Home Makala Utakatifu wa Ikulu ya Magufuli ni upi?

Utakatifu wa Ikulu ya Magufuli ni upi?

4527
0
SHARE

RAI KATUNINAPENDA kuanza makala haya kwa kutumia nukuu ya hekima ya muasisi wa Taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

‘‘…Tunataka rais Mtanzania, Hatuwezi kupata rais Mtanzania asitoke ama Zanzibar ama Tanganyika. Lakini hatumchagui kwa sababu ya Uzanzibari wake na hatumchagui kwa sababu ya Utanganyika wake.

Akiweka mbele Uzanzibar wake, akiweka mbele Utanganyika wake, tunajua huyu hatufai. Hiyo ndiyo sifa mama. Kwa sababu tunayemtaka ni rais wa Tanzania.

Rais wa nchi yetu, anachaguliwa kutokana na Katiba ya Tanzania. Na akisha kuchaguliwa, anaapishwa kwa Biblia mkristo, kama ni Muislamu kwa Quran.

Hapa katikati kumetokea na kupuuza puuza Katiba. Ufa wetu wa pili, Hatuwezi kuendelea kupuuza Katiba. Katiba ndiyo sheria ya msingi.

Sheria nyingine zote zinatokana na Katiba, haiwezi kupuuzwa. Hatuwezi kuendelea na utaratibu wa kupuuza Katiba ya nchi yetu.

Au rais anayeionea haya kuitetea Katiba, naye amechaguliwa kwa mujibu wa Katiba hiyo, ameapa kuilinda Katiba hiyo halafu anaona haya kuitetea Katiba hiyo.

Mtu ambaye hawezi kuitetea Katiba ya nchi yetu, hawezi kuilinda, hawezi kuisimamia, baada ya kiapo, hatufai. Aende akaendeshe shamba lake hukooo.

Hawezi kuwa katika rais wa nchi yetu, tunamchagua kwa mujibu wa Katiba, tunamwapisha kwa Katiba, ailinde, aitetee kwa moyo thabiti kabisa bila woga. Hawezi, hatumtaki.

Nchi zinaongozwa kutokana na sheria…, ukweli nchi zinaongozwa na watu na si malaika, lakini hao watu wanaongozwa na sheria.

Tunataka rais wetu anayejua tumechezea chezea Katiba kidogo na inamkera na akipewa nafasi na wenzake, atalisimamia hili la kuchezacheza na Katiba.

Tumeona sheria za nchi, watu wanajaribu kuendesha nchi bila kujali sheria za nchi. Huwezi kuendesha nchi bila utaratibu wa sheria, watu hawawezi kujua kesho kutatokea nini.

Unaweza kuwa mwaminifu kabisa, lakini ukawa na presha za ndugu zako, jamaa zako na marafiki zako si kwamba inatosha uwe mwaminifu, lakini uwe na uwezo wa kuwaambia jamaa, rafiki zako kwa kauli watakayoiheshimu na hawatarudia tena, Ikulu ni mahali patakatifu.

Mimi sikuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kuja kupageuza pango la walanguzi. Ukishakuwaambia hivyo, ndugu, marafiki zako na ikajulikana hivyo, mtu mwingine wala hakusogelei. Nafsi yake haimtumi kukusogelea..’’.

Ukitazama hotuba hiyo utagundua namna ambavyo sasa Rais John Magufuli ama kwa bahati mbaya au kwa makusudi ameamua kwenda kinyume nayo.

Kwanini anakwenda kinyume?  Kwanza ameshindwa kuwaeleza ndugu zake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwamba Ikulu ni mahali patakatifu na badala yake ameshirikiana nao kufanya shughuli za chama hapo badala ya serikali.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) ibara ya 72 inaelekeza na kutaja majukumu ya Rais kama, Mkuu wa nchi na kama kiongozi wa serikali.

Ibara ndogo ya 4 ya Katiba hiyo inasema kwamba, katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Ibara hii Rais ataepuka kujinasibisha, kwa namna yoyote ile, na chama chochote cha siasa au kundi lolote kwa namna ambayo inaathiri umoja wa wananchi.

Kwa mujibu wa Katiba na ibara hiyo inaonyesha wazi kwamba rais ameivunja Katiba aliyoapa kuilinda kwa kujinasibisha kwamba yeye ni mwana CCM kindakidaki.

Magufuli amesahau kabisa majukumu yake kikatiba kwamba kiongozi wa nchi hakutakiwa kutumia Ikulu kufanya sherehe za kushukuru ushindi na wenyeviti, makatibu wa mikoa, wilaya wa Tanzania bara na Visiwani wa CCM.

Jambo hili nimeamua kuligusa ili kumsaidia Rais Magufuli hivi sasa ambapo bado hajapewa nafasi ya Uenyekiti wa CCM, ili asije itisha Mkutano wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Ikulu.

Sitaki kuamini kwamba Dk. Magufuli hatambui kwamba kazi za chama anatakiwa kuzifanyia kwenye kumbi au ofisi zipi za CCM.

Sitaki kuamini kwamba atakuwa amesahau kuwa hivi sasa si Rais wa CCM bali wa Watanzania ambao wengine ni wanachama wa vyama vingine vya upinzani.

Sitaki kuamini kwamba Rais Magufuli au washauri wake wa sheria wameshindwa kutambua kwamba kufanya mkutano wa CCM ndani ya Ikulu amevunja Katiba aliyoapa kuilinda.

Kama wamefanya hivyo wakijua na kupuuza basi watakuwa wanakosea na watakuwa wanafanya yale ambayo Mwalimu alikemea akitaka rais ajaye asifanye mambo ya kupuuza puuza Katiba kama ilivyokuwa huko nyuma.

Nakumbusha haya kwa sababu naumia kama Dk. Magufuli ataanza kupuuza Katiba mapema hivi, vipi huko tuendako itakuaje? Je, kweli yeye au washauri wake hawatambui kwamba Katiba ndiyo sheria ya msingi?.