Home Habari kuu ZANZIBAR YAWATANGAZIA KIAMA WAUZA UNGA

ZANZIBAR YAWATANGAZIA KIAMA WAUZA UNGA

2571
0
SHARE

Na JOHANES RESPICHIUS

NGUVU ya kuwadhibiti wasafirishaji na wauzaji wa dawa haramu za kulevya kwa upande wa Tanzania Bara, sasa imekita kambi visiwani Zanzibar.

Siku chache kabla ya kufanyika kwa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri Zanzibar, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji visiwani humo, Balozi Ali Abeid Karume, ambaye sasa anashikilia Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo  aliliambia RAI kuwa wameshtushwa na taarifa za Zanzibar sasa kuwa lango la kusafirisha madawa ya kulevya na walichokifanya ni kuhakikisha wanalishughulikia suala hilo kikamilifu.

Alisema wizara yake tayari imeshakaa na mamlaka husika ili kuchunguza undani wa taarifa hizo na kuzifanyia kazi bila kujali kama zina ukweli ama hazina ukweli.

Alibainisha kuwa pamoja na mambo mengine, wameiona haja ya kutunga sheria mpya ambayo itaweza kuwachukulia hatua kali watu watu wote wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

“Kuna msemo unaosema lisemwalo lipo, kama halipo linakuja. Kwahiyo kama jambo linasemwa na tumelisikia, wewe (mwandishi) si wa kwanza kulisema, tayari nimekaa na watu wangu ili kuweza kulifanyia kazi suala hilo ili kujua kwanini watu wameanza kusema kwamba madawa ya kulevya yanapitishwa Zanzibar.

“Na mimi nimewahi kusikia sio tu zinatoka kupitia hapa na zinaingia pia nchini, kuna mahoteli ya kitalii, wauzaji wamejificha huko wana ulinzi wao wenyewe, wanafanya mambo haya, niliposikia taarifa hizo nikaziambia mamlaka hizo, lakini suala la Hoteli linasimamiwa na wizara nyingine.

“Suala la uwanja wa ndege nimelisikia na  nakushukuru kwa kutukumbusha  hilo tunalifanyia kazi. Sasa hivi tunafanya kazi kubwa ya kuhakikisha biashara ya dawa za kulevya inadhibitiwa Zanzibar,” alisema Balozi Karume.

Alisema Februari 24 mwaka huu walikaa kikao na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ili kujadili suala hilo kwa urefu zaidi.

Kikao hicho kilikuwa na lengo la kuhakikisha biashara ya dawa za kulevya haifanyiki Zanzibar.

“Na kuna sheria mpya tumeitunga ambayo itawezesha watu wanaofanya biashara hiyo kuchukuliwa hatua kali zaidi, ukweli ni kwamba hii biashara ya dawa za kulevya ina fedha nyingi sana,  kwahiyo katika nchi masikini kama Tanzania wauzaji wamekuwa wakiwadanganya watu kwamba wakiingia huko watapata kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya kufanya kazi ofisini nao kwa tamaa wanaingia kwenye jambo hilo na kusahahu kwamba kuna kufa.

“Wanasahau kuwa tamaa mbele mauti nyuma, niwashauri Watanzania wasijiingize kwenye biashara hiyo, kwa hapa Zanzibar tunaweka mikakati ambayo inashirikisha vitengo mbalimbali vya serikali kwa nia ya kupambana na dawa za kulevya.

“Wizara yangu inasimamia Mamlaka ya viwanja vya ndege Zanzibar, lakini wao kule wanafanya shuguli zao wenyewe ambapo kuna vitengo mbalimbali kama vile kitengo cha Usalama wa Taifa, Polisi, Uhamiaji na kadhalika kwahiyo vitengo hivyo vyote vinashugulikia mambo yote hayo kitu ambacho ninaweza kusema ni kuwa wizara haijakaa kimya inasimamia suala hilo na kuhakikisha haliendelei,” alisema Balozi Karume.

Kuhusu Watanzania wawili mke na mume waliokamatwa nchini China na kudaiwa kuwa walipita kwenye uwanja wa Ndege wa Zanzibar, alisema hana uhakika na hilo.

Alisema kuwa kama watu hao walisema walitokea Zanzibar walikuwa wanadanganya kwani haiwezekani kwa nchi hiyo kwa sababu hakuna ndege yoyote inayofanya safari zake moja kwa moja hadi China ni lazima wapitie Dar es Salaam au Dubai na maeneo mengine.

“Hiyo habari tutaifanyia uchunguzi kama kweli walipita hapa, ilikuwa lini na waliwezaje kupita uwanjani hapo wakiwa na dawa za kulevya.

“Niwashauri Watanzania, hii biashara ni biashara mbaya kwani biashara yoyote ambayo inaweza kutoa uhai wako si nzuri, hao waliokamatwa China hawana namna ni lazima waadhibiwe tu.

“Inasikitisha sana lakini ndiyo sheria yao ilivyo nabaki kuwaambia Watanzania wenzangu kwamba tunapokwenda katika nchi za watu tuhakikishe tunafuata sheria zao kwa sababu hupo kwa watu,” alisema Balozi Karume.