Home Makala URAFIKI WA VIONGOZI NI ITIKADI AU MASILAHI BINAFSI?

URAFIKI WA VIONGOZI NI ITIKADI AU MASILAHI BINAFSI?

1547
0
SHARE
Mwalimu Nyerere (kulia) akisalimiana na Fidel Castro

NA MARKUS MPANGALA


 MARA nyingi tumesikia kuhusiana na urafiki wa viongozi mbalimbali duniani. Vilevile tumesikia urafiki wa nchi moja na nyingine katika sehemu taofauti hapa hapa duniani. Urafiki wa viongozi unaweza kuathiri mambo mengi sana katika maisha yao binafsi au uongozi wao kwa ujumla. Athari hiyo inaweza kuwa mbaya au nzuri kwa namna moja ama nyingine.

Kwa mfano, Mwalimu Nyerere alikuwa rafiki wa Fidel Castro. Urafiki wao ukachangia mahusiano mazuri kati ya Cuba na Tanzania. Nchi zote mbili zilibadilishana wataalamu. Zote zilikuwa kwenye umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM).

Tanzania pia imekuwa na mahusiano mazuri na nchi ya China. Tangu zama za akina Mao Tse Tung, Chou Enlai, Deng Xiaoping, Hu Jintao hadi Xi Jinping tumekuwa karibu nao kwa kiasi kikubwa. Urafiki wa China na Tanzania unajikita kwenye suala la itikadi. Nchi zote mbili zimekuwa zikiamini katika itikadi ya ujamaa. Mwanzo wa urafiki wao umejikita katika misingi ya itikadi. Ni China ndiyo ilimpa somo Mwalimu Nyerere ambaye alikuja kuanzisha vijiji vya Ujamaa.

Kwetu Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, tumeyaona hayo katika Mji wa Lituhi na maeneo ya karibu ambapo watu mbalimbali wahamishwa kutokana na ardhi ya eneo hilo kutokuwa na uwezo mkubwa wa uzalishaji. China na Tanzania zimeshikamana hadi sasa.

Marais wawili wa China wa miaka ya karibuni wametembelea Tanzania. Hu Jintao na Xi Jinping wamekuja nchini katika utawala wa Rais Mstaafu Kanali Jakaya Kikwete. Kwenye urafiki wa China na Tanzania tunalo jawabu la itikadi.

Wakati mwingine kuna ule urafiki wa viongozi watupu pasipo kuhusishwa nchi. Hapana shaka yoyote Mwalimu Nyerere alikuwa rafiki wa Rais wa zamani wa Marekani, John F. Kennedy. Wengine wanatafsiri kutokana na Ukatoliki wa Kennedy ulimfanya awe karibu na Nyerere.

Baadhi wanasema ni kutokana na viongozi hao wenyewe kukubaliana kwa mambo mengi ingawaje walitofautiana kuhusiana na itikadi za nchi zao. Nyerere aliongoza taifa lililofuata itikadi ya Ujamaa, wakati Kennedy aliongoza taifa la kibepari lililojikita kwenye ubeberu mkongwe. Hata hivyo, urafiki wa Nyerere na Kennedy haukufua dafu ule wa Cuba pamoja na China kwa Tanzania.

Joyce Banda hakuwa rafiki wa Jakaya Kikwete, lakini Malawi na Tanzania zilibaki kuwa marafiki licha ya kupitia nyakati ngumu za kugombea umiliki na mpaka wa Ziwa Nyasa. Pengine Rais Banda alikuwa rafiki mzuri wa Uingereza na mataifa mengine ya magharibi ndiyo maana alikuwa tayari kumkamata Rais wa Sudan, Omar al Bashir anayetetewa na viongozi wengi wa Afrika.

Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, mzawa wa Kijiji cha Lupaso, mkoani Mtwara, anatajwa kumhusudu zaidi Rais Mstaafu wa Kenya, Daniel Arap Moi, ambaye hakuwa rafiki wa Mwalimu Nyerere. Na vilevile Yoweri Museveni anatajwa kumhusudu zaidi Mwalimu Nyerere na Tanzania yetu.

Museveni anatajwa kati ya marais ‘watiifu’ kwa Tanzania. Urafiki wa Museveni na Tanzania unatokana na historia mbili; elimu yake aliyoipata akiwa hapa nchini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na mapambano ya kuikomboa Uganda kutoka kwenye makucha ya Nduli Idd Amini ambayo alianzia safari yake hiyo hapa nchini (tunaweza kurejea tukio la The Moshi Conference).

Katika historia zao za ukombozi, Joseph Kabila na baba yake Laurent Desire Kabila, walikuwa na uhusiano mzuri na Mwalimu Nyerere pamoja na Tanzania kwa ujumla. Ukaribu huo ulitengeneza mahusiano mazuri baina ya pande hizo mbili.

Rais Mstaafu Kanali Jakaya Kikwete hakuwa na urafiki wowote na Paul Kagame wa Rwanda. Uhusiano mbaya baina ya Kikwete na Kagame ulivifikia vyombo vya habari na vikaripoti kwa nguvu. Hatuwezi kujua undani zaidi wa “kukorofishana” kwao ingawa ilielezwa ulianzia kwenye mkutano wa Umoja wa Afrika nchini Ethiopia, ambapo Kikwete alipendekeza kwa Kagame kuketi mezani na waasi wanaopigana na serikali yake.

Hata hivyo, tunafahamu hawakupikika chungu kimoja. Madhara ya uhusiano mbaya baina ya Kagame na Kikwete ulisababisha kuyumba kwa “ujirani” wa Tanzania na Rwanda katika awamu ya mwisho ya  utawala wa serikali ya Kikwete.

Mojawapo wa matokea yake ni kuanzishwa kwa Umoja wa hiari COW (Coalition of the willing) ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wakati huo Tanzania iliamua kwenda mwendo wa kobe katika kuafiki makubaliano ya EAC ilipokuwa chini ya Kikwete. Lakini kila upande ulikuwa na sababu zake na ulilinda maslahi yake. Inafahamika bayana wawili hawa hawakuwa marafiki.

Tangu kuingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk. John Magufuli, mahusiano yetu na Rwanda yamebadilika. Tanzania na Rwanda tumeathiriwa na urafiki uliopo kati ya Magufuli na Kagame. Mara kadhaa Rais Magufuli amesema kuwa, “yeye” ni rafiki wa Kagame na wakati mwingine anaomba ushauri kwake.

Ndiyo kusema ukaribu wa Magufuli na Kagame umeleta uhusiano “mwema” baina ya nchi hizo mbili, ikiwamo kujenga kituo cha pamoja cha ukaguzi wa bandari (TPA) na bandari kavu ya Rwanda hapa nchini. Msingi wa urafiki huu bado haujulikani kama ni itikadi au mambo binafsi yenye maslahi ya pamoja na nchi zao, kwa sababu haikuwahi kutokea huko nyuma wakati ambao Rais wetu alikuwa waziri katika Serikali ya awamu ya nne ya Kanali Kikwete.

Lakini jambo moja kubwa unaloweza kujiuliza ni hili, urafiki wa viongozi wa aina hiyo huwa unazingatia itikadi au mambo binafsi? Kwamba kama Nyerere alikuwa rafiki wa Kennedy si Marekani. Lakini kwa Cuba tunaona Nyerere na Tanzania walishibana nayo sana nchi hiyo ya Fidel Castro. Urafiki wao ulijengwa kwa msingi wa itikadi pekee au kulikuwa na mambo binafsi?

Katika uongozi wa awamu ya nne wa Kanali Kikwete, ulikuwa kipenzi cha Marekani tofauti na Mwalimu Nyerere au Ali Hassan Mwinyi. Je, urafiki huo ulitokana na itikadi baina ya viongozi au mambo binafsi?

Ni swali hilo hilo unaweza kuuliza katika urafiki wa Rais Magufuli na Paul Kagame, unajengwa katika msingi gani, itikadi au mambo binafsi? Tunaweza kukisia kuwa wawili hawa wanakubaliana katika uchapaji wa kazi na kusaka maendeleo ya nchi zao. Je, hilo linatosheleza swali letu?

Tunao mfano mwingine, urafiki wa Raila Odinga na Rais Magufuli. Nakubali pia kuwa siasa zetu za wakati huu tumekuwa tukitazama urafiki na mahusiano ya viongozi badala ya itikadi na mrengo wa vyama vyetu kama tulivyozoea ndio maana tunapata shida hata katika kujenga utetezi au hoja juu ya itikadi ya vyama vyetu.

Kwa mfano, Rais wetu Magufuli na Raila Odinga wanashabihiana nini; itikadi ya vyama vyao au mambo binafsi? Urafiki mwingine nilioona hivi karibuni ni kati ya Chadema ya Freeman Mbowe na Chama cha Jubilee.

Uchaguzi wa mwaka 2013 Chadema walimuunga mkono Raila Odinga aliyekuwa akichuana na Uhuru Kenyatta. Mwaka 2017 Chadema wamekataa kumuunga mkono “Swahiba” wao Raila Odinga badala yake wameungana na Uhuru Kenyatta. Jawabu ni rahisi, Chadema hawataki kumuunga mkono rafiki wa Rais Magufuli, hivyo wanalazimika kuungana na Kenyatta kujenga kambi yao. Je, wanaungana kwa sababu ua itikadi za vyama vyao au mambo binafsi?

Ukiangalia umoja wa vyama vya kidemokrasia Afrika (DUA) vyama vya muungano wa NASA ni wanachama ikiwa pamoja na Chadema kwa hapa kwetu, leo kwa kuwa viongozi wetu wana mahaba yao tunakana misimamo ya pamoja tuliyokuwa nayo kwa kipindi kirefu.

Vivyo hivyo CCM imekuwa rafiki na vyama vyote vilivyopigania uhuru wa nchi mbalimbali ikiwa pamoja na KANU na muungano wa Jubilee ni zao la chama tawala lakini leo CCM imeshindwa kujitokeza ama na Nasa au Jubilee, kwangu mimi naliona kama tatizo katika siasa mambo leo.

Hitimisho letu linabaki pale pale kuwa urafiki wa viongozi au wanasiasa unatokana na itikadi za vyama vyao au maslahi binafsi ambayo yanajulikana au hayajulikani?