Home Habari Ubia sekta binafsi, serikali kumaliza changamoto ya miradi

Ubia sekta binafsi, serikali kumaliza changamoto ya miradi

4373
0
SHARE

Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Zena Said Kamishina wa PPP Dkt John Mboya

NA AMINA OMARI, TANGA

NCHI nyingi duniani zimeweza kupiga hatua kubwa za kimaendeleo, zikiwemo za kiuchumi kutokana na ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi (PPP).

Kwani kwa sasa mataifa mengi yanatumia utaratibu huu kama njia muafaka ya kutekeleza miradi ya maendeleo, kwa kasi na ufanisi mzuri zaidi.

Mfano nchi za Uingereza, Australia, Afrika Kusini, Misri, India na Korea ya Kusini,  zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kuzingatia kikamilifu hatua zote za maandalizi ya utekelezaji wa miradi ya PPP .

Ushirikiano huo umeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa harakati za kimaendeleo, hususani  katika ujenzi wa miundombinu, nishati,viwanda  pamoja na maendeleo ya kuchumi katika nchi husika.

Katika kipindi cha  mwaka 1990 hadi 2018, uwekezaji kwa kutumia utaratibu wa PPP kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, umehusisha jumla ya miradi 383 yenye thamani ya Dola ya Marekani Milioni 69.054

Hata hivyo dhana ya PPP siyo mpya kwa nchi ya Tanzania kwani ilianza kutekelezwa kuanzia mwaka 1990 hadi mwaka 2018 kwa  uwekezaji kwenye miradi ya PPP umehusisha miradi 20 yenye thamani ya Dola ya Kimarekani  milioni 863. 39.

Hivyo kutokana na mafanikio hayo ndipo Benki ya Dunia iliiwezesha Serikali ya Tanzania mafunzo kwa wataalamu wake ili waweze kutekeleza kwa vitendo dhana hiyo ya PPP.

Sambamba na kuweka Mfumo wa Mazingira Wezeshi, ikiwemo  kutungwa kwa Sera ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi mwaka 2009, pamoja na sheria yake ubia ya mwaka 2010.

Jitihada hizi za Serikali kutunga Sera, Sheria na Kanuni za ubia, kunalenga kuweka mazingira wezeshi ya kuwezesha ushiriki wa Sekta Binafsi katika kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo inayokidhi vigezo vya PPP.

Kamishina wa PPP Dk. John Mboya anasema kuwa hatua hiyo itasaidia kuiwezesha Serikali kutoa huduma za umma kwa ufanisi na kwa ubora unaotakiwa.

Amesema kuwa lengo la serikali kuishirikisha sekta binafsi ni katika jitihada za kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo hapo awali ingeweza kusimamiwa na serikali pekee

Vile vile, utekelezaji wa miradi kwa mpango wa PPP utaweza kuiepushia serikali gharama ya kusubiri bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa miradi Fulani na sasa utaoa fursa kwa sekta binafsi kutekeza miradi hiyo kwa haraka zaidi

“Kwa sasa tunatekeleza sera ya viwanda hivyo ilituweze kupiga kasi ya haraka ni muhimu kuishirikisha sekta binafsi kwa utaratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kuharakisha mchakato huo”amesema Kamishna huyo.

Aidha Kamishna huyo amesema kuwa utaratibu wa PPP ni njia bora ya kukabiliana na changamoto za kibajeti na kuiwezesha Serikali kutimiza wajibu wake katika utoaji wa huduma bora, kwa ufanisi na kwa bei nafuu kwa umma

Ambapo Dk. Mboya ameitaja miradi ambayo inaendeshwa kwa ubia kuwa ni pamoja na Serikali Mradi wa Uendeshaji wa Huduma ya Usafiri Jijini Dar es Salaam Awamu ya kwanza (UDART) ambao uko katika hatua ya utekelezaji.

Aidha, miradi mingine ambayo iko katika hatua za mwisho za uidhinishwaji wa upembuzi yakinifu ni pamoja na  Mradi wa Kuzalisha Madawa Muhimu na Vifaa Tiba, Mradi wa Ujenzi wa Vyuo Kumi (10) Vya Ufundi Stadi unaotekelezwa na VETA .

“Kuna miradi  ambayo iko katika hatua za  kuandaa taarifa za awali (Pre-feasibility Studies) ikiwemo Mradi wa Kusambaza Gesi nchini unaoandaliwa na TPDC, Mradi wa Kujenga Hosteli za wanafunzi unaoandaliwa na CBE na Mradi wa Kujenga Taasisi  ya Taifa ya Saratani unaoandaliwa na Taasisi ya Ocean Road Cancer Institute.

Kwa upande wake  Mwakilishi wa Benki ya Dunia Ned White, amesema kuwa wamevutika kufadhili mafunzo ya uwezeshaji wa mpango huo  kutokana na namna ambavyo Tanzania ilivyopiga hatua katika utekelezaji wa programu hiyo kwa vitendo.

Amesema kuwa kwa kipindi kifupi wamefurahishwa na utekelezaji wa miradi ya ubia katika sekta ya nishati na gesi hivyo wameona ni jambo jema kuja kuwajengea uwezo.

“Miradi ya ubia inasaidia kuharakisha maendeleo hivyo kupitia mafunzo haya tutaweza kuwajengea uwezo katika maeneo ya mikataba na sheria ili miradi hiyo iweze kuwa ni yenye tija kwa serikali na wananchi”amesema White.

Hata hivyo katika kuharakisha maendeleo kwa haraka serikali imedhamiria kupeleka Mpango wa PPP katika ngazi za Halimashauri ambapo huko ndiko kwenye wananchi wengi ambao wanauhitaji wa huduma bora.

Kwani mpango huo utakuwa ni fursa nzuri kwa Halmashauri zote Nchini kubuni miradi yenye sifa za PPP chini ya uratibu wa Kitengo cha PPP cha TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango.

Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa ambayo itaweza kunufaika na fursa hiyo ambapo Katibu tawala Zena Said anasema kuwa jambo la msingi sana ni utayari wa kila Halmashauri kuwajibika kuhakikisha kuwa wanazingatia kikamilifu utaratibu huu kwa manufaa mapana ya Taifa.

Anasema kuwa iwapo wataweza kuchapa  kazi kulingana na matakwa ya utaratibu huu itasaidia kupatikana kwa  miradi yenye sifa na ubora unaotakiwa na hivyo kuchochea kasi ya maendeleo nchini.

“Ni dhahiri kuwa endapo Wizara na Taasisi za Serikali zitawajibika kikamilifu kwa kuwa  makini katika usimamizi wa miradi na uingiaji wa taratibu za ubia na kufuata hatua zote muhimu za utekelezaji wa miradi ya PPP tutaweza kupiga hatua kubwa ya utekelezaji wa miradi”alibainisha RAS Said

Amesema kuwa changamoto kubwa iliyopo katika Halimashauri ni kutopatikana kwa wakati kwa fedha za utekelezaji wa miradi lakini kwa kuwepo kwa mpango huo utawezesha Halimashauri hizo kutekeleza miradi yake kwa haraka.

“Hili ni jambo la faraja na ni fursa kubwa kwa Halmashauri zetu kutumia utaratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii hususani ujenzi wa hospitali za kisasa, miundombinu iliyobora,” alisema RAS Said.

Hata hivyo licha ya malengo mazuri ya serikali katika mpango huo Katibu tawala ameweza kubainisha baadhi ya changamoto zinazokabili Halimashauri katika utekelezaji wa mpango huo ikiwemo ukosefu wa wataalamu  wa kuibua na kuandaa maandiko ya miradi,

Pia alizitaja changamoto nyingine kuwa ni wataalamu kushindwa kufanya uchambuzi wa upembuzi yakinifu ikiwemo kuandaa na kuchambua nyaraka za zabuni.

Vile vile  uwezo mdogo wa wataalam katika kufanya majadiliano ya mikataba, kutokuwepo  kwa timu mahiri za kusimamia miradi ya PPP pamoja na ukosefu wa rasilimali fedha kwa ajili ya maandalizi ya maandiko ya miradi.

Hata hivyo Dk. Mboya amesema kuwa katika kumaliza changamoto hizo Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imeendelea kutekeleza programu ya mafunzo ya PPP kupitia Mfuko wa kusaidia utekelezaji wa Miradi ya PPP ulioanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya PPP wenye lengo la kuboresha utekelezaji wa Programu ya PPP nchini.

Pia ametumia nafasi hiyo kuziasa halimashauri nchini, kutumia fursa hiyo kutekeleza miradi ya kimaendeleo kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizopo hapa nchini ili kuchangia kusaidia bajeti ya Taifa.