Home Makala Watoto shuleni wanapofia motoni huku wakililia nafsi zao!

Watoto shuleni wanapofia motoni huku wakililia nafsi zao!

1277
0
SHARE
Kaimu Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, DCF Charo Mangare akimpa pole mmoja wa wazazi wa watoto waliokuwepo eneo la tukio la ajali ya moto iliyosababisha vifo vya wanafunzi 10 katika Shule ya Msingi ya Byamungu iliyoko Kata ya Itera,Wilayani Karagwe mkoa wa Kagera.Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

NA JAVIUS KAIJAGE

USIKU wa kuamkia Septemba 14 mwaka huu, jumla ya wanafunzi 10 walifariki dunia kwenye ajali ya moto iliyotokea katika Shule ya Msingi ya Kiislamu ya Byamungu iliyopo Kata ya Itera wilayani Kyerwa mkoani Kagera.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Rashidi Mwaimu, bweni lililoungua ni la watoto wa kiume na lilikuwa limebeba watoto 74 na watoto 6 wamepelekwa katika Hospital ya Nyakahanga iliyopo wilayani Karagwe kwa ajili ya matibabu.

Kuungua kwa watoto hao wadogo kabisa waliokuwa na umri kati ya miaka 6 hadi 10, ni tukio la kusikitisha na kuhuzunisha katika mioyo ya Watanzania na dunia nzima kwa ujumla kwa kuzingatia kuwa tukio hilo ni mwendelezo wa matukio mengi ya shule nyingi kuungua kwa moto hapa nchini, huku ajali hizo za moto zikisababisha madhara makubwa ikiwemo vifo na mali kuharibika.
Mnano June 18 mwaka 1994, moto mkali ulizuka bwenini katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Shauritanga iliyoko katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro na kusababisha vifo vya wanafunzi 42 wa kike.

Ajali hiyo iliyosababisha wanafunzi hao waliofariki kuzikwa kwa kaburi la pamoja kutokana na kuungua kwao vibaya, iliacha simanzi kubwa isiyoweza kufutika haraka kwa ndugu, jamaa, rafiki na Watanzania wote kwa ujumla ambao kimsingi walihitaji mchango wa wanafunzi hao katika ujenzi wa taifa.
Februari 29 mwaka 2016, mabweni mawili ya Shule ya Sekondari ya Iyunga jijini Mbeya, yaliungua kwa moto kutokana na chanzo kilichohisiwa kuwa ni shoti ya umeme.

Julai 10 mwaka 2016 Shule ya Sekondari ya Lindi mkoani Lindi, iliteketea kwa moto lakini moto huo uliweza kudhibitiwa na hatimaye kutosababisha vifo licha ya mali za shule kuharibika.
Mwaka 2018,  taharuki ilitanda katika Shule ya Msingi ya St Joseph Rutabo iliyopo Kamachumu wilayani Muleba mkoani Kagera baada ya mabweni ya wanafunzi kuungua moto ambao inasemekana ulisababishwa na hitilafu ya umeme.

Kutokana na tukio hilo la ajali ya moto shuleni hapo, mwanafunzi wa darasa la tano aliungua na kufariki dunia huku wanafunzi wengine wakisalimika.

Februari mwaka 2018 katika Shule ya Sekondari Katunguru iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza palitokea janga la moto lililosababisha bweni la wavulana kuungua.

Mei 23 mwaka 2019, majira ya saa 6:00 mchana ulizuka moto katika Shule ya Ashira na kusababisha kuungua kwa mabweni ya wanafunzi.

May 23 mwaka 2019, moto uliounguza  bweni la Shule ya Sekondari Marangu iliyoko mkoani Kilimanjaro.

Julai 4 mwaka 2020, moto ulizuka katika Shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Ilala jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya wanafunzi watatu, huku ukiharibu mali za shule hiyo.  

Moto ulioanza muda wa saa nane usiku, ulitokea kwenye moja ya hosteli wanapokaa wanafunzi wa kiume huku chanzo cha moto huo kikiwa bado hakijajulikana.

Shule ya Sekondari ya Lowassa iliyoko wilayani Monduli mkoani Arusha iliwahi kuungua kwa moto na kwa mujibu wa  Mwalimu Mkuu na wanafunzi wa shule hiyo, ni kwamba moto huo ulianza majira ya usiku wakati wanafunzi walipokuwa wameenda madarasani kwa ajili ya kujisomea.

Moto huo uliteketeza mali zote zilizokuwa katika jengo ikiwa ni pamoja na vitanda na magodoro; nguo, vitabu na madaftari ya wanafunzi hao.

Aidha Mkuu wa Shule hiyo, Salim Janitu aliwaambia waandishi wa habari kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyotokea katika jengo hilo.

Moto huo ulioanza saa tatu usiku chanzo chake hakijajulikana na wanafunzi wote walikuwa madarasani wakijisomea hivyo waliofikishwa Hospitali ya Wilaya Magunga, walipata mshtuko tu.

Septemba 18 mwaka 2019 Shule ya Sekondari ya Old Tanga nchini  iliteketea kwa moto ambao kimsingi ulisababisha baadhi ya mali za shule hiyo kuharibika.

Julai 18 mwaka 2019, Shule ya Sekondari ya Mkolani iliyoko katika Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza iliungua kwa moto na kusababisha uharibifu wa mali.

Akikabidhi msaada wa vifaa kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk. Phills Nyimbi alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya wakishirikiana karibu na kamati ya maafa wameishachukua hatua ya kuunda kikosi kazi cha kuchunguza chanzo cha tukio la moto .

Dk. Phills Nyimbi aliongeza kusema kuwa  kinachoshangaza zaidi ni moto kuunguza chumba namba 27,37 na 47

Julai mwaka  2020, Shule ya Kiislamu ya  Sekondari ya Mavuno na ile ya Kiislamu ya Kinondoni ni miongoni mwa shule ambazo ziliungua kutokana na moto.

Kutokana na tukio la shule hizo za Kiislamu kuungua, serikali iliamua kuunda tume ya uchunguzi iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge na kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akihutubia Baraza la Eid El Adh’aa Julai 31 mwaka 2020 aliwaeleza waumini wa Kiislamu kuwa tume hiyo iliundwa baada ya kupokea mfululizo wa ajali hizo pasipo chanzo chake kujulikana.

‘‘Mheshimiwa Mufti na Waislaam wenzangu mmezungumzia suala la madhara makubwa yanayoendelea sasa ya majengo yetu ya shule za sekondari na msingi, kuungua moto jambo hili serikali tumelipokea,”alisema Majaliwa.

Hayo yakiwa ni baadhi ya matukio  machache ya shule kuungua moto katika vipindi tofauti kuna haja ya kujiuliza kuhusu chanzo halisi cha majanga hayo.

Je, ni uzembe uliosababishwa na mafundi wa umeme wakati wakitengeneza miundombinu ya umeme kwa maana ya kufanya ‘‘wiring vibaya?’’

Je, matengenezo hayo ya umeme yalifanywa na mafundi vishoka ambao kimsingi hawakuwa na ujuzi wowote?

Je, ni miundombinu ya umeme kuchoka kutokana na kuwa ilitengenezwa kwa muda mrefu uliopita bila ya kufanyiwa marebisho?

Je, ni matumizi mabaya ya umeme kwamba inawezekana katika baadhi ya shule wanafunzi wake wanaweza kuwa wanachokonoa miundombinu ya umeme na kupelekea shoti?

Je, ni mifumo ya Shirika la Umeme (Tanesco) kwamba inawezekana walikata umeme bila kuweka tahadhari?

Je, kuna hujuma yoyote inayoweza kuwa inafanyika kwa malengo ya ushindani kibiashara au kuoneana wivu hususan katika shule binafsi?

Je, kuna hila nyingine ya kutaka kulipizana kisasi kwa kuondoa uhai wa watoto wasiokuwa na hatia?

Kimsingi maswali yote haya pamoja na mengine kuna haja ya kufanya tafakari ya kina, ili hatimaye kuja na majibu ya uhakika kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu.

Tukifanya rejea ya visababishi vya moto huko shuleni, ikumbukwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brig. Jen. Nicodemus Mwangela aliwahi kuwachapa viboko wanafunzi watano waliohusika katika tukio la kuchoma moto Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Oswe na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 26.

Brig. Jen. Mwangela alifikia hatua hiyo mara baada ya kamati aliyoiunda ya kuchunguza chanzo cha ajali ya moto uliotokea shuleni hapo kubaini kuwa kuna wanafunzi wawili waliochoma mabweni ya shule hiyo huku wenzao watatu wakiwa na taarifa za mipango hiyo na hawakuripoti.

Rejea nyingine ni ile shaka ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana wakati akitoa msaada wa vifaa katika shule iliyoungwa ya Mkolani aliposema kinachoshangaza zaidi ni moto kuunguza chumba namba 27,37 na 47

Rejea nyingine ilikuwa ni kufuatia mfululizo wa matukio ya shule za Kiislamu kuungua hapa nchini, ambapo Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Mussa Kundecha, aliposema wakati akihojiwa aliposema: kwa sababu kumekuwa na misigano kati ya shughuli za kidunia na vituo vyetu vya kidini. Kwa hiyo, tunafanyia kazi vitu vya aina mbili; kwanza kukaa na viongozi wetu kuelimishana juu ya jambo hili, pili tumefanya mpango wa kuomba watu wa jeshi la zimamoto ili tukae nao kufanya semina kuhusiana na vyanzo vya moto na sababu zake ili tuvipe somo vyetu.’’

Aidha kiongozi huyo wa kidini aliongeza kusema waliamua kuchukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa maeneo ya misikiti, tahadhari za moto zipo kwa sababu ni sehemu ambayo watu wanaingia na kutoka.

 “Lakini hicho kipindi cha kuingia na kutoka, kunaweza kutokea jambo, na tunafikiri kuna haja ya semina hizi ili kuongeza tahadhari za kuzuia moto.

 “Lakini pia kama ilivyo kwenye mahoteli, kuna vifaa vya kuzuia moto, lakini bado kwenye majumba yetu ya ibada na shule, hayajajengwa kwa mfumo huo. Kwa hiyo, tunajaribu kuyaona haya mapungufu ili tuone wataalamu watakavyotushauri.’’

Shehe Kundeka alipohojiwa kama ni hujuma  alisema, kwa sasa haiwezekani kusema moja kwa moja kuwa kuna hujuma kutokana na mfululizo wa matukio hayo kwa sababu misikiti na taasisi hizo zinaonesha bado hazina mifumo thabiti ya kudhibiti moto.

“Usimlaumu anayekutilia shaka, angalia ulipokaa, ukikaa mahali panapotia shaka usimlaumu anayekuangalia vibaya, lakini kama tukiwa na tahadhari zote, ni rahisi sasa kwenda kunakofuata, kwa hiyo tusikimbilie hujuma kwanza.’’

Hoja ya Shehe Kundecha iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Shehe Hamis Mataka ambaye naye alisisitiza kuwa kuhusu uchunguzi wa matukio hayo, wanasubiri matokeo ya uchunguzi wa vyombo vya usalama.

 “Tunasubiri wakamilishe uchunguzi wao wa kitaalamu ili tujue tuanzie wapi. Kwa sababu uchunguzi ukikamilika, utaondoa dhana zinazoibuka,” alisema Shehe Mataka.

Kimsingi tukio lililotokea juzi katika shule ya Kiislamu ya Byamungu, kuna haja ya vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi wa haraka tena wa kina ili kuja na majibu ambayo yatawaridhisha watanzani kuhusiana na ajali za moto huko shuleni.

Hata hivyo kuna haja ya Jeshi la Zimamoto kwa kushirikiana na vyombo vingine kuweka utaratibu wa kufuatilia mara kwa mara  taasisi mbalimbali ili kujua kama ziko sawa sawa katika mifumo yake ya kujikinga na moto na ikiwezekana kutoa elimu na ushauri wa namna ya kujikinga pindi ajali zinapotokea.

Barua pepe: HYPERLINK “mailto:javiusikaijage@yahoo.com” javiusikaijage@yahoo.com Simu: 0756521119