Home Habari Wananchi hawachagui CCM sababu ya Azimio la Arusha

Wananchi hawachagui CCM sababu ya Azimio la Arusha

1007
0
SHARE

Na BALINAGWE MWAMBUNGU

NIMEWAHI kumnukuu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Bashiru Ally, alipotamka maneno haya akiwa Zanzibar kwamba: ‘Hakuna chama cha kushindana na CCM’. Nikakubaliana naye kwamba ni kweli, lakini sababu kubwa niliyotoa ni kwamba hapawezi kuwapo chama cha kushindana na CCM kwa sababu bado ni ‘chama dola’ na Dola haija sawazisha uwanja ili vyama vya siasa vilivyopo, vicheze katika uwanja ulio sawa.

Juzi kati hapa, Bashiru ameandika katika akaunti yake paragrafu 15, akieleza au akijibu hoja ya kwa nini yeye na Katibu Mwenezi wake, Hamphery Polepole, wanafanya mikutano ya hadhara mikoani, wakati vyama vingine—hasa chama kikuu cha upinzani—Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wanazuiwa. Kwa nyakati tofauti wote wawili wamesema wanafanya  hivyo kwa sababu wanakagua miradi inayotekelezwa na serikali inayoongowa na chama chao, kama ilivyotamka Ilani yao ya uchaguzi.

Lakini, kama kumbukumbu zangu ni sahihi, sababu kuu aliyoitoa Rais John Magufuli, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, ni kwamba anataka nchi itulie, wananchi wapate muda wa kufanya kazi. Baada ya hapo Serikali ikapitisha muswada bungeni ulioondoa haki ya wananchi kufuatilia Bunge lao na kujua yaliyokuwa yanajiri kupitia televishenizote. Serikali ilipobanwa kwamba haikuwa sawa na ilikuwa ni kinyume cha Katiba, ikaja na jibu kwamba wananchi na wafanyakazi walikuwa wanatumia muda mwingi wa kazi kuangalia Bunge, na kwamba hatua hiyo ilikuwa ni sehemu ya kubana matumizi. Televisheni binafsi ambazo hazigharamiwi na Serikali, pia hazikuruhiwa kurusha matangazo! Walioelewa wakaelewa kwamba ilikuwa njia moja wapo ya kulidhibiti Bunge.

Lakini kiuhalisia hivi sasa sababu zote mbili, ni sababu mfu kwa kuwa kila Rais anapofanya ziara mikoani Televisheni ya Taifa, huonesha vipindi laive. Kusudi la kuonesha shughuli za Rais nini? Watazamaji wake ni nani? Nani anagharamia?

Tukirudi kwenye twit ya Bashiru nanukuu para ya kwanza: “Nawakumbusha wana CCM wenzangu wasitangulize Mashati ya  Kijani bali Haki na Usawa  Kuvaa shati la kijani huku unapora watu na Dhuluma ni Unafiki.”

Ni haki gani anayoizungumzia wakati viongozi wengine hukatazwa kufanya mikutano ya ndani? Ni usawa upi wakati upande mmoja kila mara huhamisha magoli? Wanafiki walikuwapo toka zamani—walivaa magwanda ya kijani, lakini hawakuwa wafuasi wa Mwalimu Julius Nyerere na siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea. Walifurahi alipoondoka.

Dk. Bashiru nadhani kwa usomi wake, amepitia Mwongozo wa  TANU wa 1984 ambao ulikielekeza chama kuwa msimamizi wa shughuli zote za umma. Kwa wakati tulionao, viongozi wa CCM sio watendaji—hawapaswi kuingia jikoni. Chakula kikiharibika wao ndio watakaotupiwa lawama.

Pili ni vizuri Katibu Mkuu anapozulu sehemu, kukagua utekelezaji wa Ilani yao, akutane na watendaji tu. Mbona anafanya mikutano na wananchi ambao hawahusiki na miradi hiyo? Atuambie tu kwamba yeye na Polepole, wanazunguka wilayani kukijenga chama upya na kuingiza wanachama wapya, kwa sababu CCM almanusura kipinduliwe mwaka 2015, lakini wapinzani hawaruhusiwi kufanya hivyo, japo ni kinyume na Katiba ya nchi.

Ametwit kwamba kama chama chake kinataka kuendelea kutawala kihalali lazima kitake kisitake, kishughulikie shida za wakulima na wafanyakazi, tena wanyonge. Kwa mtazamo wangu, Katibu Mkuu anaimba wimbo tofauti na Wabunge wa CCM ambao wameunga mkono hoja ya kuwanyima wafanyakazi wanyonge, nyongeza ya mishahara! Ni wanyonge gani hasa anao wazungumzia?

Anasema CCM sio chama cha uchaguzi tu, bali ni Chama cha Maendeleo (?). Hatishwi hata Kilosa nzima ikienda upinzani sio shida na kwamba hawezi kuacha kutenda haki eti chama chake kitanyimwa kura.  Hapana shaka kuna madudu aliyoyaona ya kuwakandamiza wananchi na kuwapoka haki kwa sababu tu wanaunga mkono upinzani. Ndivyo ilivyo katika baadhi ya nchi za Kiafrika—mtu hapewi mgawo wa chakula wakati wa shida kwa sababu si mwanachama wa chama tawala! Tumeyaona wakati wa ‘hama hama za kuunga juhudi’ na viongozi wa juu walifurahia.

“Kama CCM haiwezi kusimamia Haki na Usawa kwenye uchaguzi ujao (wa Serikali za Mitaa), acha tupigwe ili tuwe na adabu kuwaheshimu Wananchi.”

Hapa tena naona Katibu Mkuu huwa hafuatilii kauli za Mwenyekiti wake ambaye alitamka bayana kwamba ifikapo 2020 hapatakuwa na upinzani. Wananchi kujiunga na upinzani ni haki yao ya Kikatiba. Ukifuta upinzani huwezi kujitathmini. Upinzani makini na wenye nguvu ndio ‘litimus’ ya chama—kipimo cha chama chochote cha siasa kilicho madarakani duniani.

Bila upinzani wenye nguvu, viongozi hudhania wao ni miungu na wataendelea kutawala ‘addendum’. Na hiki ndiyo chanzo cha kukanyaga kanyaga haki za wanyonge na kuwatupa lupango wote wanaopiga kelele kwamba wanaumizwa, eti ni wachochezi.

Ni Bashiru na Polepole tu wanaotamka wazi kwamba Sera ya CCM ni Ujamaa. “Lazima tusimamie misingi ya Azimio la Arusha bila woga. Hii ndio salama yetu CCM kubaki madarakani’’

Azimio la Arusha? Limefufuliwa lini? Nani anataka turudi kwenye ujima? Lini CCM walikaa kitako na kukiri kwa dhati kwamba wanaamini katika injili ya Azimio la Arusha. Hakuna, kwa sababu italeta mgongano na Serikali ambayo hivi sasa inatekeleza Sera ya Uchumi Huria na Utandawazi. Inawahamasisha wenye mitaji wa nje na ndani, kuwekeza kwenye viwanda, ili Tanzania iingie katika nchi zenye uchumi wa kati ifikapo 2025-2035. Ujamaa unasisitiza kwamba wananchi, kupitia Serikali yao, lazima washike njia zote kuu za uchumi. Bashiru anaishi na nadharia iliyopitwa na wakati. Wenye nacho ndio wanao amrisha wimbo wa kuimba.

Hakuna nchi duniani ambako watu wote wana hali ya kiuchumi iliyo sawa. Nadhani hata mwenyewe amejionea maisha ya wananchi yalivyo huko vijijini ambako CCM kimejikita—wakipigia kura sio kwa kwa sababu ya Sera ya Ujamaa. Hata Sera ya Vijiji vya Ujamaa haitekelezwi huko—imeisha sahaulika.

Katibu wa 10 wa CCM anasema yeye amebeba mazuri na mabaya yote ya watangulizi wake—kwamba na yeye ataacha ya kwake—kama hili la kutamka kwamba watumishi wa umma ambao hawawezi kufuata maelekezo ya CCM Tanzania nzima waache kazi wakalime. Kwani watumishi hao ni waajiriwa wa CCM?

Katika nchi zenye demokrasia iliyo komaa, watumishi wa umma ndio mhimili wa serikali, hawatikiswi tikiswi. Hawaondolewi kazini kwa matakwa ya wanasiasa, hawagomewi na Madiwani au Wabunge kwamba hawawezi kufanya kazi nao. Watumishi kwa upande wao, wanajitambua, wanasimama kwe masharti yao ya kazi, huwa hawababaiki na maamuzi ya kisiasa ambayo mara nyingine yanatolewa ‘at the whims of’ mamlaka teuzi—hawa hawanyanyaswi kwa kutumbuliwa hadharani kwa kuwa kunataratibu za kufuata.

Watumishi ndio serikali, wanaweza kuendesha nchi bila ya wanasiasa, kwa kuwa kuna taasisi imara za kuchungana –checks and balance—hawaondolewi kazini kwa sababu chama kingine kimeingia madarakani—ni wateule tu ndio huondoka na aliyewateua. Hii ndio nguzo kuu ya utulivu (stability) na ndiyo inayoimarisha misingi ya Haki, demokrasia na Utawala Bora.

Dk. Bashiru ambaye alitegemewa kuleta mabadiliko chanya katika chama chake, anaturudisha nyuma kwenye falsafa mfu—isiyo na mashiko tena. Nyakati zimebadilika, hata hao vijana wanaovaa mashati ya kijani, bila hata kufanya risechi, hawajui mambo ya ujamaa, au dhana ya utawala msonge na Dola kushika hatamu na njia kuu zote za uchumi.