Home Latest News Waliopewa dhamana wawakilishe wananchi kwa vitendo

Waliopewa dhamana wawakilishe wananchi kwa vitendo

2149
0
SHARE

Na MWANDISHI WETU 

MIONGONI mwa hoja zinazotolewa pindi zinapotokea kasoro katika utendaji ni kujipima kama mhusika anafaa kuendelea kuwa kwenye nafasi anayoitumikia kwa wakati huo na unaweza kuwa na msukumo kutoka kwa mtu au kikundi cha watu kulingana na hitaji na kubwa zaidi msukumo unaweza kutoka kwa mwajiri.

Katika kujipima na kuachia mamlaka ili kutoa nafasi kwa wengine wanaoona kuwa wanafaa huwa mara nyingi ni kipimo cha kiongozi aliye makini na baadaye wanajamii wanaweza kumkumbuka kwa ujasiri wa kuikabili hali hiyo.

Hivyo katika mazingira ya aina hiyo ni dhahiri kuwa kila mmoja na hasa wenye ofisi za umma ama zozote zenye kutoa huduma kwa umma, wanapopewa ushauri au mwaliko wa kujipima, hicho ndicho huwa ni kipimo kuwa wanajali kwa kiasi gani maslahi ya wananchi walio wengi dhidi ya maslahi binafsi.

Kiongozi anapopata fursa ya uongozi anatakiwa kufanya hivyo kwa niaba ya wananchi walio wengi; na ili aongoze vyema kuna mkataba unaomwelekeza.

Mwanafalsafa Jean-Jacques Rousseau (1712-1778) kwenye kazi yake ya Mkataba wa Jamii (The Social Contract (1762)) aliwahi kusema kiongozi anafanya yale anayoelekezwa na wananchi na si anayotaka yeye.

Kwa mtazamo rahisi tu ni viongozi wangapi hivi leo wanazingatia kauli hiyo iliyo wazi ya  mwanafalsafa huyo?  Walio wengi wamekuwa hawafuati makubaliano baina yao na wananchi, na kwa hali hiyo wanalazimika kuacha mamlaka kwa wananchi wengine ili waongoze.

Hali hiyo inajibainisha kwa kuzingatia kauli ya mwanafalsafa mwingine wa Kiingereza    John Locke (1632-1704) ambaye alisema kuwa kiongozi mzuri anatakiwa awe na kumbukumbu ya makubaliano yake na wananchi moyoni mwake, vinginevyo aachie mamlaka au kwa maneno mengine aachie ngazi.

Kwa kiwango kikubwa viongozi wanatakiwa kujiangalia kwenye kioo kuhakiki kiwango cha uzalendo walio nao. Hapo ndipo panapotakiwa kujiangalia kama wanafaa kwenye  nafasi zao za utumishi au la.

Kinachogomba  hapo ni dhana ya utumishi maslahi badala ya utumishi wa umma kwa kufuata maelekezo ya mikataba baina yao na wananchi.

 Katika nchi ambayo inaamini kwenye mfumo wa demokrasia utendaji unaoonesha kwenda kinyume na mahitaji yanayofungamanishwa na demokrasia  ambayo ni uhuru kwa mwananchi kushiriki moja kwa moja katika kujadili na kutoa maamuzi kwa mambo yote yanayoihusu jamii na yeye mwenyewe unakuwa ni utendaji batili.

Hali hiyo inamaanisha kuwa, kila mtu angependa kushiriki yeye binafsi, lakini kwa kuwa idadi ya watu ni kubwa mno na hivyo kuwa ni vigumu kuwakutanisha wote kwa pamoja, kwa sababu sio rahisi kuwaweka watu wote kwa pamoja sehemu moja kujadili yanayowahusu.

Kwa kuzingatia hali hiyo ndani ya mfumo wa kidemokrasia ndio unakuwepo  uwakilishi kupitia Bunge ambao unamaanisha kuwa walio wengi wanawachagua wachache ambao wanawaamini kuwa  wana akili timamu na uwezo kama sio ujuzi ili kuwawakilisha kwenye kuyafanyia maamuzi na kupata ufumbuzi wa matakwa na mahitaji yao.

Kimsingi kupitia mfumo huu haimaanishi kuwa utendaji wa kidemokrasia  unaweza kufanyika kiholela bali ni namna ya ushiriki hubadilika au utendaji hubadilika kwa kuwapa fursa wananchi kutoa nafasi ya ajira kwa wawakilishi kupitia chaguzi ambazo mara nyingi huhesabika kuwa ni huru na za haki pia. Chaguzi hizo ni huru na za haki kwa maana hazina uchakachuaji.

Katika ajira hiyo wanatakiwa kulinda na kuwezesha  majadiliano yaliyo huru na yenye ukweli ndani yake na katika mazingira ambayo hayatatofautiana na  uwepo wa watu wale wanaowawakilisha kwa kuzingatia kuwa kama nafasi hiyo ingewezekana kupatikana na wangekuwepo ndani ya kumbi za bunge.

 Katika mazingira hayo mbunge  au mwakilishi ambaye anaingia ndani ya bunge na kwenda kinyume na ajira aliyopewa na wananchi, huyo wakati akijinadi kuomba ajira hiyo  alikuwa na yake moyoni kuwa alikuwa anaomba kula sio kura. Hawa wa aina hii ni wengi na ndio wanaokiuka mikataba baina yao na wananchi. Hawa ndio wachumia tumbo.

Majadiliano huru, haki na ukweli Bungeni, vina lengo la kuikosoa Serikali ili iwatumikie vyema wananchi walioiweka madarakani. Lakini  inapotokea majadiliano kutokuwa kwenye mizania inayokubalika  hilo huifanya mioyo ya  waliowapa ajira kunyong’onyea na kujikuta wakikata tamaa na kujishika tama kwamba walitoa ajira kwa wasiowajibika kwao.

Ili kujiondoa kwenye maudhi kwa waajiri (wananchi) ni kutumia uhuru na demokrasia iliyopo kukubali yanayokidhi matakwa ya waajiri na kuyakataa yale yanayowaudhi wanaowawakilisha.

Kmsingi ni kwamba ajira ya uwakilishi inatokana kwa wananchi hivyo uwakilishi unapaswa kuongozwa na matakwa ya wanaowakilishwa badala ya kuongozwa na ushabiki usio na tija.

Ni muhimu kujenga fikra sahihi kwamba watoa ajira wanatakiwa kuheshimiwa pamoja na matakwa yao chanya kwani wao wanabakia wakiwa kimya wakiwa na subira yenye heri lakini mambo yanapokwenda kinyume huwataacha kuikumbuka  kauli ya   Martin Luther King aliyowahi kusema, “Maisha yetu huanza kuonekana  hayana maana pale tunapokuwa kimya wakati mambo yasiyofaa yanaendelea kufanyika mbele yetu.”