Home Afrika Mashariki Viongozi wajifunze kuukubali ukweli

Viongozi wajifunze kuukubali ukweli

3075
0
SHARE

MOJA kati ya tatizo linalowakabili watawala tulionao Tanzania na barani Afrika kwa ujumla, ni kutokuwa tayari kukiri kushindwa hata kama nchi inaonekana dhahiri kushindwa kupiga hatua za kimaendeleo. Wengi wanaamini kuwa kukiri kwa mapungufu ni sawa na kuanika udhaifu na kuwawezesha wapinzani wake kupata vitu vya kusema wakati wa kampeni ndiyo maana wengi wao hupoteza muda mwingi kufikiria chaguzi badala ya shughuli za kimaendeleo. Katika miezi michache iliyopita moja ya mashirika makubwa duniani yaliripoti kuwa baadhi ya wafanyabiashara kutoka China kwa kushirikiana na watu kutoka Tanzania wamekuwa wakijihusisha na biashara ya ujangili.

Taarifa hiyo ilienda mbali kwa kuitaja nchi ya Tanzania kama nchi ambayo ni hatari kwa maisha ya tembo katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na Kati. Kwa mfano taarifa ilisema kuwa kila siku tembo wapatao 13,000 huuawa na majangili huku kukiwa na Serikali, waziri husika na askari wenye dhamana ya kuwalinda wanyama hao. Huu ni mfano wa eneo moja ambao watawala wetu hushindwa kukiri udhaifu wao kuwa wameshindwa kutikiza majukumu yao waliyokabidhiwa kwa makusudi kwa malengo wanayoyajua wao na marafiki zao Tatizo hili la watawala kuficha udhaifu wao limezalisha tatizo lingine linalofahamika kama unafiki ambao huwasababishia kusema uongo katika jamii Kwa mfano katika kampeni zinazoendelea mmoja wa wagombea amekuwa akijinadi kujenga viwanda ilhali ni mmoja wa walioshiriki kuviuza viwanda kwa bei ya kutupwa kwa wawekezaji uchwara. Wakiwa hadaa kwa kuhimiza kudumisha amani na utulivu huku pengo kati ya matajiri na masikini likizidi kuongezeka kila kukicha, huku chuki kati ya wakulima na wafugaji zikiongezeka, huku mafisadi wakizidi kuitafuna nchi bila ya kuchukuliwa hatua na mikataba ya hovyo ikizidi kuitafuna nchi.

Pamoja na kutokuwa tayari kukiri mapungufu lakini wamekuwa ni mabingwa wa kujibebesha mifumo mingi ya kimaendeleo bila hata ya kufanya tathmini hata kama mifumo hiyo haina tija ilimradi wawafurahishe wakubwa kutoka Ulaya, Marekani na kwingine. Tabia hii ya kujibebesha mifumo mbalimbali imekuwa na matokeo yasiyoridhisha katika nchi hizi kwani tumeshuhudia zikizalisha matajiri wachache huku walio wengi wakibaki kwenye umasikini wa kutupwa. Kwa hapa kwetu napo tumekuwa ni wahanga wa mifumo hii ya kuiga toka kwa hao wakubwa, kwani kwa miaka mingi tumekuwa tukihangaika jinsi ya kujikwamua bila ya mafanikio.

Ni miaka mingi imepita huku tukiwa hodari wa kukopi na kupesti mifumo hii bila hata kufanya utafiti kama inatija kwa maendeleo yetu au laa. Kinachotuumiza ni sisi kukubali kuwa watumwa wa kifikra kwa kudhani kuwa chochote kinacholetwa kutoka Ulaya na Marekani ni halali kwetu bila ya kujua kuwa ukombozi wa kweli hauwezi kuletwa na yeyote zaidi ya sisi wenyewe. Tumeshindwa kupiga hatua za kimaendeleo kwa sababu tumekubali kudanganywa na kudanganyika kuwa tunaweza kupata maendeleo kwa kufuata misingi ya nchi za ulaya bila ya kufuata misingi na hitoria ya nchi yetu.

Ni aibu kwa Taifa kama Tanzania kujinadi kuwa uchumi wake unakuwa ilhali ikiwa njia kuu zauchumi ikiwemo viwanda vimeuzwa na kutelekezwa na kutufanya kuwa soko la bidhaa feki kutoka nje. Sasa imebaki kama historia kuwa Tanzana imewahi kuwa na viwanda kama vile vya zana za kilimo vya ubungo, UFI Mbeya, sido na vingine vingi vilivyokuwa vimetapakaa nchi nzima.

Kiko wapi kiwanda kama cha Kilimanjaro machinery tools, viwanda vya sabuni, nguo, viwanda vya kuunganisha magari na ile mitambo ya kusafirishia mafuta ya TIPPER huko Kigamboni vyote vimebaki historia halafu tunatarajia kupata maendeleo?. Hivi vyote ni matokeo ya watawala wetu kukopi na kupesti kitu kinachoitwa soko huria toka huko ugaibuni bila ya kuangalia athari yake kwa nchi kama Tanzania.

Matokeo ya hizo sera za hovyo ni utitiri wa misaada ya hovyo kutoka huko huku tukizidi kupumbazwa kuwa uchumi wa nchi yetu unakua kwa kasi katika ukanda huu. Kwa tabia au mazoea hayo ya kutopenda kusema ukweli kwa viongozi wa bara hili ndiyo maana hata kwenye Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ya 1977 tunaimba ujamaa huku tukicheza ngoma za kibepari.

Hivi hatuwezi kujifunza mafanikio kutoka nchi nyingine zenye mazingira ya kufanana na ya kwetu kwanini tukubali kujishusha kwa kiwango hiki mpaka tunakuwa mabingwa wa kuomba omba kila mara?. Hivi kwanini inakuwa ngumu kwa watawala wetu kujifunza kitu kutoka kwa nchi kama Vietnam iliyokuwa masikini wa kutupwa baada ya kuharibiwa na vita lakini leo wako mbali.

Historia ya nchi hiyo inatueleza kuwa mara baada ya miaka mingi ya vita iliyoiacha nchi hiyo na umasikini wa kutupwa viongozi wa nchi hiyo waliamua kujenga viwanda vya nguo kama njia ya kulikwamua taifa hilo.

Mpaka hivi sasa nchi hiyo ina makampuni 3,700 ya nguo yenye uwezo wa kuajiri watu wapatao milioni mbili na nusu mauzo ya nguo kutoka nchi hiyo kwa sasa yana thamani ya dola za kimarekani bilioni 11.2 hii ni kwa mujbu wa takwimu za mwaka 2010. Maendeleo kwenye sekta hiyo ya nguo yaliendana na sekta kama ya kilmo. Kwa mfano mwaka 1990 nchi hiyo ilikuwa ikiagiza mchele kutoka nje lakini ilipokuja kufika mwaka 2005 walikuwa wa pili duniani kwa kuuza mchele nje ya nchi yao.

Takwimu hizo zinazidi kueleza kuwa asilimia 31 unaouzwa na nchi hiyo huuzwa katika nchi za kiafrika zenye ardhi kubwa yenye rutuba kuliko nchi hiyo, aibu kwa watawala wetu. Hii ni aibu kwa nchi kama Tanzania baada ya miaka 50 ya uhuru nusu ya bajeti yetu bado inategemea misaada kutoka nje tena kwa masharti ya ajabu. Huu ni wakati mwafaka kama taifa kukiri kushindwa katika baadhi ya maeneo ili tuweze kujisahihisha kuliko kuendelea kujidanganya sisi wenyewe vinginevyo tujiandae kujibu huko tuendako.