Home Makala Utafiti taasisi za afya kutoa majibu sababu chanzo saratani nchini?

Utafiti taasisi za afya kutoa majibu sababu chanzo saratani nchini?

1422
0
SHARE
naibu waziri wa afya maendeleo ya jamii, jinsi wazee na watoto dk. faustine ndugulile

NA TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

KUMEKUWA na ongezeko la idadi ya watu wanaogua saratani duniani kote huku Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) likionya kuwa maradhi ya saratani yataendelea kuenea ulimwenguni, hasa katika nchi zinazoendelea huku wagonjwa wakitarajiwa kufikia milioni 22 ifikapo mwaka 2030 ikilinganishwa na milioni 14 mwaka 2012.

Takwimu mpya ya Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC) na WHO, zilizotolewa mwaka jana, zinaonesha kuwa kila mwaka duniani kote wagonjwa wapya milioni 18.1 hubainika.

Vilevile zaidi ya wagonjwa milioni 9.6 hufariki dunia kila mwaka, huku watu milioni 43.8 wakiishi na ugonjwa huo.

Hapa nchini idadi ya watu wanaougua saratani imekuwa ikiongezeka ambapo takwimu za IARC zinaonesha kuwa wagonjwa wapya 42,060 hubainika kila mwaka huku watu 28,610 sawa na asilimia 68 wagonjwa wapya hufariki kwa mwaka.

Ongezeko la watu wanaougua ugonjwa huo ni mzigo mzito kwa serikali na Taasisi ya Tiba ya Saratani ya Ocean Roads (ORCI).

Mkurugenzi wa Idara ya Matibabu ya Saratani ya Hospitali ya Aga Khan, Dk. Harrison Chuwa, anasema Serikali pekee haiwezi kukabiliana na maradhi hayo japokuwa kuna jitihada na dhamira ya dhati ya kupambana nao.

Katika kukabiliana na ugonjwa huo Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan (AKHST) iliamua kuunga mkono juhudi hizo kwa kuanzisha program maalumu ya uchunguzi wa awali, matibabu ya saratani kwa dawa za dripu, upasuaji na tiba shufaa mwaka 2014.

Dk. Chuwa anasema tatizo hilo limezidi kuongezeka hasa kwa wagonjwa kufika hospitali ugonjwa ukiwa katika hatua ambayo ugonjwa huo hauwezi kutibika kirahisi.

“Tuliamua kuandika andiko la mradi ambao utashirikisha taasisi za umma na binafsi kuimarisha juhudi za Serikali kupambana na ugonjwa huu.

“Lengo lilikuwa uboreshaji wa miundombinu na vifaa tiba, kuendeleza na kukuza raslimali watu wa taaluma mbalimbali za matibabu, uboreshaji wa huduma za uhamasishaji wa saratani katika jamii na kudumisha ushirikiano na utafiti hukusu ugonjwa huo,” anasema Dk. Chuwa.

Mradi huo unaogharimu Sh. Bilioni 38 umefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na Taasisi ya Afya ya Aghakan na utatekelezwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Ocean Road, hospitani ya Aga Khan na Bugando.

Dk. Chuwa anasema mradi huo utatekelezwa katika wilaya 13 za mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza katika kipindi cha miaka minne na manufaa yake yatakwenda nchi nzima ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 60 ya Watanzania wote watafikiwa na kampeni ya uhamasishaji.

“Kwa kutumia kliniki za upimaji zinazotembea zaidi ya watu milioni 1.7 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa saratani baada ya kusogeza huduma hizo,” anasema Dk. Chuwa.

Hatua hiyo itasaidia kuongeza idadi ya wagonjwa watakaofika hospitalini kwa matibabu kutoka asilimia 20 hadi 40 na kupunguza idadi ya wagonjwa wa saratani wanaogundulika wakiwa katika hatua ya tatu na nne za ugonjwa kutoka aslimia 75 za sasa hadi nusu yake baada ya kukamilika kwa mradi huo.

“Mradi huu utaboresha maabara ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kuiwezesha kuwa kitovu cha maabara ya kisasa ya pathiolojia ya molekuli na vinasaba ambayo itahudumia nchi nzima kusaidia madaktari kuchagua aina ya matibabu na dawa sahihi kwa wagonjwa.

Mradi huo pia utaongeza mashine mpya za kisasa za tiba ya mionzi kwa ajili ya matibabu na hivyo kupunguza mrundikano wa wagonjwa wanaosubiri tiba hiyo.

“Walau vituo 100 vya afya katika ngazi ya jamii vitafikiwa na mradi huo kwa kujengewa uwezo wa kutoa baadhi ya huduma za saratani hususani uchunguzi wa awali.

“Watumishi 330 wa afya watawezeshwa na kusomeshwa kwa nia ya kuongeza ufanisi wa kutoa huduma za matibabu,” anasema Dk. Chuwa.

Dk. Chuwa anasema mradi utasisitiza utoaji wa matibabu ambayo yanazingatia tafiti kwa kupitia majopo ya matabibu wa saratani na kuhimiza kutumia miongozo ya matibabu ya saratani inayotambulika nchini na kimataifa.

Mradi huo pia utapunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi, kuboresha huduma za upasuaji wa saratani na kupunguza gharama za matibabu yake kwa kushirikiana na bohari ya dawa katika manunuzi ya dawa na vifaa tiba. 

Dk. Chuwa anasema taasisi shiriki za mradi huo zitatengeneza mtandao wa matibau ya saratani nchini ambao utasimamia tafiti zenye ubora wa kusaidia kutengeneza sera, vipaumbele na kundaa mikakati ya mapambano.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, anasema mradi huo ni mzuri na utasaidia jamii kuongeza uelewa wa ugonjwa huo na kufanya uchunguzi mapema kabla haujafikia hatua mbaya.

“Wekezeni katika kubaini saratani ikiwa katika hatua za awali kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huu na baada ya miaka minne kuisha tutaona uelewa matokeo ya mradi,” anasema Dk. Ndugulile.

Ndugulile anawataka kuwekeza katika mafunzo ya wataalamu wa afya ili waweze kuboresha utoaji wa huduma za saratani na ushawishi wa upimaji. 

Pia anazitaka taasisi za tiba za umma na binafsi zilizopo katika mradi huo pamoja na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kufanya utafiti kubaini sababu nyingine zinazosababisha saratani tofauti na zile za zamani. 

Anasema kuwa taarifa ya utafiti huo siyo tu itaonesha uwapo wa tatizo bali pia itasaidia kufahamu kiini na nini kifanyike kukabiliana na nalo.

Ndugulile anasema pamoja na wananchi kuepuka visababishi vinavyotajwa kuwa ni chanzo cha saratani lakini bado tatizo hilo limezidi kuongezeka.

“Saratani bado ni tatizo kubwa kwa nchi yetu ambapo kwa sasa Ocean Road Cancer Institute wanatoa huduma kwa wagonjwa 64,000 kwa mwaka ukilinganisha na mwaka 2014 walipokuwa wakiwahudumia wagonjwa 34,000 tu,” anasema Dk. Ndugulile.

Anasema kuwa changamoto iliyopo ni upatikanaji wa huduma za saratani kwa wananchi kutokana na taasisi zinazotoa matibabu kayo kupatikana Dar es Salaam na Mwanza hivyo kuwalazimu wagonjwa kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.

“Matibabu ya ugonjwa huu yana gharama kubwa, kutibu saratani ya shingo ya kizazi ni zaidi ya Sh milioni tano na ya matiti ni zaidi ya Sh milioni 10, jambo ambalo Serikali imebeba jukumu hilo,” anasema Dk.Ndugulile.

Dk. Ndugulile anaamini kuwa kufanyika tafiti zitakazobaini vyanzo vingine vinavyosababisha ugonjwa huo itaisaidia serikali kupanga vizuri bajeti zake.

Anasema kwa sasa Serikali  imewekeza nguvu katika kukinga ikiwa ni pamoja na upimaji wa awali, kutoa chanjo ya kukinga saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana wenye umri wa kuanzia miaka 14 na tiba kwa gharama za Serikali.

Serikali pia imeongeza bajeti ya dawa kwa Ocean Road hadi Sh bilioni 10 kwa mwaka huu wa fedha na kuwekeza katika mashine mpya za matibabu zenye thamani ya Sh bilioni 9.5.

Pia wamezijengea uwezo taasisi za tiba za Bugando na Mbeya kutoa matibabu ya ugonjwa huo ili kupunguza msongamano Ocean Road.

Dk. Ndugulile anasema tayari NIMR wameanza kulifanyia kazi agizo hilo hivyo taasisi nyingine za tiba zianze mara moja. Pia ziongeze uwekezaji katika miudombinu ya matibabu ya saratani pamoja na kukuza uelewa kwa wananchi ili waweze kuepuka visababishi vya maradhi hayo.

Naye Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Grace Maghembe, anasema tafiti zinazotumika sasa zinatoka nje ya nchi hivyo hushindwa kupata sababu halisi za kuongezeka kwa kasi kwa saratani.

“Utafiti wa visababishi vya ugonjwa huu unatolewa na nchi za nje jambo linalosababisha tushindwe kujua sababu lakini sasa tunakwenda kufanya wenyewe na tatizo litabainika,” anasema Dk. Grace.

Anasema kwa sasa Serikali imewekeza katika upimaji wa awali wa ugonjwa huo ambapo jumla ya vituo 626 vinafanya uchunguzi huo.

Grace anasema kupitia mradi huo wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi utasaidia kupunguza gharama za matibabu ambayo kwa sasa ziko juu ukilinganisha na hali ya kiuchumi ya wananchi. 

Kanda ya Ziwa inayoundwa na mikoa ya Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu na Geita inaaminika ndiyo inayotoa asilimia 50 ya wagonjwa wote wa saratani wanaotibiwa Ocean Road.