Home Makala Vijana wa AfriYAN wanavyoelimisha wenzao juu ya Corona

Vijana wa AfriYAN wanavyoelimisha wenzao juu ya Corona

1598
0
SHARE
Mwenyekiti wa Shirika la Vijana AfriYAN hapa nchini, Dianarose Leonce Lyimo.

NA FREDERICK FUSSI 

BAADA ya kuandika makala kadhaa juu ya mapambano dhidi ya virusi vya Corona kupitia safu hii ya Jicho la Tatu, nilibahatika kuonana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Shirika la Vijana AfriYAN hapa nchini, Dianarose Leonce Lyimo. 

Nikiwa ndani ya ofisi zao nzuri zilizopambwa wa nakshi za Kiafrika zilizopo maeneo ya Victoria, Mwananyamala jijini Dar es Salaam ambapo ni eneo rafiki kwa vijana balehe kukutana, tulizungumzia mchango wa shirika lao katika mafanikio ya ajenda za maendeleo ya vijana bahele hapa nchini. 

Katika mazungumzo yangu na Dianarose alinidokeza namna AfriYAN inavyoshirikiana na UNFPA kusambaza elimu kwa vijana balehe juu ya mapambano ya virusi vya Corona. Kazi ya vijana hao ya kutoa elimu ya kujikinga na Covid-19 kwa vijana bahele ilinivutia na nikajikuta nataka kufahamu zaidi juu ya namna wanavyotumia teknolojia kusambaza taarifa za jinsi ya kujikinga na kuwakinga wengine. 

Kwa sababu nilichapisha hapa kwenye safu hii ya Jicho la Tatu makala kadhaa juu ya namna Watanzania wanavyoweza kupambana na virusi vya Corona, nikazidi kuvutiwa zaidi na mazungumzo yale na Dianarose. 

Baada tafakuri na kujifunza kwa kina kutoka kwa vijana hawa nikaona sio vibaya niwape faida pia wasomaji wangu katika safu hii ndani ya juma hili. 

AfriYAN ni mtandao wa Afrika wa vijana na vijana bahele hapa nchini Tanzania na kwingineko duniani. Wao wanapenda kuuita mtanado wao AfriYAN-Tanzania wakimaanisha ‘African Youth and Adolescent Network’. 

Mtandao huo siku za hivi karibuni umekuwa ukifanya kazi ya kutoa elimu juu mapambano ya virusi vya Corona kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu UNFPA. 

Sasa unaweza kujiuliza kuna tofauti gani kubwa kati ya neno vijana na vijana bahele? Vijana balehe wanatofautishwa na vijana kwa tafasiri za maneno hayo mawili. 

Vijana balehe kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ni watu wa umri kati ya miaka 10 na 19. Katika umri huo inaaminika kuwa mtu anapitia mabadiliko ya kibaiolojia, kiakili, kisaikolojia na kijamii. Vijana balehe wamegawanywa katika makundi matatu, vijana balehe wa umri wa awali (miaka 10-12), umri wa kati (miaka 13 mpaka 15) na umri bahele wa hatua za mwisho (miaka 16 mpaka 19). Wakati huo huo, Sera ya Maendeleo ya Vijana ya Tanzania ya mwaka 2007, inamtafasiri kijana kuwa mtu wa umri kati ya miaka 15 na 35. 

Hapa nchini kwetu Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Wazee na Watoto imeandaa mkakati wa Taifa wa afya na maendeleo ya vijana bahele wa mwaka 2018 mpaka 2022. Mkakati huo umefanya uchambuzi wa namna ambavyo magonjwa mbalimbali hasa yale ya kuambukizwa ukiwemo ugonjwa huu wa Covid-19 yanavyoweza kuwa mzigo kwa vijana bahele. Mkakati huo umeangazia mbinu zinazoweza kutumika kuzuia vijana bahele wasiumizwe na magonjwa. Mbinu hizo ni pamoja na uwepo wa sera wezeshi, sheria, bajeti na mifumo ya taarifa inayoweza kuratibu mkakati huo kufanikiwa na vijana bahele kunufaika vyema. 

Mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 unaongeza hatari ya vijana balehe kuendelea kuumizwa na magonjwa mengine kwa kukosa huduma muhimu za afya. Hatari zinazotajwa kuwepo ni pamoja na huduma dhaifu za afya ya uzazi ikiwa ni pamoja na maambuzi ya magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana. Hatari nyinginezo ni utapiamlo, matumizi ya dawa za kulevya, matatizo ya afya ya akili, ukatili ikiwa ni pamoja na ukatili wa kijinsia. 

Ili kukabiliana na hatari hizo zinazowakabili vijana balehe, AfriYAN wakishirikiana na UNFPA na mtandao wa Prezi waliamua kutoa elimu kwa kurekodi video zaidi ya mia moja za vijana wakitoa ujumbe kwa vijana wenzako katika lugha mbalimbali za Kifaransa, Kingereza, Kireno, Kirusi, Kichina, Kijapani, Kiarabu na lugha nyinginezo zaidi ya 20 katika matoleo sita tofauti na kuzisambaza video hizo kwenye mitandao ya kijamii kote duniani.  Video hizo zimetazamwa na zaidi ya vijana 500,000 ulimwenguni kote.

Katika kampeni yao ya kutoa elimu mtandaoni kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano, walitumia kiunganishi cha alama ya #VijanaDhidiyaCovid19. Bibi Irem Tumer kutoka UNFPA katika utambulisho wa video hizo zilizochapwa kupitia mtandao wa Prezi.com, alinukuliwa akisema kuwa “wanatoa elimu kuwafundisha vijana katika maeneo mbalimbali ya dunia juu ya Covid-19 na hatua wanazotakiwa kuchukua ili kulinda marafiki, familia na jamii nzima” 

Tumer anaendelea kusema kuwa katika toleo la kwanza la video hizo watoa elimu ya virusi ni nini, vinasambaaje, ni jinsi ya kujikinga navyo. Toleo la pili limeelezea namna vijana wanavyoathiriwa na Covid-19. Toleo la tatu limeainisha masuala ya kujamiiana na afya ya uzazi, wakati sehemu ya nne imeainisha masuala ya vijana, afya ya akili na virusi vya Corona. 

Sehemu ya tano imeainisha hatua ambazo vijana wanazichukua kupambana na virusi vya Corona, huku sehemu ya sita ikiangazia ukweli juu ya vijana, jinsia na Covid-19. 

Kijana Omnia El Omrani ambaye ni mwanafunzi wa fani ya tiba ya binadamu kutoka nchini Misri, alinukuliwa katika moja ya video akitoa ufafanuzi wa maana ya virusi vya Corona ambapo alisema “Ugonjwa wa Corona unaambukizwa kwa njia ya majimaji ya virusi vipya vya Corona kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine endapo mtu akipiga chafya au kukohoa na kwamba ni ugonjwa usio na tiba wala kinga na wataalamu wengi ulimwenguni wamejikita katika utafutaji wa kinga na tiba yake”. 

Akiendelea na ufafanuzi wake Omrani alikiri kuwa baadhi ya watu wanaweza wasioneshe dalili za ugonjwa huo ambazo ni pamoja na homa kali, uchovu, kushindwa kupumua pamoja na kikohozi kikavu. 

Naye Egle Janusonyte kutoka taifa la Lithuania kwenye video nyingineyo akieleza namna ambavyo vijana wanaathiriwa na virusi vya Corona alidai kuwa “vijana hawana kinga dhidi ya virusi vya Corona hata kama idadi ya vifo vya vijana ipo kidogo, hivyo vijana wachukue tahadhari zote” aliendelea kusema kuwa vijana wengine wanaweza kuugua na kufikia hatua ya kulazwa hospitalini. 

Kijana mwingine kutoka nchini Slovenia Kristijan Angeleski katika moja ya video akitoa maoni yake juu ya kujamiiana na afya ya uzazi wakati wa janga la virusi vya Corona alisema, “wakati wa janga hili vijana wanaweza kujikuta wanakosa taarifa muhimu juu ya kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya kujamiiana” pia aliendelea kusema kuwa “kugusana wakati wa tendo la kujamiiana kunaweza kuongeza hatari ya maambukizi ya virusi vya Corona endapo mwezi mmoja ana virusi hivyo, ingawa haijathibitishwa kitabibu endapo virusi vya Corona vinaambukizwa kwa njia ya kujamiiana” aliwataka vijana kuchukua tahadhari zote za kujilinda na kuwalinda wenzi wao. 

Kijana Safaath Zahir kutoka visiwa vya Maldives akizungumzia namna ugonjwa wa virusi vya Corona vinavyoweza kuathiri afya ya akili alinukuliwa akidai kuwa “kuitilia maanani afya yako ya akili ni muhimu kama vile ambavyo ni muhimu kujilinda dhidi ya virusi vya Corona” na kuwa endapo ukiona unahitaji afya yako ya akili iwe sawa katika kipindi cha janga la Corona basi usisite kutafuta msaada wa wataalamu wa tiba ya afya ya akili kwa usaidizi zaidi. 

Aliwashauri vijana kuchukua muda wa kutosha kupumzika, kula chakula bora, kufanya mazoezi na kupata muda mrefu wa kulala na kuepuka kujitenga binafsi mbali na jamii ya watu wa karibu. 

Naye kijana Abideen Olasupo kutoka nchini Nigeria alitoa ushauri kwa vijana jinsi ya kuchukua hatua dhidi ya virusi vya Corona. Olasupo alikuwa na haya ya kueleza kuwa “vijana wana nafasi kubwa ya kuchukua hatua na kupunguza kasi ya maambuzi ya virsi vya Corona katika nchi zilizoendelea kwa kuwa wao ni wengi” Olasupo anasisitiza kuwa ni vyema vijana kote duniani wakatii maagizo na malekezo ya wataalamu wa mamlaka za afya katika nchi zao ili wajilinde na kuwalinda wengine pia”. 

Katika hitimisho la mlolongo wa video hizo za kampeni ya kuelimisha vijana, binti mmoja kutoka nchini Indonesia, Lismawati Lapasi alitoa elimu ya namna virusi vya Corona duniani vinavyoathiri watoto wa kike kwa wakiume pamoja na wanawake kwa ujumla. 

Lapasi anadai kuwa kitendo cha watu kufungiwa ndani katika mtindo wa karantini umesababisha ongezeko la vitendo vya unyanyasaji wa kingono na kijinsia dhidi ya watoto wa kike na wa kiume. Lapasi anadai kuwa tathimini ya UNFPA inaonesha kuwa kama sera za kuweka watu karantini zikiendelea kwa zaidi ya miezi sita mfululizo basi huenda visa vya unyanyasaji wa kijinsia zikaongezeka mpaka kufikia visa milioni thelathini na moja. 

Pia anadai vijana wanawake wanaweza wasipate huduma za uzazi wa mpango kwa wakati kulinga na mahitaji yao. Alisisitiza kuwa pia mnyororo wa usambazaji wa huduma za afya ya uzazi unaweza kuathiriwa. 

Lapasi alihitimisha kuwa kuwataka vijana kuziomba Serikali zao na watunga sera kutunga sera zinazozingatia mahitaji ya makundi dhaifu ya wanawake na wasichana wanaoweza kuathiriwa na Covid-19. Pia kufanya utetezi wa sera zinazongatia usawa wa kijinsia katika maeneo ya kazi kwa ajii ya wanawake, kuwatunza salama wasichana maeneo ya shule na kuwapatia taarifa za utoka za kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.