Home Latest News USHINDI WA CCM NA WALAKINI MKUBWA!

USHINDI WA CCM NA WALAKINI MKUBWA!

3144
0
SHARE

NA JULIUS MTATIRO,

JUMAPILI ya Januari 22, 2017, kulikuwa na uchaguzi wa marudio katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Marudio hayo yalihusisha jimbo moja la uchaguzi na kata 20 japokuwa awali Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilitangaza uchaguzi ungefanyika kwenye kata 22 kabla ya kupunguza mbili. Katika kata 20 zilizofanya uchaguzi, zote zinatoka Tanzania Bara na kwa namna moja au nyingine, wawakilishi wa kata hizo aidha walijiuzulu, kuondolewa na mahakama au kufariki. Zanzibar ndiko ambako kulikuwa na jimbo linaloshindaniwa, Dimani ambalo mbunge wake alifariki na nafasi hiyo kuwa wazi.

Ulipofanyika uchaguzi mkuu mwaka 2015, kata 17 kati ya 20 zilichukuliwa na wagombea wa CCM. Kata mbili kati ya hizo zilichukuliwa na Chadema na nyingine moja ilichukuliwa na CUF. Uchaguzi wa Januari 22, 2017, umeleta matokeo yanayofanana na yale yale ya mwaka 2015, japokuwa iko tofauti ndogo, kwani CCM imetetea viti vyake vyote na kuchukua kimoja cha Chadema na kingine cha CUF, Chadema imetetea kiti chake kimoja na kupoteza kimoja huku CUF ikipoteza kiti chake kimoja na kupoteza nafasi ya pili ambayo chama hicho kilikuwa nayo kwenye jumla ya kata nyingine tatu, nafasi ya CUF imechukuliwa na Chadema.

Zipo sababu muhimu ambazo zimeifanya CCM ishinde na kulinda ngome yake lakini pia kusogea mbele na kuvipora vyama vya Chadema na CUF kata moja kila kimoja, huku Chadema ikifanikiwa kulinda kata yake moja na kupoteza  moja kwa wakati huo huo. Leo tutaangazia sababu za kimfumo zinazosababisha hali hiyo na toleo lijalo tutaangazia sababu na mapungufu ndani ya vyama vya mbadala.

Sababu za kimfumo/kidola

Rushwa, hila na mbinu mbaya ni sababu ya kwanza inayolinda ushindi wa CCM. Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, aliwahi kusema: “CCM imekithiri kwa rushwa na akakionya chama chake ambacho alikuwa akikiongoza kama Mwenyekiti, kwamba kama hakitaachana na michezo ya rushwa katika kila lifanyikalo, ipo siku kitaanguka.” Onyo hiyo ya JK bado haijafanyiwa kazi na CCM. Kata ya Nkome iliyoko Halmashauri ya Geita, ni mfano halisi wa kukithiri kwa vitendo vya rushwa vinavyoibeba CCM. Wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo Serikali ya CCM ilipeleka zoezi la kuandikisha wananchi wanaotaka kupewa Bima ya Afya kwenye kata hiyo. Zoezi hili halikujali kuwa hiyo ni kata inayofanya uchaguzi wakati huo.

Viongozi wa wilaya na kata (wa kiserikali) walipohojiwa walisisitiza kuwa Serikali inaposimamia maendeleo ya nchi haizuiwi na uchaguzi. Jambo la kushangaza, kata nyingine za Wilaya ya Geita hazikufanyishwa zoezi hilo. Baadhi ya vyama vya siasa vililalamika kupitia  Tume ya Taifa ya Uchaguzi na ikatoa ufafanuzi ambao hadi leo uko kwenye tovuti yake ikikiri kuwa imepokea malalamiko ya Chama kimojawapo juu ya watendaji wa Halmashauri ya Geita kuwakusanya wazee katika Kata ya Nkome, wazee hao wakiwa na vitambulisho vyao vya kupigia kura kwa lengo la kuwapatia huduma ya afya bure. Tume ya Taifa ya uchaguzi ikaishia kusisitiza kuwa chama kilicholalamika kipeleke malalamiko kwa ngazi husika ambayo kimkakati haina meno na haijawahi kukichukulia hatua Chama cha Mapinduzi (CCM) au Serikali dhidi ya vitendo vinavyohujumu uchaguzi.

Sababu ya pili iliyoisaidia sana CCM katika uchaguzi huu, ni vyombo vya dola kwa maana ya vikosi vya ulinzi na usalama. Katika Jimbo la Dimani, Zanzibar, upo ushahidi kuwa vyombo vya dola vimetumika vibaya kwenye uchaguzi huo. Na ndiyo maana, Chama Cha Wananchi CUF kimemwandikia Mkuu wa Majeshi kumlalamikia juu ya hali hiyo. Uchaguzi wa Dimani ulivamiwa na vyombo vya ulinzi na vikosi vya SMZ, mapandikizi ya wapiga kura kutoka katika majimbo mengine na hata marehemu nao walifufuka kutoka makaburini na kwenda vituoni kupiga kura.

Sababu ya tatu ya kidola ni Daftari la Wapiga Kura. Awali vyama mbadala vilifanya upembuzi na uhakiki wa daftari la kudumu la wapiga kura lililotumika mwaka 2015/16 katika Jimbo la Dimani na kubaini wapiga kura hewa takribani 1,700, huku ikibainishwa kuwa zaidi ya wapiga kura 168 wamefariki na wengine kuhama jimbo. CUF ilimwandikia Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi-NEC kumjulisha dosari hizo na inaonekana hakuchukua hatua zozote. Ndiyo maana kwa waliofuatilia uchaguzi wa Dimani walishuhudia mawakala wa vyama mbadala wakitolewa vituoni na vyombo vya Ulinzi na Usalama, baada ya mawakala hao kuhoji uhalali wa baadhi ya wapiga kura waliokuwa wakifika vituoni ambao ilionekana wana tofauti kubwa na wapiga kura halisi walioko kwenye daftari la wapiga kura na upo ushahidi uliotolewa na mawakala wa vyama vilivyoshiriki uchaguzi wa Dimani, kwamba kulikuwa na dazani za mamia ya wapiga kura hewa  wenye majina tofauti na yale yaliyotumika 2015/16 katika baadhi ya vituo.

Sababu ya nne, vyama mbadala pia vimelalamikia hali ya kushangaza juu ya masanduku ya kupigia kura. Kumekuwapo na malalamiko ya kwamba kwenye baadhi ya vituo wasimamizi walikuja na maboksi ya kupigia kura yakiwa na karatasi zilizopigwa kura kabisa na kutumbukizwa katika masanduku hayo na kwamba, imeshuhudiwa baadhi ya wapiga kura wakiingia vituoni kupiga kura wakiwa na vitambulisho vya uraia peke yake wakaruhusiwa kupiga kura bila vitambulisho vya kupigia kura. Mawakala wa vyama vingine walipojaribu kuhoji hali hiyo na kutaka irekebishwe, walichukuliwa hatua kali na kuondolewa kwenye vituo haraka bila kuchelewa.

Sababu ya tano ya kidola, ni wagombea wa vyama mbadala kunyanyaswa chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Mathalani, mgombea wa Chama cha NRA, Ali Khamis Fallah, aliondolewa katika zoezi la kupita na kukagua hali ya upigaji kura kama ambavyo sheria na kanuni za uchaguzi zinataka na wakati huo huo, mgombea wa CUF, Khatib Ramadhan, naye alizuiliwa kukagua vituo vya kupigia kura na mgombea huyo alichukua jukumu la kulalamika rasmi kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia barua yenye Kumb. Namba /AB/T/001/2017 22/01/2017 na kuelezea ukiukwaji wa sheria na taratibu za uchaguzi unaofanywa katika vituo mbali mbali vya uchaguzi.

Vitendo vya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia kwa wasimamizi wa uchaguzi ambao wamewekwa na tume hiyo vinavyohusu kuwatoa nje mawakala wa upigaji kura wa Chama chochote cha siasa, vinavunja  sheria ya uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985, (Sura ya 343) na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Na. 4 ya mwaka 1979 (Sura ya 292).

Vitendo vingine nilivyovitaja ikiwa ni pamoja na kubadilishwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK), kuruhusiwa kwa wapiga kura wasio halali, uchaguzi kuendeshwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania wakishirikiana na polisi na kubakishwa kwa wapiga kura waliofariki kwenye daftari la Dimani, ni ushahidi mwingine wa uvunjifu wa sheria zinazosimamia uchaguzi kama anilivyozibainisha hapo juu.

Sababu ya sita iliyoibeba CCM ni kuwapo na mtandao wa uongozi wa Kkserikali ambao umekuwa na ushawishi mkubwa na uwezo wa kuingilia uchaguzi kila inapohitajika. Mathalani, wakuu wote wa mikoa na wilaya nchi nzima ni makada, viongozi, wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Viongozi hawa wa kiserikali pia ndio wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa yao na ama wilaya zao. Huwezi kuwaweka pembeni linapokuja suala la kulitumia Jeshi la Polisi vibaya na kwa malengo ya kukiokoa au kuisaidia CCM. Katika uchaguzi wa marudio wa  Januari 22, 2017, yameripotiwa matukio ya ama kukamatwa viongozi wa vyama mbadala na wafuasi wao kutokana na sababu mbalimbali.

Baadhi ya magazeti yameripoti kuvamiwa na kupigwa kwa viongozi au wanachama wa vyama mbadala, lakini polisi hawakuchukua hatua yoyote. Hizi ni dalili mahsusi kuwa Jeshi la Polisi haliko huru dhidi ya makucha ya wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama ambao ni makada wa CCM na huku wakiwa na uwezo wa kulielekeza jeshi hilo nini cha kufanya dhidi ya vyama mbadala. Hadi uchaguzi huu umekamilika ninafahamu viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani wanasakwa na polisi na wengine tayari wamefunguliwa mashtaka kwenye kata zilizokuwa na uchaguzi. Viongozi na wanachama wa CCM hawana kesi mahali kokote kule na hii inaweza kuhitimisha kuwa bado kazi kubwa sana iko katika mfumo wa demokrasia hapa Tanzania.

Mtandao huu wa kidola unakwenda chini zaidi, unawahusu pia makatibu tawala wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, watendaji wa kata na watendaji wa vijiji. Kama mtu alifuatilia uchaguzi huu wa marudio alijionea mifano mingi ikiripotiwa kwenye vyombo vya habari juu ya namna watendaji wa ngazi za chini walivyohusika kwa namna moja au nyingine kuvishughulikia vyama vilivyokuwa vinapambana na CCM. Mathalani, katika Kata ya Kijichi, Dar Es Salaam, viongozi wa chama kimoja walivamiwa kwenye kambi yao na Jeshi la Polisi baada ya polisi kuelekezwa hivyo na mtendaji muhimu wa Serikali. Viongozi hao walipelekwa polisi na kuhojiwa hadi usiku siku ya kuamkia upigaji kura.

Itaendelea Jumapili ijayo.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kijamii na Kisiasa, Mtafiti na Mwanasheria. Simu; +255787536759/ Barua Pepe; juliusmtatiro@yahoo.com/ Tovuti; juliusmtatiro.com.