Home Makala UCHAGUZI MKUU KENYA UNAWEZA KURUDIWA

UCHAGUZI MKUU KENYA UNAWEZA KURUDIWA

1348
0
SHARE
Upigaji kura katika uchaguzi Kenya.

NAIROBI, KENYA


Uchaguzi mkuu wa Kenya unaotarajiwa kufanyika Agosti 8 mwaka huu na unaowapambanisha rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga unaweza kurudiwa iwapo matokeo ya uchaguzi huo yatakaribiana sana.

Pia iwapo upinzani utaweza kuhamasisha wapigakura wengi kwenda vituoni siku ya kupiga kura, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo marudio ya uchaguzi baina ya wagombea wawili wa juu.

Hayo yamebainishwa katika ripoti ya taasisi moja ya upembuzi wa masuala ya uchaguzi ya Verisk Maplecroft wiki iliyopita.

Taasisi hiyo inaeleza kwamba wakati uungwaji mkono wa upande wa upinzani umekuwa unahuzunishwa na mgombea wao Raila Odinga ambaye ameshindwa urais mara tatu, lakini anaweza kulazimisha kura ya marudio iwapo wafuasi wa kutosha watahamasishwa kwenda vituoni kupiga kura.

Ripoti inasema kwamba Raila na Kenyatta  wana ufuasi sawa miongoni mwa makabila makuu, na iwapo wapinzani watajitokeza kwa wingi katika majimbo ambayo ni ya hati-hati kwa angalau asilimia 10 tu, hiyo italazimisha kura ya marudio.

“Haitarajiwi Kenyatta kushinda kwa zaidi ya asilimia 10, na hii inaelezea kwa nini mpambano ni mkali,” inaongeza Ripoti hiyo.

Vurugu ambazo huambatana na chaguzi za Kenya huwa ni wakati wa changamoto kubwa kwa wawekezaji. Shirika la Fedha (Funiani (IMF)limetoa tahadhari kwamba upigaji wa kura utapunguza ukuaji wa uchumi katika uchumi wa ukubwa wa Dola za Kimarekani 69.4 bilioni mwaka huu.

Shirika hilo lenye makao yake makuu Washington Marekani lilipunguza tarajio la ukuaji uchumi wa nchi hiyo kutoka asilimia 6.1 hadi 5.3 likitaja uwezekano wa kuwepo kwa hali ya kisiasaa isiyo tulivu.

Matokeo ya uchaguzi yaliyobishaniwa vikali miaka kumi iliyopita yaliibua vurugu zilizodumu miezi miwili na kuacha vifo vya watu 1,100.

Mwaka 2013 Kenyatta mwenye umri wa miaka 55 alishinda kwa kupata asilimia 50.07 ya kura, huku mpinzani wake Raila Odinga, ambaye mwaka 2007 alikuwa wa pili kwa Mwai Kibaki.

Wapinzani walidai matokeo ya kura katika chaguzi zote hizo mbili yalikuwa ya kupikwa. Ripoti ya Versik inasema ushindi wa Kenyatta unaweza kuibua vurugu hasa katika ngome kuu za upinzani katika miji.

Kwa upande wake taasisi ya Ipsos Kenya inayoendesha tafiti pamoja na kura za maoni imesema wiki iliyopita kwamba rais Kenyatta na naibu wake William Ruto wameshindwa kuongeza ukubwa wa ngome zao za ufuasi kwa zaidi ya asilimia 50 kuanzia 2013.

Inasema hii inanonesha kuwepo kwa matokeo ambayo yatakaribiana sana iwapo upigaji kura utakuwa katika misingi ya ukabila.

Wachunguzi wengine wanasema manung’uniko ya wananchi kuhusu kupanda kwa gharama za maisha nchini Kenya, hali ambayo pia imeshuhudia upungufu wa unga wa mahindi, kunaweza kumsaidia Raila kupata kura za kutosha na kulazimisha marudio.

Taasisi hiyo inaongeza kwa kusema kwamba bado kuna nafasi kwa Odinga kujiongezea wapigakura wanaomuunga mkono hasa wale wa Kenyatta wasiyoridhishwa na sera zake.

Hata hivyo inasema utokezaji wa wapigakura na uhamasishaji mkubwa unaoweza kufanywa na chama cha Jubilee unaweza kumsaidia Kenyatta kupata ushindi mwembaba katika duru la kwanza la uchaguzi, hivyo kutolazimika kufanyika kwa marudio.