Home Uchambuzi Viongozi ni watu wajali utu

Viongozi ni watu wajali utu

2054
0
SHARE

NA ERICK SHIGONGO

KATIKA awamu hii ya tani ni jambo la kawaida kusikia mkuu wa wilaya kamkamata yule, mara kaagiza awekwe mahabusu.

Vivyo, kwa mawaziri kumfukuza mkurugenzi au ofisa yeyote ndani ya chumba cha mkutano kwa kosa la kuchelewa kwenye mkutano husika au hata makosa anayotuhumiwa, pia limekuwa jambo la kawaida.

Mwenendo huu wa baadhi ya viongozi hasa mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na wakurugenzi kutishia, kuadhibu na wakati mwingine kuwaweka ndani baadhi ya wananchi, wanasiasa na hata watendaji wa Serikali, ni mojawapo ya sababu ya kudumaza ari ya  utendaji nchini.

Ikumbukwe kuwa katika siku za karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la kuripotiwa kwa matukio ya wateule hao wa Rais, kutoa adhabu kwa viongozi wenzao hadharani jambo ambalo pia linazidisha woga kwa baadhi ya watendaji.

Suala la Waziri kumfanya ofisa wa serikali kuonekana kama kiranja wa shule ya msingi ambaye anaweza kutimuliwa wakati wowote na mwalimu mkuu pasipo kuhojiwa ni ishara mbaya na isiyokubalika.

Dhana ya utumbuaji majipu katika serikiali ya awamu ya tano imekuwa ikienendwa kwa njia potofu kwa baadhi ya viongozi wetu.

Sote tuliompigia kura Rais John Magufuli tulikuwa tunaamini anaweza kubadilisha mambo mbalimbali mabovu pamoja na kuongeza ufanisi kwa mafanikio machache yaliyopatikana.

Hata hivyo, wasaidizi wake wanapotekeleza dhana hiyo wanajaribu kumpendezesha Rais Magufuli badala ya kutekeleza kwa mujibu wa taratibu za kiongozi. Sina masilahi yoyote na watumbuliwaji majipu ila nalilia taratibu na heshima kwa wanaotumbuliwa.

Mathalani Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, alimfukuza kikaoni Kamishna Jenerali wa Magereza, Juma Malewa kwa kuchelewa katika kikao cha kimkakati cha viongozi wa taasisi za wizara hiyo.

Wiki moja baada ya kukumbwa na kadhia hiyo Dk. Malewa alistaafu na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Naibu Kamishna wa Magereza, Phaustine Kasike.

Itakumbukwa pia Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dk. Said Nassoro alitimuliwa mkutanoni na Waziri  wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki. Dk. Nassoro alisimamiwa kazi pamoja na maofisa wengine wawili, Silvanus Ngata(Mkuu wa Chuo Tawi la Tabora) na Dk. Joseph Mbwilo (Mkuu wa Chuo Tawi la Dar es salaam).

Ni jambo lenye kheri kabisa kuona kuwa mawaziri wanachukua hatua badala ya kumngojea Rais Magufuli. Lakini litakuwa jambo baya zaidi kama waziri yeyote anadhani kumtimua mkosaji kwenye mkutano na waandishi au watumishi wengine.

Tunafahamu kuwa zipo taratibu za wazi kabisa namna ya kushughulika na wakosaji. Tumefahamishwa kuwa waliotimuliwa wametuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha na utendaji usioridhisha ambao umeisababishia hasara serikali yetu.

Aidha, mapema mwezi huu Mtendaji wa kata ya Kitengule wilaya ya Bunda, Deus Bwire aliamrishwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Lidya Bupilipili kupiga magoti mbele ya viongozi wenzake kwenye kikao.

Mtendaji huyo alikumbwa na kadhia hiyo baada ya kuwatetea watendaji wenzake ambao walichelewa kupata taarifa ya kikao hivyo kushindwa kuhudhuria kikao cha mkuu huyo wa Wilaya.

Pia Septemba mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi alimsimamisha kazi na kumtupa rumande kwa saa 48 Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Iringa, Sitta.

Sita alipewa adhabu hiyo kwa kosa la kuwaambia Chama Cha Viziwi kuwa Manispaa hiyo haiwezi kuwasaidia kwa sasa kwa sababu fedha nyingi zimetumika kwenye ziara za mkuu wa mkoa.

Nakubaliana na mkakati wa kuwaondoa watendaji wa wazembe kokote walipo hapa nchini. Nakubaliana na hatua kali dhidi ya watu wote wanaotuhumiwa na au waliodokoa fedha za umma. Nakubali kuwa serikali yetu imekuwa ikiumizwa mno na fedha zake kutokana na usimamizi mbovu.

Aidha, nakubaliana na mpango wa kurudisha nidhamu ya utumishi wa umma pamoja na kuhakikisha miradi ya maendeleo yote inajengwa kwa kiwango kinachotakiwa. Tatizo linalonikabili kila nikiwatazama mawaziri wetu ni hatua wanazochukua dhidi ya wahusika.

Ni lazima tukiri kuwa hapo si jeshini ambako neno linalofahamika ni ‘amri’ na ‘utekelezaji au ‘utiifu’. Zipo taratibu ambazo waheshimiwa mawaziri wetu wanatakiwa kutekeleza pia na si kuwaita wahusika kwenye mikutano mbele ya waandishi au mkiutano ya watumishi na kuwawatangazia kuwafukuza.

Siwapangii kazi mawaziri, wakuu wa mikoa au wilaya lakini wanatakiwa kufuata weledi wka kuwasimamisha kazi wahusika kwa mujibu wa taratibu si kutangaza kibabe babe kisha kuwaambia makosa yao.  Watuhumiwa huelezwa makosa yao kwa mujibu wa taratibu si kuitisha mkutano wa watumishi au vyombo vya habari na kumwambia mtuhumiwa “ondoka kuanzia sasa umesimamishwa kazi”.

Natambua desturi mojawapo ya kushughulikia watuhumiwa ni kutowasikiliza sana, lakini huwezi kuwafananisha watuhumiwa wanaondolewa kwenye taasisi za umma huku wakitafsiriwa majina mengi ya ovyo.

Tunahitaji ustaarabu na kujenga kanuni zilizopo kwenye sheria kwamba watuhumiwa hao wafanywe kwa stahiki ya sheria zao. Hatufukuzi kama watoto walioko maliwatoni kimakosa badala yake tunawahukumu kistaarabu.

Hebu tuvute picha, Rais Magufuli ameitisha mkutano na vyombo vya habari pamoja na mwaziri wake pasipokuwaeleza ajenda za mkutano. Lakini ‘Live’ kwenye mkutano anawaambia  mawaziri fulani nawafukuza kwa sababu ni wazembe, wabadhirifu, uwezo mdogo na kadhalika.

Kwa vyovyote vile kiubindamu mshtuko utakuwa unatokea(hata kama intelijensia zao zinawajulisha kitakachotokea). Ifike mahali ni lazima viongozi wetu wawe na utu na watambue kuwa hatua wanazochukua zinajenga na kuleta faida gani kwa taifa.

Kwamba unapomtimua kazi mbele ya mkutano wa watumishi au vyombo vya habari ndiyo kusema mfano bora wa uongozi? Kwamba kutumbua majipu ni kuwadhalilisha watuhumiwa kwa kiwango cha mwisho cha ukosefu wa utu? Ifahamike kuwa ukweli hauna uonevu.

Naamini waliotumbuliwa hawaonewi, lakini natambua ukweli una heshima,adabu na nidhamu. Ukweli ni mnyenyekevu, mkali wenye mipaka na kadhalika. Tunajenga taifa pamoja, tunapoadhibu na kuhukumu tuzingatie haki za watuhumiwa wetu.

Kwa mfano sheria ya kuwaweka watu mahabusu saa 48 ilikuwapo lakini sivyo wanavyoitumia, kuna vigezo, kuna wengine mfano mkuu wa mkoa wa  anasema ‘mweke kwa masaa yangu’.