Home Makala Unafiki utachelewesha upinzani wa kweli

Unafiki utachelewesha upinzani wa kweli

1728
0
SHARE

UNAFIKI ni hali ya kujifanya kuwa ni rafiki na hali ni adui, hali ya kutokuwa mkweli, nifaki, gea. Tafsiri hii ni kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, toleo la pili.

Kwa tafasiri hiyo ni bayana baadhi ya viongozi wa juu wa vyama vya siasa nchini hasa vile vya upinzani wanafanya unafiki katika harakati zao za kusaka dola.

Wapo ndani ya vyama vyao kwa maslahi yao, ingawa wamejifunika mwamvuli wa mageuzi ya kiutawala.

Waongo. Ni wanafiki na hivyo ndivyo walivyo, wengi wao  ni magawadi na vijumbe, wanaoishi kama gaogao majini huku wakifurahia gawo kutoka kwa mabwana zao.

Mikono yao wameifunga gao, imenasa fulusi kwa mnaso wa gamu, wanasikia raha wakiingiza na kutoa visivyo vyao, vinavyowalewesha mpaka lupwili. Ni kama walevi wa mataputapu.Hawana tofauti.

Hawana izara, haya wala soni, nyuso zimewaparama kwa kugombea njuluku zinazotolewa kwa maelekezo maalum, na kuwalazimisha kuudanganya umma kwamba wao ndio wakombozi wa kweli. Unafiki mtupu!

Walikuwapo, wapo na wataendelea kuwapo, si wapinzani ni wanafiki na washindani wanaoshindana wao kwa wao kwa sababu zile zile za uroho.Uroho wa dinari.

Hakika ni unafiki. Ni unafiki kwa sababu yanayotukia leo ndani ya Chama cha Wananchi –CUF si mapya kwa upya wa kimwenendo. Ni mwelendelezo wa safari ya Izraili ndani ya vyama vya siasa iliyoanza tangu kale.

Ni wao, wanaojiona kama makuhani wakuu, walioshikilia itilo katikati ya Bahari. Kwa makusudi wanaiachia ili mashua izame.

Nia na dhamira yao ni kutoyafikia maji ya upondo yatakayowafikisha fukweni salama, kiu yao ni kuendelea kutangatanga bahari kuu, huku wakiendelea kudanganya kuwa wamebeba dhamana ya kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani. Hizi ni sawa na hekaheka za mwenda tezi na Omo, arejeae ngamani. Uongo mtupu!

Mgogoro uliopo ndani ya CUF kwa sasa ni wa kupikwa na umepikwa kwa nia ile ile ya kujidhoofisha, lakini sasa lengo likiwa pana zaidi. Lengo la sasa ni kudhoofishana kile kinachoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao na wenyewe umejawa sura ile ile ya kinaa.

Ni ukweli usiopingika kuwa CUF kwa sasa hakina nguvu za kisiasa za kutosha Tanzania Bara, ukilinganisha na kilivyo Zanzibar, kimesalia jina na historia yake ya ngangari na jino kwa jino, haina matao tena zaidi inawayawaya kama hamsa mbovu kwa muuza kahawa.

Chama hicho kwa makusudi kinapitishwa kwenye pito la kisaliti, pito la kifedhuli linalohalalishwa na wajanja wengi kwa maslahi ya wachache.

Kwa hali hiyo ni wazi salio lililosalia kwa wenye mapenzi mema na chama hicho ni kuomba ardhilhali kwa wakubwa ili wakionee huruma na pengine kukiacha au kukigeuza chao kama kilivyofanywa chama cha mzee wa Kiraracha.

Kwa mwenendo huu, siuoni upinzani ukiingia Ikulu, siuoni hata kwa kutumia tundu la kivo kilichokauka kau mithili ya mbata.

Mauzauza haya hasa yanawahusisha majemedari wawili na wapambe wao ambao nina hakika wengi wa walio nyuma ya makuhani hao wanaicheza ngoma wasiyoijua.

Nasema wanacheza ngoma wasiyoijua kwa sababu, baadhi ya wakubwa zao ambao ndio vinara hawajawahi kufikiria kukifikisha chama hicho malishoni hata siku moja. Mara zote wamekuwa wakifikiri wao kwa niaba ya wengi.

Wamekuwa wakifanya hivyo kwa sababu kadha wa kadha. Pengine yatupasa kukumbuka kuwa mgogoro huu si wa kwanza na kamwe hautakuwa wa mwisho si kwa CUF tu bali hata kwa vyama vyote vya siasa vya upinzani.

Mgogoro huu wa kiuongozi ambao mrengo wake ni wa kimabavu zaidi ni wa tano ukitanguliwa na ule uliomuhusisha James Mapalala, Naila Jidawi, Michael Nyaluba na Hamad Rashid.

Wanaoujua unafiki unaoendelea sasa ndani ya chama hicho wanaweka wazi kuwa huu si mgogoro kwa maana hauwezi kuwatikisa, badala yake unaimarisha nia na dhamira zao mbele ya nyuso za wadanganyika.

Wanayasema hayo kwa sababu wanatambua wazi kuwa haijawahi kutokea hata siku moja dhamira ya dhati ya chama hicho na vyama vingine vya upinzani kuiondoa CCM madarakani, ukweli huu ni tangu kuumbwa na kurejea kwa siasa za upinzani nchini. Kwa uongozi huu wa sasa uliotawaliwa na kizazi cha zidumu fikra za Mwenyekiti. Haitakuja kutokea.

Kwa wale wasiojua wanaweza kudhani na kuamini kuwa ndani ya chama hicho upo mgogoro mzito na mkubwa unaoweza kukipoteza chama hicho! Hilo halipo.

Halipo kabisa, kwa sababu hata NCCR-Mageuzi ya leo, nayo ilipita hapa inapopita CUF leo. NCCR- Mageuzi iliingia kwenye mgogoro uliokigawa chama hicho makundi mawili.

Kundi moja lilikuwa likimuhusisha mwalikwa ambaye alipewa uenyekiti wa chama hicho,  Augustine Mrema na watu waliokuwa wakimuunga mkono na kundi la pili lilikuwa chini ya Katibu Mkuu wake, Mabere Marando.

Mgogoro huo uliwalazimisha wawili hao kugawana ofisi, Mwenyekiti Mrema alipewa hifadhi kwenye ofisi za Thomas Ngawaiya ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa chama hicho, huku Marando na kundi lake walijihifadhi kwenye ofisi zao mpya zilizokuwa ndani ya kontena katika eneo la Kisutu.

Kwa wenye jicho pofu waliuona ule kama mgogoro mzito, lakini wajuzi wa mambo waliutazama kama mwanzo wa kufanikisha dhamira ya kukiimarisha chama hicho chini ya uongozi wa wenye nacho, ambao mara zote masikio na macho yao hayako tayari kuona upinzani wa kweli ukishamiri.

Hali hii bado inaendelea na itaendelea mpaka pale kizazi cha usaliti na unafiki kitakapofutika na ili kifutike ni lazima yafanyike mapinduzi ya kifikra, mpango ambao utachukua miaka dahari.

Ili upinzani usadifu nia na dhamira yao ni budi kujiua ili uzaliwe upya na njia pekee ya kuchukua uamuzi huo mgumu ni walipo sasa kuwa na utayari wa kuwaachia wengine. Hasa vijana huku wale wakongwe wakisalia kuwa watazamaji tu.