Home Makala WACHUMI KUWENI WAZALENDO, MSAIDIENI RAIS

WACHUMI KUWENI WAZALENDO, MSAIDIENI RAIS

1820
0
SHARE

Mwaka mmoja wa utawala wa Rais John Pombe Magufuli, unajadiliwa sana. Gumzo lililopo mitaani kote hivi sasa, iwe ni mjini au kijijini, ni ukata.

Kila kona watu wanazungumzia kutokuwapo kwa fedha taslimu. Hali ni tete. Inahitaji kupatiwa maelezo ya kina na ya kuridhisha, vinginevyo uzushi utatamalaki na kuchukua nafasi isiyokuwa stahiki yake.

Katika mijadala inayoendelea kote nchini, jambo ambalo linazungumzwa zaidi ni hili la ukata. Kila siku hauishi kusikia watu wakisema kwamba Magufuli amebana au amekaza, wakimaanisha kwamba kuna upungufu wa fedha katika mzunguko.

Bidhaa haziuziki tena kwa wingi ule ule, kama ilivyokuwa kabla ya Rais Magufuli kuingia madarakani na kutangaza vita dhidi ya ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.

Watu wengi wanajikuta njia panda. Kwanza hakuna uelewa mzuri wa jinsi gani uchumi unavyoendeshwa. Pia hakuna uelewa mzuri wa uhusiano wa fedha zilizopo katika mzunguko na huduma na bidhaa katika soko.

Aidha, ni wazi kabisa kwamba uelewa wetu wa masuala ya uchumi unahitaji kuboreshwa, ili kutambua ni kitu gani hasa kinaendelea katika nchi yetu na kujiridhisha ni kwa kiasi gani tunajua kinachoendelea.

Ni kweli kuna upungufu wa fedha katika mzunguko. Kuna watu wanauza mali zao mbali mbali zinazohamishika na zisizohamishika na wanapata taabu sana kupata wanunuzi.

Kinachoelezwa ni kwamba siku hizi, fedha imekuwa ngumu sana kuipata. Kwa mantiki hiyo, inamaanisha kwamba kulikuwa na kipindi katika uchumi wetu, fedha ilikuwa rahisi kuipata.

Upatikanaji wa fedha kwa urahisi maana yake nini katika lugha ya kichumi? Hili nalo linawahitaji akina Profesa Honest Ngowi, kulitolea maelezo kwa namna ambayo mwanannchi wa kawaida ataelewa.

Sanjari na hilo, ni wajibu wa magwiji wetu wa uchumi, kutueleza pia ni kitu gani kinaendelea katika uchumi wa nchi, na pengine kusaidia kutoa ushauri kwa Serikali yetu kwamba nini kifanyike, ili fedha halali iweze kurejea kwenye mzunguko na watu wakawa na fedha kama zamani, lakini si kwa kupitia njia za mkato za ‘kupiga dili’.

kweli kabisa kwamba biashara imedorora. Lakini ni kweli pia, kwamba kwa miaka kadhaa sasa, kulikuwapo na mzunguko mkubwa sana wa fedha katika uchumi wetu. Kitu ambacho kimefanyika ni kuondoa sehemu ya fedha hiyo kutoka katika mzunguko. Sababu gani fedha ikatolewa kutoka katika mzunguko?

Itakumbukwa kwamba alipoingia madarakani Rais Magufuli, aliamua kuhakikisha kwamba anaisafisha nchi. Hii kutamka kwamba anaisafisha nchi, ni ushahidi kwamba kulikuwa na uchafu mwingi na mkubwa, ambao ulimfanya aone na kuhisi kwamba asipochukua hatua za makusudi za kuufanya huo uchafu huo, asingweza kufanikiwa katika ndoto yake ya kuikwamua nchi.

Huwezi kujenga uchumi imara kama hakuna uzalishaji imara na endelevu. Unapotaka kujenga uchumi wa viwanda, ni lazima uhakikishe kwamba unakuwapo na uelewa mzuri wa nini cha kufanya, ili kuweza kufanikisha azma hiyo.

Rais Magufuli alikuta kuna fedha nyingi zisizokuwa na uhalali wa kuwapo kwenye mzunguko. Ni fedha ambazo zimekuwa zikitumika kujenga taswira kama vile mambo ni mazuri sana katika uchumi wa nchi, kumbe si lolote si chochote. Ni fedha ambazo zilikuwa zimeingizwa kwenye mzunguko kwa njia haramu.

Zilikuwapo fedha za watumishi hewa. Hiyo maana yake ni kwamba kuna watu walikuwa ama wanapata mishahara bila ya kufanya kazi, au wanalipwa mshahara zaidi ya mmoja.

Mtu anayelipwa fedha haramu, matumizi yake pia yatakuwa ya kiharamu na kiharamia. Mahali pa kununua soda moja kwa mtoto mmoja, atanunua kreti.

Mahali pa kununua kilo moja atanunua mbili au tatu. Hiyo maana yake ni kwamba anaingiza fedha kwenye mzunguko ambazo hazilingani na hali halisi, na hivyo basi anajenga taswira potofu kuhusu hali ya uchumi.

Aidha, kutokana na kile kinachojulikana kama ‘over invoicing’ Serikali inalazimishwa kununua huduma na bidhaa kwa bei mara mbili au hata mara nne ya bei ya soko. Hiyo maana yake ni kwamba kunakuwapo na watu wanaopata fedha nyingi kutoka serikalini ambazo hazina uwiano wowote na kile kilichouzwa au huduma iliyotolewa.

Ukizungumza na wafanyabiashara na watoa huduma utasikia kuna kinachoitwa bei ya serikalini. Hiyo bei ya serikalini maana yake ni fedha za kilemba ambazo zinabambikwa huduma ama bidhaa kwa lengo la kuwanufaisha watu wachache. Hao wanaozibeba hizo fedha, huwa ni watumiaji wazuri sana wanapokuwa katika manunuzi ya bidhaa au huduma.

Fedha hizo hivi sasa hazipo tena kwa wingi katika mzunguko kwa sababu Rais Magufuli, ameamua kupambana na aina hiyo ya wizi. Ni wizi ambao ulitamalaki mno ndani ya Serikali Kuu na serikali za mitaa, kiasi kwamba kila aliyekuwa akifanya kazi huko, alionekana na kukubalika kwamba ni mwenye fedha.

Ni fedha hiyo haramu ndiyo iliyokuwa ikitumika kuchangia katika harusi, kipaimara, misiba, mahafali na kadhalika. Ili mradi kila kona ya nchi ilikuwa ni ya nderemo na vifijo na hata katika majonzi bado ukwasi mkubwa ulionekana ambako watu walidiriki kuwakodisha wapishi, waombolezaji, miziki ya washereheshaji na kutumia mamilioni.

Ni wazi kwamba katika mazingira ambayo Serikali inasimamiwa kwa makini, na kila huduma inalipwa kwa kiasi kinachokubalika kwenye soko fedha za ziada ambazo watu walikuwa wakigawana na kuzitumia kujitanua, zitatoweka au kupungua kwa kiasi kikubwa.

Ukiachilia mbali hizo fedha za kuibambika Serikali, pia kulikuwa na fedha nyingine ambazo zilikuwa zikiingizwa kwenye mzunguko kupitia wizara na idara mbali mbali za Serikali na mashirika ya umma kama posho za vikao.

Lilikuwa ni jambo la kawaida kamati kukutana ndani ya idara, au wizara na sio tu kwamba vikao vilifanyika katika mahoteli au mabwalo ya kukodisha, bali wahudhuriaji walilipana posho. Fedha hiyo hivi sasa haipo kwa sababu Rais Magufuli alitoa maelekezo ya kusitishwa mara moja kwa utaratibu huo uliokuwa unaitwisha serikali mzigo usiokuwa wa lazima.

Maelekezo ni kwamba vikao vifanyike ndani ya majengo ya Serikali, watu wasilipane posho na hata suala la staftahi na vitafunwa kwa fedha za umma likomeshwe mara moja.

Bila shaka fedha imepungua sana kwa sababu hizo hapo juu.

Lakini kingine ambacho kimepunguza fedha kwa kiasi kikubwa kutoka katika mzunguko, na pengine ndizo zilizokuwa nyingi zaidi, ni ufisadi mkubwa ambao ulikuwa ukiendelea ndani ya mashirika ya umma.

Ufisadi huo ni ule wa kuchukua fedha na kuzihifadhi katika benki za biashara kwa namna ambayo hizo hizo fedha za umma zinatumika kuikopesha Serikali, tena kwa riba kubwa. Yaani fedha ya shirika la umma inawekwa katika benki ya biashara ya binafsi, halafu inatumika kwa ajili ya kuwatajirisha maofisa wa shirika la umma, huku Serikali ikiambulia sifuri.

Ni kweli kabisa kwamba Rais Magufuli ameelekeza fedha za mashirika ya umma na Serikali kwa ujumla, zihifadhiwe katika Benki Kuu ya Tanzania. Uamuzi huo umetekelezwa na kwa mantiki hiyo, takriban fedha shilingi trilioni 9, zimeondolewa katika mikono ya benki za biashara.

Hapana ubishi hata kidogo kwamba hatua hiyo imezitikisa sana benki hizo. Benki zilikuwa zikifaidika kwa kutumia fedha za umma kufanyia biashara, bila ya umma wenyewe kufaidika na chochote.

Bila shaka wachumi wetu wanaiona hii hali, kwamba si nzuri. Lakini pia ni wazi kwamba ufumbuzi wa upungufu huu wa fedha katika mzunguko, sio kuzirejesha fedha hizo katika mzunguko kwa kutumia utaratibu wa zamani.

Hatuwezi kuirekebisha hali hii kwa kurudia makosa yale yale. Yaani turejeshe fedha kwenye uchumi kwa kuwaruhusu ‘wapiga dili’ waendelee na upuuzi wao, au kwa kuwaruhusu mabosi wa mashirika ya umma kuzikabidhi fedha hizo katika benki za biashara, halafu zitumike kuipiga Serikali.

Au eti turejeshe fedha katika mzunguko kwa kuwaruhusu wafanyakazi hewa kuendelea kulipwa, au kuruhusu uwepo wa bei za kipigaji kwa ajili ya Serikali. Huo utakuwa ni uchizi.

Pamoja na kuona umuhimu wa kurejesha fedha katika mzunguko, lakini ni lazima wananchi waweze kufaidika na fedha hizo kwa kuwajengea uwezo wa kiuchumi, na kuwafanya waweze kushiriki kikamilifu katika uzalishaji mali. Kinyume cha hapo, hatufiki tunakotakiwa kwenda yaani katika uchumi wa kati.