Home Latest News UKITAKA KUMDANGANYA MWAFRIKA, MDANGANYE MSOMI (2)

UKITAKA KUMDANGANYA MWAFRIKA, MDANGANYE MSOMI (2)

1771
0
SHARE

Na Victor Makinda

Kama ilivyo ada  na kauli mbiu ya gazeti la Rai, kwamba kinachozingatiwa hapa ni nguvu ya hoja na kamwe hatuzipi nafasi hoja za nguvu kwani hoja za nguvu huzaa ukandamizwaji, uonezi, majivuni, kujisikia, kudhani kuwa wewe pekee ndio una mtazamo thabiti , uteswaji na ukikwaji wa demokrasia.Tanzania ni nchi ya kidemokrasia. Demokrasia ni kushindanisha hoja. Hoja za nguvu sio demokrasia bali nguvu ya hoja ndio demakrasia.

Wasomaji wangu wa safu hii kwanza nianze kwa kuwashukuru kwa namna ambayo mmekuwa ni wafuatiliaji na wasomaji msipitwa na nakala ya gazeti Rai. Wengi wenu hawaishii kusoma tu bali wamekuwa wakinipigia simu na kunitumia ujumbe wa maoni juu ya kile kinachoandikwa. Ninawashukuru wote ambao mmekuwa mkitumia Nguvu ya hoja kujenga hoja zenu na mijadala mipana juu ya mada zangu ukumbini hapa.

Hoja za nguvu zilizo kinyume na ngunvu ya hoja, nazo pia niwashukuru ambao mmekuwa mkizitoa kwangu ijapokuwa zinakwenda kinyume na demokrasia inayosisitia uhuru wa maoni lakini sio maoni yenye hoja za nguvu, bali ni maoni yenye nguzu za hoja. Lengo letu kubwa ni kuhakikisha kuwa tunafanya kazi moja  tu muhimu nayo ni kurekebisha palipopindishwa na kuucha ukweli ulivyo ukitamalaki. Hoja za nguvu ni maoni na mtazamo wa mtu binafsi lakini ninawashauri wale wote wenye kutumia hoja za nguvu kuacha kufanya hivyo na wazigeukie nguvu za hoja kwa mustakabari wa ujenzi wa demokrasia na uhuru wa mawazo yenye kujenga.

Wiki ilopita nilianza mfululizo wa makala haya, Ukitaka kumdanganya Mwafrika mdanganye msomi. Nimepata jumbe na simu nyingi. Niliahidi kuuendeleza mjadala huu, ninawaalika tena tuuendeleze mjadala huu na  tuipanue hoja kwa manufaa ya Watanzania na bara letu la Afrika kwa ujumla wake.

Msomaji mmoja kati ya wasomaji wangu wengi walionipigia na kunitumia jumbe za simu, ameniuliza kuwa nini kifanyike ili waafrika wasomi waache kurubuniwa na kuendelea kuwarubuni na kuwakandamiza waafrika wasio wasomi?

Swali hili linajibiwa swali kwa nini waafrika wasomi wanakengeuka na usomi wao na kuwahadaa, kuwanyanyasa na kuwauza waafrika wasio wasomi.? Majibu ya swali hili niliyatoa katika makala ya wiki jana.  Nadhani ni muhimu sasa  kuangazia kwa kina kitu gani waafrika tusio wasomi tukifanye ili tuwadhibiti kikamilifu waafrika  wasomi.

Sifa za mtu kuwa kiongozi

Nilisema wiki jana  kuwa waafrika kwa kuwa tunawaamini sana waafrika wenzetu wasomi, tunawapa madaraka ya kutuongoza na kutuamulia mambo yetu. Hii inawafanya waafrika hawa wasomi kuwa na maamuzi juu ya hatma ya maisha yetu, kiasiasa, kiuchumi, kiulinzi na hata kiutamaduni. Kama hali ndiyo hiyo, je nani anafaa kuwa kiongozi, msomi au asiye msomi? Ukweli unabaki pale pale kuwa hatuwezi kwenda kinyume na ulimwengu unavyokwenda. Ni lazima twende na kuenenda kadri ya ulimwengu ulivyo. Usomi unabaki kuwa sifa ya kuwa kiongozi. Hatuwezi kuwakwepa viongozi wasomi na kuwapachika wasio wasomi. Je ni viwango gani vya elimu viwe ni sifa ya mtu mtu kuwa kiongozi wa kisiasa? Jibu ni kwamba kiwango chochote cha elimu kinafaa mtu kuwa kiongozi. Kujua kusoma na kuandika kunatosha kumfanya mtu kuwa kiongozi? Hili ni swali linalowakanganya wengi.  Na tafsiri halisi ya nani msomi imebaki kuwa ni ngumu.

Binafsi nina tafsiri tofauti juu ya dhana ya usomi. Kuna kusoma na kueleimika. Huwezi kuelimika juu ya jambo fulani pasipo kusoma kuhusu jambo hilo. Wapo waliosoma lakini wakaishia kusoma tu na kufaulu vizuri katika mitihamni yao.

Wapo waliosoma na kuleimika pia. Lakini wapo wasomi/waliosoma ambao waliishia kusoma tu pasipo kuelimika kwa kile walichokisoma. Izingatiwe kuwa kusoma na kuelimika ni kusoma na kuitumia elimu uliyoipata kuwakomboa na kuwasaidia wahitaji. Usomi usio na tija kwa jamii yako  unaishia kuitwa msomi lakini hujaelimika kwa kuwa elimu yako haijasaidia watu wa jamii yako.  Wasomi wa kiafrika wengi wao ni wasomi tu na hawajaeleimika.  Wana elimu ya makaratasi isiyo na tafrisi hali halisi na imewaondolea uzalendo. Kwani usomi/elimu waliyoipata imetumika kinyume na matarajio ya jamii watokazo. Imegeuka kutoka kuwakomboa wahitaji mpaka kuwakandamiza wahitaji.

Suluhu yetu itatoka wapi? Suluhu yetu ni kubadili fikra zetu. Ni kubadili mifumo kandamizi na onezi dhidi ya tabaka la waafrika wasio  wasomi. Waafrika tubadilike, tuwe wakali  na tuutilie maanani uzalendo kama sifa pekee ya kuwapa watu kazi ya kutuongoza.

Ndiyo, nasema uzalendo kwa kuwa hii ni dhana inayotakiwa kuzingatiwa na kusimamiwa kwa kiwango kikubwa. Mzalendo awe msomi au asiye msomi anabaki kuwa ni mzalendo tu.

Labda tutajiuliza mzalendo ni nani? Mzalendo ni mtu yoyote Yule ambaye yupo tayari kupambana kwa hali na mali kuhakikisha maslahi ya walio wengi hasa hasa wanyonge yanalindwa.

Mzalendo ni mtu yule ambaye yupo tayari kusema hapana kwa mabepari na wanyonyaji dhidi ya tabaka la chinim dhidi ya Taifa.

Mzalendo ni mtu yoyote aliye tayari kupambana na mifumo kandamizi ya ndani na  nje ya nchi yake kuhakikisha kuwa wananchi anaowaongoza hawapatwi na madhira ya kukosa huduma muhimu, mzalendo hajilimbikizii mali, hatumii cheo chake kama dhamana ya matwaka yake kwa manufaa yake na jamaa zake, bali hutumia rasilimali za Taifa lake  kwa maslahi mapana ya wananchi wote. Mzalendo husimamia rasilimali za nchi yake na pia anakuwa tayari kuchukiwa, kugombana na kununiwa na mabepari na mabeberu kwa ajili ya manufaa na Taifa lake. Mwenye sifa hizo anafaa kuwa kiongzozi wetu hata kama ana elimu ndogo. Cha msingi jamii za kiafrika ziwe na katiba rafiki wa maendeleo na demokrasia pana. Viongozi waheshimu katiba hizo na kuziishi katika maisha yao ya uongozi.

Naam waafrika njia pekee ya kuondoa dhana ya kuendelea kunyanyaswa, kukandamizwa, kuuzwa na kuonewa na waafrika wenzetu wasomi ni kuhakikisha tunawapa madaraka na vyeo waafrika wenzetu iwe ni wasomi au wasio wasomi malmaladi tu mwafrika huyo ana sifa ya uzalendo uliotuka kwa nchi yake.

Elimu isiwe ni kigezo pekee cha kuwa kiongozi. Yapo na zipo baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa zikizingatia na kutilia maanani elimu tu kama kigezo cha kuwa kiongozi. Ukweli ulivyo elimu isiwe kigezo pekee, bali kigezo pekee kiwe ni uzalendo, uwezo wa kujitoa na kujitole, uchungu na uchu wa maendeleo  kujumlisha ubunifu wa njia thabiti za kupambana na changamoto zinazowakabili  jamii ya wahitaji.