Home Makala WAKAZI WA CHAMWINO WAMSUBIRI  JPM AWAPE MAJI

WAKAZI WA CHAMWINO WAMSUBIRI  JPM AWAPE MAJI

1536
0
SHARE

NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA


CHAMWINO  Ikulu ni kijiji ambacho kipo katika Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma. Hapa ndipo ilipo Ikulu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ikulu hii ipo tangu enzi za Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ukifika katika eneo hilo utakutana na miti iliyopandwa kwa ustadi mkubwa kuelekea katika eneo hilo.

Hapa unapata picha kwamba enzi za Mwalimu Nyerere katika eneo hilo kulikuwa na maji ndio maana miti iliweza kustawi na na kuvutia.

Lakini jambo la kushangaza katika Wilaya hiyo ambayo anatarajiwa kwenda kuishi Rais wa sasa Dk. John Magufuli kuna shida ya maji.

Pia wakazi wa eneo hilo wako hatarini kuugua magojwa ya mlipuko kama kipindupindu na homa ya matumbo kutokana na kukosa maji safi na salama. Kwa sababu maji machache wanayobahatika kuyapata wamekuwa wakichangia katika matumizi na wanyama kama mbuzi na ng’ombe katika visima viwili vilivyopo katika kijiji hicho.

RAI lilifika katika kijiji hicho na kuzungumza na wakazi wake ambao pamoja na mambo mengine wanaiomba serikali iwasaidie kupata maji safi na salama.

Mmoja wa wakazi hao, Josephine Msakanga, anasema kutokana na shida ya maji na mvua kunyesha kidogo, madimbwi ya maji yanayotwama wanatumia na wanyama ili kupata maji ya kutumia.

Naye Haruna Chedego, anasema katika kijiji hicho kuna visima viwili ambavyo vinategemewa na vijiji vinne vya Buigiri, Chamwino, Chinangali 11 na Msanga.

‘’Maji yenyewe tunayachota katika mazingira ambayo sio safi wala salama kuna visima vingine vitatu lakini hakuna pampu, hapa kwetu kuna shida sana ya maji wanaohusika na hili jambo tunaomba watusaidie tuweze kupata maji safi na salama’’ anasema.

Denis Kitoziri  ambaye pia ni mkazi wa eneo hilo anasema kwa ujumla Halmashauri ya Chamwino imekuwa na tatizo la maji huku wanaohusika wakiziba pamba masikioni na wananchi wakiendelea kuteseka.

‘’Ndugu umejionea jinsi kulivyo na shida ya maji miundombinu yenyewe imechakaa na ukienda kwa viongozi wetu wana maneno matamu kweli, acha tuje tuishi huku na Rais Magufuli labda watatukumbuka’’ anasema

Naye Mwajuma Athumani anasema visima  viwili vilivyopo katika kijiji cha Chamwino Ikulu havitoshi kutokana na idadi kubwa ya watu wanaoongezeka kutokana na Makao Makuu ya Nchi kutangazwa kuhamia Dodoma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho, Joseph Seganje,  anakiri kuwepo kwa tatizo la maji katika eneo hilo na kudai kuwa limesababishwa na ongezeko la watu ambapo miundombinu iliyopo ilikuwa ni kwa ajili ya kuhudumia kaya 250 zilizokuwepo awali.

‘’Sasa hivi tuna jumla ya watu 26,000 tena kwa miundombinu ile ile ya zamani lazima kuwe na shida ya maji ila Serikali hii ni sikivu hivyo itaboresha na maji yatapatikana ndani ya muda mchache’’anasema

Naye  Meneja wa mamlaka ya maji safi na maji taka Chamwino ikulu (Chuwasa), George Mwakamele, anasema ili kukabiliana na tatizo la maji katika Wilaya ya Chamwino wanajenga tanki la maji la lita 2,000 katika kijiji cha Buigiri, ambalo litakuwa na uwezo wa kusambaza maji kwa watu 1,000.

‘’Tutakarabati miundombinu pamoja na kujenga tanki kubwa la maji katika kijiji cha Buigiri hili litaweza kusambaza maji kwa watu wengi hivyo shida ya maji itaisha’’anasema

Hoja hiyo inaungwa mkono na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Athumani Masasi, ambaye anasema, halmashauri hiyo  inatarajiwa kuwa na ongezeko la watu kufikia 35,000 hadi 40,000 ambapo anadai  mikakati iliyopo ili kuhakikisha watu wote wanapata maji safi na salama.

“Tutatajenga  matanki mawili makubwa kwa kushirikiana na Wizara na Mkoa  ambapo zitapatikana lita 800,000  lengo ni watu wote watakaokuja Wilayani Chamwino waweze kupata maji safi na salama’’ anasema