.