Home Makala Kimataifa Utulivu Afrika kwa mtazamo wa Ulaya

Utulivu Afrika kwa mtazamo wa Ulaya

1085
0
SHARE


NA HILAL K SUED

Katika ongezeko la hali ya wasiwasi na ya kutoridhika katika nchi nyingi Barani Afrika, serikali za nje na hasa nchi fadhili zinazidi kutilia mkazo kuendelea kwa uwepo wa “utulivu.” Lakini hadi lini?

Si “utawala wa sheria”, “demokrasia”, au “uchaguzi ulio huru na wa haki,” bali ni “utulivu.” Sasa hivi maandamano ya wananchi yanayochochea mabadiliko ya tawala Algeria na Sudan yanaangaliwa na nchi za nje kwa wasiwasi mkubwa na tumekuwa tukisikia kauli zao za kuwepo kwa utulivu – kuliko kuangalia iwapo wananchi walikuwa na hoja/haja ya kudai mageuzi.

Katika kipindi cha miaka miwili hivi iliyopita kuanzia Togo hadi Kenya, Uganda hadi Misri, Chad hadi Gabon – Algeria hadi Sudan – nchi zote hizi kumeshuhudiwa maandamano makubwa yakikabiliwa na nguvu kubwa za dola – na hivyo kuufanya msisitizo wa “utulivu’ kuwa muhimu zaidi ya “maelewano ya kisiasa”.

Wakati serikali ya Cameroon ikiwafyatulia risasi za moto waandamanaji, kuwatia mbaroni wanaharakati kwa makumi yao na kufungia mtandao wa Internet katika maeneo ya wananchi wanaozungumza Kiingereza, nchi za nje zilikuwa zinasisitiza ‘utulivu.’

Na hali kama hiyo nchini Ethiopia pia ilipelekea kufungwa kwa Intaneti, matumizi makubwa ya vyombo vya dola na kutangazwa kwa hali ya hatari katika maeneo mengi. Wanadiplomasia wa nchi za Magharibi waliunga mkono serikali pale ilipoamua kurejesha hali ya zamani – yaani kuondoa amri ya hali ya hatari.

Na imekuwa hivyo hivyo kwa Eritrea, taifa linaloonwa kama lenye utawala wa kidikteta, lakini sasa ndilo linalosababisha sera mpya ya uhamiaji kwa nchi za Ulaya. Kwa ujumla katika makabiliano na masuala ya siasa Barani Afrika, nchi za Magharibi hushikilia kwamba ‘utulivu” ndiyo sera sahihi. 

ITIKADI YA UTULIVU

Kutokana na “Itikadi ya Utulivu” kuhusu Afrika nchi za nje hujikita zaidi upande wa tawala zilizopo madarakani na siyo upande wa wanaonyimwa nafasi kufanya siasa kwa uhuru. Hazisiti kuunga mkono hali iliyopo, hata kama kwa kufanya hivyo zitakuwa zinapuuzia hali halisi ya uminywaji wa demokrasia na haki za wananchi unaofanywa na serikali hizo. Wanachagua mamlaka kuliko waandamanaji, na masilahi yao na ya walio madarakani kuliko ya wananchi. 

Sababu kubwa ya kufanya hivi haziachani na zile zilizopelekea kuwapo wimbi duniani lililosukuma mfumo wa kiliberali-mamboleo (neoliberalism). Unyonyaji wa rasilimali za Bara la Afrika si kitu kipya, lakini hali ya sasa – ile ya umuhimu wa kuendelea kuwepo kwa hali ya kijamii na ya kisiasa iliyo tulivu ndiyo inayotakiwa katika kuendeleza unyonyaji wa mali maliasili hizo.

Njaa kubwa iliyopo kwa makampuni makubwa ya magharibi kutaka yashamiri inaonekana ni muhimu zaidi kuliko kuanzisha na kusukuma mijadala ya kisiasa Barani Afrika. Kwanini kuleta uwezekano wa kubadili tawala na hivyo kuibua hali ya wasiwasi kuhusu hatima ya uporaji wao? Methali ya “Jini likujualo…” ni sahihi hapa.

Tofauti na ilivyokuwa katika vipindi vya nyuma katika historia, lengo kwa wakati huu ni kuwa na mipango ya “muda mfupi.” Wakati wa Vita Baridi, mataifa ya Afrika yalionekana kama washiriki katika mipango ya muda mrefu ya kujenga miradi ya itikadi duniani. 

Lakini ‘Itikadi ya Utulivu” ya sasa inalenga kwa kipindi cha miaka michache tu ijayo. Haina habari ya kujenga taasisi imara za utawala bora, au hata kufahamu visababishi vinavyotishia utulivu inayosisitiza Barani Afrika. Aidha itikadi hiyo haijali athari za misimamo yao baadaye kwa sababu wakati huo litakuwa ni tatizo la mtu/watu wengine.

Kuna mambo makubwa mawili yamebadilika katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ambayo yameleta aina hii ya Itikadi ya Utulivu. Kuibuka kwa China, Uturuki na nchi nyingine zisizo za Magharibi kumeleta tishio kwa ushawishi mkubwa wa kiuchumi uliokuwa nao nchi za magharibi kwa Bara la Afrika. 

Hali hii iliwapa watawala na wakuu wengine katika nchi za Afrika – ambao ndiyo wafaidika wakubwa wa huo “utulivu” nyenzo kubwa na hivyo kutoa mwongozo wa watengeneza-sera wa nchi za magharibi, wakiogopa kupoteza mitandao yao ya ufadhili (patronage networks) na hivyo kudhoofisha agenda zao za utawala bora.

La pili ni mwanguko wa uchumi duniani wa 2007/2008 ambao ulitengeneza fursa za kunyonya kutoka Bara la Afrika vyote vile vilivyoonekana muhimu kwao. Tukumbuke kwamba masoko ya Afrika, nguvukazi na maliasili hata siku moja havikuwahi kutiwa maanani katika kusuluhisha changamoto za kiuchumi katika sehemu nyingine duniani.

Lakini swali kubwa: kuna tatizo gani kwa utulivu kuwekwa juu ya yote? Kwanza kabisa inaziweka nchi za Afrika katika rehani katika vipindi vyao vya baadaye. Ni ushirikiano baina ya watu wan je na wakuu wa mataifa hayo ambao dira yao kubwa ni “kula sasa, chelewesha na kataa yatakayotokea.”

MAHALI PA KUTENGENEZA PESA

Itikati ya Utulivu inalifanya Bara la Afrika kama ni mahali pa kutengeneza pesa nyingi na kwa haraka kadri iwezekanavyo, na siyo mahali ambapo watu wanaishi, na wenye mapenzi. 

Sera hiyo inazihakikishia nchi za Afrika kuendelea kushiriki, ingawa kinje-nje siasa za dunia, huku zenyewe zikitoa mali ghafi, masoko na nguvukazi kwa ajili ya makampuni makubwa ya kibiashara na ya kiviwanda duniani.

Lengo la utulivu ni kuweka nguvu kubwa na hatari (risk) kwa wanaharakati na wanasiasa katika kubadilisha mwelekeo wa kisiasa kwa masilahi ya serikali za nje. 

Linayaona madai zaidi ya haki, demokrasia na uwajibikaji si muhimu sana kuliko kuishikilia hali iliyopo – angalau kwa kiwango cha kuwezesha biashara za nje kuendelea kufanya kazi.

Lakini hali halisi ni kwamba wakati watu wa nje wanasisitiza kuilea hali iliyopo, tawala nyingi Barani Afrika zinazidi kuwa siyo sikivu kwa wananchi wao – hususan kwa vijana. 

ATHARI KUBWA KWA VIJANA BARANI AFRIKA

Mwaka 2017 maelfu yao walikufamaji wakijaribu kuvuka Bahari ya Kati (Mediterranean Sea) kwenda nchi za Ulaya, wakati huo Umoja wa Afrika (AU) inakadiria watu wengine 200,000 wamo njiani wakielekea huko huko.

Hawa wanaondoka kwa sababu ya athari (collateral damage) zitokanazo na kusimika “utulivu.” Wanaondoka kwa sababu hakuna sehemu ya ardhi ya kufanya kazi – maeneo mengi yameuzwa au yameathirika kutokana na “janga” la  mabadiliko ya tabia-nchi.

Wanaondoka kwa sababu elimu yao ni duni kwani ubinafsishaji umeua vyuo vya umma (vya serikali). Wanaondoka kwa sababu viongozi wa nchi zao wanatumia fedha nyingi za umma katika kununua silaha ili kuendelea kubaki madarakani kuliko katika huduma za afya.

Wanaondoka kwa sababu maafisa wa polisi hujitokeza huwakamata, kuwashikilia na hata “kuwapoteza” wale wanaokuwa na msimamo wa kisiasa tofauti – yaani ile inayotishia ‘utulivu” wa nchi. Lakini utulivu kwa ajili ya nani?

Mwaka 2018, katika nchi nyingi Barani Afrika mambo yanatarajiwa kuwa mabaya zaidi kabla hayajawa mazuri. Mamilioni ya vijana watafikia umri ambao nchi zao hazitakuwa na nafasi kwa ajili yao.