Home Latest News Ubaguzi Marekani unatonesha madonda ya miaka 400 iliyopita 

Ubaguzi Marekani unatonesha madonda ya miaka 400 iliyopita 

2538
0
SHARE

NA ALOYCE NDELEIO 

YAPO maeneo mawili ya Afrika ambayo watu wawili mashuhuri wa Marekani  wameyatembelea ambayo yanahusiana na Biashara ya Utumwa ya Pembe Tatu au Biashara ya Utumwa Kupitia Bahari ya Atlantiki (Triangular Slave Trade/Trans Atlantic Slave Trade).

Wakati wa ziara ya Rais wa Mstaafu wa Marekani, Barrack Obama barani Afrika moja ya sehemu aliyoitembelea ni pamoja na bandari iliyokuwa ikitumiwa kusafirisha watumwa nchini Senegal na Ghana ambako alitembelea lango lililokuwa la Waafrika kuaga na kusafishwa kupelekwa Marekani na visiwa vya Caribbea wakati wa Biashara ya  Utumwa ya Pembe Tatu

Aidha mke wa Rais wa sasa wa Marekani, Melanie Trump naye alifanya ziara katika nchini Ghana na kutembelea ngome hiyo iliyokuwa sehemu ya watumwa kuiaga Afrika na kwamba ilikuwa ni lango la mwisho na kwamba hawatarudi tena.

 Melanie Trump aliweka shada la maua na alitembelea sehemu hiyo huku akiuliza maswali hadi kufikia eneo ambalo watumwa wanaume walikuwa wakifungwa minyororo na baadaye akasema inasikitisha kutokana na yale yaliyotokea kipindi hicho.

 Aidha kwa upande wake Obama akiwa na mkewe walitembelea maeneo hayo ambapo alibainisha maeneo hayo yaliyomsikitisha mno na alisema, “hali hiyo  haitakiwi iirudie tena.” 

Hata hivyo uswahiba ambao uliooneshwa na Obama kwa Afrika kwa upande wa Trump haupo hususani baada ya kuwadhihaki wabunge wanawake mmojawapo mwenye asili ya Afrika kwamba waende nchini mwao walikotoka.

Hali hiyo ilionesha ubaguzi ambao umejikita ndani yake na kuichukia Afrika. Pamoja na hali hiyo tukio la kuuawa kikatili kwa Mmarekani mweusi George Floyd, kitendo kilichofanywa na polisi wa nchi hiyo tena kwa kukandamiza shingoni kwa mguu na wakati huo huo akilalamika kuwa anashindwa kupumua kulifufua kwa mara moja mateso waliyofanyiwa watumwa kutoka Afrika. 

Miaka 400 iliyopita watumwa wa kwanza  kutoka Afrika walifika Virginia nchini Marekani na kupitia watumwa hao ndio walioujenga uti wa mgongo wa uchumi wa kibepari wa Marekani na kuifanya ikue na kubakia kuongoza kiuchumi duniani hivi sasa. 

Matokeo ya kuitumikisha nguvu kazi ya watumwa wa Afrika bila malipo ndiko kulikosababisha kuwepo kwa pengo la utajiri kimatabaka, ambao hadi sasa ni mkubwa kuliko ilivyokuwa kipindi cha miongo minne iliyopita. 

Licha ya kwamba utumwa ulifutwa rasmi mwaka 1865, hali ya kutotendewa usawa kwa Wamarekani wenye asili ya Afrika imeendelea. Historia ya ubaguzi wa kutowiana kiuchumi imeendelea kuongezeka na kuhakikisha unakuwepo kutokana na mtazamo unaoelekea katika hali mbaya ya kutowiana nchini Marekani.  

Katika kuonesha uhalisia wa hali hiyo taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Taaluma za Sera, ilibainisha kuwa kati ya mwaka 1983 na 2016 familia za weusi zenye kipato cha kati uchumi wake ulishuka  kwa kiwango cha zaidi ya nusu ikilinganisha na ongezeko la asilimia 33 kwa familia za watu weupe walio na kipato sawa na hicho. 

Uchumi wa Marekani umekuwa ukistawi kupitia migongo ya watu weusi na watu wengine ambao ni maskini.  Wakati uchumi wa watu weusi ukididimia idadi ya kaya zilizo na dola milioni kumi au zaidi uchumi wake ulikuwa ukipaa kwa asilimia 856 katika kipindi cha miaka hiyo. 

Kwa upande mwingine asilimia 37 ya familia za weusi zilikuwa hazina kitu au uchumi wake ukiwa ni hasi ikimaanisha kuwa madeni yanazidi thamani ya amana walizonazo, ilhali ni asilimia 15 tu ya familia za watu weupe walikuwa katika hali hiyo. 

Pengo la kibaguzi kiuchumi ni suala ambalo linawahusu Wamarekani wote na kwa ujumla ustawi wa uchumi wa Marekani. 

Wakati idadi ya watu weusi iliongezeka, kiwango cha chini cha uchumi wa watu weusi ilikuwa ni sababu iliyochangia  kuanguka kwa  uchumi wa kati wa  Mmarekani  kutoka  dola 84,111 mwaka 1983 hadi dola 81,704 mwaka 2016. 

Katika makundi yote kuuzoea ustawi hasi  ndani ya kaya  idadi yake  iliongezeka kutoka  kaya moja hadi sita mwaka 1983 na kufikia kaya moja kati ya tano hivi sasa. 

Ubaguzi ni mkubwa kiasi kwamba familia ambazo elimu yake ni ya chuo kipato chake kimekuwa ni cha chini ikilinganishwa na familia ya watu weupe ambao wamesoma shule za elimu ya juu. Wakati huo huo familia inayosimamiwa ni mzazi mmoja mweupe  inayo kipato mara mbili ya familia inayolelewa  wazazi wawili ambao ni weusi. 

Taasisi hiyo ya taaluma za Sera inabainisha kuwa matokeo hayo hayatokani na tabia za mtu binafsi bali ni matokeo ya kuwa na rasilimali chache za kuanzia  na ambazo Wamarekani weusi wamenyimwa kwa miaka 400 tangu mtumwa wa kwanza alipotekwa  kutoka Afrika  na kupelekwa Marekani ili kuitoa nguvu kazi yake bure kwa kutumia misuli pamoja na kazi ngumu. 

Aidha taasisi hiyo inafahamisha kuwa ajira, kipato, umiliki wa mkazi, kuwa na amani, ujasiriamali na vidokezo vingine vya uchumi vinaonesha pengo kubwa la kibaguzi. Kukabiliana na hali hiyo ya mapengo  kunahitajika uwekezaji ambao unaendana na pato la watu weupe. 

Kutokana na hali hiyo kunahitajika mabadiliko ya kimfumo na mwitiko wa kisiasa kufikia hatua rasmi ya haki ya kiuchumi kwa Wamarekani weusi kwa kuwa kumalizika kwa utumwa hakutoshi wala kukidhi hali iliyopo. 

Kuuawa kwa  Floyd  Mei 25 mwaka huu na kufuatiwa na maandamano katika kila majimbo ya Marekani inasadiifu kusema kuwa miaka 400 baadaye makovu ambayo hayajakauka yamebanduliwa bandeji na kuwaletea machungu ya utumwa wa Wamarekani. 

Rais Trump naye hakuonesha kujali  na ile dhana inayofahamika kama ‘Wimbo wa Taifa wa Ubinadamu, unaosema binadamu wote ni kaka na dada na sio baadhi bali ni wote’  ambayo ni sawa na ‘binadamu wote ni sawa”  haina mashiko kwake kutokana na kuushadidia ubaguzi. 

Aidha hisia ambazo zinatolewa na wimbo na maneno yanayotamkwa yanafanana katika suala la uzalendo  lakini katika mapana yake zaidi, na katika hali hiyo  binadamu anakuwa amejenga familia ambayo mahitaji yake yanafanana katika elimu, vyombo vya habari na hata katika masuala ya kiimani.

Hali hiyo kwa Marekani ni tofauti licha ya kwamba imeshajidhihirisha kwamba muziki, sanaa na fasihi kutoka sehemu mbalimbali duniani, na mafanikio ya kisayansi yakitumiwa na wote bila kujali  nchi anayotoka. Kwa maana hiyo tunatakiwa kujenga msingi wa ubinadamu kwa wote ili uwe ni utamaduni wa kudumu.

Jambo ambalo jamii iliyozoea ubaguzi haijui ni lile lililosemwa na mwanazuoni mmoja  aliyesema, “dunia yetu ni ndogo lakini ni nzuri, imefanywa kuwa ndogo na teknolojia, uzuri wake ni wa asili, ipo nafasi moja kwa kundi moja: familia ya ubinadamu au utu.”