Home Habari WAWEKEZAJI SITA KILIMANJARO KIKAANGONI

WAWEKEZAJI SITA KILIMANJARO KIKAANGONI

1786
0
SHARE

 

 

          18748566_303

NA SAFINA SARWATT, KILIMANJARO

MKOA wa Kilimanjaro

ni miongoni mwa iliyokuwa mikoa ya viwanda  pamoja namashamba makubwa ya kahawa, hata hivyo kwa sasa imekuwa tofauti hali inayomsukuma Mkuu wa Mkoa huo Anna Mghwira kuwaweka kikaangoni wawekezaji sita.

Katika miongo kadhaa iliyopita tatizo  la ajira mkoani hapa lilikuwa ni ndoto, kwani vijana walipata ajira zilizowawezesha kumudu maisha yao ya kila siku.

 

Hata hivyo, hali ilianza kubadilika katika miaka ya 1990 pale ambapo

serikali iliazimia kubinafsisha viwanda husika kwa watu binafsi au makampuni binafsi.

Huenda nia ya serikali kuanzisha sera ya ubinafsishaji ilikuwa ni njema ya kujiondoa  katika biashara iwe inachukua kodi lakini

waliopewa kazi ya kubinafsisha viwanda hivyo inaaminika walifanya dili na  kupewa posho matokeo yakawa kuviuza viwanda hivyo kwa bei ya chini au ya kutupwa.

 

Miongoni mwa viwanda hivyo vilivyobinafsishwa mkoani Kilimanjaro ni

pamoja na kiwanda cha Kiltimber Utilization, Imara Funiture, Kilimanjaro Machine Tools, Rongai Saw Mills, Tanzania Bag Corporation (Mill I na Mill 2), Nation Chemical Industries na Playwood.

 

Viwanda hivyo kwa sasa vimekufa na vingi vimegeuzwa kuwa maghala ya bidhaa za watu binafsi waliobinafsishwa viwanda hivyo.

Tanzania Bag Corporation ambacho kilikuwa kinatengeneza  magunia kupitia katani na mmea wa kenaf ambacho kilibinafsishwa ili kuendeleza uzalishaji wa magunia, kwa sasa hakuna uzalishaji wa magunia unaoendelea.

 

Hata hivyo, watanzania walidanganywa na wafanyabiashara ambapo katika hali  ya kushangaza majengo ya kiwanda hiki yamegeuzwa kuwa  kituo cha kusambaza  bidhaa kama sukari, juisi, unga wa ngano, mafuta ya kupikia, mchele  kwa  mikoa ya kanda ya kaskazini.

 

Kiwanda cha Kill timber kilichokuwa kikitengeneza nguzo za umeme ambazo  zilikuwa  zikitumika nchini, sasa kinachoendelea  ndani ya kiwanda hicho ni biashara ya vifaa vya ujenzi ikiwemo  mabati, nondo  na misumari ambavyo hazitengenezwi kiwandani hapo bali vinaletwa na kuuzwa.

 

Kiwanda kingine ni Nation Chemical Industries kilichokuwa kinazalisha

madawa ya kilimo hususani kwa zao la kahawa ikijulikana kama Blue Copper sasa kimegeuzwa ghala la kuhifadhia madawa kutoka nje ya nchi kinyume na malengo ya uazishwaji wa kiwanda husika.

 

Aidha, biashara  zinazoendelea hapo ni kwamba waliouziwa wanafanyabiashara ya kuleta madawa kutoka nje na kuhifadhi katika majengo ya kiwanda hicho  na si uzalisha kama ilivyokuwa awali.

 

Kiwanda cha mashine tools ambacho kilikuwa kikihusika na  uzalishaji wa mashine za  kati zilizokuwa zikitumika katika viwanda vidogovidogo pamoja na vipuri vya mashine, kwa sasa hali yake ni taabani kwani kwa

zaidi ya miaka 30 haikuzalisha  licha ya kwamba serikali imetangaza kukifufua.

 

Hata hivyo, kuna habari njema kuhusiana na kiwanda hiki kwani katika siku za karibuni Shirika la National Development Corporation (NDC) limeamua kukifufua kiwanda hiki ili kiendelee na uzalishaji wake.

 

Kiwanda cha Imara Funiture ambayo kilikuwa kikitengeza vifaa vya maofisi na nyumbani, ni miongoni mwa viwanda mfu.

 

Akizungumzia hali ya viwanda hivyo Mghwira anasema serikali imeaanza kuorodhesha viwanda vyote vilivyokufa ili kuanza kuchua hatua za kisheria kwa wawekezaji waliokiuka taratibu.

 

Anasema tayari amefanya ziara katika wilaya sita  za mkoa Kilimanjaro ambapo kuna halmashauri saba na kwamba katika ziara hizo

alibaini changamoto  mbalimbali ikiwemo  uwajibika  baadhi ya watumishi kwenye sekta za umma.

 

“Nimezunguka mkoa mzima kwakweli kuna fursa nyingi sana za uwekezaji katika viwanda  pamoja utalii tatizo kwamba hali ya  utendaji kazi kwa baadhi ya watumishi siyo ya kuridhisha wamekuwa wakifanya kazi kimazoea na kusahau majukumu yao na kuchangia kuwepo malalamiko ya

wananchi,” anasema.

 

Anasema katika maendeleo ya nchi uchumi wa viwanda ni muhimu sana, “Ni kweli serikali ina nia ya dhati ya kufufua viwanda hasa kwa mkoa wangu wa Kilimanjaro lakini sasa jibu ni kwamba tumejipangaje na viwanda hivyo je, tuna umeme wa kutosha kwa mahitaji ya viwanda na maji, je, watumishi wajipangaje kuvisimamia ,”anasema.

 

Anasema mkoa Kilimanjaro kuna viwanda zaidi ya sita mabavyo vipo mikononi mwa wawekezaji na vimekufa kutokana na kushindwa kuviendeleza.

Anasema kutokana wawekezaji hao kushindwa kufuata taratibu na kugeuza majengo ya viwanda hivyo kuwa maghala yao ya kuhifahidia bidhaa serikali imeanza kupitia upya mikataba ya wawekezaji.

 

“Nimetembelea viwanda vyote nilichokikuta ni kwamba watu wamehifadhi bidhaa mbalimbali na siyo uzalishaji wa bidhaa kama ambavyo mikataba yao inasema hivyo hao ni sawa na wahujumu uchumi kwani wameikosesha Taifa mapato na kuua ajira za watu kwa makusudi,” anasema Mghwira.

 

Anasema serikali haiwezi kulifumbia macho suala hilo na kwamba  hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wawekezaji hao ikiwemo kuvirejesha viwanda hivyo mikononi mwa serikali.

 

“Hao wawekezaji walivyoshindwa kuendesha viwanda hivyo walipaswa kurejesha viwanda hivyo ili wapishe wawekezaji wengine wenye nia ya dhati ya uwkezeaji kwa masilahi ya taifa na kwa masilahi ya mtu mmoja mmoja,” anasema.

 

Anasema kwamba kufa kwa viwanda hivyo imesababisha serikali kupoteza mabilioni ya fedha kila mwaka ambayo ingeisaidia katika utekelezaji wa miradhi ya maendeleo ikiwemo elimu, afya na maji.

 

Akizungumzia uwekezaji wa mashamba makubwa ya kahawa mkoani Kilimanjaro , Mhgwira anasema serikali imebaini mashamba hayo  ya kahawa ambayo hayajaendelezwa na yamebadilishwa matumiza kwa kuendeleza kilimo cha mbogamboga pamoja na kilimo cha mahindi kinyume na taratibu.

 

Anasema serikali imeanza kupitia upya na kuifanyia marekebisho mikataba ya uwekezaji katika mashamba yanayomilikiwa na wawekezaji pamoja na vyama vya msingi vya ushirika.

 

“Kutokana na nusu ya mashamba hayo kati mashamba makubwa 19 kuibua migogoro  mingi kati ya  wawekezaji na viongozi wa vyama vya ushirika. Njia sahihi ya kutatua tatizo hilo ni kupitia upya mikataba hiyo,” anasema.

 

“Migogoro hiyo inatokana na mikataba mibovu isiyokidhi vigezo kutokana na baadhi ya viongozi wasiokuwa na nia njema na mashamba ya wananchi na kushiriki kutengeneza mikataba mibovu ya miaka mingi

ambayo inakandamiza vyama vya msingi huko ikiwabeba wawekezaji,” anasema.

 

Aidha, anasema serikali katika kipindi cha uhuru ilitaifisha mashamba hayo na kuwapa vyama vya msingi vya ushirika kwa lengo la kulima kahawa lakini vyama hivyo vilishindwa kuyaendeleza na kuingia mikataba na wawekezaji  kwa makubaliano ya kuendeleza zao la kahawa.

 

“Mikataba mingi ya mashamba yale ni yamuda mrefu,na mengine vimeshapitwa na wakati lazima vipitiwe upya na kufanyiwa marekebisho na kusainiwa upya ,inasaidia katika kupatia ufumbuzi wa kero hiyo ya

muda mrefu,”alisema.

 

Anasema kuwa umuhimu wa kuyapitia upya mikataba hiyo ni kuangalia yale mambo ya msingi ambayo wawekezaji ambao ni wapangaji katika mashamba hayo walikubaliana na vyama hivyo, kama wawekezaji wametekeleza makubaliano ya mikataba hiyo.