Home Latest News WAKALA, UWE JAWABU LA UFANISI WA KILIMO NCHINI

WAKALA, UWE JAWABU LA UFANISI WA KILIMO NCHINI

5003
0
SHARE
NA NASHON KENNEDY     |

KWA muda mrefu kumekuwa na misamiati kwamba kilimo ndiyo kimekuwa uti wa mgongo kwa Taifa letu na kusudi la msamiati huu bila shaka, ni jinsi watalaamu wetu walivyotambua umuhimu wa kilimo na wakulima katika uchumi wa taifa letu.

Mchango wa Sekta ya Kilimo na mazao yatokanayo na kilimo chenyewe, hautiliwi shaka juu ya ustawi na siha za Watanzania wa kariba mbalimbali kuanzia vijijini hadi mijini, bila kujali wadhifa wa mtu katika jamii, au vyombo vya kiutawala na kiutendaji katika Serikali na mashirika binafsi.

Kila mmoja kwa nafasi yake, anatamani chakula cha hadhi yake au wakati mwingine kinachoweza kupatikana kwa wakati huo, alimradi alijaze tumbo lake na siku yake iweze kupita salama.

Ikumbukwe pia kwamba uchumi wa uzalishaji, kwa muda mrefu umekuwa ukitegemea na unaendelea kutegemea, upatikanaji wa mazao ghafi ya kilimo—matunda, nafaka, mbogamboga, na maua kama nyenzo kuu inayostawisha biashara kati ya taifa letu na mataifa ya nje.

Mchakato huu, kwa miongo mingi, umetegemea juhudi binafsi, ujuzi duni, nyenzo zisizoaminika, na mbinu dhaifu katika uzalishaji jambo ambalo limeendelea kuteng’eneza ombwe la ufanisi (Vacuum of efficiency), na hivyo kulifanya soko la nje kukosa ushindani sitahiki kutoka Tanzania.

Ushindani unaokusudiwa katika makala haya, ni kukosekana kwa ujuzi, nyenzo, utashi wa kisiasa na kimuundo, utakaohamasisha watu wote kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi wa kilimo.

Ukosekanaji wa soko la uhakika na bei iliyosimama katika vikuku vyake (price stability), umesababisha mara nyingi watu kukosa uhakika wa bei ya mazao yao na hivyo kuishi kwa mashaka katika kilimo ambacho wamekichagua kuwa na nyenzo na tegemeo la kudumu la uchumi katika maisha yao na hivyo kuwa na urafiki wa mashaka na tarajio lao la kudumu ambalo ni uchumi wa kilimo.

Tabia hii imesababisha kuzorota kwa uzalishaji na hivyo taratibu au kwa kasi kusababisha kutokuaminika kwa soko—hasa kule tunakouza bidhaa zetu. Kukosekana kwa ujuzi na nyenzo muhimu, ikichangiwa na mbinu dhaifu za uzalishaji bora wa kulikabili soko la ushindani, kwa muda mrefu kumekisababishia kilimo chetu madhara makubwa.

Tumeshuhudia kwa kiasi kikubwa nchi yetu na wakulima wetu wakishindwa waziwazi kukabiliana na vishindo vya utandawazi wa kibiashara dhidi ya walanguzi wa kigeni, na matokeo yake Tanzania imegeuka kuwa “soko mjinga”, la wajanja kutoka nchi jirani wanaosaidiwa na matapeli wa ndani wanaojiita madalali wanaonunua bidhaa au mazao kwa bei ya ndani (dhalili) na kuwapa wageni ambao huondoka na bidhaa/mazao yetu kwa wao wenyewe kulipwa posho ndogo na kuliacha taifa likipoteza ushuru, heshima na kuonekana kama nyumba ya kambale ambako kila mmoja ana ndevu (Banana Republic).

Kwa mfano, kahawa inayonunuliwa kwa magendo huko Kagera, samaki wanaouvuliwa majini na kuvushwa kwenda nchi jirani bila nchi kujua wala kunufaika, pamba ghafi inayovushwa katika maghati bubu na kupelekwa nje ya nchi, kokoa inayopelekwa Malawi na Zambia bila mamlaka za nchi yetu kufahamu, mchele unaozalishwa kwa wingi Kahama mkoani Shinyanga na kuhamishiwa nchi jirani za Rwanda, Burundi, Congo-DRC, Uganda, Kenya na Sudan ya Kusini, Karafuu inayotoroshwa toka Pemba na Unguja na kuishia Comoro- Madagscar, Shelisheli na Djibout kwa uchache.

Hujuma hizi ambazo watu huziita dili, au biashara , imesababisha umaskini mkubwa kwa wakulima wetu lakini pia imelemaza uchumi wetu kwa kwa viwango visivyoweza kukarabatiwa (beyond repair). Miongoni mwa mambo mengine yaliyosababisha udhaifu huu ni kuvunjika moyo kwa wakulima wetu na hivyo kusababisha upungufu wa nafasi za kazi na mlipuko wa vijana kukimbilia mijini, jambo ambalo linauvuruga uchumi kwa kuondoa mizania ya uchumi kati ya mijini na vijijini.

Kutokana na hali hiyo, kinachotarajiwa kutoka vijijini kama malighafi ya kuendesha viwanda vilivyoko mijini inakosekana, lakini pia jamii isiyo na ujuzi wa viwanda na mifumo ya maisha ya mjini kuamia mjini na kufanya kazi zisizolingana na hadhi yao na hivyo husababisha msongamano usio wa lazima na matokeo yake, ni umachnga na vurugu zisizotarajiwa kati ya mamlaka za miji na raia wake.

Kingine ni kusababisha viwanda vya kuchakata vilivyoko mijini vinavyotegemea malighafi ya mazao ya kilimo kutoka vijijni kushindwa kupata malighafi hiyo na kulazimika kutumia fedha kidogo kununua malighafi kutoka nje ya nchi, hatua hii inadumaza uchumi wetu.

Mfano, hivi sasa mafuta ya mawese na pamba, yananunuuliwa kutoka nje, karibu Tsh 500bn. kwa mwaka, zinatumiwa na wafanyabiashara kuagiza  mafuta hayo. Iwapo malighafi ya kuteng’eneza mafuta ingetokana na uzalishaji wa ndani, kwa mfano, mbegu za pamba, ufuta, karanga, pareto na alizeti, manufaa haya yangekuwa ni pamoja na kodi inayotozwa katika mchakato wa uzalishaji, na kodi ya mauzo, vyote vingekuwa ni sehemu ya ya pato la nchi yetu, na hivyo kuisaidia Serikali kukabiliana na mahitaji ya fedha katika uendeshaji wa miradi mbali mbali.

Hali hii imesababisha maisha kupanda na kuwaweka wananchi katika hali ngumu hadi kuteng’eneza misamiati ya maneno yanayoashiria ugumu wa maisha kama vile vyuma kukaza n.k.

Kwa kuzuka msemo maarufu wa kukaza vyuma, kumekuwepo na kufikirishwa kusikokuwa sahihi kwa jamii kuwa pengine mamlaka chini ya uongozi wa Rais Magufuli, umekuwa ukihusika vikubwa na kukosekana au kuimarika kwa udhaifu wa mzunguko wa fedha na hali ngumu nchini.

Pamoja na jitihada na matamko mbalimbali ya serikali bado kuna ombwe la jitihada za wazi katika kuimarisha sekta hii ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi sambamba na nguvu ya uchumi ya wananchi wa kada zote zote, kuanzia wafanyabiashara wakubwa hadi mkulima maskini wa migundani.

Kwa miaka mingi, nchi nyingi za Afrika zimechukua hatua zisizokidhi haja ya utashi na umuhimu wa sekta ya kilimo kutokana na kukosekana kwa mipango thabiti ya kimkakati katika kuinua na kusimamia kilimo chenyewe na ubora wa kinachozalishwa kutoka mashambani.

Kutokana na kukosekana kwa utashi na mkakati wa kudumu wa kusimamia kilimo tumejishitukia kwa pamoja kama nchi tukishindwa kunufaika na sekta hii takatifu zaidi ya kunufaika kwa kiasi kidogo na kinachozalishwa kwa maana ya kupata chakula kidogo mara nyingi bila ziada ya kuhimili mahitaji ya kiuchumi kwa msingi wa fedha.

Baada ya kupitia katika maisha magumu ya kilimo, ni vyema sasa serikali na vyombo vyake haswa watu wa mipango, watunga sera na Wizara yenyewe ya kilimo kuanza utaratibu wa kuunda chombo maalum cha kusimamia mbali na wizara yenyewe utaratibu utakaowezesha usimamizi na uhamasishaji wa karibu, udhibiti na mafunzo pamoja na uwezeshwaji wa wakulima walio tayari katika shughuli ya kilimo pamoja na vijana wanaotoka vyuoni, wakazi wa mijini wanaofanya shughuli tofauti na kilimo kuwawezesha kuwekeza katika kilimo biashara.

Hapa ndipo pahala pa kufikiri, baada ya miongo mingi kupita huku jitihada za kuimarisha sekta ya kilimo zikionekana wazi wazi, lakini mafanikio yakififia baada ya muda fulani tokea juhudi hizo zilipanzishwa, kumekuwa na pengo la kiusimamizi katika Wizara ya Kilimo kwa muda mrefu, pengo hili lazima litafutiwe dawa, lakini dawa haiwezi kuwa mujarabu iwapo pengo hilo halitajulikana ni pengo la kitu gani.

Kwa mtazamo wa kiuweledi, kunatakikana “Chombo” katika Wizara ya Kilimo ambacho kinaweza kuitwa jina lolote kwa ajili ya kusimamia haya tuliyoyazungumza kwenye aya za makala hapo juu. Pengine watu wanaweza kupendekeza majina au jina la chombo hiki liwe jina lolote liwalo, lakini hatimaye litakwenda kuwa Wakala wa kusimamia maendeleo na ufanisi katika kilimo nchini Tanzania.

Wakala huu utafanya kazi sio ya usimamizi wa Sera bali tafsiri ya kinachokusudiwa kwenye sera husika ya kilimo katika taifa letu. Wakala huu pamoja na mambo mengine upewe jukumu la kuhakikisha kwa mfano, uzalishaji wa mbegu bora za aina mbalimbali kwa ajili ya kilimo kutokana na matakwa ya ubora wa ardhi kwa ajili ya mazao mbalimbali ya kilimo.

Kwa mfano kuwepo kwa Wakala wa barabara katika wizara ya ujenzi na uchukuzi kumesababisha kuboreka kwa kiasi kikubwa kwa huduma na shughuli za usimamizi na ubora wa barabara hapa nchini hali ambayo imeliweka taifa letu kuwa taifa lenye barabara bora zaidi katika nchi zote za Afrika Mashariki na kati, ambapo katika ujenzi wa barabara Tanzania imefanikiwa kujenga jumla ya kilomita 120,000 za lami kwa nchi nzima.

Hakuna ubishi wowote kwamba kabla ya kuundwa kwa Wakala wa barabara katika Wizara ya ujenzi na uchukuzi, mafanikio yalikuwa kwa mwendo wa kinyonga, tofauti na sasa ambapo karibu nchi nzima imeunganishwa kwa mtandao thabiti wa barabara kutoka kaskazini hadi kusini, na Mashariki hadi magharibi, mbali ya maelufu ya kilomita ya vipande vya  barabara vinavyoisaidizana na barabara kuu katika huduma ya usafirishaji nchini.

Wazo la kuwa na wakala wa ubora na huduma za kilimo si wazo la kubeza, bali lizue mjadala wenye tija katika kujenga ufanisi na kuimarisha sekta ya kilimo hivyo kuifanya sekta hii kupendwa na kuipa tafsiri sahihi kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu ili iungane na kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais ya kujenga uchumi wa viwanda nchini.