Home Habari Uhuru akomaa Katiba kufanyiwa marekebisho Kenya

Uhuru akomaa Katiba kufanyiwa marekebisho Kenya

2324
0
SHARE
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta

NA ISIJI DOMINIC 

KUNA kila dalili Wakenya wakapiga kura ya maoni kufanyia marekebisho Katiba iliyopitishwa mwaka 2010 baada ya machafuko ya kisiasa yaliyotokana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2007. 

Ikumbukwe kuwa moja ya ahadi waliyotoa muungano wa vyama vya siasa kupitia mwamvuli wa NARC kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2002 uliyohitimisha utawala wa chama cha KANU tangu Kenya ipate uhuru mwaka 1963, ilikuwa ni kubadilisha Katiba ndani ya siku 100. 

Hata hivyo hilo lilishindikana na matokeo yake ni mtafaruku mkubwa ukaibuka kati ya aliyekuwa Rais Mwai Kibaki na Raila Odinga ambaye alikuwa moja wa mawaziri wake. 

Raila na kundi lake walijiondoa serikalini na kurudi upinzani ambapo uchaguzi mkuu wa 2007, ulisababisha ghasia baada ya Kibaki kutangazwa mshindi na kuapishwa usiku. 

Ilibidi mataifa mengine yaingilie na jopo la upatanishi chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, marehemu Koffi Annan, Rais wa Awamu ya Tatu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa, na mke wa marehemu Nelson Mandela, Graca Machel, ilileta suluhu baina ya Kibaki na Raila. 

Mchakato wa kubadilisha Katiba ulianza na hatimaye kupatikana mwaka 2010 na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa uliopachikwa jina la ‘nusu mkate’ na kushuhudia Raila akiteuliwa Waziri Mkuu. 

Miaka 10 baadaye, Rais Uhuru Kenyatta ameonyesha kila dalili ya kufanyika marekebisho ya Katiba kupitia Building Bridges Initiative (BBI) iliyobuniwa kufuatia mapatano yake na Raila Machi 9, 2018.

Jopo kazi ya BBI ilizunguka nchi nzima kukusanya maoni na kuchapisha rasimu ya kwanza uliyozinduliwa mwishoni mwa mwaka jana huku Rais Uhuru akiwasisitizia Wakenya kusoma kwa makini na kutoa tena maoni. 

Kamati hiyo ya BBI chini ya Seneta wa Garissa, Yusuph Haji, imeelezwa kumaliza kuandaa ripoti ambayo hivi karibuni itawasilishwa kwa Rais Uhuru na Raila, huku mjadala mkubwa ukitarajiwa bungeni. 

Lakini kitendo cha Rais Uhuru kufanya mabadiliko ya wajumbe wa kamati mbalimbali ndani ya mabunge yote mawili; Kitaifa na Seneti, huku pia chama cha upinzani ODM nacho kikifanya mabadiliko, ni dhahiri hayo yote yanalenga kuhakikisha ripoti hiyo ya BBI haitapata pingamizi. 

Ikumbukwe kuwa baadhi ya wajumbe waliyoondolewa kwenye nyadhifa nyeti na kamati mbalimbali za Bunge, ni wale wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto ambao wanaonekana kikwazo kwa muswada wa marekebisho ya Katiba endapo itawasilishwa bungeni. 

Katika hotuba yake kwa taifa wakati wa sherehe za Madaraka Juni Mosi zilizofanyika viwanja vya Ikulu jijini Nairobi, Rais Uhuru alisema lengo si kubadilisha Katiba ya 2010 lakini kuifanyia maboresho. 

“Mwaka 2010, tuliunda na kupitisha Katiba mpya ambayo ilibadilisha kabisa Katiba iliyokuwa inatumika tangu uhuru. Miaka 10 baadaye, nipo tayari kutambua marekebisho yanahitajika. Huu sio muda wa kubadilisha Katika ya 2010 lakini muda wa kuifanyia maboresho,” alisema Rais katika hotuba yake wakati wa sherehe za 57 za Madaraka ambazo pia zilihudhuriwa na Naibu Rais Ruto na Raila miongoni mwa watu wengine mashuhuri. 

Uhuru amesisitiza sasa ndiyo muda muafaka wa kuweka sawa kile ambacho kilikwenda kombo kwenye Katiba ya 2010, akiamini marekebisho hayo yatawaunganisha zaidi Wakenya na kuondoa wasiwasi na fujo kila inapofika kipindi cha uchaguzi mkuu.

Tangu Kenya irudishe mfumo wa vyama vingi 1990 na kupelekea kufanyika uchaguzi mkuu wa kwanza 1992, hadi sasa zimefanyika uchaguzi mkuu sita huku ule wa 2002 tu ukifanyika kwa amani pasipo na vurugu. 

Ulikuwa uchaguzi ambao pia ulishuhudia utawala wa miaka 24 wa Hayati Mzee Daniel arap Moi na hususan chama cha KANU ukifika kikomo. Tofauti na wengi walivyodhani, Mzee Moi amkabidhi Kibaki kwa amani madaraka huku kiongozi wa KANU wakati huo, Uhuru, akikubali matokeo na kuchukua kiti cha Kiongozi wa Upinzani. 

Rais Uhuru ameshuhudia namna watu wanavyopoteza maisha na mali kila inapofika uchaguzi mkuu na anaamini Katiba iliyopitishwa 2010, ikifanyiwa marekebisho kwa kuzingatia mapendekezo ya wananchi yaliyowasiliswa kwa jopo kazi ya BBI, hakutakuwa tena na suala la hofu kila baada ya miaka mitano. 

“Tusiwe waoga kubadilisha mfumo huu kama haituhudumii wakati tuliyopo,”alisema Rais katika hotuba yake iliyotoa ishara ya kufanyika marekebisho ya Katiba kabla mwaka huu haujamalizika. 

Aidha dalili za Wakenya kupiga kura ya maoni kuhusu marekebisho ya Katiba yalishaanza kuonekana kwa namna Raila alivyokuwa anazunguka baadhi ya kaunti kuhamaisha kuungwa mkono kwa ripoti ya BBI kabla ya mlipuko ya janga la virusi vya corona iliyopelekea Serikali kusitisha shughuli zote za mikusanyiko ikiwemo mikutano ya siasa. 

“Wakati wa mapumziko kutokana na mlipuko wa Covid-19, tuliwapa nafasi kamati ya BBI kuendelea na kazi yao ya kuweka sawa mapendekezo ya wananchi yaliyowasilishwa kwenye mikutano na kazi ipo katika hatua nzuri. Ripoti hiyo itawasilishwa kwa mabunge yote mawili kisha upigaji kura ya maoni utafuata ikiwezekana kabla mwisho wa mwaka huu,” alinukuliwa kiongozi huyo wa ODM.

Moja wa watu wa karibu na jopo kazi la BBI, alisema hakuna ubishi nchi inaelekea kupiga kura ya maoni hivi karibuni na kwamba tayari swali la zoezi hilo limeshapendekezwa. 

“Swali linalopendekezwa ni ‘Je, unakubali mapendekezo ya marekibisho ya Katiba?’ lakini bado itategemea ruhusa kutoka kwa wataalamu kulingana na mapendekezo ya kamati ya BBI,” alisema. 

Alidokeza kuwa utekelezaji wa ripoti ya BBI utachukua mfumo wa sehemu tatu: utawala, kupitia Bunge na mwishowe kura ya maoni ya kitaifa.

Bunge tayari lipo katika mkao wa kupitisha ripoti hiyo kufuatia Kiranja wa Waliowengi Bunge la Senati, Irungu Kang’ata, na mwenzake wa Bunge la Kitaifa, Junet Mohammed, kusisitiza kura ya maoni itafanyika kabla ya mwaka kuisha. 

“Ndiyo, kura ya maoni itafanyika. Bajeti imeshatenga fedha kwa zoezi hilo… Tatizo pekee ni janga la Covid-19 lakini ifikapo Septemba tutakuwa tumefungua nchi hivyo kura ya maoni kufanyika Oktoba,” alisema Kang’ata.

Ni kauli ambayo iliungwa mkono na Mohammed na Mbunge wa Kieni, Kanini Kega, ambaye ni rafiki wa karibu wa Rais Uhuru.

“Nina uhakika tutafanya hivyo kabla ya mwisho wa mwaka huu ukizingatia haitakuwa mashindano lakini kuidhinisha,” alisema Kega huku akiongeza kikwazo pekee mwaka huu ni bajeti iliyosomwa wiki iliyopita, namna ya kushughulikia Covid-19 na kushughulikia miswada katika mabunge yote mawili. 

Wataalamu wa Katiba nao wanatoa maoni yao tofauti na tamko la Rais Uhuru kwamba huu ndiyo wakati wa kufanya marekebisho kwa Katiba ya 2010. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mawakili Abdikadir Mohammed, Bobby Mkangi na Ekuro Aukot walisema marekebisho hayo anayoyasema Rais yanawahusu zaidi wasomi wa kisiasa na sio Wakenya wa kawaida.

Aukot, ambaye ni mjumbe wa zamani wa Kamati ya Wataalamu Kuhakiki Katiba alisema marekebisho yanafanyika tu wakati kuna shida.

“Sudan Kusini baada ya uhuru wao walikumbwa na wakati wa marekebisho ya katiba. Liberia baada ya vita ya miaka 14 kumalizika walihitaji kuandika katiba mpya. Hizo ndizo vitu vinavyopelekea kufanyika marekebisho ya katiba,” alisema Aukot ambaye katika uchaguzi mkuu uliopita aligombea urais kupitia chama cha Thirdway Alliance.

Alisema Kenya haina presha ya katiba mpya lakini inahitaji kuwekeza katika maeneo yatakayoangazia afya, elimu na miundombinu miongoni mwa sekta zingine.

Naye Abdikadir alisema Wakenya wakati huu wanataka mapendekezo yatakayotoa mwanga wa changamoto wanazopitia huku akihoji ni kwanini wanasiasa wasishinikiza utekelezaji wa sheria?