Home Makala Kimataifa Uingereza ni Tai aliyechoka kuwinda ndege wa Afrika

Uingereza ni Tai aliyechoka kuwinda ndege wa Afrika

2073
0
SHARE

NA IGAMANYWA LAITON

TAI ni ndege mwenye sifa za kipekee sana, kati ya ndege wala nyama yeye amekuwa maarufu kuliko ndege wengine kufikia kuwekwa katika nembo za mataifa mbalimbali duniani.

Tai ana sifa nyingine pekee kama vile huruka juu zaidi ya ndege wengine katika anga la juu zaidi. Kamwe haruki na ndege wa aina wengine kama wale kunguru, kwezi, au mbayumbayu.

Aidha, pia wana sifa pekee ya kunuia kitu yaani kama ameamua kuhakikisha anafanya jambo basi huhakikisha anaitimiza. Kwa mfano kama amenuia kunyakua kifaranga aliyemuaona umbali wa kilometa tano huhakikisha amelenga shabaha na kuteremka kwa kasi kunyakuwa windo hilo  lake bila kuruhusu hali yoyote imzuie au  kuingiliana na mpango wake wa kunyakua windo lake.

Sifa nyingine pekee ya Tai ni huwa hali vibudu au vya kutafutiwa na ndege wengine hii ikimaanisha kuwa Tai huwa hakubali kuwindiwa na ndege wengine, hutaka kula kile alichowinda mwenyewe. Kwamba kushirikiana na ndege wengine katika windo kwake yeye ni mwiko.

Kuna sifa nyingine pekee ya ya Tai, kujiridhisha katika nguvu za ujana kwa kuchukua hatua muhimu na yenye maumivu. Inasemekena kadri umri unavyokwenda manyoya yake huzeeka na kumpunguzia nguvu ya kuwinda na kupaa, na kucha zake pia huwa butu katika kunyakuwa windo.

Inaelezwa pia Tai huchukua uamuzi muhimu na hatari wa kujitoa manyoya yote mwilini, zoezi ambalo huwa ni lenye maumivu na hatari kwa kuwa linaweza kusababisha kifo. Vilevile inasemekana pia huchukua uamuzi wa kunoa kucha na midomo yake katika miamba kama vile mchinjaji wa kuku anoavyo kisu katika jiwe.

Zoezi hilo linadaiwa huwa ni la maumivu makubwa, lakini humpatia Tai sifa za kipekee na za kishujaa azifanyazo ili kujirudisha katika nguvu zake za ujana na kuendeleza mawindo.

Mwaka 1997 wakati chama cha Labour kikishika hatamu ya uongozi katika nchi ya Uingereza, chini ya Tony Blair mapema alionesha wazi wazi kutokuwa na mapenzi na jambo lolote kuhusu Afrika.

Kati ya vipaumbele vyake bara la Afrika halikuwa na nafasi, lakini  baada ya miaka kumi ya Utawala wa kinyume Afrika iligeuka kuwa wazo na dhamira kuu ya siasa za Uingereza na Tony Blair mwenyewe, hasa katika sera ya mambo ya nje, ndani ya Utawala wake maelfu ya wanajeshi walitumwa Sierra Leone, akazidisha mara tatu kiwango cha misaada iliyokuwa ikitolewa Afrika na serikali ya Uingereza.

Akashika Uenyekiti wa vikao mbali mbali vilivyokuwa na ajenda mbalimbali kama vile kuzungumzia masuala ya usalama, uchumi na kisiasa zililizokuwa zikilihusu bara la Afrika. Akajisogeza karibu zaidi na viongozi wa nchi za Afrika. Akafanya ziara mbalimbali kulizunguka Afrika.

Nini kilichobadilisha mtizamo wa Tony Blair kulihusu bara la Afrika? Kwa mamia ya miaka Afrika imekuwa msingi muhimu katika ujenzi wa Ulaya kiujumla.  Tony Blair alishtukia umuhimu wa Afrika baada ya kukaa madarakani kwa muda na kuelewa vizuri jinsi Uingereza ilivyokuwa ikilihitaji bara la Afrika katika kusimama kiuchumi kwa kutegemea rasilimali na Soko kutoka Afrika.

KWA NINI ALIBADILI MTIZAMO WAKE?

Miaka kumi ya serikali ya chama cha Labour kulitawaliwa na hofu ya kutokea matatizo katika upatikanaji wa nishati ya mafuta, sababu zikiwa ni mambo mawili kwanza kukua kwa viwanda katika bara la Asia.

Pili kuzorota kwa usalama katika nchi wazalishaji wa mafuta, ikichangiwa na vita kama ile ya Iraki, ushindani,umuhimu wa mafuta na hofu ya kuadimika kwa mafuta duniani mambo yaliyosababisha kuipa ung’amuzi serikali ya Tony Blair na chama chake cha Labour kutoka katika usingizi, kila nchi duniani ilikuwa barabarani kutafuta  mahala popote duniani penye hifadhi ya mafuta(kama vile ndege wazururavyo angani kutafuta mawindo yao) na kuhakikisha inakuwa na mahusiano na nchi zilizokuwa na hifadhi kubwa ya mafuta.

Wakati huo nchi kadhaa barani Afrika zilikuwa tayari na hifadhi ya mafuta ardhini nchi hizo ni Angola, Nigeria, Sudani na Ghuba ya Guinea. Pia utafiti ulikuwa umeonesha kuwa nchi za Afrika mashariki na ukanda wa pwani ya Afrika mashariki kuna hifadhi kubwa ya mafuta.

Ripoti ya Tume ya Afrika iliyotolewa na EU ilieleza kuwa inakadiriwa kuwa Afrika ina zaidi ya asilimia 25 ya Mafuta duniani. Uingereza kama nchi iliyokuwa imendelea kiviwanda ilihitaji Afrika kuliko Tony Blair alivyodhani chini ya serikali yake mtizamo na malengo yake kuelekea bara la Afrika yalibadirika haraka sana.

Kwa mfano Uingereza kupitia shirika lake la mafuta la Bristish Petroleum (BP) ilikuwa mwekezaji anayeongoza katika mtaji na operesheni ya uchimbaji wa mafuta nchini Angola. Pia Anglo- Dutch Shell Oil Company (shirika tanzu kati ya Muingereza na Muholanzi) lilikuwa ni shirika lenye nguvu na mtaji mkubwa kuliko yote nchini Nigeria.

Tukiweka suala la nishati ya mafuta pembeni maslahi ya Muingereza Afrika ni mapana zaidi, kwa  mfano mashirika ya Muingereza kama vile Rio-Tinto, Anglo-American, Lonrho na Ashanti Gold yamewekeza mitaji mikubwa katika Afrika.